Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, utangulizi. Nichukue nafasi hii kuwapongeza watumishi wote wa umma wanaokadiriwa kufikia 1,000,000 kote nchini wakiongozwa na mtumishi wa umma namba moja, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna mnavyojitoa kuhudumia wananchi usiku na mchana pamoja na changamoto nyingi mnazozipitia, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa na kutangaza ajira mpya katika kada mbalimbali ambapo inatibu tatizo la upungufu wa watumishi, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kutoa ajira kwa vijana wetu nchini wakiwemo vijana wangu wa Jimbo la Kisesa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunajadili hotuba ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2024/2025, Wizara ambayo ni engine ya utekelezaji wa shughuli zote za Serikali na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na umuhimu huo, ni vyema kufahamu dhana ya utumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, utumishi wa umma ni mfumo wa kiutawala na kimenejimenti uliokabidhiwa jukumu la kuhakikisha kuwa jamii inapata huduma inayokusudiwa kutoka kwa Serikali yao au taasisi yoyote kwa niaba ya Serikali kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili watumishi wa umma waweze kutoa huduma bora kwa wananchi, ni lazima kuwepo mazingira wezeshi katika kutekeleza jukumu hilo muhimu, lakini pia wazingatie misingi na nguzo za utawala bora ambazo ni uwazi (transparency) ambapo shughuli za umma huendeshwa kwa uwazi bila siri na kificho ili wananchi wawe na uwezo wa kupima utendaji na uzingatiaji wa kanuni, taratibu na sheria, uwajibikaji (accountability) ambapo kiongozi na mtendaji huwa tayari kujibu, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi au matendo aliyoyafanya katika kutekeleza dhamana aliyopewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, misingi mingine ni pamoja na utawala wa sheria (rule of law), ushirikishwaji (participation), usawa (equity), ufanisi na tija (effectiveness and efficiency), mwitikio (responsiveness), maridhiano (reconciliation) na uadilifu (integrity).

Mheshimiwa Naibu Spika, nguzo za utawala bora ni katiba, utawala wa sheria, uhuru wa mahakama, uhuru wa habari na vyombo vya habari, mgawanyo wa madaraka, kulinda na kuheshimu haki za binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yoyote duniani isipozingatia nguzo na misingi ya utawala bora, hutokea athari kubwa ikiwemo matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, kuongezeka kwa umasikini, ujinga na maradhi, kuongezeka kwa rushwa, huduma mbovu za jamii, kutoheshimiwa haki za binadamu na kuongezeka kwa dhuluma na uonevu.

Mheshimiwa Naibu Soika, kama Taifa ni lazima tujipime je, tunafuata na kutekeleza misingi ya utawala bora au tumebakiza kuuzungumza kwa nadharia tu, huku tunazisigina nguzo na misingi ya utawala bora?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Tanzania kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa ya uwazi na uwajibikaji, lakini utekelezaji wa dhana ya utawala bora katika nchi yetu umeshuka na unatishia ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie changamoto za utekelezaji wa mifumo ya utumishi na dhana ya utawala bora. Ukisoma Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Sura ya Sita ukurasa wa 161 mpaka 169, ukipitia utekelezaji wa shughuli za Serikali katika maeneo mbalimbali na baadhi ya matukio yanayoendelea nchini, utabaini kuwa nchi yetu kwa sehemu kubwa ilishaacha nguzo na misingi ya utawala bora, kwani kuvunja katiba, sera, sheria, kanuni na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu imekuwa ni jambo la kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiukwaji huu unafanyika kwa makusudi ili kufanikisha maslahi binafsi ikiwemo wizi, rushwa na ufisadi, uonevu na dhuluma kwa wananchi. Kama Taifa ni lazima tuitathmini upya mifumo ya utumishi wa umma na utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tusikubali mambo haya yaendelee, kwani yanaweza kuua Taifa letu kutoka kuwa Taifa lililostawi hadi kwenda kuwa Taifa lililoanguka (failed state). Hii ni vita kubwa, lakini ninaamini tutaishinda endapo kama Taifa tutaendelea kuunganisha nguvu kwa pamoja na kuviangamiza vyanzo vyote vinavyotishia uhai wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naib Spika, nakumbuka Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere siku alipokuwa akitangaza vita vya kupambana na uvamizi wa majeshi ya Nduli Idd Amini tarehe 02 Novemba, 1978 alisema na nanukuu; “...tunayo kazi moja tu, Watanzania sasa, ni kumpiga (Nduli Idi Amini), uwezo wa kumpiga tunao, sababu ya kumpiga tunayo na nia ya kumpiga tunayo. Tunataka dunia ituelewe, hivyo kwamba hatuna kazi nyingine, na tunawaomba marafiki zetu wanaotuambia maneno ya suluhu waache maneno hayo…” Mwisho wa kunukuu kauli ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ilishapitia mitihani na vita nyingi na kuzishinda. Hivyo hatuwezi kushindwa kubadili hii mifumo ili kurejesha heshima na uadilifu katika Taifa. Binafsi ninayo ndoto kuwa siku kasoro hizi zikitatuliwa, nchi yetu itaingia kwenye mageuzi makubwa ya uchumi na maendeleo. Katika kuweka msingi wa hoja yangu kuhusu changamoto ya mifumo ya utumishi na utekelezaji wa dhana ya utawala bora, nitatolea mifano katika maeneo nane kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni maslahi duni ya watumishi wa umma, mishahara midogo, madeni ya uhamisho na likizo, kutokulipwa kwa wakati masurufu ya kazi na safari ni mambo ambayo yanawaumiza sana watumishi wetu wa umma hali inayopelekea kukosa morali ya kazi na kutoa huduma duni kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kujiuliza, kama uchumi wetu unakua, mapato yanaongezeka, bajeti zinatengwa kila mwaka, je, kuna sababu gani ya kushindwa kuwalipa mishahara mizuri na kuwalipa stahiki zao kwa wakati? Mfumko mkubwa wa bei za bidhaa na chakula uliobuka miaka ya hivi karibuni umepelekea ugumu wa maisha kwa watumishi wetu wa umma hasa wale wa kada za chini za Ualimu, Uuguzi, Uganga, vyombo vya ulinzi na usalama, Watendaji wa Vijiji na Kata, Maafisa Misitu, Maafisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Madereva, Wahudumu, Walinzi na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwango cha mishahara wanayolipwa watumishi wetu hakitoshi, kwani bei ya nishati ya mafuta, chakula, nauli na bidhaa nyingine muhimu zimepanda bei maradufu na kuwafanya washindwe kukidhi kupata mahitaji muhimu. Baadhi yao kutumbukia kwenye mzigo mkubwa wa madeni ya mikopo ikiwemo kausha damu, hali inayopelekea kuwaondolea ari na utulivu wa kufanya kazi za kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya changamoto hizi kubwa za watumishi wa umma, lakini Waziri wa Utumishi ameshindwa kueleza chochote juu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kutatua changamoto za watumishi. Hivyo basi, Bunge lichukue nafasi yake ili ikawe mwisho kwa watumishi wa umma kudhalilika na kunyanyasika katika Taifa lao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni kuhusu kikotoo cha mafao kwa watumishi wa umma. Tangu Serikali itangaze kuanza kwa matumizi ya kikotoo kipya, kumeibuka manung’uniko na malalamiko makubwa kwa watumishi wa umma. Pia nimesikia michango ya Waheshimiwa Wabunge wakilalamikia kikotoo kipya mara kwa mara hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kama Bunge tuamue leo na kama Serikali itaendelea na msimamo wake wa kung’ang’ania hiki kikotoo kipya kinacholalamikiwa na watumishi, ikifika wakati wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa kupiga kura ya Ndiyo na Hapana, Wabunge wote tutoke nje ya Ukumbi wa Bunge tumwachie Waziri Mkuu na Mawaziri peke yao wapitishe bajeti ya Serikali ili Bunge hili Tukufu lisiingie kwenye dhambi ya kuwaangamiza watumishi wetu wa umma nchini wanaofanya kazi usiku na mchana na kwa uadilifu na uzalendo wa hali ya juu.

Tatu ni kuhusu mkanganyiko wa mifumo ya utumishi wa umma. Hivi sasa mfumo tulionao unaruhusu kuwepo mgongano wa kiutawala kutokana na kuwepo kwa mifumo sambamba ya kiutawala (parallel system) ambapo anakosekana nani mkubwa? Nani anayepaswa kumwagiza mwenzake?

Mheshimiwa Naibu Spika, kukosekana kwa mgawanyo sahihi wa majukumu (clear separation of power) na kusababisha kuingiliana katika utendaji na kusababisha viongozi na watendaji wa Serikali kutumia muda mwingi kulumbana na kugombana kila uchao, badala ya kutekeleza majukumu ya umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ajira na uteuzi wa baadhi ya nafasi hufanyika bila ushindani, hali inayopelekea kupata viongozi na watendaji wasiokuwa na uwezo wa kumudu majukumu yao na ndiyo maana tunashuhudia teuzi na tenguzi kila mara. Mheshimiwa Rais amepewa kazi ngumu ya kuhangaika na teuzi za kila siku na kusoma CVs za watu huku akipokea mashinikizo kutoka kwa ma-godfather wa watu wanaowania teuzi mbalimbali Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo pia ni rahisi kundi fulani la watu kutengeneza utawala wenye mrengo fulani (empire). Utaratibu wa upekuzi (vetting) unaotumika hivi sasa hauwezi kuhakikishia kutokuwepo kwa upendeleo na upatikanaji wa viongozi bora. Pia siyo rahisi kuwatendea haki Watanzania zaidi ya milioni 60 wenye ujuzi na taaluma mbalimbali kupitia utaratibu wa vetting.
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi sioni sababu ya kwa nini tuendelee kuwapata kwa njia ya uteuzi badala ya ushindani Mawaziri, Makatibu wa Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Bodi za Mashirika ya Umma na Wakurugenzi wa Mashirika na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa utumishi tulionao sasa ni rahisi kuwabeba watumishi wazembe na wasio waadilifu ambapo badala ya kuadhibiwa huishia kubadilishiwa vituo na kulipwa gharama za uhamisho. Pale inapotokea wametenguliwa katika nafasi zao za uteuzi, huendelea kulipwa mshahara huo huo hali iliyopelekea daftari la mshahara la Serikali (payroll) kuzidiwa na uzito wa malipo yanayojirudia na kuliingiza Taifa kwenye hasara kubwa. Wengine wanapokea mishahara mikubwa kuliko hata ya mabosi zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado hatujasahau kipindi cha mwaka 2016 tulibaini kuwepo kwa ajira za watumishi wenye vyeti fake 15,508 na watumishi hewa 19,708 ajira zilizokuwa zinaligharimu Taifa shilingi bilioni 19.8 kila mwezi. Pia mfumo wa utumishi unaruhusu kuajiri watumishi wasio raia wa Tanzania hali inayopelekea kukosekana kwa uzalendo, kuziba nafasi za Watanzania wenye sifa stahiki na kuhatarisha usalama wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Taarifa ya CAG ya mwaka 2022/2023 inaonesha kuwa kupitia mfumo huu huu wa utumishi, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wameweza kuajiri watumishi sita bila tangazo na bila kufanya usaili wa ushindani na watumishi hao hawajulikani walipatikanaje hadi kuajiriwa na shirika hilo la umma na huu ni mfano mmoja tu ya yanayoendelea katika ajira za watumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna watumishi 190 kwenye taasisi mbalimbali za Serikali wanaokaimu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka miwili hadi sita, jambo ambalo ni kinyume na Kanuni za Utumishi wa Umma na inashusha ufanisi wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne ni kuhusu kutokutolewa taarifa kamili ya kifo cha Rais Magufuli. Baada ya kusikiliza kwa kina maelezo ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo aliyoyatoa tarehe 16 Machi, 2024 nimeshawishika na ninalishauri Bunge kukubali iundwe Tume Huru ya kuchunguza utata wa kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ili kumtendea haki Hayati Magufuli na watu wengine wanaohusishwa kwa mema au kwa ubaya kuhusiana na kifo hicho. Pia tume hiyo itabaini watu waliokataa kuapishwa kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati lilikuwa ni takwa la kikatiba.

Tano ni kuhusu kupuuzwa maagizo ya viongozi. Tumekuwa tukishuhudia kushuka kwa nidhamu na uwajibikaji Serikalini kiasi kwamba baadhi ya viongozi na watumishi wa umma wamekuwa wakikaidi hata maagizo ya viongozi wa juu.

(i) Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitangaza uamuzi wa kujiuzulu nafasi yake ya Makamu wa Rais ifikapo Juni, 2024 endapo mradi wa maji wa Same – Mwanga - Korogwe hautakamilika kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia. Mradi huo umechelewa na sasa ni zaidi ya miaka kumi, pamoja na Makamu wa Rais kufedheheshwa na kuamua kutangaza kuacha kazi, lakini hatujasikia hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi na viongozi waliosababisha mradi huo kuchelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa tusikubali viongozi wetu wakafikishwa hapo na baadhi ya watumishi wa umma wasiowajibika katika nafasi zao kwani kila mtu abebe msalaba wake, lakini pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango kwa kuweka wazi msimamo wake na kuwa mfano bora wa uwajibikaji.

(ii) Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa akifanya majukumu mengi ya huku na kule (multitasking ambassador) lakini amekuwa akitoa maagizo ambayo kwa sehemu kubwa hayatekelezwi na watendaji wa Serikali walio chini yake, mfano maagizo 12 aliyoyatoa hapa Bungeni tarehe 27 Aprili, 2023 ya kupiga marufuku kukamata wananchi na mifugo kiholela bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maagizo 12 ya Waziri Mkuu yalipuuzwa na Mawaziri na watendaji wa sekta husika, kwani licha ya kupiga marufuku operation hizo ambazo hazizingatii sheria, kanuni na taratibu na pia kuwepo ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, operation hizo ziliendelea na kuleta madhara makubwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kuwa tarehe 3 Mei, 2023 nikiwa Bungeni nililalamikia watendaji wa Mamlaka za Uhifadhi kupuuza maagizo ya Waziri Mkuu ambapo Mheshimiwa Spika Dkt. Tulia Ackson alinitaka kuleta ushahidi kuthibitisha madai yangu niliyoyatoa Bungeni kuhusu kupuuzwa kwa maagizo ya Waziri Mkuu ndani ya siku saba, kazi ambayo niliifanya na kukabidhi vielelezo na nyaraka zote kwa wakati kama ilivyoagizwa. (Kiambatisho Na. 1)

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 28 Juni, 2023 Spika wa Bunge, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson wakati wa kuhitimisha Bunge la Bajeti la mwaka 2023/2024 alitoa maamuzi na kukiri kuwa Mheshimiwa Mpina alikuwa sahihi, kwani ni kweli kuwa maagizo 12 aliyotoa Waziri Mkuu kuhusu migogoro baina ya wananchi na maeneo ya hifadhi aliyoyatoa Bungeni tarehe 27 Aprili, 2023 yalikuwa yamepuuzwa. (Kiambatisho Na. 2 na Kiambatisho Na. 3).

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo tangu tarehe 27 Aprili, 2023 na hadi nilipolalamika Bungeni tarehe 3 Mei, 2023 wiki moja baadaye operation ziliendelea na hata baada ya Mwongozo wa Spika wa tarehe 28 Juni, 2023 na hadi leo Aprili, 2024, mwaka mzima sasa operation zinafanyika bila kuwashirikisha wananchi na viongozi wa maeneo husika, wananchi kupigwa, kuteswa, kujeruhiwa, kusababishiwa ulemavu wa kudumu na kuuawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wananchi hupigwa faini kinyume cha sheria, wananchi huvamiwa na kuharibiwa mazao yao na kunyang’anywa mifugo, mifugo kukamatwa na kuuzwa kiholela, mifugo kukosa matunzo na kufa ikiwa imeshikiliwa hifadhini na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushahidi wa kamatakamata isiyozingatia sheria inaendelea na licha ya mimi kutoa vielelezo vya kujitosheleza vilivyothibitishwa na Ofisi ya Bunge kama nilivyotakiwa na Spika wa Bunge, lakini hadi leo hatujaona hatua zozote mahususi zikichukuliwa na badala yake dhuluma na mauaji yanaendelea kwa wananchi wetu katika maeneo mbalimbali ya nchi. Mfano Meatu, Mbarali, Ngorongoro, Tarime, Kaliua na kadhalika hadi leo Wabunge wengi bado wanalalamikia operation hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisikiliza vizuri mchango wa Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mara na Mheshimiwa Emmanuel Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, michango ambayo iliugusa moyo wangu na kutokwa na machozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulitegemea kuwa baada ya maagizo 12 ya Waziri Mkuu kupuuzwa, mambo mawili yangefanyika. Mawaziri na Watendaji wa Serikali waliopuuza maagizo ya Waziri Mkuu wangekuwa wameshafukuzwa kazi na kuchukuliwa hatua kali za kisheria au Waziri Mkuu mwenyewe angekuwa alishajiuzulu kwa kushindwa kumudu majukumu ya Uwaziri Mkuu kama anavyotakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 51(3)(e) kuhusu ukomo wa kushika madaraka ya nafasi ya Waziri Mkuu na Ibara ya 52 kuhusu kazi na mamlaka ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika dhana ya utawala bora haiwezekani akakosekana mtu wa kuwajibika, leo damu za wananchi zinazoendelea kumwagika, mateso ambayo wananchi wanayapata kuishi kama wakimbizi kwenye nchi yao, dhuluma na uonevu unaoendelea, haiwezi kuwaacha salama wahusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya uwajibikaji ipo duniani kote na siyo jambo geni katika nchi yetu na tunayo mifano mingi ya viongozi waliowajibika kwa tuhuma mbalimbali. Tunakumbuka Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alijiuzulu kwa makosa yaliyofanywa na watendaji walio chini yake na kumwandikia barua Rais wa wakati huo Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye aliridhia kujiuzulu kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hayati Edward Ngoyai Lowassa, akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania alijiuzulu nafasi yake kwa tuhuma tu. Pia Dkt. Emmanuel Nchimbi, akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye leo ni Katibu Mkuu wa CCM na Mawaziri wenzake sita walijiuzulu nyadhifa zao kwa madhila yaliyotokana na operation Tokomeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa George Simbachawene ambaye leo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora alijiuzulu nafasi yake ya Waziri wa TAMISEMI baada ya kutuhumiwa kwenye mikataba ya madini kipindi alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini. Hapa pia Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameonesha njia kuwa huwezi kuendelea kuwepo kwenye nafasi ambayo huwezi kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko Uingereza nako aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair alijiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu baada ya kubainika kuwa sababu za kuivamia na kuipiga Iraq (Casus belli) hazikuwa na ukweli, kwani nchi hiyo haikuwa inamiliki silaha za maangamizi (WMD Trinity) kama ilivyokuwa imeelezwa awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sita ni kuhusu kutowiana kwa taarifa za uchunguzi na taarifa za ukaguzi. Kumekuwepo kwa kukinzana kwa Taarifa za Uchunguzi na Ripoti za Ukaguzi. Taarifa za uchunguzi zinazotolewa na TAKUKURU, DCI na DPP zimekuwa haziakisi Ripoti za Wakaguzi za CAG, PPRA, FIU, IAG na Mbio za Mwenge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia Ripoti ya Wakaguzi na Wachunguzi ya mwaka 2020/2021, 2021/2022 na 2022/2023 na kubaini tofauti kubwa. Hii ina maana kuwa ripoti za wakaguzi hazifanyiwi kazi kikamilifu na mamlaka za uchunguzi hivyo kuchochea wizi, rushwa na ufisadi nchini. Mamlaka za uchunguzi zimekaa kimya katika maeneo mengi yaliyotolewa taarifa za viashiria vya kuwepo wizi, rushwa na ufisadi katika ripoti za wakaguzi. Iko mifano kadhaa katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, uchunguzi kutofanyika kwa wakati. Katika kipindi cha miaka miwili takwimu zinaonesha kuwa malalamiko yaliyopokelewa TAKUKURU ni 14,773 lakini majalada yaliyokamilika uchunguzi ni 993 tu, sawa na 6.7% tu, huku majalada 93.3% yakiachwa bila kufanyiwa kazi katika mwaka husika, lakini pia kati ya kesi 638 zilizopelekwa mahakamani Serikali ilishindwa kesi 275 sawa na 43%.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu hizi, hivi kweli tunayo nia ya dhati ya kupambana na rushwa nchini kwetu? Uchunguzi umefanyika, 6.7% tu kwa malalamiko yote yaliyopokelewa katika mwaka husika, huku tukipoteza 43% ya kesi zote zilizofikishwa mahakamani, na hapa unajiuliza majalada yaliyofanyiwa uchunguzi na TAKUKURU na kuridhiwa na DPP yakiwa na ushahidi wa kutosha inawezekanaje mahakamani tushindwe kwa kiwango hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 inaonesha kuwa malalamiko yaliyopokelewa ni 7,225 lakini majalada yaliyokamilika uchunguzi ni 1,828 sawa na 25% huku kesi zilizoshindwa ikiwa ni 33%. Kila mahali watuhumiwa wa rushwa na ufisadi wamekingiwa kifua na mamlaka za Serikali ukienda TRAB na TRAT (kodi zilizoshikiliwa kwenye mapingamizi ni shilingi trilioni 10.48) bila sababu za msingi, FIU (kuwepo miamala shuku yenye thamani ya shilingi trilioni 280 ambayo haijakamilika kufanyiwa uchambuzi hadi sasa), vilevile katika Ripoti za CAG, PPRA, Mbio za Mwenge na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukipitia tovuti ya TAKUKURU unakuta waliohukumiwa kwa makosa ya rushwa kwa sehemu kubwa ni viongozi wa vijiji, kata, wilaya na bodaboda, huku watuhumiwa wakubwa wa rushwa na ufisadi wakiwa kwenye ofisi za umma na mitaani wanatamba. (Kiambatisho Na. 3)

Pili, ni kuhusu watuhumiwa wa rushwa na ufisadi kutofikishwa mahakamani licha ya mamlaka za ukaguzi kuibua tuhuma mbalimbali za rushwa na uhujumu uchumi, lakini ni idadi ndogo tu ya watuhumiwa wanaofikishwa mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka miwili, ni kesi tisa tu za rushwa na uhujumu uchumi zilizofikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi licha ya kwamba watuhumiwa wengi wa rushwa na ufisadi hawakupelekwa mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hizo kesi tisa hazifahamiki kwa umma zinamhusu nani? Katika eneo gani? Huku TAKUKURU ikipambana kuwaficha watuhumiwa wa rushwa na uhujumu Uchumi, lakini Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) inatawangaza hadharani kwa majina na nafasi zao.
(i) Taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 inaonesha kuwa TRC, Wizara ya Fedha na Wizara ya Uchukuzi waliacha njia ya ushindani na kutumia njia ya single source katika zabuni ya ujenzi wa reli ya SGR kipande cha Makutupora - Tabora na kuisababishia hasara Serikali ya shilingi trilioni 1.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata katika kipande cha Tabora - Kigoma Wizara hizo zilitumia njia ya single source bila sababu za msingi na kuisababishia hasara Serikali ya shilingi trilioni 1.7 na hivyo kufikia hasara ya shilingi trilioni 3.4. Matrilioni hayo ya Watanzania yamepotea, lakini watu waliohusika bado wako kwenye ofisi za umma na hawajafikishwa mahakamani. Taarifa ya TAKUKURU imekaa kimya kuhusu jambo hili.

(ii) Kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 Serikali Kuu, jedwali Na. 17 ukurasa wa 56 linaonesha kuwa Serikali imekopa nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge na bila ridhaa ya Bunge kiasi cha shilingi trilioni 1.285. Pia jedwali hilo linaonesha kuwa kiasi cha shilingi trilioni 2.531 fedha za mikopo hazikupokelewa katika Mfuko Mkuu wa Serikali, kwani fedha hizo zilipokelewa kwenye akaunti za wafadhili na nyingine zilipokelewa moja kwa moja kwenye miradi. Hii ni kinyume na Katiba, sheria na dhana ya misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mara tumemtaka Waziri wa Fedha kuwasilisha Bungeni jedwali la matumizi ya mikopo hiyo bila mafanikio, hapa kinafichwa nini? Serikali inataka mpaka taarifa ya akaunti na majina yaliyotumiwa miamala ya fedha hizo yavuje mitandaoni ndiyo mtoe maelezo ya ufafanuzi? Kuendelea kuchukua mikopo hii kwa kificho na nje ya sheria kumelipelekea Taifa letu kutumbukia kwenye mzigo mkubwa wa madeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia tarehe 30 Juni, 2023 deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 82.2 ikilinganishwa na shilingi trilioni 71.3 mwaka 2022. Kuna ongezeko la shilingi trilioni 10.9 (15%) ikilinganishwa na ongezeko la shilingi trilioni 6.7 (10%) kwa mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, deni la Taifa limekuwa likikua kwa kasi kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo lilikuwa likikua kwa wastani wa asilimia nne hadi tano tu. Usiri na kasi ya uchukuaji mikopo unaoendelea nchini, unatishia uhai na uhuru wa Taifa letu. Benki ya Dunia (WB) imezionya nchi za Afrika kuacha kukimbilia kuchukua mikopo ya nje ili kurahisisha kutatua shinikizo la ukwasi (liquidity pressures).

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina amezitahadharisha nchi za Afrika kuacha kutumia rasilimali zake za asili kama dhamana ya mikopo. Nchi nyingi za Afrika zimeanza kuchukua mikopo inayolindwa na dhamana ya maliasili za nchi kama madini, gesi, mafuta, bandari na kadhalika, hali inayopelekea kuingiliwa katika utungaji na usimamizi wa sera, sheria, kanuni, miongozo, programu na mikakati (kunyang’anywa uhuru wa kujiamulia mambo), mikopo kukosa uwazi, ulinganifu na yenye riba kubwa na masharti mengi ya kinyonyaji.

(iii) Mfano mwingine ni Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP-2115) ambapo fedha za faini ya ucheleweshaji, CSR na tozo ya Mahakama kwa IPTL kiasi cha shilingi trilioni 1.4 hadi leo haijadaiwa na Serikali. Hapo dhana ya utawala bora iliyojengwa katika misingi ya uwajibikaji na utawala wa sheria iko wapi? Taarifa ya CAG ya mwaka 2022/2023 inaendelea kulalamikia kutokulipwa fedha hizi lakini taarifa za uchunguzi ziko kimya na wahusika bado wako kwenye ofisi za umma na hawajafikishwa mahakamani hadi leo.

(iv) Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekuwa haitangazi hadharani majina ya watuhumiwa wa rushwa na ufisadi na imegeuza kuwa jambo la siri hali inayorudisha nyuma mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini. Tofauti na upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) imekuwa ikiwatangaza kwa majina, vyeo na hasara waliyoisababisha watuhumiwa wote wa rushwa na ufisadi wanaopelekwa mahakamani. (Kiambatisho Na. 4)

(v) Kila ripoti ya CAG inapowasilishwa haioneshi watuhumiwa waliofikishwa mahakamani wala hatua zilizochukuliwa. Sheria ya Ukaguzi inampa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwapeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) watuhumiwa wote aliojiridhisha pasipo mashaka kuwa kosa limetendeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 47(3) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008, nanukuu: “ 47(3) When the Controller and Auditor General has reason to believe that an offence has occurred, he shall refer the matter to the Director of Public Prosecutions for appropriate action (The Public Audit Act),” huku taarifa za wakaguzi zikionesha dalili za kuwepo wizi, rushwa na ufisadi wa matrilioni ya fedha za umma, lakini TAKUKURU inaripoti kuokoa fedha shilingi bilioni 15.5 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, saba ni kuhusu kuingia mikataba ya siri ya rasilimali za Taifa. Serikali hairuhusiwi kuingia mikataba ya rasilimali za umma kwa siri na badala yake inatakiwa kuweka wazi mikataba hiyo ili wananchi wawe na uwezo wa kupima utendaji na uzingatiaji wa kanuni, taratibu, sheria na utawala bora. Hivi sasa Serikali inaingia mikataba kinyume cha Katiba na sheria za nchi.

(i) Katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2022/2023, Serikali inakiri kuingia mikataba 43 ya rasilimali za nchi. Mikataba hii imeingiwa kwa siri na kwa kificho, hata tulipoomba kuletewa mikataba hiyo au kuelezwa inahusu nini, Serikali imekaidi agizo hilo na kuamua kukaa kimya. Mikataba hii imeingiwa kinyume na kifungu cha 16(1) cha Sheria ya The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act 2015, pia kifungu cha 12 cha Sheria ya The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act No. 5 of 2017 ambazo zinataka mikataba yote ya rasilimali kuwekwa wazi kuanzia hatua za awali za makubaliano hadi kusaini mkataba na baadaye kuridhiwa na Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, usiri huu wa mikataba unaleta hofu kubwa sana kuhusu hatima ya rasilimali za Taifa letu. Hii mikataba 43 ya rasilimali inahusu kuuzwa, kukodisha, kuwekwa dhamana au kubinafsishwa? Hapa dhana ya utawala bora iko wapi? Waziri wa Utawala Bora yuko kimya au anasubiri mikataba hii yote 43 ivuje kwenye mitandao ndiyo ufafanuzi utolewe!

(ii) Serikali imesaini mikataba saba ya ujenzi wa barabara saba zenye jumla ya kilometa 2,035 kwa gharama ya shilingi trilioni 3.75 kwa kiwango cha lami kwa kutumia utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC + F) bila kueleza kwa kina masharti yaliyoko kwenye mkataba huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa ni takribani mwaka mmoja umepita miradi hiyo haijaanza. Mikataba ya EPC+F awali aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba walieleza kwamba mkandarasi anakuja na fedha zake kujenga barabara hizo na baadaye Serikali kuanza kulipa kidogo kidogo, ghafla baada ya kusainiwa mikataba hiyo Serikali inabadilisha tena maelezo kwamba mkandarasi anatakiwa apewe 10% ambayo ni shilingi bilioni 375.51 ndiyo miradi iweze kuanza ujenzi wake. Hizi fedha hazimo katika bajeti ya mwaka 2023/2024 na siyo utaratibu wa EPC+F. Madai haya hayamo katika mkataba wa EPC+F, fedha hizi zinatotewa kwa ajili gani na tunapata unafuu gani kama Taifa kwa kutumia utaratibu huu wa EPC+F?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ya mwaka 2022/2023 imethibitika kuwa mikataba hii ilisainiwa bila kuwa na ufadhili wa uhakika wa miradi hiyo na wakandarasi wameshindwa kuwasilisha dhamana ya benki ya utendaji kazi yenye thamani ya shilingi bilioni 375.51 kama matakwa ya mkataba na ndiyo sababu ya miradi hii kushindwa kuanza hadi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wakandarasi walipatikanaje hadi wakasaini mikataba wakiwa hawana sifa na uwezo wa kifedha? Mkataba wa EPC+F uliwezaje kusainiwa bila kujiridhisha na masuala ya msingi ikiwemo ufadhili wa fedha za mradi? Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi – Prof. Mbarawa na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kulipotosha Bunge na umma wa Watanzania kwa makusudi kuhusu faida za miradi ya EPC+F huku ukweli wakiwa wanaujua.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni dhahiri kuwa Mawaziri hawa walijipanga kulihadaa Taifa ili kufanikisha maslahi yao binafsi na kulitumbuliza Taifa kwenye mzigo mkubwa wa madeni yasiyolipika. Haya yote yamefanyika Waziri wa Utawala Bora yupo na Waziri Mkuu yupo.

(iii) Mradi wa ujenzi wa barabara ya kulipia, ghafla tukasikia Serikali inasaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya express way kutoka Kibaha hadi Chalinze yenye urefu wa kilometa 78.9 kwa njia ya ubia (PPP). Mkataba huu umesainiwa bila kulieleza Bunge masharti yaliyopo katika mkataba huo. Serikali haina mamlaka ya kutwaa ardhi ya umma ambayo ni hifadhi ya barabara na kuikabidhi kwa mwekezaji bila kibali cha Bunge. Hii ni kinyume cha Sheria ya Ardhi na Sheria ya Rasilimali, hapa utawala bora tunaozungumza uko wapi? Hakuna uwazi, hakuna ushirikishwaji wa wananchi wala uzingatiaji wa sheria. Haya yanafanyika Waziri wa Utawala Bora yupo na Waziri Mkuu yupo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nane ni kuhusu Mawaziri kutoa taarifa za uongo kwa Mheshimiwa Rais na umma wa Watanzania. Katika siku za karibuni, kumeibuka tabia ya Mawaziri kutoa taarifa za uongo mbele ya Rais na mbele ya Watanzania bila hofu wala woga wowote, kinyume kabisa na misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hapa majuzi Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba akimweleza Mheshimiwa Rais kwenye mkutano wa hadhara kwamba hakuna wizi Serikalini huku akijua fika kuwa kuna Ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 aliyoiwasilisha Bungeni ikiwa imejaa tuhuma za wizi, ubadhirifu na ufisadi wa kila aina wa zaidi ya shilingi trilioni 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya TAKUKURU na Ripoti ya CAG ya mwaka 2022/2023 nazo zimejaa tuhuma za ubadhirifu wa kila aina. Pia tumeona Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa naye mbele ya Mheshimiwa Rais akimhadaa kuwa wizi unaosemwa mitandaoni ni wa miaka ya 2017 hadi 2021 huku akijua fika CAG katika ripoti yake ya mwaka 2021/2022 na 2022/2023 amebaini wizi na ubadhirifu wa kila aina kwenye Wizara yake ya TAMISEMI, halafu Waziri mbele ya Rais anaita taarifa za wizi zinazoibuliwa na CAG na TAKUKURU kwamba ni taarifa za kwenye mitandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu naye huko Mara alikutana na wizi mkubwa hadi fedha zinasafirishwa kwenye mabegi kama nguo kutoka Mara kuja Makao Makuu ya TAMISEMI Dodoma zaidi ya shilingi milioni 200. Hili dili limejulikana, je, ni madili mangapi ya aina hii yanayofanyika kwenye halmashauri zote nchini kwa kificho?

Mheshimiwa Naibu Spika, ujasiri huu wa Mawaziri hawa kusema uongo tena mchana kweupe mbele ya Mheshimiwa Rais na Watanzania wanautoa wapi? Mawaziri hawa wanafanya hivyo ili kufanikisha nini? Hayo yanafanyika, lakini Waziri wa Utawala Bora na Waziri Mkuu wako kimya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tisa ni kuhusu kuwepo viongozi na watumishi wa umma ndani ya Serikali ambao siyo raia wa Tanzania. Zipo taarifa za uhakika kwamba baadhi ya nafasi za uongozi na watendaji wa Serikali zimechukuliwa na raia wa kigeni kinyume na Katiba na sheria za nchi yetu na kupelekea usalama wa nchi yetu kuwekwa rehani mwa wageni, kukosekana kwa uzalendo na uadilifu, ajira za Watanzania kuchukuliwa na raia wa kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda wakati wa Mkutano wa Saba wa Mkuu wa Majeshi (CDF) na Makamanda wa mwaka 2023 uliofanyika tarehe 22 Januari, 2024 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema, nanukuu: “Taarifa zilizopo, baadhi ya waomba hifadhi hao au wakimbizi au familia zao wameajiriwa Serikalini kwa nafasi mbalimbali na wengine wamepewa teuzi Serikalini katika nafasi zenye maamuzi.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ina maana kwamba vyombo vya dola vimeshajiridhisha kuwepo kwa viongozi na watendaji ndani ya Serikali, tena katika ngazi ya maamuzi ambao siyo raia wa Tanzania na orodha ya majina hayo wameshaikabidhi Serikalini kwa hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Waziri wa Utumishi wa Utawala Bora kupitia hotuba hii ameshindwa kusema chochote juu ya hili jambo kubwa ambalo ni tishio la usalama wa nchi yetu. Hii ina maana kuwa, tangu vyombo vya dola vitangaze hadharani suala hili mwezi Januari, 2024 hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali. Utawala bora uko wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kumi ni kuhusu kuwepo kwa taarifa nyeti zisizothibitishwa. Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na taarifa nyeti zinazotolewa na baadhi ya viongozi waandamizi Serikalini kutoa matamko yanayotishia usalama wa nchi, lakini taarifa hizo zimekuwa hazikanushwi wala kuthibitishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka Mheshimiwa Albert John Chalamila wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera mwezi Oktoba, 2022 alisema baadhi ya Mawaziri wameacha majukumu ya kumsaidia Mheshimiwa Rais na kuhangaika nje ya nchi kusaka fedha za kuja kumng’oa mwaka 2025, lakini pia hivi majuzi Mheshimiwa Paul Christian Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha tarehe 12 Aprili, 2024 akiwa na viongozi wakuu wa nchi na wananchi wengine katika kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Hayati Edward Moringe Sokoine, Monduli alisemam ninanukuu: “Nitumie fursa hii kuwaambia hasa kaka zangu mnaotuma watu na kulipa kumchokoza mama yangu, ninawajua na ninyi mnanijua. Narudia tena, hasa kaka zangu mnaotuma na kulipa watu kumchokoza mama yangu Samia, mnanijua na ninyi nawajua. Mheshimiwa Rais, kwa majina yao nawajua, na leo tarehe 12 nataka iwe mwisho kuwatuma watu hao wanaokutukana kwenye mitandao ya kijamii. Jumatatu ikiendelea, nakutajia majina. Wwengine ni Mawaziri na wengine wanapewa nguvu na watu tunaowaheshimu. Naomba iwe mwisho, tumwache Daktari Samia afanye kazi aliyopewa na Mungu.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha kuhusishwa baadhi ya Mawaziri kuwa sehemu ya mkakati wa kumpinga na kumkwamisha Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu yake na kushiriki njama za kumwondoa madarakani ni kosa la uhaini na kosa la kimaadili na hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 54 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo ilitarajiwa baada ya kauli hizi kutolewa na viongozi hao waandamizi wa Serikali, vyombo vya dola vingeueleza umma usahihi wa taarifa hizo na hatua zilizochokuliwa dhidi ya wahusika. Tulitegemea Wakuu wa Mikoa hao wawili Chalamila na Makonda wangelazimishwa kuwataja kwa majina na nafasi zao Mawaziri wanaotuhumiwa kumsaliti Rais ambao wangekuwa wametenguliwa katika nafasi zao na kufikishwa mahakamani, lakini pia kama Wakuu wa Mikoa hao wametoa taarifa za uongo na wameshindwa kuwataja kwa majina wahusika, basi wao wakamatwe na washitakiwe kwa makosa ya uhaini. Rais ni taasisi nyeti, ni lazima tuilinde kwa wivu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine katika dhana ya utawala bora; utoroshaji wa fedha nje ya nchi (Illicit Financial Flows - IFFS) umefikia wastani wa shilingi trilioni 3.5 kwa mwaka, Tanzania ni nchi pekee ambayo wahalifu wa makosa ya transfer pricing wamefutiwa adhabu, pia ripoti ya Transparency International ya mwaka 2023 kwenye kipengele cha Corruption Perception Index (CPI) Tanzania ilipata 40% na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 189 zilizopimwa. Kwa tathmini hii, nchi yetu inaonekana kufanya vibaya katika usimamizi wa dhana ya utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hitimisho. Mambo yanayofanyika hivi sasa nchini kwetu katika baadhi ya sekta hayaendani na misingi ya utawala bora. Kama nilivyosema awali kuwa Katiba, sheria, kanuni na miongozo na misingi ya utawala bora haifuatwi katika maeneo mengi ya utekelezaji wa shughuli za Serikali na hivyo kusababisha kuwepo matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, kuongezeka kwa umaskini, ujinga na maradhi, kuongezeka kwa rushwa, huduma mbovu za jamii, kutoheshimiwa haki za binadamu na kuongezeka kwa dhuluma na uonevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.

VIAMBATISHO
Kiambatisho Na. 1, Maelezo ya Ushahidi ya Mbunge Luhaga Mpina
Kiambatisho Na. 2, Maagizo 12 ya Waziri Mkuu ya Tarehe 27 Aprili 2023
Kiambatisho Na. 3, Uamuzi wa Spika kuhusu kupuuzwa kwa Maagizo ya Waziri Mkuu
Kiambatisho Na. 4, Taarifa ya ZAECA ya kuwafikisha Mahakamani Watuhumiwa wa Rushwa na Ufisadi.

(Hapa Mhe. Luhaga J. Mpina hakuweka viambatisho katika mchango wake wa maandishi)