Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ally Mohamed Kassinge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii jioni hii ili nami nichangie Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora ambayo inaongozwa na Waziri nguli, kaka yangu, bosi wangu wa kipindi hicho akiwa TAMISEMI, mwanasheria msomi kabisa Mheshimiwa Boniface Simbachawene, pembeni yake akisaidiwa na wakili msomi, mjomba wangu Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani mamlaka haijafanya makosa kuwaweka wanasheria wote wawili katika Wizara hii. Tunapozungumzia utumishi wa umma na utawala bora, tafsiri yake ni kwamba tutaongozwa mahususi kabisa na Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 na kanuni zake za mwaka 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutaongozwa na sheria, ninaamini kabisa Mheshimiwa Rais aliona kwamba Mawaziri wawili hawa; Mheshimiwa Simbachawene na Mheshimiwa Kikwete wataweza kusimamia vyema sheria zinazoongoza Wizara na zinazoongoza utumishi wa umma katika Tanzania hii ili watumishi wa umma wapate haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, eneo langu la kwanza la uchangiaji niwakumbushe Wizara majukumu makubwa matatu ya uteuzi; ajira pamoja na nidhamu. Mamlaka za uteuzi, mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu wakati mwingine zinafanya kazi kwa kuingiliana, lakini wakati mwingine zinafanya kazi kila moja kwa nafasi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili, naomba niweke wazi kabisa kwamba mtumishi wa umma anapoajiriwa, mamlaka yake ya ajira ndiyo inayotakiwa isimamie taratibu zake zote kuanzia kuajiriwa kwake, kuendelezwa kwake, haki zake, mpaka kustaafu. Hiyo haina mjadala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma sura 298, ndani yake zipo mamlaka za nidhamu na mamlaka za ajira. Inatokea wakati mwingine kwa bahati njema kwa baadhi ya watumishi wanaofikia katika principal levels, wakati wengine hata katika senior levels za vyeo vyao wanapata bahati ya kuonwa na mamlaka za uteuzi wakateuliwa kwenye nafasi mbalimbali kutumikia utumishi wa umma, kwa nafasi kama vile Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri au Mamlaka za Serikali za Mitaa, Makatibu Tawala wa Wilaya na kadhalika na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inapotokea mamlaka ya uteuzi ambapo katika hizo nilizozitaja nyingi katika hizo mamlaka zake za uteuzi ni Mheshimiwa Rais, zimeteua hao watu ambao wametoka katika utumishi wa umma wakatumikia hizo nafasi, utumishi wao wa umma unabaki pale pale na stahiki zao na haki zao zipo vilevile, haziwezi kubadilishwa kwa namna yeyote ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ni bahati mbaya sana na ni masikitiko makubwa kwamba mamlaka za uteuzi, na hapa niseme tu Mheshimiwa Rais inapotokea kwamba anatengua nafasi za uteuzi za watumishi hawa walioteuliwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, imekuwa na kizungumkuti kwa kuhakikisha kwamba wanalinda ajira za watumishi hawa kuanzia mwanzo. Hii ni changamoto kubwa. Imeonekana mtumishi wa umma anapoteuliwa kushika nafasi za uteuzi na baadaye mamlaka ikatengua, ni kana kwamba ameadhibiwa na hana haki nyingine yeyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuishukuru Serikali, tumelipigia kelele hili kwa uchache wameliona, wale wote ambao waliteuliwa na wakatenguliwa walirudishwa kazini, lakini nitoe ushauri kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ipitie database, bado wapo. Wengine imefikia hatua wanakaa pending baada ya kutenguliwa kwao zaidi ya mwaka mmoja, miaka miwili mpaka wanakwenda kutafuta haki zao Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifano tunayo na ndiyo maana tunasema kwamba bado wapo, na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ikapitie hizi database. Haipendezi mtumishi wa umma ambaye anaajiriwa kwa Sheria za Utumishi wa Umma ana haki zote halafu akatafute haki Mahakamani, haipendezi. Hilo ni eneo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni maslahi ya watumishi kuendana na majukumu yao. Hapa kwa upekee wake nakusudia kuzungumzia walimu. Kwa muktadha wa mchango wangu nakusudia kuzungumzia walimu wale ambao wapo chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa maana ya walimu wa shule za msingi na walimu wa sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, tungekuwa tunaangalia maslahi ya utumishi kwa mujibu wa majukumu yao, nadhani walimu wangekumbukwa kama wanavyokumbukwa watumishi wengine. Imekuwa bahati mbaya sana kwamba watumishi wa kada ya ualimu kwa kiwango kikubwa wanakuwa wakiishi kwa mishahara tu, wanategemea mishahara pekee ambayo mwisho wa ajira yake ndiyo unakuja ule mzigo au msalaba ule wa kikokotoo. Hii kidogo inasikitisha kwa kada ya ualimu ilhali wa kada nyingine wanapata maslahi ya kujikimu ili siku ziende. Wapo watumishi ambao wanapata Rational Allowance, wapo watumishi ambao wanapata Responsibility Allowance, On Call Allowance na allowance kama hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe kwa unyenyekevu mkubwa sana Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, tufanye kitu kinachoitwa job analysis kwa mwalimu, tuchanganue majukumu ya mwalimu. Mwalimu ana jukumu la kufundisha, lakini katika kufundisha huku kabla ya kuingia darasani ana jukumu la kuandaa Mpango Kazi wa Mwaka na wa Muhula; ana jukumu la kuandaa utaratibu wa kufundisha darasa hilo kwa siku hiyo ya kipindi husika ambayo ndiyo Lesson Plan. Pia kuna document zingine kadhaa za mapitio kwa mwalimu kama vile Class Journal, Log Book, anapitia text books, reference books, Kiongozi cha Mwalimu, kuandaa teaching aid na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiondoa majukumu ya msingi haya ya ufundishaji, Mwalimu pia amekuwa na majukumu mengine ya ziada ambayo naweza nikasema yamekuwa ni makubwa pengine hata kuliko kufundisha kwenyewe. Mwalimu anakuwa ni Mwalimu Mkuu. Mwalimu Mkuu tu peke yake ni jukumu tosha. Mwalimu anakuwa Mwalimu wa Zamu. Kusimamia zamu ni jukumu tosha. Mwalimu anakuwa Mwalimu wa Darasa, kusimamia darasa siyo mchezo. Mwalimu anakuwa Mwalimu wa Malezi, Mwalimu anakuwa Mwalimu wa Michezo. Kama ingekuwa walimu hawakufanya vyema katika kusimamia sekta ya michezo tangu shuleni, leo hii tusingewapata wachezaji mahiri tunaowategemea katika timu zetu. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Mzamiru Yassin, Bakari Nondo Mwamnyeto, Fei Feisal Salum (Fei Toto); hawa wote wamekuwa wachezaji wanaotegemewa na timu zetu tunazozitegemea kwa sababu waliandaliwa vizuri tangu shuleni. Hayo ni majukumu ya walimu. Mwalimu amekuwa mwalimu wa uzalishaji; wote tumefundishwa hapa tulio wengi kwa umri wangu huu na wengi nikiwaangalia hapa tumefundishwa uzalishaji mali shuleni. Kwa hiyo, kwa ujumla wake Taifa lililopo sasa na Taifa lijalo ni matokeo ya kazi ya walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wanasimamia mpaka miradi. Wamekuwa na jukumu la kuwa wahandisi, wamekuwa na jukumu la kuwa mameneja; ni mzigo mkubwa kwa walimu. Sasa mimi naikumbusha Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Utawala Bora na Utumishi wa Umma, kwamba hebu wafanye job analysis ya majukumu ya mwalimu na baadaye waje na kitu kinachoitwa teaching allowance kwa walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili kama sitapata maelezo ya mkakati wa Serikali kujiandaa na teaching allowance kwa walimu, nitakamata shilingi ya bosi wangu wa zamani Mheshimiwa Simbachawene. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nizungumzie kwa uchache sana kuhusu kikokotoo. Walimu hawakihitaji kikokotoo, na ndiyo kwanza wakati kimeanza walikuwa tayari kustaafu kwa hiari wakiwa na miaka 55 kwa kuchelea kikokotoo. Wengi walistaafu na miaka 55 wakati kinaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumza hayo naunga mkono hoja. (Makofi)