Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda nimshukuru Mungu kwa namna ambavyo siku ya leo imeanza na inaenda kwisha na sasa umenipa nafasi ya kuhitimisha hoja ambayo niliitoa asubuhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yetu imepata wachangiaji wengi sana na ninakupongeza sana. Kwa siku moja kupata wachangiaji 23 pamoja na Kamati ni 24, ni wachangiaji wengi sana na michango ilikuwa ni mizuri sana. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla wale ambao mmechangia na wale ambao hamkuchangia, lakini kwa nyakati tofauti mmekuwa mkileta maoni yenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi haya yote tunayachukua na pengine inaweza ikawa siyo rahisi sana kuyajibu yote, lakini tutafanya utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kila hoja iliyotolewa hapa itajibiwa vizuri kwa maandishi na kila Mbunge ataipata kwa utaratibu ambao upo hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niseme mwelekeo na dhamira ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ni kutaka kujenga utumishi wa umma unaowahudumia wananchi na ndiyo maana tumeomba fedha hizi. Tunataka kujenga utumishi wa umma unaowahudumia wananchi na ambao unachagizwa na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma kwa wananchi na kupeleka huduma kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo dhamana ya Watanzania wote ambao wameweka dhamana yao kwake, lakini hawezi kufanya kazi yeye peke yake. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Katiba yetu amekasimu majukumu haya kwa wasaidizi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kazi kubwa ya sisi wasaidizi pamoja na watumishi wote wa umma ni kuhakikisha kwamba tunawahudumia wananchi na kufanya huduma hizo ziwe bora. Huduma hizo zinapaswa ziwe za heshima, zisizokuwa na rushwa na kusimamia uwajibikaji wa watumishi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nasema suala la kuwahudumia Watanzania kwa msukumo wa teknolojia na hasa mifumo ambayo tumeijenga ni maelekezo yake Mheshimiwa Rais na ndiye atakayetutoa katika misukosuko ya kutokuwa na huduma stahiki kwa wananchi wetu. Ndiyo maana tunafikiri tangu tumeanza kutumia mifumo, kumekuwa kuna huduma bora na tutaendelea kuboresha hii mifumo kwa sababu tumeona ndiyo njia na nyenzo pekee ya kututoa hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema asubuhi na nikanukuu maelezo ya Hotuba ya Mheshimiwa Rais ya tarehe 22 Aprili, 2021 wakati akihutubia Bunge la Kumi na Mbili, mstari ule wa mwisho amesema; “Wajibu wa Watumishi wa Umma ni lazima uendane na haki zao.” Tangu ameingia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mabadiliko na mapinduzi makubwa katika utumishi wa umma yametokea, tena ni makubwa sana sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna mkwamo wa kupanda madaraja kwa muda, kulikuwa kuna mkwamo wa kupanda kwa mishahara kwa muda, kulikuwa hakuna annual salary increment kwa muda na kulikuwa kuna madeni ya watumishi ya muda mrefu. Haya yote, kwa muda wa miaka mitatu toka alipoingia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema Hapana, lazima watumishi wa umma wapate haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, annual salary increments kwa mwaka 2023/2024 ilichukua kiasi cha fedha ya bajeti ya Serikali shilingi bilioni 153.9, hizi zililipwa kwa mwaka ule. Katika mwaka huu wa fedha ambao tunakwenda nao, huu tunaokwenda kuuombea fedha 2024/2025, fedha zimeombwa kwa ajili ya kuwalipa hiyo annual salary increment, kwa sababu sasa consistency inaenda kila mwaka, kitu ambacho hakijawahi kutokea, tunaomba shilingi bilioni 150.8. Hali hii itaendelea consistently kwa spirit hii ya Mheshimiwa Rais kwamba hataki dhuluma kwa mtu, kila mtu apate anachostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, suala la madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 26,331 yenye jumla ya shilingi bilioni 39.055 kutoka Wizara, idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mashirika na taasisi za umma yamehakikiwa na kulipwa kwa watumishi stahiki. Kulipa fedha hizi kutoka kwenye bajeti katika mazingira tuliyokuwanayo, tumetoka kwenye COVID na uchumi umedorora duniani, ni utashi wa kiongozi wa nchi na siyo maamuzi mepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama vile haitoshi, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imerejesha utaratibu wa kuwapandisha vyeo watumishi wenye sifa stahiki kila baada ya miaka mitatu, badala ya minne iliyokuwa inapigiwa kelele na watumishi. Sasa utaratibu wa kupanda vyeo ni baada ya miaka mitatu kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi kama inavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameridhia kupandisha vyeo watumishi 81,515 waliokasimiwa katika bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa gharama ya kiwango cha shilingi bilioni 130.47. Hii siyo fedha ndogo. Pia, Serikali imepanga kuwapandisha vyeo watumishi 219,924 waliokasimiwa katika bajeti hii tunayoiomba na gharama yake ni shilingi bilioni 252.7. Fedha hizi ni nyingi, na unapokuwa Rais ukaamua kuzipeleka huku na nchi ina mahitaji mengi, maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Rais huyu anawapenda watumishi wa umma wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima watumishi wa nchi hii wamwone Mheshimiwa Rais ni mkombozi wao, lazima wamuunge mkono, na pia wamwombee kwa sababu ana changamoto katika meza ya matumizi mengi, lakini anawagawia wao anawaweka wa kwanza na mambo mengine yanafuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imelipa mishahara ya wafanyakazi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa 113 zilizopo chini zenye jumla ya watumishi 691 kwa awamu. Kwa awamu ya kwanza Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya kugharamia mishahara ya watumishi 474 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa 101 ambazo zimebainika zina uwezo mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka Waheshimiwa Wabunge na wengi wamechangia hapa, bila kutaja majina ya waliochangia kwa sababu ya muda, halmashauri zilizokuwa hazina uwezo zilikuwa zinashindwa kulipa watumishi hawa, lakini Serikali imechukua watumishi hawa kutoka halmashauri 101. Ninaamini kwenye awamu inayofuatia tutamalizia na wengine wote waliobakia ili walipwe kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kule kwenye halmashauri tutaweka utaratibu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize, madeni ya watumishi hawa ambayo wanadai Mamlaka za Serikali za Mitaa ziwalipe. Sisi tutaanza kuchukua hatua kwa wale Wakurugenzi ambao tunawapelekea maelekezo ya kulipa stahiki za madeni yanayotokana na watumishi waliokuwa chini yao, halafu hawafanyi hivyo. Tutachukua hatua za kisheria ya kiutumishi kwa sababu sasa inakuwa kama mchezo. Watumishi wanakuja ofisini kwetu, wanalalamika, tukiwaambiwa walipwe na tunawandikia, lakini Wakurugenzi hawataki kuwalipa. Tutachukua hatua kali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mtiririko wa michango ambayo tumeipokea, mchango wa kwanza kabisa ni mchango wa Kamati. Kamati yetu pendwa, Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria yenye Wajumbe makini sana. Nasema kwamba ni Wajumbe makini kwa sababu ya namna tunavyofanya nao kazi. Tunafanya nao kazi kitaalam sana. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wote na maoni yenu yote sita, tunayachukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na hili la msawazo wa watumishi. Ni kweli maelezo ya Waheshimiwa Wabunge yana ukweli ndani yake, kwamba yako maeneo ambayo yana upungufu wa watumishi, lakini yako maeneo mengine ambayo yana watumishi wengi kupita kiasi. Watumishi hawa wanang’ang’ania maeneo yale ambayo yana mazingira mazuri na kuacha yale maeneo ya pembezoni na vijiji yakiwa yana uhaba wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumeshaamua, sisi Wizara ya Utumishi, TAMISEMI na wenzetu wa Wizara ya Fedha, tumemaliza kujadiliana na maamuzi yamefikiwa kwamba tukimaliza bajeti hii tutakuwa na fedha ya kuhakikisha kwamba tunaenda kufanya msawazo wa watumishi nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme hapa, Waheshimiwa Wabunge msirudi tena kuanza kulalamika kwa sababu tutakapoanza hii operation haitamwacha mtu na haitakuwa na upendeleo, lakini tutazingatia hali na sababu mahususi walizonazo watumishi wetu. Katika kufanya hili, liko suala limezungumzwa hapa la wenza kufanya kazi maeneo tofauti tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwajiri ni Serikali na Serikali tunahimiza maadili, lakini tunapenda sana na mpaka tuna Sera ya Magonjwa ya Kuambukiza ukiwemo UKIMWI. Tunapowaweka wenza maeneo tofauti kama kuna mambo ambayo mimi huwa yananiuma ni pamoja na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kwa kutumia nafasi hii ya msawazo, tutahakikisha kila mwenye mwenza wake wa kweli wanakwenda kufanya kazi katika eneo moja. Siyo lazima iwe kituo kimoja cha kazi. Kama ni walimu, basi huyu atafundisha shule hii na huyu atafundisha shule hii, lakini ni maeneo ambapo jioni wanakwenda kulala pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwe wakweli, jambo hili limekuwa linatukera. Waheshimiwa Wabunge wote na wengi mna maombi na mnaleta kwa Mheshimiwa Mchengerwa na kwangu kwamba tusaidie hawa wamefunga ndoa. Ukiwa na cheti cha ndoa na umefunga ndoa ya kweli, maana kuna ndoa nyingine za uongo uongo, hili hatuwezi kulikubali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutahakikisha kwa kutumia mwanya huu wa msawazo, basi kila mtumishi ambaye mwenza wake yuko mbali, basi tunawaunganisha ili waweze kufanya kazi kwa raha na mustarehe. Mimi naamini hii itaongezea tija katika utendaji wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu akiwa na mwenza wake yuko mbali, kuna kesi tunazipokea. Mimi nina mwalimu wangu mmoja mwanamke katoka Kigoma, kamfuata mume wake Shule ya Sekondari Mbuga. Amefika pale, sasa likizo imeisha anatakiwa kurudi. Unamwona anavyosikitika kwamba anaacha mume wake anakwenda mbali ambako hawataonana kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu hiki hakikubaliki na inaweza ikawa ni kinyume cha haki za binadamu. Kwa hiyo, ni lazima tutakisimamia na tutahakikisha kwamba tunatumia fursa hii ya bajeti kuweza kuweka msawazo na kuhakikisha kwamba wenza wanakaa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, mmezungumzia suala la ndege za Serikali, kwamba suala la TGFA, zile ndege ambazo zimenunuliwa na Serikali na kwamba zipelekwe ATCL kwenye shirika letu la ndege ambalo linaendelea kufanya vizuri sana, hili jambo tumeshalizungumza kwenye Kamati na kwamba tuko kwenye hatua za mwisho za kumalizia kuhamisha hizi ndege kwenda ATCL.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhamisha ndege siyo sawasawa na kuhamisha gari au pikipiki. Ina mchakato wake wa kitaifa, lakini pia wa kimataifa. Kwa hiyo, kuna mambo mengi ya kuyaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni vitendea kazi vya mifumo. Hili tunalichukua. Mifumo tuliyoijenga na hasa inayosajili watumishi ili waweze kuweka malengo yao, ili wapandishe details zao na kuweka malengo yao na mpango kazi na baadaye waweze kupimwa na mpango huo, unaoitwa PEPMIS, mfumo huu wala hauhitaji teknolojia kubwa, ni uwepo tu wa internet, na kama hakuna internet, basi unaweza ukasogea mahali ambapo inapatikana na ukaweza kuingiza takwimu zako.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni sababu tu zinatolewa na wala vishikwambi haviwezi kutusaidia sana. Kinachoweza kutusaidia ni watumishi wenyewe kuamua kuingiza data zao kwenye mfumo. Mfumo huu baadaye ndiyo utakaochuja na kupandisha vyeo na ndiyo utakaochuja na kupandisha madaraja. Sasa kama hawataki kuingia, mathalani, mpaka sasa hivi 4,700 na ushei wamegoma kujiingiza kwenye mfumo kwa sababu ambazo hazieleweki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia humo ndani tumegundua wako wengine hawana vyeti stahiki vya kuingiza. Vilevile, humo ndani tumegundua wako wengine ni watoro wa muda mrefu, na huko ndani tumegundua kuna watumishi hewa. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge mkiona mnapigiwa kelele, muulize tu nipe details zako, halafu mwambie twende nikupeleke, kisha mlete kwangu. Halafu tuingie tuangalie, aniletee vyeti, tuingize kwenye mfumo. Mimi nafikiri kwenye hili ikitokea mtu anasema mimi sijaingia, nimefungiwa mshahara, mwambie twende nikupeleke, utaona ananyamaza. Watumishi wana sababu nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la fedha kupatikana kwa wakati, tumelichukua hilo. Pia suala la kuboresha maslahi na mishahara, kama nilivyoeleza, huu ni mpango endelevu na Mheshimiwa Rais anayo political will katika hili, ameamua kupandisha mishahara. Amefanya hivyo kwa vitendo na anaendelea kufanya hivyo. Kwa hiyo, tuamini kwamba hakuna kitakachosimama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la rufaa za watumishi, mmesema juu ya rufaa za watumishi na ninyi mnakumbuka kwamba mmetuongezea bajeti kwa ajili ya ile Tume ya Utumishi wa Umma. Kwa hiyo, tutaenda kuongeza vikao na kuhakikisha kwamba rufaa nyingi zinashughulikwa kwa kasi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja zote ambazo zimetolewa, nyingi wamenisaidia kujibu na namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye amezijibu hoja nyingi. Pia Mheshimiwa Katambi naye kazungumzia kuhusu kikokotoo na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie hili la kukaimu, ambalo Mheshimiwa Francis na Mheshimiwa Rashid Shangazi wamelizungumzia. Kwanza kabisa, kukaimu kuna sifa yake, siyo kwamba mwajiri anaamua kukukaimisha tu. Kukaimu kuna sifa yake na sifa ya kukaimu ni lazima uwe na sifa ambayo cheo hicho kikitaka kuthibitishwa kwako unakuwa una sifa za cheo hicho. Usikaimishwe na ukikaimishwa ni lazima taarifa itolewe kwa Katibu Mkuu Utumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa waajiri wengi na hasa Mamlaka za Serikali za Mitaa na hata taasisi zetu wanawakaimisha watu kwa mapenzi yao na urafiki wao. Hata mahali ambapo yuko mwenye sifa ya kukaimu nafasi hiyo hakaimishwi na anakaimishwa rafiki yake au jamaa yake ambaye hana sifa. Ukianza mchakato wa kumthibitisha unagoma na anapoambiwa kwamba huyu hana sifa, anaenda kukaa kimya na lile file au ile barua na yule anaendelea kukaimu, ndicho kinachotokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na uharaka katika kufanya vetting na kuhakikisha kwamba wataalamu hawa ambao wana sifa hawakaimu katika nafasi zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo limezungumzwa ni hili linalohusiana na malimbikizo ya mishahara, amesema Mheshimiwa Shangazi, na hili tumeshalitolea majibu lakini mengine amejibu Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ajira kwa Watendaji wa Kata; WEO, VEO na MEO, ajira hizi kwanza zinatolewa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa na wala hazitolewi na Sekretarieti ya Ajira. Mchakato ule unafanyika kwenye Halmashauri na Sekretarieti ya Ajira inakwenda kusimamia tu.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, ajira hizi ziko kwenu na Waheshimiwa Madiwani wetu wanashiriki kujua ziko kiasi gani, lakini Kamati za Ajira ndizo zinazofanya kazi ile zikishirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama. Kwa hiyo, tunaweza tukauliza yanayofanyika kule, kama mnadhani siyo sahihi tunaweza kushauriana nini kifanyike zaidi, lakini kwa kweli zimepelekwa kule na wala haziko central kwa maana ya Sekretarieti ya Ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uzingatiaji wa maadili sehemu za kazi, Mheshimiwa Kakunda hili limejibiwa na Naibu Waziri pia. Mheshimiwa Janejelly mmetambulishwa viongozi, lakini jinsia haikuzingatiwa. Tuangalie standards katika nchi. Kwenye nafasi nyingi za kitaifa kwa mwaka 2023, makatibu kwa mfano Makatibu Wakuu, wanawake walikuwa 22.2% lakini mwaka 2024 waliongezeka na kuwa 25.6%. Kwa hiyo, ni ongezeko kubwa la wanawake katika nafasi hizi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Makatibu Tawala wa Mikoa Wanawake kwa Tanzania Bara kwa mwaka 2023 walikuwa 30.8%, lakini wapo mpaka mwaka 2024, hivi tunavyozungumza wameongezeka kwa 46.2%. Ongezeko hili ni kubwa sana. Kwa hiyo, nchi yetu ni gender sensitive na tunazingatia sana na Mheshimiwa Rais ni champion katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajira za uwiano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, uwiano tuliuweka kwa formular, ni 79% kwa 21% kwa ajira zile za Taasisi za Kimuungano. Kwa hiyo, kama yanayotokea kule Zanzibar pengine hayako sawasawa, tutajaribu kuwasiliana na wenzetu, tuwaambie kwamba kuna hili na pengine tutapata zaidi kwamba changamoto ni nini, kwa sababu umesema Mheshimiwa Mbunge, hatuwezi kuacha ku-respond.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Alice amezungumzia mtumishi anapobadili kada kwamba asianze na cheo cha chini, aanzie na cheo kile kile. Tumekusikia, lakini ipo changamoto kubwa, kwa sababu, kama watu watatakiwa kuhama kada, hata ile career development huwezi kuipata vizuri. Kuna watu wana-struggle, yaani kuna watu wengine mimi nawajua nimesomanao, toka nilivyosomanao wameshasoma vitu vitatu vya aina tofauti na mpaka leo hata hawaajiriki.

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani kuna watu wako hivyo, anapenda tu kusoma, hataki hata career development. Umeajiriwa kama Mwalimu, soma kutoka Mwalimu wa Msingi, ukawe Mwalimu wa Sekondari, ukawe Mwalimu wa Chuo Kikuu. Sasa wewe unataka kuhama, umekuwa Mwalimu unataka ukawe Mhasibu, ulikuwa Mwalimu unataka ukawe Afisa Mipango na ndiyo inaleta confusion.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiruhusu hii kiholela, ndiyo maana tumeweka caveat pale, kwamba ukisoma ujue unakuja kuanza na moja, kwa sababu uzoefu unaotizamwa ni wa kazi ile, siyo wa kazi nyingine. Kwenye kazi ile ya Afisa Manunuzi, wewe huna uzoefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mwanao uliyemsomesha utamkuta akiwa boss wako, wewe unakuja kuanza chini yake. Kwa hiyo, rai yangu kwa watumishi wa Tanzania, hebu tuchague career tunazozipenda tukiwa bado wadogo na tuendelee nazo kuelekea mpaka juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Wakuu wa Vitengo, Idara na Mamlaka za Serikali za Mitaa wanakaa miaka mingi; saba hadi kumi lakini Wakurugenzi wanateuliwa kutoka kokote kule? Mamlaka ya kuteua nafasi za kuteuliwa ni Mamlaka ya Rais na yanatokana na Katiba, kwamba Rais ana uwezo wa kuunda chombo chochote, lakini Rais anao uwezo wa kumteua mtu yeyote kwa ajili ya kufanya jukumu lolote katika nchi kwa maslahi ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hii itabakia hivyo kwa sababu haijaleta tatizo. Kwani wakiwa wamepewa ule uongozi, wewe si unaendelea na utumishi wako na hawa wanaoteuliwa. Jamani, kuteuliwa siyo raha. Mkitaka mwaulize walioteuliwa, halafu baadaye uteuzi ukaondoka, ni mateso. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuteuliwa siyo jambo la kujisifusifu na kufurahia na pengine ukiteuliwa, ujiulize kama huwezi bora useme, nashukuru sana, lakini mimi naomba niendelee na career yangu. Kwa hiyo, itakuwa hivyo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo ya awali kwa Watumishi yanafanyika sana. Ni kweli kwamba Chuo cha Utumishi wa Umma hakija-loose focus ila kimeongeza zaidi, lakini zimeongezeka Taasisi nyingine zinazosaidiana na Chuo cha Utumishi wa Umma kuwajengea uwezo watumishi wa umma. Vyuo hivyo ni kama Chuo cha NDC, kinafanya kazi hiyo, Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kinafanya kazi hiyo, Chuo cha Lushoto cha Mahakama kinafanya kazi hiyo, Chuo cha Uhusiano wa Kimataifa kinafanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, vyuo vimeongezeka siyo kwamba Chuo cha Utumishi wa Umma kimehama katika majukumu yake, vimeongezeka na vinafanya kazi ya kuwajengea uwezo watumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, mambo ni mengi, wenzangu wamenisaidia kuyajibu, yapo mengine ambayo yamepata majibu na mengine kama nilivyosema tutajaribu kuyajibu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa liko jambo moja lilisemwa na Mheshimiwa Mpina, ni jambo zito na ukilichukulia kwa wepesi wepesi hivi unaona amezungumza kitu chepesi, lakini Mheshimiwa Mpina amezungumza kitu kizito na lazima tukijibu kama Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mpina anasema, Ilani na utekelezaji wa Serikali haviendani. Anasema pia kuna uvunjaji mkubwa wa sheria bila hatua kuchukuliwa, yaani utawala ambao hauna sheria (no enforcement). Anazungumza kwamba Watanzania wanauawa, kuna wizi wa kutisha, no separation of powers, teuzi za ajira bila ushindani. Pia anasema kuna ufisadi na anatoa mifano ya Mradi wa SGR, Nyerere Hydropower, deni la Taifa halieleweki na viongozi hawaheshimiani.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani ukaacha kwa sababu yeye ameshaipeleka kwenye mitandao. Sasa ni nchi gani hiyo ambayo ina sifa kama hizi ikabaki stable kama ilivyo nchi yetu? Hiyo nchi inaitwa Tanzania, nchi ambayo demokrasia chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan iko kwenye viwango vya juu kuliko wakati mwingine wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo vya habari viko huru, Vyama vya Siasa viko huru, vinafanya mikutano inavyotaka na kuandamana wanavyotaka. Wewe unasema nchi hii imevurugika. Unajua anachokisema hapa Mheshimiwa Mpina. Ni kwamba hapa kuna a failed state. Anataka kusema kwamba there is a weak state. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa weak state ina characteristics zake. Moja ya characteristic ni hizi ninazozisema. Nchi ikiwa failed state, mipaka yake haidhibitiki, mipaka ya nchi hii niambieni katika ukanda huu kuna mipaka ya nchi inayodhibitika kama ya Tanzania?

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi haichezewi! Niambieni nchi ambayo ni a failed state kama kwa maneno haya anayoyasema Mheshimiwa Mpina inaweza ikawa na GDP inayokua consistently kati ya asilimia saba imeshuka pamoja na COVID, pamoja na mdororo wa uchumi wa dunia, lakini haikushuka below 4.7 wakati kuna nchi zimeenda negative. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi anayoisema kwamba imeshuka, ni failed state inatoa elimu bure kutoka shule ya msingi mpaka sekondari na ukimaliza kupata elimu bure hiyo unaenda kupata mkopo wa Chuo Kikuu. Unasema it is a failed state. Nchi anayoizungumza Mheshimiwa Mpina inatekeleza miradi mikubwa kama Mradi wa Mwalimu Nyerere Hydropower ambao una-cost more than six trillion shillings, mradi ambao hakuna nchi imeweza kuujenga kwa muda mchache kama tulivyojenga Tanzania, wewe unasema is a failed state! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi anayoizungumza Mheshimiwa Mpina kwamba imefeli, inaweza kutengeneza Mradi wa SGR ambao kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ni kilometa 300, kutoka Morogoro mpaka Makutupora ni kilometa 422, zimefika 98% katika muda wa miaka chini ya mitano kwa gharama ambayo kilometa moja ni zaidi ya dola 3,000,000. Mradi huu ni mkubwa, nchi nyingine zikitekeleza mradi kama huu zinafilisika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hiyo ambayo unasema it is a failed state, inakusanya kodi kati ya shilingi trilioni moja mpaka shilingi trilioni tatu kwa mwezi na inatekeleza miradi yake, unasema it is a failed state! Nchi unayoisema imefeli leo Moody’s Credit is a Global Rating Agency ambayo inaaminika duniani inasema Tanzania ni kati ya nchi ambazo ina uchumi very stable na kwamba uchumi wake umekua kwa viwango vyao, kutoka B.2 mpaka B.1. Kwa hiyo, imekuwa rated kama ni nchi yenye uchumi unaokua na stable katika nchi za East Africa zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hii imetolewa Moody’s, tarehe 23 Machi, 2024, mwezi haujapita na kwamba, katika ku-rate hizi kwa sababu gani wametu-rate katika hii, ni kwamba tuna diversified economy, kwamba tuna uchumi ambao umekamata sekta zote na unashirikisha watu wote. Pili, wanasema we have a strong export. Tatu, wanasema stable debt. Wewe unazungumzia nchi ambayo ipo kwenye stable debt, haidaiwi ikapitiliza, nchi yake iko stable unasema is a failed state!

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme tusijidharau kiasi hicho. Ni dhambi kujidharau. Kama mtu una mambo yako, ni vema ukayazungumza kwa namna nyingine, lakini siyo mambo ya kitaalamu kama haya. Nchi yetu inaheshimika, Rais wetu anaheshimika na ndiyo maana kila anapokwenda duniani wanampa Shahada ya Udaktari. Ni heshima, wanampa zawadi zote za kubeba, wanaona hazifai, mpaka wanaamua kumpa zawadi ya kichwani. This global appreciation to a Woman President, haiwezekani ikadharauliwa na sisi wenyewe ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujenge tabia ya kujiamini na kuheshimiana. Huwezi ukaizungumzia a failed State halafu ukasema unamheshimu huyo Rais anayeongoza hiyo nchi. Hii ni insubordination.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuomba sana kwamba ni lazima nchi yetu katika kipindi hiki cha changamoto kubwa duniani, COVID-19 imepiga, uchumi unadorora duniani, tunatekeleza miradi kila mahali. Mfano, miradi ya afya, miradi ya elimu kule Meatu kwake, TARURA wamepeleka pesa, SEQUIP wamepeleka shule mbili mpya kwa Mheshimiwa Mpina, BOOST wamempelekea madarasa chungu nzima, kapokea ambulance moja katika kituo cha afya kimoja. You say this is a failed state? Hapana! Nadhani pengine kuna agenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, inaomba Waheshimiwa Wabunge waniidhinishie mimi na wenzangu katika Wizara yangu tukasimamie kiasi cha shilingi 1,101,069,467,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.