Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya mchana huu kuweza kutoa mchango wangu katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu juu ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2023/2024 na Mwelekeo wake wa Mwaka 2024/2025 katika Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa afya njema, amani tuliyonayo katika nchi yetu. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kwa kutupa Rais wetu mahiri kabisa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anayesimamia Ilani ya CCM kwa weledi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitazungumzia mambo mawili tu. Kati ya yote aliyozungumza Mheshimiwa Waziri Mkuu, niseme naunga mkono hoja yake, lakini nataka tu ufafanuzi na labda niseme nataka utekelezaji katika maeneo mawili. Maeneo hayo ni eneo la mifugo na eneo la pili ni la nishati safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi nimekuwa nasimama hapa Bungeni kwa kipindi chote nilichokuwepo nikizungumzia mifugo. Niseme kwamba wafugaji wapo wa aina mbili; wale wanaofuga kwa kuswaga ng’ombe na wale wanaofuga kwenye zero grazing. Wafugaji wote hao wanatamani kuchangia pato la Taifa, nami mwenyewe natamani kuona kwamba mifugo inachangia pato la Taifa katika mapana yake kama ilivyo kwa kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo na mifugo ni mapacha, haviwezi kutenganishwa. Ukiwa na mifugo mizuri itakupa mbolea, kilimo kitaboreka. Ukiwa na kilimo kizuri, pia mifugo itapata malisho na wananchi wote watakula na kuwa na Taifa lenye wananchi wenye afya nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukizungumzia hapa mifugo, wanasema mifugo na uvuvi, tumeona kasi katika eneo la uvuvi ni kubwa sana na mpaka sasa hivi ikielezewa kama ingekuwa ni kupima kwenye mizani, tunaona kwamba kwenye uvuvi kumeenda kasi na kunazalisha zaidi ya mifugo. Tatizo liko wapi? Tumeona katika ripoti ya Waziri Mkuu ametueleza kwamba kwa kipindi chote cha mwaka mmoja imenenepeshwa mifugo 2,176, hao ndiyo ng’ombe walionenepeshwa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina watu milioni 62, Tanzania ni kubwa, na Tanzania ina tija iwapo kila mmoja atawezeshwa katika hali nzuri ya mifugo. Sasa najiuliza tatizo liko wapi?

MBUNGE FULANI: Kweli.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, mifugo haijapewa uzito. Ukiwa na mifugo mizuri, siyo siri, utapata ngozi nzuri, utapata samadi ya kutosha, utapata maziwa kwa afya ya watoto na watu wazima, na pia utapata nyama ambayo itauzwa ndani na nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali hii makini na sikivu ni kutoa nafasi na uwezo kwa wananchi wengi kufuga wakiwemo wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro. Siyo rahisi kuizungumzia Tanzania nzima kwa mapana yake, ila nina hakika kila mfugaji angependa kuchangia katika pato la Taifa, lakini wale wa Kilimanjaro wako wanaongoja kuboreshewa mitamba mizuri ili wafuge, wapate mazao niliyoyataja awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, endapo mifugo hii ambayo inanenepeshwa, ingenenepeshwa kwa ushindani kihalmashauri. Halmashauri zetu ziko 184, ukigawa kwa hii mifugo, tuseme kila halmashauri imenenepesha ng’ombe 10 tu kwa mwaka mzima, sasa hiyo ni nini? Yaani hainiingii akilini kabisa kwamba tumefanya kadri tunavyoweza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara ya Mifugo na Uvuvi iweze kupanua uwezo wake wa kuelimisha wananchi katika kunenepesha hiyo mifugo na pia katika kuzalisha maziwa kwa wingi zaidi ili Sekta ya Mifugo iweze kuchangia pato la Taifa kwa ukubwa wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vijana wanaomaliza shule wanakuwa idle, wapo tu. Wao wanaona kasi ya Mheshimiwa Rais; barabara zinajengwa, hospitali zinajengwa, miundombinu ya maji iko vizuri, miradi ya kimkakati inaenda vizuri, na hiyo wanakwambia imeshafanyika, imeenda hiyo. Nami nakubaliana nao. Hata katika management, Maslow alisema, “once a need is satisfied, is no longer motivation.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kwenye another need, ndiyo maana kila mwaka tutakaa hapa tunazungumzia ubora na uendelevu wa bajeti yetu na hakuna siku ambayo tutakaa tuishiwe namna ya kuishawishi Serikali ifanye zaidi na zaidi. Naungana na wote wanaompongeza Mheshimiwa Rais, lakini namwomba atupie jicho pia kwa wale ambao wamekaa katika majimbo yao, au kwa wananchi wetu wanaosubiri wawezeshwe ili waende na hiyo kasi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo nimesema kuna vijana ambao ni wahitimu, kuna wanawake ambao wana afya zao nzuri sana, pia kuna ambao walikuwa wanafanya kazi na sasa ni wastaafu, wana chochote walicholipwa, lakini hawawezi kwenda na kasi kwa sababu wanangoja Serikali nayo iwawezeshe kiasi fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena lile ombi na nitalirudia mpaka nimalize Bunge hili la Serikali kutupa mitamba ambayo inastahili kufugwa katika nchi hii. Wazee wetu walianza, Kenya, Uganda na Tanzania. Uganda ina mitamba mizuri sana na inauza maziwa mpaka Tanzania. Kenya ina mitamba mizuri sana na inauza maziwa mpaka Tanzania. Sisi hatuuzi popote zaidi ya hapa hapa. Tuna nini? Tatizo liko wapi? Naiomba Serikali iangalie jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake wa Kilimanjaro wako tayari kufuga, wako tayari kunenepesha, lakini pia kama nilivyosema awali, tunaomba tuweke ushindani katika halmashauri ili kila mmoja aweze kuifaidi cake ya Taifa aliyoichangia. Tusije kunyang’anyana hapa tu, tunamkemea Waziri wa Fedha ambaye pia hatuchangii sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nataka nitoe shukrani za dhati sana kwa Mheshimiwa Rais kwa hii ajenda ya kuboresha nishati safi na salama kwa sababu wanawake wengi waliugua vifua kwa kukoka moto na sasa tunakwenda kujikomboa. Naomba tuendelee kuongea na wadau, naye mwenyewe aendelee kutusemea zaidi anakojua.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshukuru sana mdau mmojawapo anayeitwa Oryx. Imeweza kugawa mitungi mingi na kuweza kufikia eneo kubwa wakiwepo viongozi wa dini, wananchi walio kwenye wilaya au kata ambazo ziko pembezoni na sasa kila mtu anapika chai ambayo hainuki moshi. Tunaomba Oryx isiishie hapo, bado Tanzania inataka kuona kwamba nishati safi na salama ndiyo agenda ya Tanzania. Tunataka kunywa chai inayonukia mdalasini au karafuu na siyo chai inayonukia moshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Wizara ya nishati, pamoja na nishati bora zilizoboreshwa za aina zote ukiwemo umeme, majiko sanifu na mengineyo mengi, zile gesi za kilo sita ziendelee kugawiwa kila kukicha ili watu waweze kuona manufaa yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaomba elimu. Siko tayari kusikia kwamba nyumba imelipuka na gesi ya Oryx, hapana. Waitwe kwenye mikutano waje wasikilize, wafundishwe namna ya kutumia gesi, wafundishwe namna ya kujikinga na gesi ikilipuka na kadhalika. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, itakapokuja semina ya Oryx, wote mhudhurie. Nitaileta ili mweze kupata mafunzo na pia mweze kujua namna ya kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, jambo lile ambalo lilikuwa limeombwa siku nyingi la kuunganisha ile mifuko yote ili sasa iende kule kwenye Wizara mojawapo iweze kuwafikia vijana, lifanyike katika speed ya juu zaidi. Nasema hivyo kwa sababu gani? Siyo rahisi sana vijana kuandika barua kule waliko wakaifikia mifuko hiyo. Kwa hiyo, naunga mkono lile tamko la awali kwamba tuiunganishe mifuko hiyo, iongezewe fedha hata kama na halmashauri au na bajeti ili vijana wengi zaidi wafaidike kuliko ilivyo sasa, kwamba unaanza kupiga simu unaulizwa, unapiga kama nani? Napiga kama mwakilishi. Hapana, kijana mwenyewe alete barua, kijana mwenyewe alete kitambulisho cha NIDA. Mlolongo, red tape hizo na bureaucracy zimekuwa ndefu sana. Sasa vijana wamekaa mitaani wanakata tamaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba jambo moja, kuna maeneo ambayo wamekuwa wengi lakini eneo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Raymond. Ni kengele ya pili.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)