Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na pumzi ya kuendelea kuishi. Natoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwanza kwa kuridhia kwake na kuleta mabadiliko ya sheria na kurudisha Tume ya Mipango. Kipekee nampongeza pia kwa kuchukua muda mfupi sana, akaunda Wizara ambayo ndiyo hii leo tunajadili hotuba yake ya Mipango na Uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia naomba kumpongeza Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo. Huyu ni mwanazuoni mahiri ambaye hatuna wasiwasi naye. Timu ambayo Mheshimiwa Rais amesaidia kuiunda kwenda kusimamia eneo hili la Mipango na Uwekezaji imejaa watu mahiri. Hatuna wasiwasi na utendaji wa Katibu Mkuu, Tausi Kida, hatuna wasiwasi na Katibu wa Tume ndugu yetu Lawrence Mafuru, pia hatuna wasiwasi na Ndugu Nehemia Mchechu ambaye ni Msajili wa Hazina. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara hii pia ina jukumu la kutazama Dira ya Maendeleo ya Taifa letu na miongozo yote. Napenda leo kushauri maeneo machache hasa kwenye upande wa Sera. Nitagusia kwenye eneo la elimu, kilimo kidogo na pia kwenye ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sera yetu ya Elimu ambayo imehuishwa hivi karibuni, bado inahitaji kufanyiwa maboresho zaidi na hasa iwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba yote yaliyoingia katika sera yanakwenda kutekelezeka, kwa sababu tunapozungumza elimu tunazungumza rasilimaliwatu, hapa ndipo tunapoandaa rasilimaliwatu ambao watakwenda kuwa watumishi wa maeneo mbalimbali katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni lazima tuwe na sera ambayo inaweza ikazalisha Watanzania ambao watakuja kuwa wazalishaji wazuri kwenye Taifa hili ambalo sasa hivi vijana ni wengi zaidi kuliko makundi mengine. Kwa maana vijana ndiyo nguvu kazi ya Taifa, sasa ni muhimu sana tukaiwezesha kwa kuipatia elimu na maarifa ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, jambo mahususi ambalo nataka kulishauri hapa ni kuona kwamba bado tunazalisha sana watumishi katika kada ya Ualimu. Kada hii imeshakuwa saturated, haiwezi tena, ni wengi sana wako mtaani ambao hawajaajiriwa, lakini bado vyuo vyetu vinaendelea kuzalisha tena walimu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaiomba sasa Wizara hii ya Mipango ilitazame hili jambo kwa mapana, kwamba, kuna vyuo 35 vya Serikali ambavyo traditionally vinazalisha walimu ngazi ya Certificate na ngazi ya Diploma. Je, kuna umuhimu wa kuendelea kuzalisha kwa wingi tena katika ngazi ya Degree? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna umuhimu wa chuo kama Chuo cha Kilimo - SUA kuwa na udahili na wanafunzi wa Ualimu? Hili ni lazima tulitazame. Mimi nadhani ni vizuri mipango ikatuelekeza tuwe na wanafunzi wengi katika ngazi ya Degree au Diploma kwenye vyuo vya aina ya DIT, taasisi ya teknolojia. Huku ndiyo tuwe na wanafunzi wengi ambao hata baadaye hawatatusumbua kulazimika kuwatafutia ajira kwa sababu wanaweza wakajiajiri wenyewe kulingana na maarifa ambayo watayapata kupitia vyuo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tume hii itusaidie. Tumetoka kwenye sensa, sensa inatupa projection ya idadi ya watu baada ya muda fulani. Kwa hiyo, lazima tujue pia kwamba leo baada ya miaka mitano tutahitaji walimu wangapi? Kwa hiyo, idadi hiyo ndiyo tujue tutazalisha kiasi gani cha walimu ili waweze kuziba hilo pengo ambalo tunakusudia. Tukiendelea kuwazalisha, halafu hatuna ajira na hawana shughuli mbadala watakazokuja kufanya tunakuwa tunaharibu hiyo rasilimaliwatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni rasilimali ya ardhi; Sera yetu ya Ardhi ni ya mwaka 1995 sitaki kuamini kwamba imepitwa na wakati, lakini imepitwa na wakati. Japo bado tunaaminishwa kwamba Sera yetu ya Ardhi ni Sera bora ambayo nchi nyingine zinakuja kujifunza, lakini hebu tuambiane ukweli. Haya matatizo ambayo tunayaona Waziri wa Ardhi anahangaika nayo kila siku, bado sitaki kuamini kwamba sera yetu ni bora. Lazima hili nalo tulitazame, kwa sababu tunapozungumza uwekezaji wowote, utafanyika juu ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama ardhi yetu mpaka leo haijapimwa, ndani ya miaka 60 ya uhuru tuko chini ya 50% ya ardhi yote iliyopimwa, maana yake bado tuna tatizo. Tungependa kuona mipango ya matumizi bora ya ardhi. Ardhi ipimwe, hasa vijijini ambako ndiko kwenye migogoro ya wakulima na wafugaji, lakini ndiko ambako sasa uwekezaji unaelekea huko kwa sababu tunakwenda kuwekeza kwenye eneo la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa wito kwamba ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi ambazo ndiyo hizi sera tunazozizungumza na mwisho wa siku tunahitaji good governance. Tunapokuwa na good governance maana yake tunaondoka sasa kwenye haya matatizo ya migogoro ya ardhi isiyokwisha kila mara. Ni vyema sasa eneo hilo nalo Mipango ikalitazama kwa mapana na marefu kwa ajili ya kulinda uwekezaji. Hatutarajii kwamba tuwe na wawekezaji ambao wanakumbana na kadhia hii ya umiliki wa ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kwenye kilimo. Nimetazama hapa, Sera ya Kilimo ni ya mwaka 2012. Hawa wamejitahidi, ni current sana. Hata hivyo, tunawaomba sasa wawe na masterplan ya mkakati mahususi wa kusukuma ajenda za kilimo. Miongoni mwa mikakati hiyo iwe sasa kukiweka kilimo katika umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, tutakubaliana hapa, hizi mvua ambazo tunaendelea kuhangaika nazo, zimeharibu miundombinu ya barabara, majengo na kadhalika. Tungekuwa na sera madhubuti katika eneo zima la umwagiliaji ya kuvuna haya maji ya mvua inawezekana mwezi wa saba au wa nane tungejikuta tuko kwenye kiangazi ambacho tunahitaji maji ambayo leo yamekuwa ni adha kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana, mpaka sasa hivi asilimia mbili tu ya ardhi yetu ambayo inatumika katika kilimo ndiyo ipo katika umwagiliaji, ni asilimia ndogo sana. Miaka 60 ya uhuru tunazungumzia asilimia mbili. Ni vyema sana tukawekeza hapa, tukawa na mipango ya muda mrefu kwenye Tume ya Umwagiliaji, tukaiwezesha tuwe na mpango endelevu angalau wa miaka mitano mitano kuhakikisha kwamba tunaongeza eneo la umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye kuongeza eneo, ni lazima tuangalie pia uwezekano wa kutumia maji katika maziwa yetu. Tunalo Ziwa Victoria, tumechukua maji kwa ajili ya shughuli za majumbani. Siyo dhambi maji ya Ziwa Victoria na yenyewe tukayabadilisha matumizi tukayapeleka kwenye shughuli za kilimo. Siyo dhambi tukayafanya maji ya Ziwa Victoria yakatumika kwenye shughuli za ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika Ziwa Tanganyika linazunguka karibu mikoa mitatu. Itakuwa ni ajabu sana kama na mikoa hii nayo tutasubiri mpaka mvua za vuli na masika ndiyo twende tukalime. Tutumie maji ya Ziwa Tanganyika kwa ajili ya shughuli za kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, hapa Mheshimiwa Kitila kuna jukumu kubwa sana la kufanya kwa sababu hili tatizo kubwa la ajira ambalo tunalizungumza ni kwa sababu hatujaweka mipango yetu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuweke mipango yetu katika ardhi, tuweke mipango yetu katika kilimo. Huku kukiwa kumeimarika, hatutaona Mtanzania anazunguka na bahasha kutafuta ajira kwa sababu tayari wanaweza wakajiajiri kupitia kilimo. Hatutaki kiwe kilimo hiki cha kutangatanga ambacho hakiaminiki. Tunataka kilimo kinachoaminika, ndiyo maana tunasisitiza kwamba tutengeneze mipango katika eneo zima la umwagiliaji, hata kuihusisha Sekta Binafsi katika eneo zima la kujenga miundombinu ya umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siyo dhambi kama kuna watu wenye uwezo wa kuwekeza katika eneo hili la kilimo kwa maana ya kujenga miundombinu. Naamini Watanzania wapo tayari kulipia kama ni kwa gharama ambazo zinaeleweka. Pia hata kuifanya Tume ya Umwagiliaji kuwa ni wakala.
Mheshimiwa Spika, tunazo wakala; TARURA, RUWASA zinafanya kazi zinazofanana na hiyo. Kwa nini hii Tume ya Umwagiliaji tusiifanye kuwa ni wakala na ikafanya kazi hii kuhakikisha kwamba wakati wote wananchi wanaweza kupata ardhi ya kutosha na kulima kwa msimu mzima wa mwaka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ambalo nataka kuchangia ni suala zima la uwekezaji. Katibu Mkuu wa Chama alivyokuwa Mbarali juzi ameagiza shamba la Mbarali lipewe kwa wananchi. Tunaiomba Serikali ipokee agizo hili kwa sababu tunajua kule kuna shida. Pokeeni agizo hili lakini mhakikishe mnalinda maslahi ya mwekezaji.
Mhshimiwa Spika, eneo lile ambalo halitumiki, basi wananchi wapewe ili waweze kujikimu na kuendesha maisha yao kwa sababu tunaamini uwepo wa mashamba yale ya Mbarali umesaidia kwa kiasi kikubwa sana sisi kama Taifa kupunguza kuagiza mchele kutoka nje. Sasa hivi mchele wetu pia unaweza ukapenya katika mipaka mingine kwa sababu tunazalisha mchele mzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, ninakushukuru sana kwa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)