Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Nakushukuru sana Mwenyekiti, na naomba nimshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, niwashukuru pia wapiga kura wangu wa Jimbo la Geita Mjini na wananchi wa Geita kwa ujumla wake kwa uvumilivu wao mkubwa wanaoupata kwenye matatizo ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kusoma kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 15 ambapo amesema Serikali iliajiri kampuni ya Shaka Consult Group ya Misri kuwa mshauri mwekezaji wa kusimamia utekelezaji wa mradi wa Bulyanhulu - Geita KV-220 kwenye urefu wa kilometa 55.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameendelea kusema hapa lakini interest yangu ni kule chini; anasema gharama za mradi huu ni dola milioni 23 sawa na takriban bilioni 41. Jumla ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huu ni shilingi bilioni sita, very interesting, na unatarajiwa kukamilika 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa mradi huu ambao ameukusudia kuupeleka Geita. Ninaamini kwamba una nia njema, lakini natazama fedha zilizotengwa sasa na pia natazama muda ambao umejiwekea kutekeleza nayaona matatizo makubwa ya umeme katika Mji wa Geita kwa sasa yataendelea kuwa kero kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu nimsumbua sana mara kwa mara, umeme wa Geita Mjini unazimika kila saa, umeme wa Geita Mjini ambao unatokea Sengerema kuja Geita ni mdogo, ulikuwa umefikiriwa kwa ajili ya Mji wa Sengerema na baadaye ukapelekwa Geita. Umeme ule inapofika saa moja jioni unawaka lakini taa haziwaki. Nimemueleza hili Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri analijua, sasa nilitarajia kwenye taarifa yake hii atakuwa angalau na mpango wa dharura kwa sababu Geita pale ni Mji mkubwa, lakini ni Mkoa ambao tungeweza kuweka mpango mzuri wa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninayo mapendekezo, tunao umeme kilometa 22 tu kutoka Geita Mjini ambao uko Katolo ambao ni umeme wenye nguvu. Wakati unafikiria mradi mkubwa huu ambao utaisha 2018, na inawezekana ukaisha 2020. Umeme huu ambao uko kilometa 22 tu kutoka Katoro kuja Geita, na ambao gharama yake inakadiriwa haifiki bilioni moja kuuvuta kuufikisha Geita Mjini, ingelikuwa ni suluhisho la kwanza la kupeleka umeme katika Mji wa Geita. Hivi ninavyozungumza na wewe kata zinazotengeneza Mji wa Geita wenyewe, kata za Nyankumbu, Bombambili, Buhalahala, Mtakuja zote hazina umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani umeme upo pale pale kati kati ya Mji lakini Vitongoji vyote vya Geita Mjini havina umeme. Pamoja na huo uliopo kutokuwa hautoshi lakini havina umeme. Kuna sehemu wameweka transfoma ambayo kila inapofika jioni saa moja umeme unazimika. Nilikuwa nakuomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na nia njema ya mradi huu unaokwenda mpaka 2018 ambao pia naona fedha zake zimewekwa za kuanzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe suluhisho la sasa, kwa sababu umeme uliopo Katoro una nguvu, utolewe umeme upelekwe pale. Bahati nzuri sana Geita tuna Meneja mzuri wa TANESCO, ana-respond haraka, hana matatizo makubwa, kinachosumbua pale sasa ni kumwezesha ili aweze kufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwenye umeme wa REA. Katika Jimbo la Geita Mjini umeme wa REA bado katika kata zote 13 haujaenda, nimefanya mawasiliano na Meneja wa REA wa Kanda ile amesema ametuingiza kwenye awamu hii, lakini nilikuwa naomba sana, kwa sababu tatizo hili naliona hata katika Jimbo la Geita Vijijini, kazi ya mkandarasi imekamilika mpaka sehemu ya kutoka Nyamadoke tayari; pale panatakiwa tu kuunganishwa ule umeme, leo karibu miezi sita hapajaunganishwa. Nilikuwa naomba sana kwenye umeme wa REA Mheshimiwa Waziri suala hili lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni suala la wachimbaji wadogo wadogo. Mheshimiwa Waziri alikuwepo Geita, na nashukuru kwamba tulifanya mkutano naye na akatoa takwimu nyingi sana. Lakini anakumba nilitoa ushauri wangu pale sikumpinga nilitoa ushauri, ana takwimu nyingi sana zinazoonesha wachimbaji wadogo wamepewa maeneo lakini wanaopewa ni wale wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anayepewa leo London – Singida, anayepewa leo Nyarugusu, anayepewa Kahama, majina ni yale yale. Nilimshauri atengeneze database, atagundua yako majina yale yale yanazunguka. Kila yanapogunduliwa madini wanakwenda wanafukuza wenyeji, wanaunda ka-SACCOS wananunua watu wanahamia pale. Nashauri kwamba wananchi wale wa kawaida bado hawapati maeneo, na ndio maana kelele za magwangala zitaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati tunazungumzia maeneo ya wachimbaji wadogowadogo lazima tuangalie watu wanaojirudiarudia, watu ambao kila mara yanapogundulika madini wanakwenda pale kwenda kutafuta maeneo mapya. Tulipokutana na Mheshimiwa Waziri kwenye ziara yetu Geita tulimgusia kuhusu milipuko. Mheshimiwa Naibu Waziri tulikuwa naye Geita, tulikwenda kwenye nyumba ambazo zimeathiriwa na milipuko, tulikwenda kwenye nyumba ambazo vigingi vya GGM viko ndani ya makazi yao, wale watu hawaruhusiwi kupima, hawaruhusiwi kuuza, wanaonekana eneo ni la mgodi lakini mgodi wanasema hawana kazi nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauriana na Mheshimiwa Naibu Waziri na akatoa muda, akawaambia wafanye declaration kama wanalihitaji lile eneo walipe fidia watu watoke na kama hawalihitaji, wawaruhusu watu waendelee na maisha yao mpaka leo hili suala halijafanyika, matatizo ya watu yanaendelea kuwa pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niseme kwamba kuendelea kukaa katika vigingi watu hawa wanaendelea kuwa maskini. Hawawezi kupima, hawawezi kukopeshwa, hawawezi kujenga nyumba za kudumu. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majibu atuambie anafanya nini kwa sababu hali hii inasababisha wananchi wangu wa Jimbo la Geita kuendelea kuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kidogo kuhusu magwangala. Kama wanavyosema wenzangu magwangala inatokana na vijana wengi na wanotaka biashara za madini kukosa maeneo ya kuchimba; si suluhisho la matatizo ya wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu nina uhakika magwangala yale hata yakitolewa leo baada ya miezi miwili, yatakwisha na yatakapokwisha yale magwangala tutatengeneza tatizo jingine kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitaka kusema pamoja na nia njema ya kutoa magwangala haya ambayo wananchi wanayapigia kelele, wananchi walikuwa na maeneo yao walikuwa wanachimba ya asili pale Geita, kama Nyamatagata, Samina wakaja wakatolewa, lakini maeneo yale dhahabu yake iko juu juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipokuwa Geita akisema yeye hawezi kubadilisha hata mtu ampige risasi. Mimi nataka nimshawishi Mheshimiwa, sheria inasema kila baada ya muda, wanapofanya revision ya license kuna maeneo watu wanayaachia, ni vizuri sana Mheshimiwa Waziri maeneo ambayo wanayaachia yawe ni maeneo ambayo wananchi wanaweza wakachimba wakapata dhahabu ya juu juu.
Mheshimiwa Mwnyekiti, matatizo tuliyonayo sasa hivi Geita ni kwamba hata kama watu wa GGM wangejenga hospitali, shule na barabara kama jamii inayowazunguka pale inalala njaa, kama jamii inayowazunguka pale bado wanaishi katika mazingira kama wako utumwani bado wataendelea kuwachukia wawekezaji na tutaendelea kuuchukia mgodi.
Kwa hiyo, mimi nilitaka niwashauri kwamba ni lazima wananchi wapewe maeneo ya kuchimba, na hili liko ndani ya uwezo wako kwa sababu maeneo tunayo. Tatizo kubwa ni moja walipelekwa maeneo ya Isamilo, wakapewa license karibu 17 za SACCOS wamechimba watu wameweka karibu milioni 200 madini hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechimba pale wanakutana na maji madini hakuna, kwa hiyo mara nyingi migodi inaachia maeneo ambayo imefanya utafiti imegundua kwamba dhahabu zilizopo pale ni ndogo na hazifai. Kwa hiyo nikuombe sana utakapotaka kutoa maeneo tuhakikishe kwamba maeneo haya yana madini ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la service levy. Mheshimiwa Waziti alipokuwa Geita, tulimwambia hatuna mgogoro na Geita Gold Mine ingawa mchango wao wa service levy ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita ule ni mgodi wa pili Afrika kwa dhahabu nyingi, wanatupa bilioni nne. Tuliuliza swali, hizi ni asilimia ngapi ya mapato yao? Kwa sababu tunaamini mapato yao ni makubwa sana, lakini la pili, wanatoa orodha ya kampuni 1,000 wanazofanya nazo kazi. Katika hizo asilimia 80 kampuni zile ziko Ulaya, Australia, New Zealand na Marekani, wanafanya nazo electronic business. Kwa hiyo, anampa Mkurugenzi wa Halmashauri aende akakusanye service levy kwa kampuni ambayo haina license Tanzania, hailipi kodi Tanzania, haina address Tanzania. Tulimwambia Mheshimiwa Waziri, watu wa mgodi walazimishwe kufanya kazi na kampuni za Tanzania ambazo tunaweza kuzi-trace na kujua zinapatikana wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wanakupa kampuni iko New Zealand halafu wanakwambia ukusanye service levy kampuni hii haijulikani, haina leseni, hailipi kodi za Serikali, hata Tanzania haina address na Mheshimiwa hili niliwahi kufika mpaka ofisini kwako nikakutana na Katibu Mkuu wa Wizara, nikamshauri, nikazungumza naye na akasema atalishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hawa watu pamoja na kuwaibia Halmashauri ya Geita, bado pia wanaiibia Serikali. Huwezi ukalipa mtu dola milioni moja kampuni yake iko South Africa, Tanzania haina leseni, hailipi kodi, haina ofisi na Serikali ipo inakubali hizo hesabu wakati wa kufanya Cooperate tax.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana hili liangaliwe vizuri. Na inawezekana kabisa haya yanafanyika kwenye makampuni yote katika nchi hii, kwa sababu visingizio ni kwamba kuna vipuri ambavyo vinaagizwa Ulaya na Watanzania wengi hawana uwezo wa kuviuza, yes tunakubali, lakini procedure za kufanya biashara Tanzania zinajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Watanzania hamuwaruhusu hata kufungua kibanda cha soda bila kupata TIN Number. Kwa nini huyo anayellipa mamilioni ya shilingi anaanza kufanya biashara na Mgodi na analipwa pesa na inakuwa declared kwenye hesabu wakati hana leseni Tanzania na halipi kodi? Ushauri wangu Mheshimiwa Waziri asaidie kupata hizi fedha kwa sababu ni fedha nyingi na tunazihiitaji kwa ajili ya maendeleo ya Mji wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kama unavyoitaza Geita sasa hivi, kuna mashimo makubwa, ambayo tayari dhahabu zimekwisha. Inawezekana kabisa miaka ishirini ijayo tukabaki na mashimo yale na wananchi wa Geita wakaendelea kubaki maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu ni kwamba wakati mgodi unafikiria kufanya CSR washirikiane na Halmashauri kuangalia miradi ambayo sisi tunadhani ina tija kwetu. Siyo wao wanabuni mradi wao halafu ule mradi wanaugeuza kuwa mradi wa wananchi wa Geita. Tunaunga mkono juhudi zao tunapenda waendelee kuwepo, tunataka wawekezaji zaidi lakini lazima waangalie mipango ya Halmashauri namna gani wataingia kwenye mipango hiyo kuliko kuja na mipango yao wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekwenda wameanzisha, chuo cha kushona cherehani wameanza na watu 90 sasa hivi wako watu kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naunga mkono hoja.