Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ili nichangie katika Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora. Napongeza utendaji wa Serikali, kwa kiasi kikubwa umekuwa unaonesha kujali watumishi kwa kuwapandisha vyeo wale ambao walisimama kwa muda mrefu na kulipa malimbikizo ya watumishi wengi ambao walikuwa na madai, sasa kiasi fulani yamerekebishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali, nampongeza Mheshimiwa Rais na timu yake kwa kuona kwamba, uhitaji wa watumishi, hasa walimu, bado ni mkubwa sana. Hapa katikati Serikali imekuwa ikileta pesa nyingi katika halmashauri zetu na tumejenga mindombinu mbalimbali ya elimu na afya, changamoto iliyobaki ni watumishi hasa wa kada hii ya elimu. Kwa bahati nzuri Serikali imesikia kilio chetu sisi watumishi wa wananchi na sasa imetangaza ajira karibu 46,000. Naamini zitafika katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, majimbo yetu ya vijijini yana uhitaji mkubwa sana na hata walimu wanaohama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine hawaombi kwenda vijijini, wanaomba kwenda mijini kuungana na familia zao maana familia nyingi ziko mijini. Huku vijijini sijui hakuna watu, lakini naomba hata uhamisho basi uzingatiwe, watu wanapopangiwa katika vijiji waweze kufanya kazi kwa muda wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya kazi kubwa sana hasa katika Jimbo langu. Kuna maeneo kijiji kimoja kina shule nane, kutoka shule mbili sasa zipo nane, kwingine saba. Sasa walimu wanahitajika sana na kwa kweli katika jambo la kuzingatiwa ambalo tunaona kuwa ni changamoto sana, ni walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu hii Serikali mtandao. Serikali Mtandao kazi yao ni nzuri sana, lakini kuna changamoto kadhaa. Pamoja na kujenga mifumo mingi ambayo inafanya kazi bora bado ziko changamoto ambazo zinatakiwa zifanyiwe kazi. Mifumo hii haisomani kwa asilimia kubwa na changamoto hii inasababisha baadhi ya vitu kukwama, tunarudi katika manual ya ma-file wakati tulikuwa tumeshatoka. Mifumo hii ikisomana ni rahisi hata kwa Serikali yenyewe, Wizara na Wizara zikazungumza katika jambo mahususi ambalo linahusiana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wataalamu wa mifumo hii wanaohudumu ni wachache sana. Tunaiomba Serikali iongeze kuwasomesha vijana wetu ili waweze kumudu na hata inapotokea changamoto ya wengine kutoka kwa namna yoyote, basi mwingine aweze kuchukua nafasi hiyo. Jambo hili bado lina ugumu, watumishi wenye taaluma ambao wanasimamia mifumo hii ni wachache sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado siri zinavuja, siri za Serikali unazikuta mtaani mtu anazo. Kwa kweli, jambo hili linatakiwa liangaliwe kwa umakini sana. Zamani jambo la Serikali lilikuwa linabaki Serikalini, lakini sasa jambo la Serikali unakuta mtu wa mtaani kabisa analo, hata unashangaa siri hii imetokaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kidogo nizungumzie TASAF. TASAF wamefanya kazi nzuri kweli kweli, lakini bado zipo changamoto ambazo nadhani zikifanyiwa kazi zitafanya mradi huu wa TASAF ambao dhamira yake ni kuondoa umaskini uondoe umaskini kweli kweli. Unapowapa watu pesa ndogo sana, matokeo yake anakula halafu zinakwisha. Nashauri kutafuta miradi katika halmashauri ambayo itakuwa ni miradi endelevu, mfano miradi ya masoko, ili watu ambao wana uhitaji wapewe meza sokoni, watazungusha gurudumu na maisha yataenda. Tumeona baadhi ya maeneo yamejengwa masoko, natamani kuona hata kwenye halmashauri yangu ya Itigi waje wajenge kitu kimojawapo ambacho na sisi tutajivunia kutoka katika mradi huu wa kuondoa umaskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakala wa Ndege za Serikali na ATCL. Hapa kuna vitu vinaleta mtafaruku kidogo, Wakala wa Ndege za Serikali ndiye mmiliki wa zile ndege, anapomkodisha ATCL, ATCL anailipa Serikali. Mmiliki wa ATCL kwa 100% ni Serikali, sasa hii ikoje? Natamani kuona hapa kuwe na mfumo ambao utaifanya ATCL imiliki hizi ndege na Wakala wa Ndege za Serikali amiliki zile ndege za viongozi tu. Sasa unapokodisha, ndege imenunuliwa na Serikali, Shirika ni la Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie jambo moja, ndege ya Serikali inapokuwa kwa Wakala wa Serikali, deni la Serikali linafanya zile ndege zikamatwe. Hapa majuzi tumekamatiwa ndege na ninyi ni mashahidi kwa sababu, ndege zinasoma ni mali ya Serikali, lakini zingekuwa za ATCL isingekuwa rahisi kuzikamata kwa sababu, ni mali ya shirika japo mwenye lile shirika ni Serikali. Kwa hiyo, hili jambo tunatakiwa tulione ili tuepuke makandokando haya ambayo yanatukuta kama nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka pia nizungumze jambo kidogo kuhusu Watumishi Housing. Shirika hili limefanya kazi nzuri, lakini liko mijini. Halmashauri zetu za vijijini hatujaona effort, nataka niwaone katika Halmashauri ya Itigi. Tutawapa viwanja bure wajenge nyumba za watumishi wetu ili waweze kukopa na tusaidie dhamira halisi ya shirika hili ambalo linafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina maneno mengi sana kwa sababu, bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri ni nzuri sana. Naunga mkono hoja ili wapewe hizi pesa wakafanye kazi. Ahsante sana. (Makofi)