Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Konde
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Utumishi na Utawala Bora. Mimi nitazungumzia mambo matatu tu kwa leo. La kwanza, ni suala la ajira. Ajira za Muungano utaratibu wake siyo sawa. Kwa nini nasema hivyo? Siku nyingi huwa nasikia kuna kero za Muungano, lakini sijui zimepatikana vipi, kwa sababu kuna mambo mengi ambayo ni kero. Moja ni suala hili la ajira za Muungano katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ninalotamani hasa, kama kuna jambo la kutatua, basi Wizara ya Utumishi nayo ingekuwa ni Wizara ya Muungano. Kwa nini nasema hivyo? Ajira ambazo zinatoka kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwenda Zanzibar hazina mfumo sahihi. Wazanzibari hawazifahamu, wanasikia tu zimekwenda na watu wameajiriwa. Sasa jambo hili siyo zuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wazanzibari tunahitaji mfumo huu wa ajira utokee huku huku Wizara ya Utumishi ili Wazanzibari wajue tuna mfumo fulani ambao unatokea Wizara ya Utumishi Tanzania ambao tunaomba kuliko kwenda kule, watu wanachaguana, hajulikani nani kapata, unasikia tu ajira zimetoka, siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nahamia suala lingine. Mwishoni mwa mwaka huu tunakwenda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka kesho Mungu akipenda tunakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu. Suala la Utawala Bora hapo litatamalaki. Kwa nini nasema hivyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokuwa kwenye uchaguzi sheria nyingi zinakandamiza na siyo kwamba sheria ni mbaya, ila watendaji. Natoa mfano mmoja; wakati wa uchaguzi watu wengi sana wanakamatwa na wanapelekwa Mahakamani. Kadhia inayotokea ni kwamba, watu wanaokamatwa ni wa vyama vya upinzani. Sasa nauliza, hawa watu wa CCM ni Malaika? Hawafanyi makosa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli jambo hili siyo sahihi kwa wananchi wote. Watu wanauawa, watu wanapigwa wakati wa uchaguzi. Suala la Utawala Bora linatakiwa lifanye kazi yake, kuwe na mizani sawa, isiwe huku ni hivi na huku ni hivi, hasa hili suala la kwamba sisi upande wa Zanzibar tunakuwa na vikosi vingi sana. Juzi Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi amesema kwamba, Jeshi linalinda mipaka, lakini wakati wa uchaguzi, hasa kwenye Jimbo langu la Konde, wanakuwepo. Sasa sijui wanakuja kwa mantiki gani? Ni mpaka au wanalinda uchaguzi? Jambo hili liwekwe sawa. Kama huku wanaolinda ni Polisi na sisi kule tusimamiwe na Polisi. Isiwe kwamba, hapa kuna kikosi kimoja, kule kuna vikosi 70, jambo hili siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ikitokea mtu ameuawa, wanaambiana aah, siyo Polisi, siyo Jeshi, siyo KMKM. Sasa tunashindwa kuelewa. Jambo hili ni lazima Serikali ibebe lawama na ituwekee mfumo kamili ambao utatufanya sisi Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla tusione kwamba uchaguzi ni balaa. Ninavyosema sasa hivi wananchi wa Tanzania wamevunjika moyo wa kuingia kwenye uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mfanye tathmini, mtaona watu ambao wanajiandikisha kwa uchaguzi kama itafikia ile asilimia ambayo ilitokea mwaka wa kwanza ule wa 1995 na 2000. Naomba mfanye tathmini hiyo halafu mje mlieleze Bunge hapa, kwa sababu watu wamekosa imani na Serikali juu ya usimamizi wa uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye suala lingine la hawa wanaomtukana Mheshimiwa Rais. Kwa kweli jambo hili mimi binafsi nalichukia sana. Ningetamani sana sasa hivi ningesikia kwamba kuna hatua ambazo zimechukuliwa kwa watu hawa. Kwa sababu huyu ni Rais wetu wote, huyu ni mama wa watu, ukimtukana Rais umetutukana sote. Sasa sisi tunashangaa mtu anatokea huko kwenye mitandao anamtukana Rais, halafu hatuoni hatua ambazo zinachukuliwa. Kwa kweli jambo hili siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie wazi, mimi ni mpenzi mkubwa wa Mheshimiwa Rais na kama chama changu hakitasimamisha mgombea na hakuna maelekezo, basi nampa kura yangu Mheshimiwa Rais. Pamoja na kwamba CCM siipendi, lakini nitampa kura Mheshimiwa Rais kwa sababu anafanya kazi nzuri, anawatumikia Watanzania. Mambo aliyofanya sasa hivi sijaona Rais yeyote ambaye amefanya. Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili lililotokea, napeleka lawama kwa kijana wa CCM, Mwenyekiti wa UVCCM kule Kagera. Kwa kweli matamshi aliyoyasema kama utawala bora upo, ningetamani awe ameshachukuliwa hatua. Ni jambo la kufurahisha Katibu Mkuu wa CCM amelitolea maelekezo jambo hiliā¦
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimjibu mwongeaji na nimpe taarifa kwamba Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi amelikemea, huo ni uzembe wa kijana mwenyewe na siyo wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Taarifa hiyo.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa naelezea hivyo hivyo, kwamba tunamshukuru Mheshimiwa Katibu Mkuu wa CCM kwa kulikemea jambo hili. Sasa ilikuwa ni nafasi ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuchukua hatua. Kwanza wameshapata kibali kwamba hakuna mkubwa. Maana yake tunajua Serikali ya CCM ndiyo inatawala. Sasa kama kuna hofu kidogo, basi hofu ya nini tena hapa?
Mheshimiwa Naibu Spika, huyu kijana ni wa kuchukuliwa hatua tukaona mfano, kwa sababu mambo haya haya ndiyo yanamchafua Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa, amewatoa watu magerezani, amewasaidia matibabu. Sasa leo huyu anakuja kutamka maneno haya. Huyu ni mtu ambaye inatakiwa alaaniwe katika nchi hii na achukuliwe hatua. Nakushukuru. (Makofi)