Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi, nianze alipoishia Mheshimiwa Janejelly kwamba wanawake wanaweza na wapewe nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Rais ambaye ndiye Waziri kwenye Ofisi hii ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kipekee Waziri wa Nchi, Ofisi hii Mheshimiwa George Boniface Simbachawene pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete pamoja na Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara zote zinazounda Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri, kwa bahati mbaya hii ni Wizara ambayo mambo yake hayaonekani sana hadharani. Lakini itoshe tu kusema kila jema tunaloliona katika nchi hii linafanyika basi linatoka katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeanza mchango wangu katika Fungu 32 - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora. Mwaka 2014 wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete zilitangazwa ajira takribani 29,000 za walimu, lakini walimu wale wamekumbana na changamoto ya kutopanda madaraja kwa mtiririko vile ambavyo inapaswa kuwa. Kwa mfano mwaka 2014 wakati wanaajiriwa waliingia kama walimu wa daraja la 3A walipaswa kuthibitishwa mwaka 2015 na mwaka 2018 ilipaswa waanze kupanda daraja la kwanza ili waende daraja la 2A ambayo pia hata mshahara ungeongezeka lakini hilo halikufanyika. Baadaye wakapandishwa mwaka 2021, maana yake hapa kuna miaka miwili wamekopesha nguvu bure Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa mtiririko huo ilipofika mwaka 2022 walipaswa kupanda daraja kutoka daraja la 2A na kwenda daraja la 1A, lakini ukiona hapo ni takribani miaka 10 wamepanda ngazi moja moja. Kwa hiyo, tunadhani kwamba ni vizuri hili likatazamwa na tukaweza kuwasaidia kwa sababu kimsingi walipaswa kuwa wamepanda aidha mara mbili au mara tatu. Kwa hiyo, wanaona hiyo ni dhuluma kwamba Serikali yao inawadhulumu, lakini tunaamini Serikali hii siyo ya dhuluma bali inawezekana kuna jambo halikuangaliwa vizuri. Naomba litazamwe vizuri, waweze kurekebishiwa hizo taratibu zao ili waweze kupata stahiki kwa mujibu wa utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapongeza pia kazi nzuri ya upandishaji wa madaraja ambayo inaendelea. Sasa hivi tunashukuru kwamba, angalau malalamiko yamepungua sana, lakini tunaomba Maafisa Utumishi chini ya Wizara hii ambayo ndio inawasimamia, hilo zoezi lifanyike kwa haki kwa sababu, bado kuna ambao wana zile kasumba za kibinadamu za kuendelea kushikilia ma-file ambapo hata hapastahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana eneo hili liweze kufanyiwa kazi maana lisipofanyiwa kazi, hili ndilo linaloenda kuathiri hata ile hatua ya mwisho ya mafao, kwa sababu, unakuta kuna mtumishi mwingine anapokwenda kuanza kudai mafao yake anagundua kwamba, kwa kucheleweshwa kupandishwa madaraja hata viwango vya mafao vilivyowekwa havilingani na hali ile ambayo anaikuta wakati wa kustaafu. Kwa hiyo, hili ni muhimu sana na lenyewe lifanyiwe kazi kwa wakati ili lisiathiri ile hatua ya mwisho ya kwenda kupata mafao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kulipa malimbikizo. Serikali inajitahidi sana katika eneo hili, lakini ni ukweli usiofichika kwamba, bado yako maeneo kuna malimbikizo ambayo hawajalipa. Tunaomba sana tuongeze kasi ya ulipaji wa malimbikizo ili tuwaongezee ari ya kufanya kazi. Miongoni mwa motivation katika utumishi wa umma ni pamoja na kulipa haya malimbikizo. Tunaamini hilo likifanyika litatusaidia sana kuongeza ufanisi wa watumishi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala zima la masuala ya nidhamu, hapa nazungumzia Tume ya Utumishi wa Umma. Tunafarijika kuona kwamba hata pesa tumeongeza na sisi pia, kama Kamati, juzi kuna mafungu tumeyaongeza hapa. Tunataka kesi zote ambazo zinasimamia malalamiko katika utumishi wa umma zifanyike kwa wakati. Haki yoyote ambayo inacheleweshwa ni haki ambayo inanyimwa. Kwa hiyo, tunaona kwamba, wako watumishi wanaanza kupata viharusi na wengine wanapata madhara mbalimbali ya afya ya akili kwa sababu, mashauri yao mbalimbali yaliyoko katika ngazi hii ya utumishi hayakufanyiwa kazi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haipendezi sana kuona kwamba, kesi ya mtumishi inakaa zaidi ya miaka mitatu haijatafutiwa ufumbuzi. Kwa hiyo, tunaomba sana tuongeze kasi katika Tume hii ya Utumishi wa Umma na pia, tuongeze kasi katika kusikiliza mashauri na migogoro yote ya utumishi ili haki iweze kupatikana kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kwa wale ambao wanakaimu. Bado tunaona kwamba, kuna ukiritimba mkubwa katika kutoa vibali kwa watu ambao wanakaimu ama kuwapandisha ama kuwathibitisha kwenye kazi. Kwa mujibu wa sheria mtu anatakiwa akaimu kwa muda usiozidi miezi sita, lakini bado tunaona kwamba, kuna maeneo ambayo watu wanakaimu kwa muda mrefu sana. Hapa nitatoa mfano na inabidi nimtaje tu huyo mtumishi kwa sababu, kinachofanyika siyo haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtumishi anakaimu ukurugenzi katika Ofisi ya TACAIDS kwa muda wa miaka saba na ni mwanamke huyu, anaitwa Adrieli Njelekela, miaka saba anakaimu ukurugenzi. Sasa hapa kama hana uwezo anawezaje kukaimu kwa miaka saba? Maana yake ni kuna tatizo. Kama ni vetting miaka saba tunasubiri vetting, hiyo vetting ni ya kutoka mbinguni au ni hapa hapa duniani? Ndio maana wakati mwingine tunaonekana kwamba, labda nchi hii bado kuna mfumo dume ambao unawafanya wanawake wasiwe katika nafasi ambazo wanastahili kuwa nazo, kwa hiyo, naomba hili litazamwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu Watumishi Housing.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hoja ya kukaimu, mzungumzaji ameisema vizuri sana. Nataka nimpe tu Taarifa kwamba, niliwahi kutoa Taarifa ndani ya Bunge hili kwamba, yupo mtumishi aliyekaimu zaidi ya miaka kumi ndani ya Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, lakini baada ya miezi miwili wakamwondoa na kumshusha kabisa wakampeleka Mkoa mwingine. Kwa hiyo, ni Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shangazi.

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa hiyo naipokea, lakini huyu tutamwangalia kwamba, watampeleka wapi na tutaendelea kumfuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni Watumishi Housing. Tumeboresha bajeti yao vizuri, wakatujengee nyumba za watumishi. Kipekee Mheshimiwa Waziri naomba sana, mimi natoka Wilaya ya Lushoto ambayo sehemu kubwa ni milima, imetawanyika mno na ndio maana sisi shida yetu kubwa kwenye eneo la utumishi ni watumishi kuendelea kuhama kutoka Halmashauri ya Lushoto kwa visingizio mbalimbali vikiwemo umbali, milima na kadhalika. Kwa hiyo, tunaomba, tunazo shule ambazo ziko pembezoni mno, kuna Shule ya Mhindulo ambayo iko kule Mbaramo na Shule inaitwa Nkombo iko huko Kata ya Mbaramo ni mbali sana zaidi ya kilometa 127 mpaka kufika makao makuu ya halmashauri. Kwa hiyo, tunaomba haya maeneo yote ya pembezoni hizi nyumba za watumishi na sisi ziweze kutufikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Wakala wa Serikali Mtandao. Tunaomba na wenyewe waboreshe, bado kuna maeneo mengi mtandao haujakaa sawa, hata ndani ya Serikali bado kuna taasisi nyingi hazizungumzi. Kwa hiyo, tunaamini kwamba, kwa zama hii ya teknolojia ambayo tunayo ni vizuri Wakala wa Serikali Mtandao nao ukaimarishwa ili mifumo mbalimbali ndani ya Serikali ikiwemo hii ya utumishi iweze kuonana na kusomana kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)