Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii inayoshughulikia watumishi ambao ni engine ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Kaka yangu Simbachawene, kwa kazi nzuri anayoitendea Wizara hii. Vilevile, nampongeza Naibu Waziri ambaye ni Mjumbe wangu wa Kamati ya Utekelezaji ya Vijana mimi nikiwa Katibu Mkuu wa Vijana kwa jinsi ambavyo anatenda haki katika kumsaidia Waziri na kuisaidia Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nampongeza Rais wetu wa nchi hii. Rais huyu katika kila idara ya nchi hii amefanya mambo makubwa kwa muda mfupi sana na naomba Watanzania watuelewe tunapompongeza Mheshimiwa Rais. Katika kipindi cha miaka mitatu tu ya Mheshimiwa Rais, ameongeza ajira, jambo ambalo lilisimama kwa muda mrefu. Mwaka 2021 aliajiri watu 80,000, mwaka 2022 watu 32,000, mwaka 2023 watu 45,000 na baadaye watu 47,000 na hivi tunavyoongea kwa kipindi kifupi cha miaka mitatu Mheshimiwa Rais ameajiri watu 155,008. Hili si jambo dogo kwa muda mfupi kiasi hicho na tunaposema ajira, implication yake ni bajeti, kwa hiyo, tunapompongeza mama tunamaanisha amefanya mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo ajira tu, mama huyu Mungu ampe maisha, amepandisha madaraja watumishi 513,490, jambo ambalo lilisimama kwa muda mrefu. Hii inamaanisha ameongeza kwenye bajeti shilingi 252,700,000,000. Kwa hiyo, Watanzania mnaotusikiliza tunaposema tunampongeza mama tunamaanisha amefanya makubwa na shukurani yetu Watanzania ni kumpa kura mama mwaka 2025. Siyo kura tu, kura zitakazovunja rekodi ya nchi hii ambazo wamewahi kupata Marais, angalau hapo tutakuwa tumetenda haki maana hatuna kingine zaidi ya hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka mchango wangu ujikite kwenye suala zima la walimu. Pamoja na mama kufanya haya makubwa, lakini bado kuna tatizo kubwa sana kwenye utumishi hasa walimu. Urithi pekee ambao tuna uhakika wa kuwaachia watoto wetu pamoja na ugumu wa ajira ni suala zima la elimu, kwa sababu, elimu ni suala mtambuka, ukishakuwa na elimu unaweza kufanya mambo mengi na unaweza kujisimamia. Kwa hiyo, ni vizuri watoto wetu wakapata elimu bora na njia ya kwanza kabisa ya msingi ya kupata elimu bora ni kuwa na walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa bado tatizo la walimu ni kubwa kwa hiyo, niombe Wizara hii hizi ajira ambazo mama anazitoa tuziweke vizuri kwa sababu, pamoja na kuwa tatizo ni kubwa, lakini pia kuna tatizo kubwa katika mgawanyo wa hawa walimu. Kuna maeneo yana upungufu mkubwa na kuna maeneo walimu wamejaa, ule msawazo haupo. Kwa hiyo, Waziri atuelewe, tunaposimama na kusema upungufu hili jambo lisichukuliwe kijumla jumla, yapo maeneo yana hali mbaya sana. Nitatoa mfano kwa jimbo langu na najua utakuwa umegusa majimbo mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jimbo langu linahitaji kuwa na walimu 1,376, lakini waliopo ni walimu 741 tu, ina maana kuna upungufu wa walimu 635. Huu ni upungufu mkubwa. Hata hivyo, nikiupeleka kiujumla hivyo bado meseji haitafika vizuri, naomba nitoe mifano tu kwa baadhi ya shule. Kwa mfano, nina Shule ya Msingi inaitwa Mwandu, iko Kata ya Iguguno, ina wanafunzi 1,102, ina upungufu wa walimu 24. Nina Shule ya Msingi Nkungi, iko Kata ya Ilunda, ina wanafunzi 1,043, ina upungufu wa walimu 23. Kuna Shule inaitwa Kikhonda, ina wanafunzi 1,285, ina upungufu wa walimu 29. Ipo Shule inaitwa Mwanigwe ipo Kata ya Kinampundu, ina wanafunzi 1,417, ina upungufu wa walimu 31. Tuna Shule inaitwa Mwangeza, ina wanafunzi 1,177, ina upungufu wa walimu 26, vilevile ipo Shule inaitwa Kinyamburi iko Kata ya Nkinto, ina wanafunzi 1,271, ina upungufu wa walimu 28 na mwisho, tena nimeamua tu kuishia hapo, Shule ya Msingi Tumuli ina wanafunzi 1,367 na ina upungufu wa walimu 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kwa upungufu wa namna hii katika hizi shule chache tu, hawa watoto wanapata elimu kweli, wanapata elimu bora kweli ili wakajitegemee? Hawa watajiajiri kweli kwa upungufu wa namna hii? Kwa hiyo ningeomba sana Mheshimiwa Waziri aelewe, hizi ajira zilizotangazwa juzi, wanapozigawa waangalie wanapeleka wapi na upungufu uko kwa kiasi gani. Tukisema tu kijumla jumla tu kwamba nchi ina upungufu bila kuangalia wapi pana upungufu kwa kiasi gani na athari kiasi gani, kuna watu wataumia na kukosa elimu ambapo tunazidi kusababisha umaskini wa kutosha katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niseme kidogo kwenye suala la interview. Utumishi wamekuwa na tabia ya kufanya interview nchi nzima. Nafasi 200 wanaitwa watu 40,000 Dodoma. Hili tatizo limekuwa likiumiza sana vijana. Watu 40,000 wanakuja kugombania nafasi 200 na hawa watu hawana kazi na wametoka huko kijijini, wamekopa nauli, akija hapa atakaa guest siku tatu. Halafu mwisho wa siku kwa sababu nafasi ni chache, wakiondoka wengi wamekosa, ndiyo inajengeka dhana kwamba kuna rushwa, kuna mwingine mpaka uwe na referee, mpaka ujuane na Mbunge, sijui mpaka ujuane na nani, tunapata tabu sana. Sababu kubwa ni hii ya kuita watu wengi namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara ya Utumishi, wakishaita watu mara moja kufanya interview kwenye kada, waweke benki ya hawa watu. Naamini wanakuwa wame-qualify watu wengi zaidi ya ile nafasi wanayotaka. Waweke hii kwenye list ili nafasi zinapopatikana wampigie tu mtu simu, kwamba, wewe fulani uko wapi? Uko Mkalama? Umeajiriwa tayari? Bado. Nenda ukaripoti Nkenge kuna kazi kule. Kwa sababu alikwishafanya interview na wamekwishamweka kwenye benki
Mheshimiwa Naibu Spika, hii kuita watu kila siku, nafasi ni chache na watu ni wengi, wazazi wanahangaika nauli na vitu vingine, inasumbua sana. Angalau baada ya miaka mitatu minne, wana-review tena ili kuweka ile benki yao vizuri, kama watakuwa wamepungua au vinginevyo. Hii itatusaidia sana, lakini kuita watu wengi katika nafasi chache (watu sijui wangapi) inatutesa, inaleta implication mbaya na inaonekana kuna watu wachache wanaopata ajira kwa sababu wana referees kumbe wala siyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni suala la wakuu wa idara kwenye halmashauri. Leo hii ili mtu athibitishwe kuwa mkuu wa idara awe ametumika kwa miaka 10 na ndiyo anaruhusiwa kwamba huyu sasa amekomaa. Hapo hapo boss wao ambaye ni mkurugenzi anaweza akateuliwa kutoka private sector, anaweza akatoka kwenye ualimu ameanza kazi juzi lakini anaonekana ni kijana mzuri na msomi, anaajiriwa na anapelekwa kwenye wilaya anakuwa mkurugenzi na kazi zinaenda. Sasa, boss wao anaweza kuajiriwa wakati wowote lakini wakuu wa idara mpaka wakae miaka 10. Niombe kitu kimoja. Aidha, Utumishi wabadilishe hiki kitu waachane na habari ya miaka kumi, watu wapate tu ukuu wa idara wakati wowote au mamlaka ya uteuzi iwe inapelekewa majina ya hawa wakuu wa wilaya ili kuwe na succession.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtinga, hiyo ni kengele ya pili, ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie sana suala la walimu Mkalama. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maimuna, wajiandae Mheshimiwa Londo na Mheshimiwa Dkt. Kaijage.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.