Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambazo anazifanya kwenye nchi yetu ya Tanzania hasa kwa upande wa wakulima, hali ya ruzuku ya pembejeo, na pia masoko yanazidi kuongezeka, bei za wakulima wetu zinazidi kupendeza. Tumshukuru sana pia Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambazo amezifanya kwenye mradi mkubwa wa maji wa Bwawa la Nyerere ambapo sasa tunaenda kuondoa kabisa kero ya umeme kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Kamishna wa Madawa ya Kulevya nchini, Ndugu yetu Lyimo kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwenye nchi yetu kuteketeza mashamba mengi ya bangi, kukamata wauzaji wa madawa ya kulevya. Ni kazi kubwa ambayo anaifanya kijana wetu, lazima tumtie moyo, lazima tumpe nguvu kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa ajili ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite sana kwenye suala la barabara. Hali ya mwaka huu imekuwa ni ngumu sana katika maeneo mengi hapa nchini hasa katika Jimbo la Ushetu. Nawapongeza Wizara ya Ujenzi kwa kazi kubwa ambayo wameifanya hasa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, ndugu yangu Mheshimiwa Bashungwa, amezunguka katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kukagua barabara, lakini kazi ambayo naiona ni usimamizi hafifu, kwa sababu maeneo mengine hata mvua ikinyesha kidogo tu, unaona madaraja yanaenda na maji, ma-calvat yanabomoka kwa sababu namna ya ufuatiliaji wa barabara zetu na usimamizi kwa wakandarasi umekuwa ni hafifu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ya Ujenzi iwasimamie wakandarasi kwa sababu kama hajafika Waziri eneo lile katika mkoa ule pia kuna Meneja wa TANROAD. Hawa watu wanafanya kazi gani kwenda kukagua wakandarasi wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia barabara nyingi zinazojengwa, haziwekewi mitaro ya maji. Sasa niendelee kuwaomba, zamani niliona Mawaziri wakati mwingine walikuwa wanazunguka, watu wa TANROAD wanazunguka mpaka na nyundo kugongagonga kuona usimamizi mzuri wa barabara. Ukiangalia hata zile lami zinazojengwa kabla hata mkandarasi hajakabidhi mradi, tayari unakuta barabara imeanza kubomoka, imeanza kuwa na mashimo na kuanza kuwekewa viraka. Unafika mahali magari yanapata ajali wakati mwingine kupitia yale mashimo ambayo mkandarasi ameshindwa kusimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama Wizara ya Ujenzi ina changamoto ya nyundo kukagua zile barabara, nipo tayari kuwapa zile nyundo ili wakandarasi wakakaguliwe kuhakikisha barabara zinakuwa imara na fedha anazopeleka Mheshimiwa Rais kwenye ujenzi wa barabara zetu ziweze kusimamiwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu baada ya mwaka mmoja, kunahitajika marekebisho, na baada ya muda mfupi yanahitajika marekebisho. Hizo fedha zingefanya kazi nyingine hata kununua madawa katika hospitali zetu. Kwa hiyo, naomba eneo la ujenzi wakandarasi wakasimamiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna changamoto ya utunzaji wa mazingira. Jana katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 78 ameongelea sana suala la nishati, lakini tunagawa gesi na gesi hizi nyingi zinagawiwa mjini. Niendelee kuwaomba Wizara ya Nishati, wakae na watu wa maliasili na kama kuna fedha ambazo wanazitenga kwa ajili ya kukusanya kwenye maeneo yetu, kwenye mageti, naomba wakusanye fedha wakawape ruzuku wananchi wetu kwa ajili ya mitungi ya gesi. Kwa sababu ukiangalia wananchi wana mwitikio mkubwa sana, na jana Waziri alitoa taarifa akasema wameanza kutoa mitungi ya kilo tatu, tano na sita. Hongera sana kwa Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuwaomba waweke ruzuku. Kama Serikali imeweka ruzuku kwenye mbolea, imeweka ruzuku kwenye mafuta na leo hii tunaenda kudhibiti ukataji miti na uharibifu wa mazingira kwenye nchi yetu, naomba waweke ruzuku pia kwenye matumizi ya gesi. Unakuta gharama ya kuweka mtungi mmoja ni zaidi ya shilingi 30,000. Sasa mwananchi yupo kilometa 30, mitungi ya gesi inayopatikana ipo mjini, ipo kwenye Makao Makuu ya Halmashauri, lakini kwenye kata zetu na vijiji hakuna mahali ambapo inauzwa mitungi ya gesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaposema kuelekea 2025/2026 tunaenda kuwa na mabadiliko makubwa sana ya utunzaji wa mazingira, wananchi wote watumie gesi, wanaenda kuipata wapi? Mwananchi ili asafiri kupata mtungi wenye gesi, leo tunagawa mtungi labda katika kijiji fulani, lakini ili aende kupata mtungi wenye gesi atembee kilometa 70; nauli ni shilingi 10,000, kwenda na kurudi ni shilingi 20,000, mtungi ni shilingi 35,000, jumla ni shilingi 55,000. Wananchi wa maisha ya kawaida wanapata wapi zile fedha?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara iweke ruzuku kwenye upande wa mitungi ya gesi ili tuwasaidie wananchi waweze kupunguza matumizi ya kukata kuni, tuelekeze nguvu sasa kwenye ruzuku. Mfano maliasili, pale wanatumia fedha nyingi sana kwenye magari mengi sana kukimbizana na wananchi wetu. Nenda kwenye mageti yote ya TFS, wameweka mageti lakini wanakamata baiskeli zetu. Mwananchi wetu wa maisha ya kawaida hasa sisi wenye majimbo ya vijijini, kuipata baiskeli, mwananchi wetu anatumia zaidi ya miaka miwili, ananunua baiskeli ya shilingi 150,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwananchi huyu anabeba gunia lake la mkaa, amelipia vibali, anakuja kufanya kosa dogo ananyang’anywa baiskeli yake, au pikipiki yake, lakini zinalundikwa kwenye mageti halafu matokeo yake hawarudishiwi, hata utaratibu kwamba watazipataje, hakuna. Yaani wananchi na watu wa maliasili ni kama wana vita hivi. Sasa mahusiano ya kikazi hayapo. Mwisho wa siku zinapigwa mnada na kuchomwa moto.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya Maliasili iweke utaratibu wa kuwarejeshea wananchi wetu baiskeli zao walizozikamata kwenye mageti, walizozikamata kwenye ofisi zao ili zisaidie kwenye kujenga uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda siyo mrefu tunaenda kuwaomba kura wananchi wetu na hawa wananchi walio wengi ndiyo wapigakura wetu wazuri na wanafanya kazi nzuri ya kujenga uchumi wa nchi yetu. Leo hii wanaenda kukamatiwa baiskeli zao, zinakusanywa, nendeni kwenye mageti yote Waheshimiwa Wabunge wenzangu hasa kwenye mageti ya majimbo ya vijijini, baiskeli zimelundikana kule. Sasa kwa nini Maliasili isiweke utaratibu mzuri na rafiki kabisa wa kuhakikisha hata kama umemkamata mwananchi, basi mpe utaratibu mzuri wa lini atakuja kukomboa baiskeli yake? Anakuja kukomboaje pikipiki yake?

Mheshimiwa Naibu Spika, madhara ya hili ni kwamba mwananchi anarudi tena kukusanya fedha yake kwa muda wa miaka mingine kununua baiskeli. Wananchi wanakuwa na hasira na sisi. Kwa hiyo, niendelee kuiomba Maliasili, leo tuna miaka 60 ya uhuru, karne ya 21 bado tunakimbizana na wananchi na magari. Sasa kwa nini zile gharama za mafuta na za kulipa wale maaskari tusizipeleke kwenye ruzuku ya mitungi ya gesi ili kuwapunguzia wananchi kukata miti?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mikopo ya asilimia kumi, kuna Halmashauri zilifanya kazi vizuri, zilikuja kuponzwa na Halmashauri chache ambazo hazikufanya kazi vizuri. Naomba ufanyike utafiti wa kutosha kabla hatujazuia kitu kama hiki, tunazuia mikopo kwa akina mama, tumezuia mikopo kwa walemavu na kwa vijana wetu waliokosa ajira, walikuwa wanapata fedha huko, wanapata hizi bodaboda wanaendesha, wanajiajiri, lakini leo hii tumezuia mikopo nchi nzima. Leo ni karibu mwaka wa pili, hawa vijana walikuwa na mitaji yao sasa wanateseka wanarejeshaje marejesho benki wakati tayari sasa utaratibu wa kukopeshwa tena umeshasimamishwa nchi nzima? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kosa la watu wachache linasababisha nchi nzima kukosa mikopo. Naomba uwe unafanyika upembuzi mzuri. Pia kuna hawa vijana wetu wanaozidi miaka 35 waliotoka vyuo vikuu, hawana ajira, hawajapata ajira, wako mitaani, lakini hili kundi bado halihesabiki kukopeshwa. Naomba Wizara inapokuja, ije pia na utaratibu wa hawa wananchi wetu vijana ambao wanazidi miaka 35, kwa sababu hata kwenye ajira hawajapata, lakini wanapoenda upande wa pili tena wanaambiwa umri umezidi. Sasa hili kundi nalo ni kubwa, tulifikirie kwenye utaratibu wa kuingia kwenye asilimia 10, liweze kupata mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naendelea kuiomba Wizara ya TAMISEMI, inabebeshwa mizigo mikubwa sana. Ukiangalia zahanati ziko TAMISEMI, shule za msingi ziko TAMISEMI, sekondari ziko TAMISEMI, Hospitali za Wilaya za Halmashauri ziko TAMISEMI, leo hii pia Maafisa Ushirika na wenyewe wako TAMISEMI, sasa hawa TAMISEMI wamepewa mzigo mzito mno wa namna ya usimamizi wa zahanati zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba Hospitali za Halmashauri na Wilaya zipelekwe Wizara ya Afya zikasimamiwe vizuri ili tuwapunguzie mzigo hawa TAMISEMI. Ndiyo maana sasa unakuta hata matukio mengine yanapotokea, namna ya usimamizi kwa wataalam wetu...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante. Ni kengele ya pili hiyo.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)