Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa George Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya. Mahususi nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuiongoza nchi kwa kufuata misingi ya utawala bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivi kwa sababu misingi ya utawala bora imeainishwa kisheria na kikatiba kwa mambo yafuatayo; Kwanza, lazima kuwe na Utawala wa Sheria na ndiyo maana tunaona hatua zinachukuliwa na Mahakama inafanya kazi kwa kuhakikisha kwamba, inatoa hukumu au maamuzi na vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuna kuheshimu Katiba na tatu, msingi mwingine ni independence of judiciary kwa maana ya kuwa na uhuru wa Mahakama katika kufanya kazi zake bila kuingiliwa. Jambo lingine ni kuwa na heshima au kuheshimu haki za binadamu. Sambamba na hilo kuna suala la kuheshimu maamuzi yanayoamuliwa na Bunge lako Tukufu, hivyo hivyo, kuheshimu misingi ya kidemokrasia kwa mana ya principle of democracy.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yamethibitika ndiyo maana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda Tume ya Haki Jinai kuhakikisha kwamba kutakuwa na Utawala wa Sheria. Pia aliweka uhuru katika vyombo vya maamuzi ikiwemo PCCB kwa maana ya TAKUKURU kuweza kufanya maamuzi yake pale ambapo hatua zimekuwa zikichukuliwa, na wapo watu wenye kesi Mahakamani, pia wapo ambao wamechukuliwa hatua mbalimbali. Kwa hiyo, kwenye msingi wa Utawala wa Sheria, nchi yetu imekuwa kielelezo na tutaendelea kusimamia hivyo na Katiba yetu tutaendelea kuiheshimu, kuitii na kuilinda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ni muhimu niweze kulizungumzia ni hili la kikokotoo. Kumekuwa na mixed feelings, na ni kweli tunakubali katika upande wa Serikali kwamba suala la kikokotoo kulikuwa na changamoto kubwa. Lazima turudi kwenye historia. Nakumbuka changamoto hii imejitokeza kutokana na historia ya awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kupitia Bunge hili Tukufu tulitunga sheria ya kuanzisha Mfuko wa LAPF, tulitunga sheria ya kuanzisha Mfuko wa PSPF, tukatunga sheria ya kuanzisha Mfuko wa PPF, pia tulikuwa na Mfuko wa GEPF na hivyo hivyo tulikuwa na Mfuko wa NSSF katika kipindi cha nyuma. Tusisahau kwamba Bunge hili ndilo lilipitisha sheria hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadaye katika uendeshaji wa mifuko hii zilitokea changamoto mbalimbali zikiwemo za uendeshaji na kuwa mzigo tena katika mfumo, kwa sababu ilikuwa inatengeneza mfumo wa kiushindani. Sasa kwenye masuala ya wafanyakazi, kwa sababu wanachokichangia ni kwa ajili ya maisha yao, ukiweka mfumo wa ushindani, matokeo yake kutakuwa hakuna uwiano wa mafao kwa wafanyakazi ambao walikuwa wakifikia hatua ya kustaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kutengeneza uwiano wa mafao na kupunguza hasara zilizokuwa zikijitokeza kama Operational Cost za uendeshaji wa mifuko, ndiyo yakafanyika maamuzi mwaka 2018 ya kuunganisha mifuko, tukawa na mifuko miwili. Mmoja wa PSSSF kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta ya umma, pia kuwa na Mfuko wa NSSF ambao utashughulika na wafanyakazi wasio katika sekta ya umma au sekta rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo haya nini kilichofanyika? Kwanza, tulienda kwenye unafuu. Yapo mafao awali yalikuwa 25%. Katika kuingia kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tulifanya actuarial evaluation na katika tathmini hiyo ilitupeleka pamoja na kukaa vikao na Vyama vya Wafanyakazi wote nchini, Vyama vya Waajiri wote nchini na upande wa Serikali kuweza kuangalia na kutafuta ule unafuu, tukatoka 25% kwenda 33%.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa ninavyosema, hatua ni nzuri. Mheshimiwa Rais, alishatoa maelekezo zaidi ya mara mbili akiwa amekutana na Jeshi la Polisi Wastaafu, Wakuu wa Jeshi la Polisi, alitoa maagizo kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba, tufanye tathmini na kuangalia upya na kufanya mapitio kuona hiki kikokotoo cha sasa kama tunaweza tukakiboresha zaidi ili wastaafu wetu wasiweze kupata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaanza kazi hiyo na pia sheria inatutaka tufanye actuarial evaluation kila baada ya miaka mitatu na tayari miaka mitatu imeshafika kuanzia mwaka 2023, na sasa tupo kwenye hatua hiyo. Tumefanya tafiti nchi nyingi, hatuwezi hata siku moja Serikali kufumba macho wala kuziba masikio katika suala ambalo linawahusu Watanzania ambao wamefanya kazi ya heshima kwa ajili ya ujenzi wa Taifa hili. Hatuwezi hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpe pole Mheshimiwa Neema Mwandabila ambaye kimsingi yeye alikuwa anaeleza kwa maana ya jinsi ambavyo tulimwelimisha kupitia mifuko lakini imeonekana kama mashambulizi yamekuwa mengi kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wamekuwa wakieleza kulingana na uhalisia.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwape pole, lakini tuseme suala hili ni la kisayansi, linahitaji kufanya tafiti za kina ili kuweza kuhakikisha kwanza kunakuwa na uendelevu wa mifuko, na zaidi, katika tija kuangalia wastaafu hawa waweze kupata fedha na wawe na uhakika wa kulipwa mafao yao pale wanapostaafu kuliko vinginevyo ambavyo imekuwa. (Makofi)
Mheshemiwa Naibu Spika, tumefanya utafiti katika nchi za Afrika, tumeona Tanzania tupo tofauti sana katika nchi zote za Afrika katika utoaji wa mafao. Hata nchi za wenzetu kule nje, tena wao hawatoi kabisa ile fedha ya mkupuo. Wakati mwingine kuzitaja hapa inaweza isilete mahusiano mazuri ya kidiplomasia lakini tunafanya tafiti kuweza kuhakikisha watu wetu wanapata mafao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mwenyewe nina maslahi, nina wazee wangu watatu sasa hivi wanaelekea kwenye kustaafu. Sasa ingekuwa ni mambo yangu binafsi, pengine au ni jambo la Mheshimiwa Waziri, au ni la mtu mwingine, maana yake angeangalia maslahi na upendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi tunachoangalia ni ile sustainability na nafuu ambayo ataipata mstaafu awaze kupata heshima ya kuwa na fedha nyingi ambazo anazipata baada ya kufanya kazi kwa kutumikia Taifa lake. Pili, ile mifuko iweze kuwaendeleza wale wengine ambao wanachangia. Kwa hiyo, ndiyo maana ilikuwa ni uamuzi wa Serikali kuhakikisha tunakuwa na mifuko miwili sasa, usimamizi wake uweze kuwa mzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia 81% ya wanufaika kwa sasa imeongezeka, ukiacha ya awali 19% peke yake ndio ambao mkupuo umepungua, lakini 81% zimeongezeka hata yale mapato yao ya mwisho wa kila mwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu jambo hili limeshatolewa maelekezo na Mheshimiwa Rais, Bunge lako Tukufu limetuelekeza, tunalipokea kwa unyenyekevu mkubwa kwenda kulifanyia kazi na pengine tutasikia kauli ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pale katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, Arusha Tarehe 01 Mei, ambapo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan rafiki wa Wafanyakazi na rafiki wa Waajiri atakutana nao na ataenda kueleza kuhusiana na suala hili. Kwa hiyo, tumelipa uzito unaostahili kuweza kuhakikisha tunaliweka sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala hili la uhamisho. Ni kweli uhamisho kwa mujibu wa sheria, kwanza unaanzia pale ambapo zinatangazwa ajira. Pili,
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja kwa ruhusa yako.
NAIBU SPIKA: Bado unazo dakika tatu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili la uhamisho, Mtanzania yeyote anapoomba ajira hasa hizi za Serikali, kuna kipengele na makubalino kwamba atakuwa tayari kufanya kazi popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Tanzania Bara au Tanzania Visiwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika kipengele hicho, anapopata ajira, changamoto ambazo tumekuwa tukizipata kwa upande wa Serikali ni pale ambapo anapata ajira, anaenda kufanya kazi na kuna sharti lingine katika sharti lake la ajira kwamba atafanya kazi kuhudumia Tanzania kwa kipindi cha miaka mitatu ili sasa baadaye katika miaka mitatu hiyo ikiisha, ndiyo aweze kuwa na uhuru wa kuweza kuhama kwenda eneo lingine lolote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, experience inaonesha pale tu ajira zinapotolewa, mtu anakubali popote kwa sababu Serikali inatoa ajira pia kulinga na uhitaji na ikama kuweza ku-balance kwenye maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ambayo ni ya pembezoni mwa Tanzania, hawapati wafanyakazi na Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiomba kwamba wakati wao wana upungufu wa Madaktari, Manesi na kadhalika, inapotokea Serikali imetoa ajira kwa ku-balance hiyo ikama na wale waliokubali kwamba wanaweza wakafanya kazi popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa zaidi ya miaka mitatu bila kuhama, akishapata ajira, hatua ya pili inayofuata ni kuanza kuomba uhamisho. Anaomba uhamisho atoke Kigoma aende Dar es Salaam kwa sababu shangazi ni mgonjwa, mama ni mgonjwa, baba ni mgonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine kuna maeneo utakuta hata vyeti vya forgery; kumekuwa na sababu za kwenda masomoni, na wengine wamekuwa wakiingia hata kwenye ndoa hata zile mkeka wakati mwingine ili tu mwisho wa siku awe na ndoa ya kwenda kuthibitisha kwamba anahitaji kutoka kwenye eneo lile. Sasa hili ni sisi wenyewe katika sababu hizi ambazo zimekuwa zikitolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo sababu nyingine. Hata viongozi tuwe wa kweli kwa ajili ya Tanzania yetu. Hata sisi Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiombwa uhamisho. Tunakuja tunaandika memo kwamba tunaweza kuwahimisha kutoka kwenye maeneo fulani tunaweka kwa memo kwamba wahamie kwenye Majiji au kwenye Halmashauri za Miji na Mikoa. Lazima tuseme ukweli kwa ajili ya Tanzania yetu. Sasa changamoto inakuja kwamba, mwingine anasema yupo tayari kuhama hata kama bila kupewa hela za uhamisho na hela za mizigo. Akishahama hatujafuta sheria, akirudi anaenda kudai hela yake ya mzigo kwamba hakupewa. Yanarudi malimbikizo tena, huku wakati huo tunahitaji ku-balance ikama ya maeneo ambayo ni remote area na difficult to reach.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna maeneo ambayo mengine kwa kweli hayapo privileged kulingana na ule umbali. Sasa wakishahama wote, tukajaa Dar es Salaam, wote tukajaa Dodoma na wote tukajaa Arusha, mwisho wa siku maeneo ya Tanganyika na maeneo mengine, hawapatikani. Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy anakubali hapa kwamba wapo Madaktari wanataka kuhama, watumishi wanataka kuhama. Lazima tufike sehemu tuitendee haki nchi yetu na tuseme kweli kulingana na changamoto ambazo tunazipata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatujakataa suala la kuhama, ni sahihi na vigezo vilivyowekewa kisheria vitakuwepo, lakini Serikali lazima itafanya uchunguzi na kuangalia na kufanya mapitio ya yule ambaye anastahili kuhama, atahama bila ajizi yoyote na bila mkwamo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hayo machache, naomba kuunga mkono hoja, lakini nikiendelea kusema kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo makini katika kuhakikisha nchi yake na Serikali yake inafikia malengo ambayo amewaahidi Watanzania. Mpango wa Maendeleo tutautekeleza, na pia Ilani ya Chama cha Mapinduzi tutaendelea kuitekeleza bila ajizi. Ndiyo maana umeona miradi yote ya maendeleo tumeshafika 90% mpaka 98%, tunamaliza. Hakuna mwananchi au jimbo ambalo halijaweza kupelekewa miradi ya maendeleo na ushahidi huo wewe mwenyewe umezidi kuona.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kama ni taarifa tutaipata baadaye muda wa taarifa ya habari saa mbili asubuhi. (Makofi /Kicheko)