Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Maimuna Ahmad Pathan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii leo ya kuchangia kwenye Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala bora. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya uzima na wenzangu wote tulioko humu ndani tunatakiwa tumshukuru Mungu kwa sababu ametupatia uzima kwa siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumshukuru Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu. Miradi mingi ambayo anaifanya inaonekana, kazi kubwa anazozifanya zinaonekana. Tunatakiwa tumpongeze sana Mama yetu Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Waziri wa Utumishi, Naibu Waziri na jopo lake lote la Utumishi kwa kazi kubwa wanayoifanya na kwa kutuletea bajeti nzuri inayoonesha mwanga endapo itatekelezwa vizuri kwa watumishi wetu wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina masuala machache kidogo. Suala langu la kwanza ni malipo ya wastaafu. Naongelea hili suala kwa huzuni kubwa na kwa uchungu mkubwa sana, kwa sababu kuna watumishi wengi wameitumikia Serikali yetu tukufu kwa weledi mkubwa, wamefanya kazi vizuri sana, lakini wamestaafu wametupwa na mpaka leo hawajapata haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana, nina baadhi ya watu na nina evidence za kutosha. Nina mtu wa kwanza hapa alikuwa ni dereva wa Chuo cha Ualimu Nachingwea, anaitwa Hamis Mnali. Huyu baba amefanya kazi yake vizuri, amestaafu mwaka 2009. Jamani, mtu amestaafu mwaka 2009 mpaka leo hajapata mafao yake. Hebu tuangalie hapo utu upo kweli? Ukitaka hii hali iume, hebu jaribu kurudisha vidole mikononi mwako wewe. Ufanye kazi, utumikie, halafu umalize utumishi wako mwaka 2009 mpaka leo hujapata mafao yako. Jamani tunakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama yetu Samia Suluhu anafanya kazi kubwa sana na inaonekana. Pia, viongozi wetu wakubwa wanafanya kazi kubwa sana, lakini huku chini kuna watu wanamwangusha. Nina mifano mingi na hata Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, tukimaliza hapa tutaonana. Huyu baba amestaafu 2009, amezungushwa na nina evidence ya barua zake zote hapa alizoandika utumishi, akaambiwa sijui leta nini, akapeleka. Mpaka baadaye akaamua kuandika barua ya kulalamika. Barua nyingine ikarudi kwenye kile Chuo cha Ualimu Nachingwea, huyo mtu afuatiliwe kisha majibu yarudishwe imefikia wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo aliyoyafanya huyu baba mpaka leo hii ninavyongea na hili Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 19 Aprili, 2024 huyu baba hajapata mafao yake. Hii ni haki kweli? Tunakwama wapi Serikali yetu ya Tanzania? Tunawafanyia nini wananchi wetu? Huyu baba mshahara wake ulikuwa ni mdogo tu, ni dereva wa Chuo cha Ualimu Nachingwea, lakini mpaka leo hajapata haki yake. Amefuatilia amemaliza, amekopa hela kwa watu, amehangaika, aliwatumia mpaka Wabunge na barua ziko humu ndani. Kitu cha kushangaza hajapata haki yake. Apate wapi na huyu ni Mtanzania halali? Documents ninazo, Waziri na Naibu Waziri, nikitoka naomba hapa tuonane ili tufuatilie suala la huyu baba, apate haki yake. Pia, wapo wengine wengi nitampa Waziri evidence zao. Inasikitisha sana na inaumiza sana. Nitapeleka hizi barua, vithibitisho na mambo mengine kwa Waheshimiwa Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kuhakiki watumishi mkoani. Hili suala nilishaliongelea kwenye Bunge na nikauliza swali. Unapostaafu uchumi unakuwa umerudi chini, umri unakuwa umesogea na hauna nguvu. Kwa nini tusiwafuate hawa watu kwenda kuwahakiki kule kila mwaka? Nilijibiwa kwamba, wanakwenda kuwafuata wilayani, hawajaanza hicho kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaamini sana viongozi, Waziri na Naibu Mawaziri waliopo kwenye Wizara hii. Naomba walishughulikie hilo ili watu waende wakahakikiwe huko, hawana uwezo wa kutoka. Hivi umtoe mtu Kilimarondo au Liwale aende akahakikiwe Lindi, hivi jamani mnajua kilometa zilizopo? Mnajua nauli ni kiasi gani? Kwa kweli hatuwatendei haki ndugu zetu kwa sababu na sisi pia ni wastaafu wajao hapo mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine tulikuwa watumishi wa umma, hii hali tunaijua. Tunaomba kuhakikiwa kusiwe mikoani, tuwafuate hawa watu. Ni bora ukamlipa mtendaji wako akaenda kuwafuata hawa watu kwenye kila wilaya akahakiki ili kuwasaidia hawa watu. Watu wazima maradhi yako mengi, uwezo wa kifedha hamna, leo wakahakikiwe mkoani? Hatuwatendei haki na naomba hii ibadilishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la ajira, hili suala la ajira ndiyo kizungumkuti kabisa kusema ukweli. Wabunge wenzangu wameshaongelea hapa, unawaita watu wanatoka Liwale, wanatoka huko, wanatoka wapi, wanakuja kufanya interview Dodoma. Anakuja hapa mzazi wake hali yenyewe ya maisha ni ngumu. Wanakopa hela huko wanakuja hapa wanakaa hata wiki kwenye hoteli. Hebu tuifikirie hii kwa kweli, inaleta msingi kweli? Naomba tubadilishe hili suala la ajira sasa hivi liwe linafanyika kiwilaya. Tena ikiwezekana tunaomba na mgawanyo wa kiwilaya, kwa sababu ajira zinafanyika kwenye system, tunaomba tugawane kiwilaya ili na wilaya nyingine zisikose. Inaonekana kuna wilaya nyingine wanapata watumishi wengi na wilaya nyingine hazipati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la lingine linaniumiza sana kichwa na evidence pia ninazo. Kuna baadhi ya askari polisi walifukuzwa kazi kwa uonevu. Nina evidence popote nitakaposimama na nitawaita na wenyewe. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, naomba walifuatilie hili suala. Mmoja alikuwa ni polisi anafanya kazi Kigamboni katika Kitengo cha Anti-Robbery, mmoja alikuwa anafanya kazi central pale kwenye Kitengo cha Rider (wale waendesha pikipiki). Siku moja wakiwa kazini usiku walikamata dawa za kulevya (ni siku nyingi kidogo mwaka 2013). Walipokamata dawa ya kulevya na gari wakaamua kuongea kwenye zile simu zao kutoa taarifa makao makuu kwamba kuna gari tumelikamata na lina madawa ya kulevya, kwa uhakika kabisa na kwa uaminifu kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamejipalia makaa. Siwezi kuthibitisha kwamba zile dawa zilikuwa ni za wakubwa, ila naomba wani-quote, “Inawezekana zilikuwa dawa za wakubwa au dawa ya watu wenye pesa sana”. Hali ilikuwa mbaya kwao, kilichofuatia waligeuziwa kesi na wakabambikiwa kesi za ajabu. Baada ya siku mbili, tatu walikwenda kukamatwa wakawekewa kesi ya kwanza kwamba, wameiba kwa Wachina, kesi ya pili wameiba bar. Mtu amekamata dawa za kulevya ameokoa vijana wetu ambao wanaharibika na madawa ya kulevya, leo wanakuja kubambikiwa kesi kubwa kama hizo? Inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichofuatia ni kwamba kesi ilikwenda mpaka 2016 ikaonekana hawana hatia na wenye hatia walikamatwa wakafungwa. Kibaya zaidi, baada ya kesi kwisha wale walianza kuandika barua ili waweze kupata stahiki zao za miaka yote ambayo walikuwa wamewekwa ndani na kurudishwa kazini, inasikitisha. Wamepigwa danadana na kibaya zaidi kuna baadhi ya watu wakaanza kuwafanya mtaji wao kwa kuwachukulia hela ya kuishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha, watu wamejitolea kutetea Taifa letu, leo hii ndiyo wanaambiwa ndiyo wametenda yale madhambi…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maimuna Pathan, muda wako umekwisha kaa chini…

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, lakini naomba hizi kesi ambazo nawapa, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, niwaone ili hawa watu wasaidiwe, warudishwe kazini, walipwe haki zao za msingi. Hii ni Tanzania, wako kwenye nchi zao, wana… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Pathan utaratibu ni kwamba kama una mengine ya ziada unaandika kwa Waziri.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nimekusikia.