Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami naomba kuchangia katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, anazunguka nchi nyingi sana duniani kwa ajili ya kutafuta wawekezaji, na wawekezaji hawa wakija Tanzania wanapewa vibali na mikataba kwa mujibu wa sheria. Sasa hivi urahisi wa wawekezaji kuhudumiwa katika ofisi zetu za umma ni wa hali ya juu sana uko katika mitandao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Sengerema sisi tuna mgodi mkubwa unaitwa Nyanzaga. Mgodi huu upo kilomita 43 kutoka Sengerema. Mgodi huu mkataba wake ulisainiwa mwaka 2023, nafikiri kama mwezi wa Nane hivi na mkataba ule kwa mujibu wa sheria za Tume ya Madini ya Taifa ni kwamba ulikuwa unatakiwa ndani ya miezi 18 jiwe la kwanza liwe limeanza kudondoka pale Sengerema kwa ajili ya kusafishwa kwa ajili ya kutoa dhahabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango yote ya ulipaji wa fidia ilishughulikiwa kwa mujibu wa sheria, lakini ulipaji wa fidia uliingia katika mgogoro baada ya wananchi wa Jimbo la Sengerema Kata ya Igalula kulalamikia malipo yale ya fidia kuwa madogo. Wenzetu wa Nyamongo ambayo ni Kanda ile ile ya Ziwa, katika mgodi wa Nyamongo katika Wilaya ya Tarime wanalipwa ekari moja shilingi milioni tano na sisi Wilaya ya Sengerema katika Jimbo la Sengerema ekari moja ilikuwa inalipwa kwa shilingi milioni mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikwenda kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, wakati huo alikuwa Mheshimiwa Lukuvi na Naibu Waziri alikuwa Dkt. Angeline Mabula kuwaomba walishughulikia lile jambo lakini bado pamoja na maelekezo ya Waziri, Mheshimiwa Lukuvi wakati ule, kwamba lazima waangalie uwiano kwa nchi nzima na waone malipo yanalipwa kwa uwiano upi, walisimamia malipo yale. Sasa sisi juzi tumekwenda Nyamongo kama Kamati ya Madini, tumekuta kule wenzetu wanalipwa shilingi milioni tano. Ni jambo ambalo lilinihuzunisha sana mimi kama Mbunge wa Jimbo la Sengerema.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgodi ule wa Nyanzaga umekuwa na matatizo makubwa ya kufanyiwa biashara, ni kama vile tunaowapata wawekezaji wote ni ma-middleman. Mgodi huu ulianza mwaka 2002. Kampuni ya Tankan Mining ilikuja kufanya pale kuja kupata leseni na kufanya usanifu wake. Wamefanya usanifu pale kwenye ule mgodi, mwaka 2006 wakawauzia watu wa Barrick, watu wa Barrick wakakaa na huo mgodi na baadaye nao wakauuza ule mgodi tena kwa Sahara Mining. Sahara Mining akauza tena kwa kampuni nyingine ambapo nayo ikawauzia OreCorp. Hawa OreCorp wakati wanakuja kupewa leseni, masharti yakaonekana kwamba, baada ya kurekebisha sheria zetu mwaka 2017 kwamba Serikali lazima ipate asilimia 16 katika mgodi, ikaundwa Kampuni ya Sotta Mining. Sasa mkataba umesainiwa, Serikali ina asilimia 16 kama Sotta Mining.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wenzetu wa OreCorp ambao walikuwa wanatakiwa mwaka jana, 2023 mwezi wa Nne, mkataba wa miezi 18 ndiyo ulikuwa unakwisha. Kabla ya mkataba kwisha, mwezi wa Tatu wakauza hisa zao, tena kwa kampuni nyingine ya Silvercorp. Wale Silvercorp waliouziwa zile hisa nao tena wakauza kwa kampuni nyingine tena ya Sypris ya Australia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa imeonekana kama kuna mchezo sisi Sengerema tunaingia kwenye matatizo. Wananchi wanasubiri kupata CSR baada ya mkataba kusainiwa, kwa sababu ulisainiwa hadharani mbele ya Mheshimiwa Rais. Hili jambo linawaumiza sana wananchi wa Sengerema.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunataka tupate majibu, je, haya mauziano yote yanafanywa Sengerema siyo CSR yetu sisi ambayo tulikuwa tunajua kwenye mkataba tunapata dola milioni sita kwa mwaka? Je, hizi pesa zitalipwa na nani? Kwa sababu hawa tayari wanafanya mauzo, lakini hizi kampuni tangu zimeanza kuuza, kuanzia Tankan Mining mpaka leo tunakuja kumpata Silvercorp tena, na Silvercorp naye anakwenda kuuza, je, kodi ya Serikali imelipwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tupate majibu. Kutokana na matatizo ya kuuzwa huu mgodi, unakuwa kama ng’ombe yupo zizini. Huu mgodi wa Sengerema, tunaonekana kama Sengerema tupo zizini tunakwenda kuuzwa kila siku, haiwezekani, wakati wenzetu tunaona wanavyowekeza kule katika suala la madini. Tunaiomba Serikali itusaidie, ije na majibu katika jambo hili. Kama haiwezekani, iundwe Tume ya Bunge kwenda kuchunguza mauziano haya tangu Tankan Mining mpaka leo kwenye Sotta Mining, kwa sababu kama mkataba huu umekwisha mwaka jana, 2023 mwezi wa Nne, tayari huu mgodi unatakiwa urudi kwa Serikali, Serikali ndiyo ifanye biashara. Hawatakiwi kufanya biashara watu ambao tayari muda wao wa leseni umekwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkataba ulikuwa ni miezi 18 kujenga mgodi ule. Watu wamekwenda pale kujiandaa, lakini hawa watu tayari wameshapotea na aliyekuwa CEO pale anaitwa Mr. Damian, yule mzungu kapotea na kabadilisha na line. Kwa hiyo, inamaanisha mikataba yote iliyokuwa imeingiwa kwa ajili ya uwekezaji, makampuni ya kufanya biashara pale, yote imebakia kuwa hewani. Sasa tunaomba Serikali ije na majibu kuhusiana na suala la mgodi wa Nyanzaga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine linaendelea katika nchi hii kuhusu suala la mizani. Hizi mizani zilizopo barabarani zinazuia kabisa uwekezaji katika Sekta ya Usafirishaji. Kwa mfano, gari la mafuta limebeba labda lita 42,000 kutoka labda Depot Kigamboni Dar es Salaam, linakwenda Kongo au Rwanda ama Burundi au Uganda. Hakuna chochote ambacho kimezidishwa pale, lakini unaambiwa gari imezidi kilo 50, au gari imezidi kilo 100. Hili ni jambo ambalo Wizara ya Ujenzi ije na majibu sahihi kwa sababu wananchi hawa wawekezaji au hawa wenzetu ambao ni nchi jirani zinazotumia bandari ya Dar es Salaam, zinakutana na vikwazo kama hivyo vya kupigwa faini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, linguine ni suala la mizani kupima mabasi. Siku moja nimesafiri na basi la SATCO kutoka Mwanza kuja Dodoma, basi liko level seat, limebeba abiria 42. Basi lile limepimwa katika mizani ya Usagara, linakuja kupimwa katika mizani nyingine kule Tinde linaonekana linazidi kilo 60. Sasa abiria hawa unaowaona, abiria tunazidiana, kuna abiria ana kilo 150, kuna abiria ana kilo 120, hawa wenye mabasi watawezaje kuwapima abiria? Kila abiria akiwa anapanda kwenye basi apimwe, hii itakuwa ni nchi ya kwanza duniani katika jambo hili. Sasa mizani ni ngapi kutokea Mwanza mpaka kufika Dar es Salaam au kutokea Dar es Salaam kwenda Mbeya, Dar es Salaam kwenda Arusha? Haya mabasi kwa nini yaingie kupimwa kwa namna hiyo na yapo katika level seat? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo ambalo tunaomba wenzetu wa Wizara ya Ujenzi waje na majibu sahihi kuhusiana na hili suala. Leo mabasi yanasafiri usiku, lakini yanavyokuwa yanaingia katika mizani, hata kama gari lipo level seat, je, abiria anatakiwa naye apimwe ili aingie kwenye basi? Waje na majibu, watueleze kwamba wenye mabasi sasa waweke mizani kwenye ofisi au stendi zilizopo?
Mheshimiwa Naibu Spika, Stendi ya Ndugai, Dodoma iwe na mizani, abiria akiingia akanyage pale kwenye mizani, aingie ndani ya basi ili haya mabasi sasa yatoke yaache kusumbuliwa. Pia waweke mizani kwenye stendi ya Magufuli pale Dar es Salaam, tujue, kwa sababu kama anaingia na package yake ya mzigo wa kilo mbili na wenyewe upimwe iwe kama viwanja vya ndege, kama tunataka kuipeleka nchi kuwa ya hali ya juu kiasi hiki. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo duniani mabasi yanapimwa? Ni Tanzania peke yake. Sisi tunasafiri nchi nyingi, tunashindwa kuelewa katika jambo hili. Tunaomba sana Wizara ya Ujenzi waje na majibu sahihi kuhusiana na suala la mizani la kunyanyasa wawekezaji na wasafirishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pole na swaumu. Naunga mkono hoja. (Makofi)