Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa wasaa huu, lakini nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye Wizara nyeti inayohusika na watumishi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amedhihirisha yeye ni mwajiri namba moja kwa alivyoshughulika na masuala ya watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote wao ndiyo wanatekeleza maono ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye nukuu aliyosema Mheshimiwa Waziri ya Mheshimiwa Rais akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili, 2021 katika Bunge la Kumi na Mbili aliposema, nanukuu; “Tutawapima viongozi na watumishi wa umma kwa namna wanavyotimia majukumu yao, hatutawaonea aibu viongozi na watumishi wazembe, wezi na wabadhirifu wa mali za umma. Tutaendeleza pia juhudi za kupambana na rushwa kwenye utumishi wa umma. Wajibu wa watumishi wa umma ni lazima uendane na haki zao.”

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nataka niongelee haki ya mtumishi wa umma katika mafunzo, maana mafunzo ndio kila kitu, mafunzo ndio msingi, mafunzo ndiyo yatawafanya watumishi wetu watumike sawasawa ipasavyo. Kwa utumishi wetu wa umma kuna itifaki ya mafunzo ya hatua sita, mafunzo ya kwanza mtumishi huyapata anapoingia kazini inaitwa induction entry course. Mtumishi hapa atafundishwa nini maana ya Serikali, anaenda kufanya nini ndani ya Serikali, aitumikieje Serikali, atofautisheje na familia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mafunzo sasa hivi hayaendi ipasavyo, tukiajiri watumishi tunawakusanya wiki moja tunasema tumewapa induction course, hiyo haitoshi na ndiyo maana huu mwanya unafanya watumishi wa umma anaweza akashindwa kutofautisha ni mambo gani ya Kiserikali hayatakiwi kusemwa hadharani na ni mambo gani ya Kiserikali ambayo familia yake haitakiwi kuyajua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mafunzo namba mbili, haya huwa ni mafunzo ya awali, mafunzo elekezi ya msasa orientation training, hii nayo tumelegea. Orientation training ilikuwa mtumishi akiajiriwa hata kama zipo idara sita ndani ya taasisi atazungushwa kwenye zile idara ili azijue na lengo lake na yeye awe mmiliki sawasawa na kujua kila kitu kinachoendana na taasisi yake. Leo hii mtumishi anaweza akaajiriwa, akawekwa idara moja mpaka anastaafu, kwa hiyo huyu hawezi kujua taarifa zingine zinazoendelea ndani ya taasisi. Ukimuuliza habari za idara nyingine anaweza akashindwa kusimama na kuielezea taasisi yake ikoje, inafanya nini na kwa wakati gani. Niwaombe hilo twende tuliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na mafunzo namba tatu, mitihani ya umahiri na hii mitihani ya umahiri sana waliobaki wanaendana nayo ni Wizara ya Ulinzi. Sisi kwetu huku aidha ni bajeti au ni kitu gani hii mitihani ya umahiri haipo. Ili mtu aende kwenye na nafasi nyingine lazima afanye mitihani ya umahiri, lazima ajue nikienda kwenye position hii nyingine natakiwa nifanye nini. Hii imebaki kwa maafisa utumishi ndiyo naona wanafanya mitihani ya umahiri, lakini huku kwenye kada zingine mitihani ya umahiri kama imesahaulika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mafunzo namba nne, haya yalikuwa yanahusu misingi ya utumishi wa umma, hapa mtumishi ndiyo unafundishwa misingi ya utumishi wa umma, unatakiwa ufanye nini ndani ya utumishi wa umma. Hapa unafundishwa hata kutoa rushwa na kupokea ni dhambi, hata unafundishwa kutoa siri za Serikali ni dhambi, lakini nani leo hii anayefundishwa hayo mafunzo ya misingi ya utumishi wa umma? Ndiyo maana si ajabu watu hamjamaliza kikao taarifa zote zipo nje kwa sababu misingi ile tumeisahau, msingi ya utumishi wa umma tumeisahau.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba tano, ilikuwa ni mafunzo ya viongozi wanaochipukia, watumishi wetu wakiwa ni Maafisa Wakuu wanaanza kupelekwa chuoni, mwanzoni ilikuwa ni IDM Mzumbe, lakini baadaye majukumu haya yakakabidhiwa Chuo cha Utumishi wa Umma, tusibaki kwenye kwamba viongozi wanazaliwa bali viongozi wanajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ndiyo Maafisa Wakuu walikuwa wanafundishwa namna ya kuwa kiongozi, namna ya kuwa mwadilifu, namna ya kuwa mvumilivu, namna ya kuwa msikivu na namna ya utendaji kazi. Tuna mifano, leo hii tunaona Mheshimiwa Rais wetu anabagazwa, anasemwa, anavumilia kwa sababu amepita IDM Mzumbe amefundishwa uvumilivu na ustahimilivu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna Katibu Mkuu wetu wa Chama Cha Mapinduzi amepita IDM Mzumbe, aangalie style yake ya kusema hata kuikosoa Serikali, hata kuwaambia nyie Waheshimiwa Mawaziri anasema kwa staha kwa sababu amefundishwa kuwavumilia wenzake. Hiyo ndiyo ilikuwa kazi ya IDM Mzumbe, ndiyo ilikuwa kazi ya kufundisha viongozi wanaochipukia. Sasa wakishafundishwa hivyo ndiyo mle wanatolewa wateule, ndiyo anateuliwa mtu, anaenda akiwa ameshajengwa kwamba anaenda kufanya nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunaona watu wanateuliwa Wakurugenzi wetu, saa zingine wanakosea ni kwamba hawakupewa haya mafunzo, saa zingine wanakosea ni kwamba hawakutolewa kwenye kundi hili la maafisa wakuu, turudi nyuma, ya kale ni dhahabu, tukayafanyie kazi yatatusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo namba sita ilikuwa hapa mstaafu anaandaliwa kustaafu, anafundishwa mafunzo ya kustaafu na alikuwa anafundishwa miaka mitano kabla ya kustaafu. Kulikuwa na Chuo kinaitwa NIP- National Institute of Productivity, ndiyo ilikuwa kazi yake kufundisha wanaotaka kustaafu, wanamfundisha anaweza kufanya nini baada ya kustaafu na kama wewe utawaambia, nikistaafu nataka nifuge kuku, nifuge ng’ombe, niwe na biashara ya usafirishaji, wanakufundisha, wanakuandikia andiko, wao wenyewe unakopa sasa kwenye pension. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakopa collateral yako ni mshahara. Mpaka unamaliza miaka mitano umeshamaliza ule mkopo lakini wanaendelea kuangalia ule mradi wako ambao unaufanya. Leo hii ikifika miezi sita wamempa mtumishi barua ya miezi sita kwamba sasa jiandae utastaafu, ndiyo wananipeleka course. Sasa nikimaliza hapo wakinipa pension naenda kununua daladala linapinduka Mbezi, tayari nimekwisha, halafu tunasema maisha ya wastaafu yanakuwa magumu. Tunayafanya kuwa magumu sisi Serikali, tumesahau kuwaandaa hawa watu, hebu turudi tukaandae hawa watumishi wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anapohitimisha nitaomba anielezee hii hati iliyoanzisha Chuo cha Utumishi wa Umma kikaitwa Public Service College, mambo haya bado yapo, bado yanaendelea kufanyika kama hayapo kuna haja ya kuendelea kukiita Chuo cha Watumishi wa Umma? Leo hii ukienda pale unakuta imejaa secretarial na record management, ndiyo yalikuwa malengo, record management si ilikuwa Uhazili Tabora? Hiki chuo kilianzishwa kujenga watumishi, kuwajengea uwezo ambao wameshaajiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba wakati Waziri anahitimisha aniambie kama bado hiki chuo kinafanya kazi zake ipasavyo. Tunaweza tukawa tunalalamikia watumishi uadilifu umeshuka, wizi umekuwa mkubwa, amejengwa huyu mtu? Hebu turudi tukawajenge watumishi. Mheshimiwa Simbachawene amejengwa na ndiyo maana anaweza akapigwa mawe, ndiyo maana anaweza akasemwa, akavumilia kwa sababu amepita kwenye chuo amejengwa, Mheshimiwa Spika kajengwa, walikuwa wakifika mahali wanajengewa uwezo. Leo hii mtumishi gani anajengewa uwezo halafu tunawalaumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukawa tunavunja sisi wenyewe kwa mikono yetu wenyewe tunawavunja hawa watumishi halafu tunasema watumishi hawa hawafai, kizazi hiki kibovu, siyo kibovu hakikujengewa uwezo. Turudi kwenye yale ya zamani tukayaangalie, tumepotea wapi na tulipopotea ni kila chuo kuacha malengo yake yaliyokianzisha tukaanza biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukienda IDM Mzumbe siyo IDM Mzumbe ile ambayo Afisa Mkuu alikuwa akitoka IDM Mzumbe mnasema kweli huyu katoka IDM Mzumbe. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwishwa kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kengele ya pili hiyo.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee dakika moja nimalizie nakuomba na hili ndiyo jimbo langu.

NAIBU SPIKA: Sasa utakuwa unachukua Mheshimiwa...

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba waende wakayafanye hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia Mheshimiwa Waziri leo ametambulisha viongozi wake pale, ina maana siku hizi hakuna wanawake wenye uwezo, nimeshangaa na nimeandika ki-memo lakini hakikufika kwake kwa sababu alishakuwa pale na kwa Mheshimiwa Ridhiwani hakikufika, aende nalo wakalifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, naunga mkono hoja. (Makofi)