Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Nami naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo ameendelea kufanya kazi kwa umakini mkubwa kwenye Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuwapongeza viongozi wangu kwa maana ya Waziri wetu Mheshimiwa George Simbachawene, amekuwa akifanya kazi kwa bidii sana bila kumsahau Ndugu yangu Naibu Waziri, Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya Mrisho Kikwete kwa muda mfupi sana ambao amekaa kwenye ofisi hiyo ameonesha umahiri mkubwa, wenzangu wataniunga mkono tunampongeza sana ndugu yangu. Pia nawapongeza watendaji wote wa ofisi hii bila kusahau watumishi ambao wako chini ya ofisi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niwapongeze watumishi wote ambao wako katika maeneo mbalimbali ambao wamekumbwa na kadhia au changamoto iliyosababishwa na mvua nyingi sana zinazonyesha katika nchi yetu. Wale watumishi wa maeneo yale wanafanya kazi siyo masaa 24, ni masaa yote, wanafanya kazi masaa yote, wanafanya vikao usiku na mchana, ni mazingira mengi sana yamepata mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikisema maeneo machache kwa maana Rufiji na Kibiti watumishi wa maeneo yale hawana kupumzika, unaona mpaka wanatembea wanasinzia na hii ni spirit ya watumishi wetu wa Tanzania. Hatukatai kuna watumishi wana mapungufu lakini watumishi wa Tanzania wameendelea kufanya kazi katika ari na uzalendo mkubwa, Wabunge tukiwa mashahidi mazingira yetu kule vijijini kwenye halmashauri tunayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona mazingira wanayoishi watumishi wetu watendaji wa kata, watumishi wetu ambao ni maafisa maendeleo ya jamii, watumishi wote katika halmashauri zetu vijijini wanaishi mazingira ambayo sisi tunayafahamu lakini watumishi hawa hatujawaona wakiingia barabarani wakifanya maandamano, wakibeba mabango kama nchi jirani. Kwa hiyo, watumishi wa Tanzania pamoja na kwamba wanapitia mazingira mbalimbali wameendelea kusimamia taratibu, sheria na kanuni za utumishi, wameendelea kuwa wazalendo, wanastahili kupokea maua yao watumishi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumnukuu Mheshimiwa Mama yangu kipenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuunganisha sifa hizi ninazozitoa wapate kujua ndiyo moyo wa Mheshimiwa Rais alisema: “Kwa kila Taifa linalokua kuna nguvu ya wafanyakazi kwa kiasi kikubwa mno.” Hakuishia hapo Mheshimiwa Rais alisema, anatambua mchango wa wafanyakazi kwenye uchumi na ustawi wa Taifa la Tanzania. Pia hakuishia hapo Mheshimiwa Rais alisema, anatoa shukrani zake za dhati kwa wafanyakazi kwa kazi wanayofanya kwa Taifa hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema wafanyakazi wa Tanzania wanafanya kazi kwa uzalendo, hatukatai kuna watu wenye mapungufu, kwa hivyo naomba hilo lijulikane, wafanyakazi wa Tanzania wanastahili kupokea maua yao, tumeona wafanyakazi wa nchi zingine wako barabarani, siyo kwamba hawana changamoto, wana changamoto, lakini wamekuwa wavumilivu wamekuwa wazalendo kwa Taifa lao watumishi wa nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda Fungu 32 ambalo ni Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Nimezungumza mara nyingi kwenye Bunge lako Tukufu jinsi ambavyo ndani ya miaka mitatu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejali eneo la utumishi, amejali maslahi ya utumishi kwa mapana yake, siwezi kurudia nimeshasema kwa idadi na kwa gharama iliyotumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu Ofisi ya Rais ambayo ndiyo Wizara yake mwenyewe Mheshimiwa Rais, imeendelea kuumba mifumo mbalimbali ambayo inaleta ufanisi katika Utumishi wa Umma. Tumeona kuna miundo na mgawanyo wa majukumu ya Taasisi mbalimbali ambako mpaka sasa imehuishwa miundo 80 kati ya miundo 120. Naipongeza ofisi hii, lakini nijielekeze, ukienda kukutana na watumishi, kama kuna top five yaani kama kuna changamoto tano basi kati ya hizo tano miundo haikosekani. Wanalalamikia sana suala la miundo, miundo ya maendeleo ya utumishi yaani scheme of service. Najua kwamba ukigusa muundo unagusa wage bill sijakataa, lakini miundo imeendelea kuwa changamoto, inapelekea watumishi kule chini kupunguza morali ya utumishi wao wa kazi, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mtumishi ameshafanya kazi katika kada yake, amefikia TGS ya juu sana, niseme mfano ni mwalimu lakini alikuwa na ambition maishani kuwa mwanasheria, akaenda kusoma sheria, sikatai kwamba akija kwenye Idara ya Sheria hawezi kupanda wakati huo huo, lakini basi kama hawezi kupanda wakati huo huo, hata ahame na mshahara wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama inawezekana waweke kanuni na taratibu au mwongozo kwamba mtumishi akitoka kusoma asishuke akaanza tena TGS ya chini, inawafanya wasiende kusoma, watu wana ndoto zao, eneo hilo limekuwa likilalamikiwa sana. Pia kuna kada zingine ili kuwa Mkuu wa Idara lazima awe ni principal lakini zingine si lazima awe ni principal, lakini watumishi wanafanya kazi eneo moja hii imekaaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna Miundo Mikuu ya Serikali na kuna Miundo ya Taasisi na Wakala mbalimbali, hebu tuendelee kuwasiliana ili watumishi wale ambao wameendelea kufanya kazi, kuna jambo kubwa watumishi wa Tanzania wanalisema, ukienda kuwasikiliza jambo la kwanza wanamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wanasema pamoja na keki ndogo anayopata pamoja na kwamba amezingatia sekta zote, awamu hii hajawaacha watumishi ameendelea kuwajali, hiyo inawapa moyo kuendelea kufanya kazi. Pamoja na kwamba tunasema haki inatokana na wajibu, huo wajibu wanaofanya, basi na haki zao wapate. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kupitisha bajeti yao, lakini pamoja na Wizara ya Fedha linapokuja suala la rasilimali watu, suala la watumishi, naomba tuliangalie kwa jicho la tofauti na bajeti yao tuipeleke kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda Fungu 67 kwenye Sekretariati ya Ajira. Nimezungumza mara nyingi kuhusu suala zima la Sekretarieti ya Ajira, nawapongeza kwanza kwa jinsi ambavyo wameendelea sasa Serikali kuweka mifumo ambayo sasa hivi waajiri au wanaoitwa kwa ajili ya ajira hawaendi sehemu moja tena. Walianza kwa zonal kwa maana ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, kote kuna center za kufanya mitihani, nawapongeza sana Serikali. Sasa hivi wameenda kiwilaya, sisi kama Kamati tumeona wamefungua center kwenye wilaya zote, sasa wanaokuja kufanya interview hawaendi tena kwenye mikoa wanaenda kwenye zonal wise, kwenye vyuo na kadhalika, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja naenda kulirudia, siyo siri kwamba miaka mitano iliyopita ajira hazikuwa nyingi sana na sasa Mama amefunguka, lakini wakumbuke narudia tena, kila mwaka vyuo vilikuwa vinatoa graduates, watoto wako nyumbani tunao, umri wao unakwenda. Wanapofanya interview sasa hivi na hawa ambao wametoka shule mwaka jana, tusitegemee kwamba watafaulu sawasawa na wale ambao wameshakaa nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisemi aende mtu aliyefeli, lakini kama pass mark, kwa sababu sasa wanafaulu sana watoto, kama ajira wanataka watu 200 na wamepata 100, 200 au 90 wote kuna watu wana 80 au 70 tuangalie mwaka wao wamemaliza lini shule, kama ana 80 amemaliza shule 2017, hebu tufanye consideration, ameshaingia mtaani amefanya shughuli nyingi, hatutegemei afaulu kama amemaliza shule juzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wanajua nini maana ya kukaa mtaani, wanakosa watu ambao watakuwa watumishi waadilifu kwa sababu wanajua nini maana ya kukaa mtaani, hebu na hawa wengine wasubiri au tuchukue 50 kwa 50. Tumewafanya hawa watu waichukie Serikali yao, wajione kama siyo sehemu ya Tanzania. Nakubali kwamba si wote ambao watapata ajira, lakini wale ambao wamekaa muda mrefu miaka mitano siyo kosa lao, naomba wanapokuja mwisho kuhitimisha waniambie hili suala limekaaje maana ni mara ya tatu nalizungumza katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la makazi, mtendaji kata kule kwenye kata, kijiji, kule kwenye mtaa au mtendaji wa kijiji heshima yake na usalama wake ni makazi pia. Naipongeza Serikali inaendelea kujenga nyumba za watumishi na tunajua sasa hivi kwenye Halmashauri zetu wamehamia kwenye makazi maalum, Halmashauri nyingi zimehamia maeneo mapya ambapo ni mbali na kule ambako wanakaa watumishi wale na hakuna makazi ya watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kupitia Utumishi Housing, wameendelea kujenga nyumba, lakini kiuhalisia mtendaji kata anashindwa kununua ile nyumba ya Watumishi Housing, wamekuja na mawazo wamesema kama inawezekana kumjengea mtumishi kila siku nyumba ya bure basi jenga piga flat moja eneo la halmashauri fulani, angalau kila mwezi akatwe shilingi 10,000, akitoka halmashauri akahamishwa, akienda nyingine kuna uhakika wa nyumba, usimpe basi nyumba ya bure kama ni kazi namna hiyo. Naamini National Housing pamoja na Watumishi Housing pia wanafanya kazi kibiashara, lakini watumishi hawa anamkamata mtu kwenye kata, mtu huyu aliyemkamata amepanga nyumba ya mjomba wake, yaani yeye mtendaji amepanga nyumba ya mjomba wake huyo mtu, heshima iko wapi? Kwa hiyo suala la makazi ni muhimu sana, nampongeza Mheshimiwa Rais anafanya, lakini tuliangalie kwa umakini wake, kujenga nyumba za bure zote kwa kuwa Serikali inajua, inanielewa hebu tufanye.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Dkt. Kaijage.

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)