Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Wete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nami kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara yetu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kwanza sina budi kumshukuru Allah Subhanahu Wa Ta’ala aliyetuwezesha kufika hapa katika Bunge hili jioni hii tukiwa wazima na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kujielekeza kwenye mchango wangu kwa kuanza kuzungumza kuhusu mshairi mmoja ambaye alitunga shairi linasema Jeraha la Moyo. Alisema kwamba:-
“Moyo uliojeruhiwa, mengi huyafikiria,
Hufikia kuzidiwa, zitawalapo hisia,
Unaweza kuamua, lolote kujifanyia,
Ni rahisi kupagawa na kutoka kwenye njia.”
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hivi kwa hisia kali. Nazungumza kwa hisia kali kwa sababu ya kikokotoo. Kikokotoo kama jina lake lilivyo, lakini kwa kweli linawakokotoa wafanyakazi ambao tumewatumia kwa muda mrefu sana. Wafanyakazi wamefanya kazi kwa miaka 30, 35, wengine ni waajiriwa wa Polisi, wengine ni Madaktari, Walimu kama mimi, kwa kweli wako katika hali mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wengine sasa hivi tunavyozungumza, kwa sababu ya kikokotoo, wanapumulia mashine, kuna wengine sasa hivi sukari inapanda kiasi cha kwamba, hawana maisha, lakini kuna wengine sasa hivi hawajui maisha yao yatakuwa yako wapi, wamebaki kuwa ombaomba hata chakula hawana, hawana cha kuvaa. Ukiwaangalia, unaweza ukamkuta mwalimu, daktari au mfanyakazi, anavaa kiatu kimoja chekundu kimoja cheupe. Unajiuliza, shida ni nini? Shida ni kikokotoo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, hapa tumefanya kitu kibaya kabisa, ingawa tulipitisha sisi katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuna haja ya kuhakikisha kwamba sheria hii inaletwa tena kufanyiwa mabadiliko, tena mabadiliko ambayo yanaweza kusaidia kuhakikisha kwamba wafanyakazi hawa wanaishi katika hali ya raha na starehe. Unashangaa na unajiuliza, hivi kweli Mkurugenzi wa Manispaa au Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye umemtumia miaka 30 ashindwe kuzitunza fedha zake ambazo umempa kiinua mgongo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni fedha yake, kweli ashindwe kuitumia wakati wewe ulikuwa unampa posho, unampa stahiki mbalimbali za wafanyakazi, lakini zile alikuwa anazitunza na anahakikisha kwamba zinafanya kazi vizuri na hakuna ubadhirifu wa aina yeyote. Aje ashindwe kutumia hela ambayo anaiendeshea familia yake? Naomba fedha hizi zirejeshwe kwa wafanyakazi ambao wametumika katika Taifa hili na kuhakikisha kwamba maisha yao na wao yanakuwa katika hali nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Polisi sasa hivi, ndiyo ambao wanalinda nchi hii. Kwa kweli utawashangaa, nenda kaangalie hali walizonazo Polisi sasa hivi, ni mbaya. Ni wastaafu ambao wamekuwa ombaomba. Leo Kamishna wa Polisi analipwa kiinua mgongo chake shilingi 200,000,000, unampa shilingi milioni 60, kweli hii ni halali? Hii ni haki? Shilingi 140,000,000 unazo wewe mfukoni, unamtunzia nani jamani? Mtu mzima anatunziwa pesa. Ikitokea akifa fedha ndiyo zimepotea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli ni mtu mzima gani mwenye akili timamu aliye na umri wa miaka 60 bado akili inafanya kazi, halafu unachukua hela unakwenda kumtunzia wewe? Serikali inatunza fedha za wafanyakazi ambao wamestaafu, kwa kweli hili ndiyo tunalolisema ndiyo hilo jeraha la moyo ambalo wafanyakazi wetu wanalo sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niondoke hapo. Sasa naenda kwenye suala zima la ajira. Dada yangu Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kazungumza sana kuhusu ajira. Kwa kweli, tunasema kuna upendeleo wa ajira. Kwa nini tunasema hivyo? Kuna vijana wetu ambao wamemaliza chuo, wanatumikia Wizara ya Elimu, kwa mfano, wanajitolea. Vijana hawa hawalali, hawanywi, wanafanya kazi na watoto wetu, matokeo yanakuja mazuri na Tanzania tunajivunia kwamba tuna elimu bora, lakini unashangaa anakaa miaka saba hapati ajira. Halafu anakuja mtu anatoka university, fresh kabisa, leo yeye ndiye anapewa ajira. Huu si ni upendeleo! Upendeleo huu unatupeleka wapi? Kwa kweli hili naomba tuliingilie kati kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ajira 46,000 zitatolewa, naomba Mheshimiwa Waziri uhakikishe kwamba vijana hawa wanaojitolea wanapata ajira ili nao mwaongezee motisha waweze kuona kwamba kweli wanaitumikia nchi yao kwa weledi na uaminifu na pia wanapata stahiki zinazowastahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naenda kwenye Mfuko wa TASAF. Hiki ni kizaazaa, kwa sababu nia ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kwamba anawafanya Watanzania wawe na maisha bora. Kila mmoja aishi maisha ambayo yanamsaidia katika familia yake. Tuna familia zilizo duni kabisa. Familia zetu ziko katika hali mbaya, lakini jambo la kushangaza ni kwamba, utaratibu unaotumika kupata kaya maskini ambazo zinasaidiwa na Mfuko wa TASAF siyo sahihi, umeingiliwa na Masheha kwa kule kwetu Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheha sasa ndiye mwenye say kwamba huyu mpe, huyu usimpe. Kuna watu wako katika hali mbaya zaidi kuliko hawa ambao sasa hivi wanapata fedha kwenye Mfuko wa TASAF.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tena la kushangaza ambalo kwa kweli linakera zaidi ni kwamba, kila siku fedha zinapungua. Kaya maskini inapewa shilingi 70,000, kesho unakuta zile fedha zimekatwa, inalipwa shilingi 30,000. Je, wale vijana waliokuwa wakihudumiwa na hiyo kaya wamekufa? Kuna kigezo gani kinatumika kukata fedha? Ukiuliza, majibu yao wanakwambia, aah, nenda, mambo haya yanatoka Bara bwana, siyo huku Visiwani, yanatoka Bara. Sasa kwa kweli, hili haliko sahihi. Naomba na hili lifanyiwe marekebisho. Ahsante sana. (Makofi)