Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia katika Wizara ya Ofisi ya Rais, Utumishi. Nawapongeza Mheshimiwa Simbachawene na wenzake wote kwenye Wizara hiyo kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo muhimu ambayo nataka kupitia kwa haraka haraka. Eneo la kwanza ni TAKUKURU. TAKUKURU wamepewa jukumu kubwa sana la kwanza kuzuia rushwa, kuchunguza na kudhibitisha na hatimaye wale watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uchunguzi usioisha katika maeneo mbalimbali, yaani siku hizi ikitokea kuna mradi fulani unashukiwa kwamba kuna rushwa, TAKUKURU wanaingilia kati, wanachukua mafaili, wanakaa nayo hata miezi sita mpaka mwaka mzima. Kwa hiyo, kazi imesimama, mradi hauendelei na uchunguzi hauishi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaomba eneo hili ni vizuri likafanyiwa kazi vizuri ili kama kuna tatizo mahali, hatua zichukuliwe, uchunguzi uishe, wanaowajibishwa wawajibishwe ili mradi uweze kuendelee na wananchi wetu waweze kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi sana pale kwangu yako namna hiyo, yako stranded mpaka leo tunasubiri ripoti ambayo haijawahi kukamilika. Nadhani hilo ni muhimu sana kulifanyia kazi. TAKUKURU ndiyo ambao wangesaidia huu uchafuzi wa mazingira wa hali ya hewa ya kazi nzuri ya Serikali ya kwamba kila ripoti ya CAG ikitoka maana yake inasema kuna ulafi wa fedha, kuna fedha imeibiwa mahali fulani. TAKUKURU wanaweza pia kusaidia kupunguza hiyo. Tunajua anafanya kazi yake vizuri, tunamfahamu Mkurugenzi Mkuu ni kachero aliyebobea, tunamfahamu tulikuwa naye, ameanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya juu. Afanye kazi yake vizuri ili aweze kupunguza hayo malalamiko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni taasisi ya uongozi. Katika eneo hili tulitarajia taasisi hii ndiyo isaidie namna ya kutengeneza viongozi wa nchi. Sasa tunapoona kuna watu ambao wanapewa mamlaka makubwa baadhi ya maeneo, halafu ana-mess up katika utendaji, tunaanza kuona kuna ombwe katika eneo hili. Tunatarajia kwamba viongozi wetu kabla ya kupewa madaraka makubwa, nimeona kwenye ripoti hapa, kuna mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wanalalamika sana ugomvi uliopo kati ya ma-DC na Wabunge; na mgongano/ugomvi uliopo kati ya Wakurugenzi na Watendaji wengine katika maeneo yale. Yaani mtu anachukuliwa wa kawaida kabisa. Sawa, ana vyeti, amesoma, lakini kazi ya Ukurugenzi hakuwahi kuifanya. Tunatarajia kabla ya kukabidhiwa ofisi ya umma ni vizuri akapata A, B, C kupitia taasisi ya uongozi ili akienda pale atambue kwamba kuna wananchi wana haki zao. Waheshimiwa Wabunge ni viongozi wawakilishi katika maeneo yale, hivyo washirikishwe, ma-DC kila mtu afanye kazi yake vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba hawa watu wafanye kazi yao. Ni muhimu mtu amepata fursa ya kuteuliwa, lakini ni vizuri akapewa A, B, C huko anapoenda ili akafanye kazi vizuri katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni eneo la TASAF. Wamesema wenzangu, lakini nataka niseme kwamba mimi sioni sababu kwa nini TASAF iendelee kubaki hapa Utumishi. Kwa nini isiende TAMISEMI? Kwa sababu watu wote ambao wanasimamia miradi ile, kwenda ku-disburse zile fedha na kadhalika, ni watu wa TAMISEMI. Kwa hiyo, mkienda kule kunakuwa na shida ya usimamizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wananchi wanalalamika namna ambavyo wanapewa fedha zao. Wanachanganywa, wakati mwingine wanaambiwa kwamba fedha ipitia benki, wakati mwingine kwenye simu, simu wanaibiwa, wakati mwingine wanapewa kwa njia ya cash, wale ambao wanapewa fedha wanazikata makato. Sasa hili jambo ni muhimu likafanyiwa kazi. Hiki ni kitu ambacho kinasaidia watu ambao ni maskini wa hali ya chini sana, sasa umempa fursa ya kusaidiwa, lakini katika utekelezaji wake wanapata changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka tufanye ziada. Kuna upotoshaji mkubwa. Kuna mpango mmeupeleka kwamba wale watu wasaidiwe fedha ile ya TASAF, lakini wanafanya miradi ya kijamii. Sasa wanasema, inawezekanaje mtu ambaye ni mgonjwa, mtu ambaye ni maskini unamfanyisha kazi? Mimi naelewa kwamba analipwa fedha yake stahiki ile ya msaada, lakini pia kama ana nguvu ya ziada, au msaidizi wake atafanya kazi ya ziada apate fedha ya ziada. Kwa hiyo, watu wanapotosha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atoke ofisini na watu wake, watoe elimu, kwamba wanaofanya kazi miradi ya kijamii wala hawalazimishwi na kwamba fedha ambayo wanapata ya mradi, haina uhusiano na fedha ya kawaida ya ku-qualify ile ya mradi wa TASAF. Wanachanganya watu, tunaonekana sisi Serikali tunawatumikisha wagonjwa wa TB, wagonjwa wa Ukimwi, wazee sana, kitu ambacho wanapotosha. Kwa hiyo, ni vizuri hiyo ikawekwa very clear ili ikawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili pia la TASAF, ni vizuri Mheshimiwa Waziri na watu wake waende wakatambue wanaostahiki kupata hiyo fedha. Kuna wizi mkubwa, kuna majina hewa mengi, yaani wale watu ambao wana uwezo, wenye dhamana wamechukua ndugu zao wamewaingiza kwenye Mfuko wa TASAF, wao ndio wanalipwa. Kila ukienda kwenye Mkutano wa Kijiji, Mbunge akifanya mkutano wanakuja maskini, vikongwe wanakuuliza hebu niambie Mheshimiwa Mbunge mimi na huyu ambaye anapata fedha, nani ana ahueni na afadhali? Ni vizuri hilo Mheshimiwa Waziri akalifanyia kazi. Wale ambao wanastahiki wapate. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwamba, kama mtu amepata miaka mitano au miaka kumi a-qualify. Wahitaji ni wengi, hatuna uwezo wa kumlipa kila mtu. Mtu amekaa miaka kumi amejiendeleza, amejenga nyumba, ajengewe uwezo a-qualify ili wengine waweze kuingizwa kwenye mfuko na waweze kunufaika katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la nne ni ajira katika utumishi wa umma. Nataka kumwambia Mheshimiwa Waziri, ukweli ni kwamba unazungumza kwamba ajira ni fair lakini nataka kukwambia, tunapozunguka na kusoma watu wenye dhamana, kuanzia ngazi ya juu kabisa, tunaangalia hilo Baraza la Mawaziri, tunaangalia Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, ma-DC, CMT, na watumishi wengine kama Watendaji wa Kata, utaona kwamba kuna maeneo fulani; yaani kuna Mbunge hapa katika hizi nafasi zote za nchi hii ambazo kwenye Katiba zimetengenezwa, hakuna mtu katika wilaya yake au jimbo lake. Huo ndiyo ukweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutuambia kwamba kuna u-balance wa utumishi, mlifanyie kazi. Kila Mbunge anataka watu wake wapate ajira. Kama ni kupata ajira ya jumla, kila nikienda mahali naona mbona ni eneo fulani wamejazana hapa. Kuna mjomba, shangazi, bibi, kaka; wao peke yao ndiyo wamesoma. Lazima tupeane nafasi hizi. Kwa hiyo, msaidie Mheshimiwa Rais na mamlaka kwamba watu wako wengi, mnapotoa zile ajira, kwa mfano mtu ameomba ajira ana miaka kumi mpaka leo ana-apply, ametembea mikoa yote hajawahi kupata ajira na wanalalamika mitaani. Hata mfumo mliotengeneza, Mheshimiwa Waziri katika jambo ambalo utakumbukwa na kuheshimika ni ku-balance. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeomba hapa Bungeni, kama una ajira 17,000, si unipe watu 20 kwenye jimbo langu. Usinipe majina, lakini wapate kule na ndiyo maana hapo kuna shida ya utumishi. Kuna watu sasa hivi wanaandika address kwa sababu wanataka ajira, anakuja unampa ajira. Mbunge anaambiwa umepata watumishi 20, baada ya miezi sita wote wamehama wanarudi nyumbani kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwenye majimbo ya vijijini imekuwa ni address ya kupatia ajira na Mbunge hana say. Sasa mtu anakwambia nimemfuata mume wangu, nimemfuata mke wangu, unafanyaje? Unanipa figure ya watu kufanya kazi, nawatangazia wananchi mtapata daktari, mtapata mwalimu katika eneo hili, baada ya miezi sita wote wamehama wamerudi nyumbani kwao. Sasa kumbe ungetakiwa ugawe tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli unabaki kwamba tunataka watu wapate ajira na vijana wengi wanalalamika. Tunataka ukitangaza ajira hizo, hebu tuone wametokea maeneo gani ili tuone kweli hiyo hali imekuwa sawa sawa. Mheshimiwa Waziri, huwezi kuwa unaajiri watu wanafanya kazi mpaka wanastaafu. Ukiajiri unakabidhi idara mbalimbali kwa mfano unapeleka TAMISEMI, unapeleka hapo Utumishi na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kushauri vizuri, kwa heshima, jambo la kikokotoo ni bomu. Nataka kurudia, suala la kikokotoo ni bomu. Ulipokee kwa heshima na Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba nisikilize hapa. Pokea jambo la kikokotoo na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika na sisi Wabunge, mpelekee Mheshimiwa Rais ushauri wa kitaalam atoe statement kwa Watanzania, hilo ni bomu, mimi nimewashauri kwa sababu…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara, kengele ya pili.

MHE. MWITA M. WAITARA: Naam!

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, shikamoo. (Kicheko/Makofi)