Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ambaye ameniwezesha asubuhi hii kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuchangia Bajeti hii ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nimshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha kwamba jamii hii ya Tanzania inastawi na inasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukurani hizo, naomba nijielekeza katika maeneo yafuatayo: Kwanza, ni kilimo. Wilaya yangu ya Nanyumbu ni Wilaya ambayo ni ya wakulima, na kilimo chetu kikubwa cha biashara ukiondoa ufuta na karanga, ni korosho. Korosho ndiyo uti wa mgogo wa Wilaya ya Nanyumbu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii tena kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa programu aliyoileta ya kuhakikisha kwamba wakulima wote wanapata pembejeo za kilimo bure. Kwa hili jambo, namshukuru sana. Vile vile Mheshimiwa Rais amekwenda mbele mwaka huu kwa kuielekeza Bodi ya Korosho iandae utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kila mkulima anapata pembejeo. Kwa hiyo, Bodi ya Korosho imekuja na utaratibu wa kusajili wakulima upya na kuhusisha taarifa za wakulima wa zamani ili nao waweze kuziboresha ziwe katika mfumo ulio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Bodi ya Korosho ina changamoto, kwani imewaajiri vijana wetu ili wafanye kazi ya kusajili wakulima, lakini hawajawapa vitendea kazi. Wamewapa kazi, lakini wale vijana wanatakiwa watumie simu zao za mkononi. Hili jambo kwa kweli halikubaliki. Bodi ya Korosho wameshindwa hata kuwapatia viatu (gumboot). Wale vijana wanaenda kusajili mashamba ya wakulima kwa kutumia viatu vyao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi hiki cha mvua vijana wale wanakwenda kufanya kazi bila miamvuli. Sasa unaanza kujiuliza, lengo la Bodi ya Korosho ni kupata takwimu sahihi za wakulima au kufunika kombe mwanaharamu apite? Kwa sababu lengo ni kupata takwimu sahihi za wakulima wetu. Hawa vijana ambao wamekuwa trained, tulitegemea Bodi ya Korosho iwape vitendea kazi kama simu, gumboot na vifaa vya kujikinga na mvua. Badala yake vijana wamekwenda hivi hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia vijana hawa hawalipwi kama inavyotakiwa. Katika makubaliano ya Bodi ya Korosho ni kuwalipa vijana hao kila wiki. Hivi ninavyozungumza, kuna vijana wana wiki tatu au nne hawajalipwa. Nini matokeo yake? Matokeo yake taarifa ambazo Bodi ya Korosho inategemea izipate, hazitapatikana. Vile vile utakapokuja msimu wa kuwapa pembejeo, wakulima wengi watakosa pembejeo kwa sababu taarifa zao hazijafika kunakohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, lile zoezi ambalo linaendelea ndani ya Jimbo la Nanyumbu likafanywe vizuri. Taarifa zilizopo nyingi siyo sahihi na wakulima wengi takwimu zao hazitapatikana na hivyo wakati wa kugawanya pembejeo watakosa pembejeo na hivyo kuathiri uzalishaji wa zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili ya zao hili la korosho ni bei kwa mkulima. Bei ya mkulima imekuwa ndogo mwaka hadi mwaka. Mwaka 2023 tumeshuhudia bei ya korosho imefika mpaka shilingi 1,200/= kwa kilo. Hili jambo linahuzunisha sana. Nilifurahi sana Bunge lililopita Waziri wetu, Mheshimiwa Bashe alipotoa msimamo kwamba kuanzia mwaka huu hasa zao la ufuta tutatumia utaratibu wa TMX badala ya utaratibu wa zamani. Naomba kusisitiza, TMX waingie sasa hivi kuanzia ufuta na mazao mengine yote yanayokwenda kwenye minada yetu. TMX ndiyo mwarobaini wa tatizo la bei ya korosho na mazao mengine ya maghala, kwa sababu utaratibu uliotumika unawanufaisha watu wachache. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, msimamo huu asije akaubadilisha, tunaitegemea TMX iingie katika zoezi la kufanya uhakiki wa bei za wakulima na jambo hili litamkomboa mkulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ushirika. Sisi watu wa Nanyumbu ni wazalishaji wakubwa wa korosho kama nilivyozungumza hapo awali. Mwaka 2022 tumezalisha tani 16,000 za korosho, mwaka 2023 tani 15 na point something. Jirani zetu Tunduru mwaka 2022 wamezalisha tani 15,000 lakini Tunduru wao wana Chama chao cha Ushirika. Sisi watu wa Nanyumbu tunategemea Chama Kikuu cha MAMCU. Nafikiri wakati umefika watu wa Nanyumbu tuwe na Chama chetu cha Ushirika ambacho kitahakikisha bei nzuri ya mkulima inapatika ndani ya Wilaya yetu. Kwa nini nasema hivyo? Ni jambo la kushangaza kwamba korosho za Nanyumbu zinakuwa na bei ndogo, lakini Korosho za Masasi zinakuwa na bei kubwa wakati ni ukanda ule ule. Sisi watu wa Nanyumbu tunazalisha korosho nyingi kuliko majirani zetu, lakini tunaendelea kuwa chini ya chama ambacho hakitusaidii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanalalamika bei ndogo, wanakosa vifungashio vya korosho na hawapati huduma sahihi kupitia Chama Kikuu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze, ni taratibu gani tuzitumie watu wa Nanyumbu ili tujitegemee tuwe na chama chetu Kikuu cha Ushirika? Vinginevyo, kwa kweli wananchi wetu wataendelea kuteseka. (Makofi)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango mzuri ambao mzungumzaji anaendelea nao, napenda kumpa taarifa kwamba, bei ya korosho inategemeana sana na ubora wa korosho. Kwa hiyo, kuna uwezekano wanalima korosho nyingi lakini labda ubora wa korosho hiyo hauko sahihi sana. Vile vile, inategemea na suala la masoko. Kuna wengine wanapenda TMX na wengine kama sisi watu wa Pwani tunapenda mfumo wetu wa Stakabadhi Ghalani wa kulaza boksi. Ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Yahya, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake siipokei. Kwanza, katika korosho bora katika Mkoa wa Mtwara ni korosho ya Nanyumbu. Mzungumzaji ili apate bei nzuri, basi anazileta korosho zake kule na kuchanganya na zetu ili auze. Kwa hiyo, hiyo taarifa siyo sahihi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili ni kuhusu ardhi. Mheshimiwa Rais aliunda Kamati ya Mawaziri tisa, iliyozunguka Tanzania nzima chini wa Waziri wa Ardhi wa wakati ule, wakafika mpaka ndani ya Mkoa wetu wa Mtwara. Ndani ya Jimbo langu, moja ya Kata yangu iliathirika sana na zoezi hili hasa katika Vitongoji vya Namalomba, Wanika na Mbunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulisafiri kutoka Mtwara hadi kwenye hizo Kata chini ya Waziri wa wakati ule Mheshimiwa Mama Mabula, na tulikubaliana kwamba wananchi wale watoke ndani ya vile vitongoji, wapangiwe maeneo mengine na watalipwa fidia. Kwa masikitiko makubwa, sasa ni mwaka mmoja, wale wananchi hawajalipwa fidia, wapo katika maeneo yale yale, hawajui hatima yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri aliyeteuliwa baada ya Mheshimiwa Mama Mabula, alikuja na Mheshimiwa Rais, akakutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nanyumbu akaahidi kwamba mara arudipo Dodoma, atahakikisha wananchi wale wanalipwa ndani ya wiki mbili. Nina masikitiko kwamba mpaka sasa hivi wale wananchi hawajalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini matokeo yake? Wananchi wale wanaendelea kubaki na umaskini, hawajui hatima yao. Sasa watakapokuja hapa kufanya majumuisho, watueleze utaratibu wa wale wananchi kutoka katika maeneo yale upo au haupo? Vinginevyo napata tabu sana ninapokwenda kwenye vikao na wananchi wangu. Wataniuliza, nini hatima yetu? Sina majibu. Ukimwuliza Waziri, naye hana majibu. Sasa aje atuambie hapa, utaratibu wa wale wananchi kulipwa fidia ili waachie yale maeneo waondoke, upo? Vinginevyo tunazidi kuwatesa wananchi na tunawatia umaskini, kwa sababu hakuna kinachofanyika wakati huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu lingine ni umeme. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa jitihada anazozifanya kuhakikisha kwamba umeme unapatikana katika nchi yetu. Hili jambo la kupongeza sana. Kwa kweli ni jambo la kushukuru sana. Kwangu, kati ya vijiji 47 ambavyo vilikuwa na changamoto kubwa ya umeme, bado vijijini vitano tu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mhata.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, muda hautoshi, lakini naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)