Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi ya kuchangia. Nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Baraza lake la Mawaziri. Napongeza sana Baraza lote la Mawaziri kwa sababu kazi waliyofanya ya kumshauri Mheshimiwa Rais ni kubwa sana hasa upande wa watumishi wa nchi hii. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kuanzia Ibara ya 151 kuhusu Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri. Nawapongeza. Nakumbuka nilipoingia Bungeni, jambo la kwanza nilililia ni Vyama vya Wafanyakazi na Serikali kupeana elimu ya ushirikishwaji, wote kuelewa wanatakiwa wafanye nini? Maana vyama na Serikali hatutakiwi kuwa wagomvi. Tunatakiwa kushauriana kwa sababu tunajenga nyumba moja, tusigombanie fito.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza kwa kuwa naona suala hili wamelifanya, wametoa semina kwa watendaji wa vyama 12 kati ya 33. Nashauri waongeze juhudi hizi ili vyama vyote vipate hiyo elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais, kwani tukiwa Morogoro Mei Mosi, tulikuwa tumeongea humu ndani ya Bunge na niliongea kuhusu vitendea kazi na ameweza kununua magari 30 kuwapa ile Idara ya Elimu na elimu tunaona imeenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Idara za Elimu kwa kweli sasa hivi ukizunguka huko unawaona kazi wanayofanya imesaidia, wameweza kutoka na kufuta migogoro ya watumishi 5,056, sasa wameenda mpaka 5,678. Siyo suala dogo, wameenda nusu ya kazi. Hii imesababishwa na kuwa na huduma ya usuluhishi wa migogoro inayotembea. Sasa tuifanye iendelee iwe ni nchi nzima. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee usalama wa afya mahali pa kazi. OSHA wanajitahidi sana, lakini kuna baadhi ya watumishi bado wanakwamisha utekelezaji wa haya wanayoyatekeleza. Mkoa wa Dar es Salaam tuna viwanda vingi sana na huwa nafanya ziara kwenye viwanda hivyo na shahidi atakuwa ni Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa sababu ana viwanda vingi sana kwenye Jimbo lake kama Mbunge wa Jimbo la Mbagala, lakini ukaguzi unaofanyika pale, nashauri tuuangalie kwa makini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna viwanda siwezi kuvitaja majina kwa sababu ni wawekezaji wetu, lakini niwape kazi ya kwenda kufanya. Unakuta watumishi wamefungiwa mle…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa, tunaomba utulivu ndani ya Bunge.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: …unakuta hewa hamna, hawana zana za usalama na wanafanya kazi hatarishi. Nilimwita Mbunge wa Temeke awe shahidi. Kiwanda kimefungwa je, hapa ikitokea ajali inakuwaje? Mwenye kiwanda anasema, “nafunga kwa usalama, wasiniibie.” Sasa maisha ya watumishi wetu na wananchi wetu ni bora kuliko mali zilizopo pale! Nawaomba OSHA waende kukagua.

Mheshimiwa Naibu Spika, usalama ni pamoja na hali ya mtumishi yule, atakuwaje wakati yupo sehemu ya kazi? Niliwahi kukutana na watumishi wa OSHA na watakuwa wananisikiliza. Niliwaambia, subiri nirudi Bungeni. Wakifika hawakagui, nami wakati mwingine huwa navaa dera, naenda kama ombaomba kwenye viwanda ili nijue kinachoendelea kwa watu ninaowawakilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wale watumishi wamekuja pale, yule mwenye kiwanda anasema wameshakuja OSHA, vyoo vinafungwa ili wasiende kuangalia usafi wa vile vyoo kule ndani, lakini kwa sababu nilikuwa nimejifanya mteja siku hiyo, nikawaambia naomba kwenda chooni. Kile choo hawezi kukitumia binadamu, lakini OSHA wanatoa certificate safi na unaikuta ukutani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna watumishi ambao bado wanaihujumu OSHA. Wanamaliza nguvu ya Mkurugenzi. Kwa kweli Mkurugenzi anajitahidi sana sana. Nadhani siku hiyo nilimpigia simu nikamwambia angalia walio chini yako wanakuangusha. Kwa hiyo, naiomba Serikali wakaliangalie hilo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uwajibikaji wa wafanyakazi. Kwa kweli kwa sasa hivi wanawajibika sana, lakini sasa wajibu unaendana na haki; na hili nitaongea sana ikifika Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Bado tuna watumishi wanadai madeni, hapa kuna mtumishi alituma message kwa Profesa hapa akasema mwambie Mheshimiwa Janejelly leo aongelee kuhusu nauli zetu za likizo. Bado kuna watumishi hawajalipwa nauli zao za likizo. Sasa kwa hili, tunaharibu maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yeye ameshaamua watumishi wakae kwa amani, wafanye kazi kwa amani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaiongea sana tukifika kwenye Wizara ya Menejimenti ya Utumishi, na Wizara ya Fedha kwa sababu hili tatizo ndiyo lipo kule. Mathalan, madeni ya Walimu, fedha zao huwa zinatoka moja kwa moja Wizara ya Fedha, lakini haipelekwi kwenye zile halmashauri. Kwa hiyo, walimu wanagombana na wakurugenzi kwamba hawajawalipa, lakini ni kwamba mkurugenzi anakuwa hajapelekewa ile bajeti kutoka Wizara ya Fedha hasa hela za nauli ya likizo. Naomba Serikali iliangalie hilo kwa makini sana. Tusiwakorofishe hawa watumishi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la maslahi ya kustaafu. Naomba waongeze speed ya kulipa fedha za kustaafu (pensheni). Hebu tufanye haraka ya kuwalipa hawa watumishi wetu. Kuna kipindi walikuja na utaratibu mzuri kwamba, kama pensheni inachelewa, basi miezi mitatu huyu mtumishi awe ameingizwa kupata yale malipo ya kila mwisho wa mwezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niomba Serikali ifanye hilo hasa upande wa walimu, maana bado wanalia sana, wanalalamika sana na hawa ndio tunaowategemea wawajenge ninyi mawaziri. Hakuna Waziri ambaye hakufundishwa na mwalimu na wala hakuna Mbunge huku ambaye hakufundishwa na mwalimu. Kwa hiyo, tujaribu kuliangalia sana hilo, kwani bado kuna malalamiko hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nikisoma message, nitamletea Mheshimiwa Waziri Jenista aone, wanalalamika sana na yawezekana hata elimu ya kikokotoo hatujaitoa ipasavyo kuwaambia faida na hasara zake. Bado wapo kwenye giza, hawaelewi kwamba wanacholipwa kimetokana na nini? Kokotozi zimeendaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ni elimu ya kuwaelimisha, yawezekana tunachofanya kina faida, lakini kwa sababu hatujawapa elimu, wanaona kama wanaonewa sana na hawajatendewa haki kwa miaka waliyokaa kazini. Naomba wapewe elimu ipasavyo ili tuwaweke sawa watumishi wa Serikali waelewe ni kwa nini tulifikia malengo hayo ya kusema pensheni sasa isiwe asilimia 50 na iwe asilimia 35.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana tutoe hiyo elimu kwani imeleta sintomfahamu. Elimu inatakiwa sana. Tukiwaelimisha watajua maana ya kwa nini iliamuliwa hivyo? Tukikaa kimya, wao wanaona kama wameonewa, hela zao zimeenda sehemu nyingine ambapo hazikutakiwa kwenda, kumbe haipo hivyo, yawezekana ni kwa nia nzuri tu. Nawaomba tukalifanyie kazi hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni promotion. Jana hapa limeulizwa swali na Mheshimiwa Jenista akiwa utumishi ndiyo alikuja na hili suala kwenye bajeti, na kweli waliitenga bajeti na vyeo vya mserereko vikaruhusiwa. Hata hivyo, kuna sintofahamu kwa wale wasimamizi, tunaenda kwa kuangaliana sura. Hili nalisema bila kuficha. Wanavyopeleka mserereko unakuta wamemsereresha mtu wa mwaka 2018, wamemwacha wa 2014. Sasa unashindwa kuelewa wanatumia kigezo gani? Maana tunaelewa kuserereka huyu aliyetangulia huku kupata cheo cha kwanza ndiye angeserereshwa ili aende kwa haki yake iliyokuwa inatakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nasubiri Mheshimiwa Waziri wa Utumishi, tutakutana kwenye bajeti yake. Katika hilo, majibu wanayotoa wataalam siyo halisi na kinachotendeka kule kwenye eneo la tukio. Wanawaletea taarifa kwamba tumesereresha, lakini kuna watu bado wameachwa na ukiuliza sababu, hawakupi majibu ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, huwa naongea na Maafisa Utumishi kwenye manispaa ninayotoka, kwamba, hivi wanaelewa wanachofanya? Sasa unamwacha huyu wa mwaka 2017, unamsereresha wa mwaka 2018, haki ipo wapi? Serikali imekuja na nia nzuri tu kwamba hao watu waserereshwe, wapate haki yao. Naomba, aidha, Maafisa Utumishi wapewe mafunzo, ni kwa sababu wanakaa muda mrefu hawajaenda mafunzo? Sielewi! Siyo kwamba nawatuhumu, ila nasema kile ambacho watumishi wanakutana nacho. Hilo la mserereko tuliangalie kwa sababu nia ya Serikali ilikuwa ni nzuri sana, kuwapa watumishi maslahi yao. Naomba tuliangalie sana hilo, kwani linatuletea sintofahamu huko chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Serikali ndiyo ilitaja watendaji wapewe ile shilingi 100,000/=. Hivi ugumu uko wapi? Nimepiga kelele, nimeuliza maswali ya msingi, lakini bado hao watendaji hawalipwi haki yao. Shida ipo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichunguza shida ilipo, hili halijafanywa kama ni first charge, halijafanywa kama ni priority kwenye manispaa zetu. Hawaoni kama ni kitu cha muhimu kumlipa huyu mtendaji haki yake? Leo nairudia, hii ni mara ya nne ndani ya Bunge hili, hata ukiangalia Hansard, naongelea hizi posho za watendaji. Shida ni nini? Tatizo liko wapi? Basi kama tuliona tulilitoa tu kwa utashi wa kisiasa, haliwezekani, tulifute.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)