Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Kwanza naomba nimpongeze yeye mwenyewe kwa jinsi ambavyo aliweza kuwasilisha vizuri. Pia niwapongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Naibu Mawaziri kwa jinsi wanavyoendelea kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoendelea kuifanya katika majimbo yetu ambapo kwa kweli ni tofauti na ilivyokuwa miradi mingi sana ya maendeleo kama vile maji, afya na elimu. Kwa kweli tunaendelea kuona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye eneo la umeme wa REA. Umeme wa REA ulikuja kwa lengo moja la kuwasaidia kule vijijini, kuhakikisha kwamba wanajikwamua na maendeleo. Pamoja na kuutumia kuwasha kwenye nyumba zao, lakini utafanya kazi kuwawezesha vijana kujikimu katika kuhakikisha wanatumia ule umeme uwasaidie kupata kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba Serikali inaendelea kupeleka umeme kwenye vijiji vyetu na baadhi ya vitongoji, lakini bado katika vijiji vyenyewe kuna maeneo hayajapelekewa umeme. Mbaya zaidi ni kwenye baadhi ya vijiji ambavyo Serikali ilivitambua kama ni miji ambayo nayo haijawa miji, bado ni mamlaka ya vijiji. Kwa mfano, Nguruka na pia pale Kijiji cha Uvinza, hivi ni vijiji kama vijiji vingine. Ni Mamlaka za Vijiji kama vijiji vingine, lakini vijiji hivi viliamriwa kutoa shilingi 320,000 kama mijini. Sasa ni kitu ambacho kiliwanyong’onyeza sana na mpaka sasa hakuna mtu ambaye ameshalipia hiyo shilingi 320,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimelalamika sana hapa Bungeni kwenye Wizara ya Nishati ili waweze kuondolewa kwenye eneo hilo la shilingi 320,000 ambayo ni rate ya mji, wakati wao sio mji. Maana yake inapingana na ile ya kuhakikisha kwamba vijiji vyote vinapelekewa umeme na wananchi wanaweka umeme ili waweze kuutumia kwa maendeleo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kwenye eneo hilo la Nguruka pamoja na Uvinza, kwa kweli nina imani na vijiji vingine katika nchi hii viko ambavyo vilipelekwa kwenye tariff hiyo ya mjini, waweze kuviondoa huko ili wananchi waweze kuanza kulipa shilingi 27,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza Serikali, pale tuliposhuhudia utiaji wa saini katika mradi wa umeme wa maji Igamba Falls kwenye Jimbo langu Uvinza kwa lengo la kupata Megawatts 49.5. Mradi ule ni wa miaka mingi sana na ulizungumziwa sana hapa Bungeni kabla sijawa Mbunge. Nampongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kurudisha mradi huu na umeweza kusainiwa, na mkandarasi sasa anatarajiwa kwenda kuanza kazi. Kwa sasa hivi, mkandarasi ambaye anajenga njia ya kusafirisha umeme kutoka hapo Igamba Falls kwenda Kidawe, alishaanza kujenga njia ya kusafirisha umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili naomba niwahakikishie kwamba, inaanza kuwaonesha wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwamba sasa mkoa unafunguka kwenye eneo hilo la nishati ya umeme. Naomba wakati mkandarasi anaendelea kujenga hiyo njia ya umeme, mweze kuhakikisha kwamba wananchi ambao watapitiwa na njia hiyo ya umeme wanalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nizungumzie kwenye eneo la barabara ya Simbo - Kalya. Barabara hii ina urefu wa kilometa 235, ni barabara ndefu sana. Ni barabara ambayo inahusu kata nane za Jimbo la Kigoma Kusini za Wilaya ya Uvinza ambao ni ukanda wa maji. Wananchi hawa kabla barabara hii haijafunguliwa walikuwa wakisafiri na maboti na wengi walikufa sana majini na wengi walipoteza mizigo yao mingi. Sasa baada ya barabara hii kufunguliwa, kwa kweli naomba niipongeze TANROADS, wanaendelea kuifanyia kazi vizuri sana barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya barabara hii kufunguliwa, wananchi wa hizo kata nane walipata ukombozi. Kwenye barabara hiyo nakumbuka Mheshimiwa Naibu Waziri, Engineer Kasekenya aliwahi kupita mara mbili. Naomba nichukue nafasi hii nimshukuru, anapenda sana kuwa anapita kwenye hiyo barabara, anaijua, alitoa maelekezo ya barabara hiyo iweze kuwekewa zege katika maeneo korofi na kwa kweli Mheshimiwa Naibu Waziri, hili jambo likifanyika litaweza kusaidia kabla barabara hii haijawekewa lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwenye eneo la Kivuko pale Ilagara. Daraja hili liko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na tayari Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Taarifa nilizonazo ni kwamba, huyu mkandarasi wa upembuzi yakinifu alishamaliza kazi, lakini bado kuna fedha kidogo anaidai Serikali ili aweze kuikabidhi hiyo document.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iweze kumlipa fedha zake ili aweze kuikabidhi document hiyo ili hilo daraja lianze kujengwa. Wananchi wa kata nane wanahitaji daraja. Juzi kivuko kilisombwa na maji kwa sababu maji ya Mto Malagarasi ni mengi na yanatembea kwa kasi sana. Pia pale ndiyo mwishoni na mto ule ni mrefu sana, unaanzia huko Kibondo, lakini unapofika pale ni mpana na maji ni mengi, yalisomba kivuko kile na watu wakiwemo ndani pamoja na magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitsha zaidi, kwa sababu barabara ile ndiyo inakwenda kule kwenye eneo la Buhigu ambako kuna TANAPA, kuna watalii walikuwemo kwenye ile gari na magari yao ambayo yalikuwa yanapelekwa kule, bahati mbaya sana kwa kweli walisombwa kupelekwa kwenye maji mengi (ziwani) na wamekaa kule mpaka jioni. Hata hivyo, naishukuru Serikali ya Mkoa pamoja na Wilaya walikwenda kuona namna ya kuweza kuwaokoa hao wananchi na waliweza kuwatoa na baadaye kivuko kile kurudishwa kwenye eneo lake na sasa hivi kinafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wananchi hawana imani na kile Kivuko. Kwa hiyo, naomba kwenye lile daraja upembuzi yakinifu ukamilike, na Serikali ianze kuona namna ya kujenga hilo daraja.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Nashon.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, basi, baada ya kusema hayo, nakushukuru. Naunga mkono hoja.