Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai ambayo ameniwezesha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu leo kuweza kuzungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa mambo mema anayolifanyia Taifa letu. Kama sijakosea hesabu zangu sawasawa, leo ninapozungumza, amesafiri angani masaa 402, akienda huku na kule kutafutia riziki Watanzania na kuiunganisha Tanzania na nchi za nje katika kutengeneza mahusiano. Hakika anafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Buchosa, nasimama hapa kumpongeza sana Rais wangu kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa wanaoelewa maana ya kusafiri kwa ndege masaa yote hayo angani ni jambo linalochosha sana, lakini hivi ninavyoongea, anatarajia kurejea nchini kutoka Uturuki. Kwa hiyo, nina kila sababu ya kumpongeza Rais wangu kwa kazi njema anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu. Pia nampongeze sana Spika wetu wa Bunge kwa mambo mema na anavyotuwakilisha kila kona ya dunia. Ametuletea heshima kubwa sana. Mara kwa mara huwa namwambia binti yangu, anasema yeye ni role model wake. Kwa hiyo, kama mwanangu anaangalia hivi sasa, basi ajue ya kwamba anatakiwa awe kama Spika. Nitakuwa mzazi mwenye kujivunia sana nikiwa na mtoto kama yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nina mambo mawili tu leo na ninaomba niongee kwa utaratibu na nimemwomba Mungu anisaidie niweze kueleweka. La kwanza ni upande wa wafanyakazi wa nchi hii kwa sababu leo tunajadili Bajeti ya Utumishi, na la pili ni suala la rushwa na ufisadi katika Taifa letu kwa sababu tunazungumzia watu wa TAKUKURU.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la TAKUKURU, muda ukitosha kule mbele nitakuja kwenye suala la watumishi, maana limeshaongelewa na watu wengi. Nilisimama hapa wakati fulani akiwa anawasilisha rafiki yangu Mheshimiwa Ndumbaro akiwa Waziri wa Sheria, nikazungumza juu ya TAKUKURU ambao wanafanya kazi kubwa sana. Kazi yao ni njema, nimesoma ripoti leo ya Transparency International, wamepanda kidogo kutoka nafasi ya 38 mpaka nafasi ya 40.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi duniani TAKUKURU ina nafasi ya 87 kwenye ubora wa kujiepusha na masuala ya rushwa. Kwa kweli nina kila sababu ya kuwapongeza. Katika Afrika Mashariki, Tanzania ni nchi ya pili ikiongozwa na Rwanda. Kwa hiyo nataka niwapongeze sana TAKUKURU kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, leo nina jambo linaloitwa Security of Tenure. Nilizungumza mara ya mwisho hapa nikasema, tunahitaji kum-protect, tunahitaji kumkinga Mkurugenzi wa TAKUKURU kwa maana ya Security of Tenure. Jambo hili linafanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulinda ajira yake, ajira ya Majaji na ajira ya CAG, kwamba ukishamteua CAG huwezi kumwondoa, labda kuwe na sababu ambayo imetajwa katika Katiba. Hata Rais akimteua CAG hawezi kumwondoa tu hivi akaamka asubuhi akaamua kumtoa. Kwa nini waliamua kufanya hivyo kwa CAG? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yao ilikuwa ni kumpa uhuru (Independence) wa kufanya kazi yake bila kuingiliwa. Ndiyo ilikuwa sababu tumpe nafasi, tuilinde ajira yake. Ukimteua leo, huwezi kumtoa kesho asubuhi. Kuna mchakato mrefu sana mpaka utengeneze tribunal ndiyo uweze kumwondoa na ushauriwe kama Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini jambo hili halifanyiki kwa Mkurugenzi wa TAKUKURU? Nataka Mheshimiwa Waziri ukija hapa unijibu, kwa nini hutaki kum-protect Mkurugenzi wa TAKUKURU? Kwa nini Wabunge hatuitishi sheria ije hapa Bungeni tuweze kufanya marekebisho ya sheria tuweze kum-protect? Kwa nini ni muhimu kum-protect? Kwa nini ni muhimu kulinda ajira ya Mkurugenzi wa TAKUKURU? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano, umemkamata leo mtu kwenye halmashauri yako, amekuja CAG amekagua ambaye ana-deal na wanasheria, halafu unamwita mtu wa TAKUKURU amkamate akamhoji amfikishe Mahakamani. CAG ana protection analindwa, akishatoka pale huyu mtu anakabidhiwa kwa mtu ambaye halindwi na sheria ambaye ni Mkurugenzi wa TAKUKURU.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uwezekano na simaanishi katika nchi yangu, kuna uwezekano katika nchi nyingine wakubwa au watu wenye ushawishi kupiga simu na kumwambia achana na hiyo kesi, lakini huwezi kumwambia hivyo CAG kwa sababu analindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni rahisi sana kumpigia Mkurugenzi wa TAKUKURU na kumwambia achana na hiyo kesi. Mkubwa ametuma ki-memo kimekuja, anatetemeka, anakuwa na hofu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nani asiyependa maisha mazuri? Ukishateuliwa tu Mkurugenzi wa TAKURURU, heshima inaanza siku ile ile, Land Cruiser V8, ofisi nzuri mpaka mjukuu wako kijijini anaitwa huyu ni mjukuu wa Mkurugenzi wa TAKUKURU. Nani yuko tayari kupoteza hadhi hiyo? Ikija memo mtu anasema aah, bwana ee, bora mimi nibaki na familia yangu. Ndiyo maana nasema kama CAG ambaye anafanya kazi similar kabisa na anayofanya Mkurugenzi wa TAKUKURU, ni lazima tum-protect, ni lazima tuilinde ajira yake kwa sheria na kwa Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili siyo geni. Nitakusomea hapa baadhi ya nchi ambazo zimefanya hivyo. Kabla sijasoma hizo nchi nikusomee Azimio la Umoja wa Mataifa Ibara ya 6 ambayo imetamka katika Ibara ya 6 (2) inasema; “Each state shall grant the body or bodies referred to in paragraph one of this article the necessary independence, in accordance with fundamental principles of its legal system, to enable the body or bodies to carry out its or their functions effectively and free from any undue influence.” Umoja wa Mataifa wamesema, kuwe na chombo ambacho kinalindwa na sheria ambacho ni TAKUKURU, ifanye kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuachane na Umoja wa Mataifa, twende moja kwa moja Ghana. Ghana sheria yao Kifungu cha 4 na 5 wametamka hivi, “The procedure for removal of commissioner and deputy commissioners shall be the same as that provided for the removal of a Justice of the Court of Appeal and a Justice of the High Court respectively.” Ghana wamesema kumwondoa Mkurugenzi wa TAKUKURU iwe sawasawa na mchakato ule wa kumwondoa Jaji. Hao ni Ghana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Seychelles sheria yao inatamka hivyo hivyo. Senegal sheria yao inatakamka hivyo, kwamba kumwondoa Mkurugenzi wa TAKUKURU iwe ni mchakato mrefu. Kwa nini wanamlinda? Ili asiingliwe na mwenye mamlaka ili asiingiliwe na wenye ushawishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huko kote ni mbali, hebu twende kwa jirani zetu Zanzibar. Naomba univumilie kidogo. Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria yao inatamka katika article ya 5 Kifungu cha 5, mimi siyo Mwanasheria, najua kupita pita kidogo inasema, “In order to protect the integrity and independence of the authority, the Director General shall not be removed…”

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudie. “…shall not be removed from office, except for reasons and procedures laid down for the removal of the High Court Judge according to the article 95 of the constitution.” Hapo ni Zanzibar, ni sehemu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo sawa kutokum-protect Mkurugenzi wa TAKUKURU, ni kama vile tumejitengenezea kamlango kwamba tunabana hapa kwa CAG halafu tukibanwa sana tunaenda tunachomokea kwa Mkurugenzi wa TAKUKURU, haitakiwi, haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nawaomba, tumeaminiwa na Watanzania na wizi, ubadhirifu, rushwa zimechelewesha maendeleo ya Taifa letu, zimechelewesha maendeleo ya Afrika. Tuhakikisheni tunapambana na adui rushwa kwa nguvu zote na tuanze na sheria. Kazi yetu sisi Wabunge tumeletwa hapa kutunga sheria na kuishauri Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sheria hii irejeshwe na sisi tuweke kipengele kama walichoweka ndugu zetu wa Zanzibar ili tum-protect Mkurugenzi wa TAKUKURU.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili. Maneno yako mengine ni ya muhimu yaandike mpe Waziri sasa hivi.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)