Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri na leo hii nimeweza kusimama katika Bunge hili. Kwanza, nachukua fursa hii kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha analeta maendeleo mijini na vijijini. Mwenyezi Mungu amjalie afya Mheshimiwa Rais wetu, azidi kutuletea maendeleo katika majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri, Jenista Mhagama na dada yangu Mheshimiwa Ummy Nderiananga, kwa kweli wamekuwa wakifanya kazi kubwa katika Wizara hii. Mwenyezi Mungu awajalie na ninawaomba waendelee kuitumikia vema Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 16 Septemba, 2023 Mheshimiwa Rais alikuja na kufanya ziara katika Jimbo langu. Moja ya changamoto kubwa ambayo nilimpa Mheshimiwa Rais ni maji katika Kata ya Nanguruwe Kijiji cha Nanguruwe. Kwa masikitiko makubwa, ule mradi Rais alisema ufanyike haraka ili wananchi wa Kata ile waweze kufurahia huduma hii muhimu ya maji safi na salama. Tokea terehe hiyo ambayo Mheshimiwa Rais alikuja mpaka kufikia leo, unasuasua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kaka yangu, Mheshimiwa Waziri wa Maji, wewe ni msikivu na unafanya kazi nzuri, naomba ufuatilie suala la maji. Wananchi wangu walikuwa na mategemeo makubwa, wana shida ya maji na wanataka kuona mradi huu umekamilika haraka ili waweze kupata huduma hii muhimu ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa inayolikabili Jimbo langu la Mtwara Vijijini ni changamoto ya maji, lakini vyanzo vya maji vipo. Tunacho chanzo cha Maji cha Mayembechini na tuna Chanzo cha Maji cha Mto Ruvuma, uthamini ulishafanyika na mchakato wa kuhakikisha wanamaliza tatizo la maji kwa ujumla katika Mkoa wetu wenye changamoto ya maji, lakini mpaka leo mradi huu unasuasua. Uthamini ulifanyika kwa wananchi, wananchi wale toka wamefanyiwa uthamini mpaka leo hii hawajui kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji hivyo ambavyo vimefanyiwa uthamini ni Kijiji cha Kitaya, Kihamba, Dindwa, Kivava, Mahurunga, Kihimika, Magomeni Nyasi, Tangazo, Litembe, Litambo, Ziwani, Namindondi, Mtendachi na Mtawanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2015 takribani miaka 10 mpaka kufika hii leo wananchi hawa hawajalipwa fidia, wanashindwa kuendeleza maeneo yao, hawana wanachokielewa mpaka sasa hivi. Sasa naomba commitment ya Serikali, ni lini wananchi hawa watalipwa fidia? Kama hakuna fidia na hakuna chochote kinachoendelea, basi wawaruhusu wananchi hawa waendeleze maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado nina chambamoto. Kuna kata moja inatwa Lipwidi, tokea tumepata uhuru kata hii haijawahi kufurahia huduma hii muhimu ya maji safi na salama. Naiomba sana Serikali iiangalie Kata hii. Wananchi wapo katika mazingira magumu sana. Wananchi wanakunywa maji machafu sana karne hii. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Maji na Serikali iangalie kata hii kwa jicho la huruma ili wananchi wangu waweze kufurahia huduma hii muhimu ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala la barabara. Tokea nimekuwa Mbunge wa Viti Maalum, nimekuwa nikiililia sana barabara ya uchumi, barabara inayotoka Mtwara Mjini kuelekea Msimbati ambako kuna mitambo na visima vya gesi kule. Natamani kulia maana hali ni mbaya. Sehemu kubwa ambayo imewekezwa na Serikali, barabara ni mbovu. Juzi nilikuwa huko, barabara haipitiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wakija hapa, nikiwauliza maswali tokea kipindi hicho mpaka leo majibu yao hayaridhishi. Mimi kama Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, naiomba Serikali iangalie barabara hii ya uchumi iwekwe lami. Hivi yakitokea ya kutokea, hatuombei yatokee, lakini kule kuna vitu muhimu Serikali inawekeza. Leo hii kukitokea la kutokea kule, kutoka mjini mpaka kufika kule si tutakuta vitu vimeshaharibika? Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie barabara hii ya uchumi na iijenge kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara ya ulinzi ambayo ni muhimu sana kutokana na ulinzi na usalama wa watu wetu. Barabara hii nayo kwa muda mrefu ni mbovu, chafu na ninyi wenyewe mnatambua kwamba Jimbo langu limepakana na nchi jirani ya Msumbiji. Mnatambua hali iliyopo kule. Leo hii watu wetu wa ulinzi na usalama wanapata tabu na wanapata ajali kutokana na ubovu wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali iangalie barabara hii kwa umuhimu wake, nayo ijengwe kwa kiwango cha lami. Nimekuwa nikipiga kelele mara nyingi kwa ajili ya barabara hii, kwa hiyo, naiomba Serikali muiangalie barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye suala la afya. Jimbo langu la Mtwara Vijijini lina changamoto mno ya watumishi kwenye kada ya afya na elimu. Tunayo shida ya watumishi upande wa afya na walimu pia. Upande wa walimu kuna shule ina wanafunzi wengi, shule ya Msingi Kivava. Kwenye shule hiyo kwanza hakuna nyumba za walimu na ukiziona nyumba za walimu utalia. Walimu wanaishi katika mazingira magumu na pili, kuna walimu watatu tu. Naiomba sana Serikali ituletee walimu wa kutosha katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini. Vilevile, tunaomba watuletee watumishi wa afya katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ardhi, kwanza nampongeza Mheshimiwa Jerry Silaa kwa kazi kubwa anayoifanya katika Wizara hii. Juzi nilikuwa Jimboni kwangu Mtwara Vijijini, Kata ya Mahurunga Kijiji cha Kivava, kumetokea mafuriko makubwa sana na hii ni mara ya pili yanajirudia mafuriko haya. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alichukue hili. Wananchi wangu wametoa maeneo, lakini inahitajika kulipwa fidia kwenye mashamba yao. Namwomba Mheshimiwa Jerry lichukue hili, twende ukalipe fidia kwa wananchi wale ili tuepukane na mafuriko haya kujirudia mara kwa mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie upande wa asilimia kumi. Wananchi wangu wamekuwa wakiniuliza sana kuhusu suala hili la asilimia kumi, hawaelewi sintofahamu iliyokuwepo mpaka leo hii. Hatuelewi hili suala limefikia wapi? Hatuelewi mwendelezo wa suala hili ukoje kwa sababu wananchi wanataka kukopa, lakini mpaka leo hii wakienda kwenye Halmashauri zetu…

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mchangiaji anayechangia kwamba suala la asilimia 10 kukwama limewadumbukiza wanawake na vijana kwenye mikopo ya riba kubwa ambayo ni Kausha Damu. Wanawake na vijana wengi wamefilisiwa badala ya kuwainua, wameenda kuanguka. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shamsia, endelea na mchango wako.

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninaipokea taarifa hii tena kwa mikono miwili. Ni kweli kwamba wananchi wetu wamekuwa na sitofahamu kuhusiana na mikopo hii ya asilimia 10. Kwa hiyo, tunataka kujua taratibu hizi za kutoa mikopo kwa ajili ya wananchi wetu wa asilimia kumi imefikia wapi? Mikopo hiyo itakapokuwa tayari isiangalie vyama. Kuna ubaguzi ambao unaendelea ndani ya mikopo hii, toeni mikopo kwa wananchi wote. Serikali hii, Rais na Mawaziri wote ni wa wananchi wote, kwa hiyo, msiangalie itikadi ya vyama katika kutoa mikopo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumza hayo, nakushukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)