Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi. Bajeti hii ni muhimu sana kwa sababu suala la utumishi ni suala sensitive na ni suala ambalo ni muhimu sana katika utawala wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye imempendeza yeye sisi waja wake kujadili bajeti hii muhimu katika utekelezaji wa moja kwa moja wa majukumu ya Serikali kwa wananchi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nimshukuru Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa maboresho makubwa ya utumishi ndani ya Serikali. Pia, itoshe kusema kwamba, utumishi kwa maana ya utawala ilikuwa ni sehemu ya Kamati ya kile kilichoitwa USEMI. Kwa hiyo, tulikuwa na maslahi ya karibu sana katika kuifuatilia na naweza kusema kwamba kuna maboresho makubwa katika utumishi ndani ya Serikali yetu. Sifa kubwa zimwendee Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan pamoja na timu yake katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kuona kero na kadhia nyingi za watumishi wetu hasa kero ya upandishwaji daraja kwa watumishi, malimbikizo na madai mbalimbali ya watumishi wetu yakichukuliwa hatua; kwa maana ya kuangalia jinsi gani ya kutoa solution ya changamoto kwa kuwapandisha madaraja, kulipa malimbikizo na madai mbalimbali ya watumishi wetu. Jambo hili haliwezi kupita kimya kimya, ni wajibu wetu kupongeza pale ambapo Rais wetu na Serikali yake inafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo naomba kutumia nafasi hii kuipongeza sana Serikali hasa kupitia tangazo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi, kaka yetu Mheshimiwa George Simbachawene lililosema kwamba Serikali na Mama yetu Samia Suluhu Hassan, ameridhia ajira mpya za watumishi 46,000. Kilio cha upungufu wa watumishi ndani ya Serikali ni kilio kikubwa miongoni mwa Wabunge na wananchi wetu. Kwa hiyo, tangazo hili limetupa faraja sana sisi wawakilishi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote ni ubunifu wa Wizara kusema kwamba hizi ajira zinakwenda mikoani. Hii inaweza kupunguza gharama kwa wazazi za kutuma watoto kwenda kwenye vituo vya Dodoma na Dar es Salaam kwa ajili ya interview. Pia, inaweza kuongeza uwazi katika suala zima la ajira. Kubwa kuliko yote ni msawazo wa ajira hizi kuwa wa haki kwa Tanzania nzima kwa sababu tunajua mahitaji ni makubwa. Nafasi ni chache lakini ni lazima kuwe na uwakilishi wa Kitaifa na ndiyo maana nasema kwamba suala la utumishi ni suala sensitive. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utumishi wa umma kama dhana, ni dhana muhimu sana, lakini umma ni nini? Mtumishi wa umma ni nani? Ni huyu Mtanzania ambaye ana check number ambaye ameajiriwa na Serikali ama ni huyu kijana ambaye amejiajiri kama dereva wa daladala ambaye anaamka saa 10 alfajiri na analala saa tano usiku akihakikisha kwamba watumishi na waajiriwa wa Serikali wanafika ofisini kwa muda, wanafanya kazi kwa muda na anahakikisha wanarudi nyumbani salama?

Mheshimiwa Naibu Spika, mtumishi wa umma ni nani? Ni huyu ambaye anaingia saa moja na nusu ofisini na anatoka saa kumi ama ni huyu mama lishe ambaye anahakikisha watu wote ambao wameajiriwa na ambao hawajaajiriwa wanakunywa chai asubuhi, wanakula chakula cha mchana na cha usiku na afya zao zinalindwa? Mtumishi wa umma ni nani katika nchi hii? Ni nani ambaye ana jukumu la kulinda maslahi ya umma? Ni hawa ambao wana check number ya Serikali ama hawa Watanzania ambao kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika katika ujenzi wa Taifa letu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nazungumza hivi? Kuna concept inaitwa tragedy of the commons (chochote cha umma hakina mwenyewe). Tunaweza tukaliona hili katika namna ya usimamizi na udhibiti wa mali za umma. Changamoto bado ni nyingi, bado changamoto ni kubwa na Serikali inaingia gharama kubwa ya usimamizi wa mali zake pamoja na uchakavu wa mali zake kutokana na usimamizi mbaya kwa sababu hakuna mtu ambaye anaona umuhimu wa kulinda mali za umma. Sasa wakati umefika kwa Watanzania wote kujiona kwamba ni watumishi wa umma. Kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika kulinda maslahi ya umma, kulinda mali za umma na kuhakikisha umma unafaidika na kile ambacho unastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la dhana ya utumishi linanipelekea kuona kwamba, ni muhimu kulinda haiba ya Serikali kwenye macho ya wananchi. Kulinda haiba ya Serikali ni jukumu la Watanzania wote ambao ni watumishi kwa namna moja ama nyingine. Mwalimu Nyerere alisema; “It can be done, play your part.” Inawezekana kila mmoja akitimiza wajibu wake kwenye eneo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kijijini kwenye level ya chini kabisa Serikali kule inaonekana kupitia waajiriwa wa Serikali kwa maana ya muuguzi, daktari, mtendaji wa kata. Mwananchi wa kule kijijini anaweza asikutane hata siku moja kwenye maisha yake na mkurugenzi, DAS ama DC, kwake yeye Serikali inaishia kwa mtendaji wa kijiji akienda juu sana mtendaji wa kata, hawa ndiyo sura ya Serikali, hawa ndiyo vioo vya Serikali. Mwananchi akisema Serikali ni mbaya ni kwa sababu amehudumiwa vibaya na muuguzi kwenye zahanati ya kijiji, akisema Serikali ni nzuri maana yake amepata huduma safi kwa mtendaji wa kijiji, lakini utendaji wao wa kazi na haiba yao inafanana na dhana ya utumishi wa umma? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili naomba nguvu kubwa ielekezwe kwenye kujenga dhana ya utumishi, kuboresha haiba ya utumishi katika ngazi za chini kwenye vijiji na kata zetu. Serikali yetu imekuwa ikibeba lawama nyingi ambazo zinatokana na utendaji mbovu wa watu katika maeneo ya chini, si wote, ni wachache lakini wanaharibu taswira nzuri ya Serikali. Mara nyingine si makosa yao, mara nyingine ni kukata tamaa, mara nyingine na wao kuona hawatendewi haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kuwekeza sana kwenye kuboresha ofisi, kuwapa vitendea kazi wengine mapikipiki, pale wilayani, magari, ofisi nzuri lakini bado kuna kitu ambacho kinakosekana na chenyewe kiko kwenye software siyo hardware, ni lazima sasa jitihada ziwekezwe katika kuboresha maisha ya mtumishi ajione kwamba anawakilisha Serikali, anawakilisha nchi kwa maslahi ya nchi katika maisha ya wananchi, katika ngazi ya chini. Kwa kufanya hivi tutakuwa tumeitendea haki na kuisaidia sana Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema tukatambua utendaji mbovu wowote katika ngazi ya chini unapunguza imani ya wananchi kwa Serikali yao. Suala hili ni muhimu sana, deficit ya public trust kwa Serikali si jambo dogo, ni jambo kubwa sana, mwananchi ni lazima aamini kwamba akifika katika ofisi ya kijiji atatendewa haki na mtendaji wa kijiji. Mwenyekiti wa kijiji ni lazima asimamie maslahi ya Serikali ya kijiji kwa kulinda interest za wananchi wake katika ngazi ya kijiji na lazima mtendaji wa kijiji ajue kwamba yuko pale kwa ajili ya kuiwakilisha Serikali na yeye ni mwakilishi wa Serikali. Tukiboresha hayo, malalamiko ya wananchi wetu yatapungua, wataendelea kupenda Serikali yao na wataendelea kushiriki katika ujenzi wa Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, langu ni kumshukuru Rais wetu kwa sababu amewekeza sana katika kuboresha maisha ya watumishi katika ngazi za vijiji, kata na katika halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)