Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza nianze tu kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati kadri ambavyo imejielekeza namna ya kutatua matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Profesa Muhongo anaondolewa kwenye Wizara hii wananchi wa Tanzania walisikitika sana na wakati amerudishwa wananchi wa Tanzania wameshukuru sana, kwa hiyo, endelea kuchapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba katika Wizara, Wizara hii ni ngumu sana, dunia yote hutafuta madini, hutafuta kupata utajiri kupitia madini, hii ni Wizara ngumu sana. Kwa hiyo lazima tukupongeze wewe pamoja na Naibu wako kwa kadri ambavyo mnachapa kazi Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina vijiji ambavyo vimepitiwa na REA Phase II, lakini vijiji hivyo ni Ng’haya, Bundlya, Kabila, Kigangama na Kisamba zimewekewa nguzo chache sana na sehemu zingine hata shule za msingi, makanisa na zahanati hazijapata umeme. Shahidi ni Naibu Waziri wa Nishati, tulitembelea maeneo hayo. Naomba mtakapokuja kujibu mseme pia kwamba mnaongeza vijiji hivyo ili vikamilike vionekane kwamba kweli REA Phase II, imevitendea haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyo vijiji viwili pia ambavyo havikuwekewa umeme, umeme huu umekwenda kwenye vijiji vingine, kwa mfano Nyashigwe, iko kwenye REA Phase II, lakini umeme wake umekwenda kitongoji cha Mawe ambacho ni kijiji cha Welamasonga. Kwa hiyo, kijiji hiki hakijawekewa umeme, mtakapokuja kutoa majibu mniambie je, mtakiingiza kwenye Phase III, aumtakipelekea umeme sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kijiji kingine cha Kitongo Ndagalu ambapo makao makuu ya kijiji ambayo ni center kubwa haijawekewa umeme, umeme umewekwa kitongoji cha Misungwi, napo mje mniambie ili wananchi hawa waweze kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ha utainga sasa hivi REA Phase II, basi uingizwe REA Phase III. Lakini umeme ambako wamekamilisha kama Kabila, Ng’haya haujawaka, naomba Wizara kwa maana ya Waziri muhimize ili kama umekamilika umeme huu uweze kuwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Magu havina umeme asilimia 70, ninaomba sasa kupitia REA Phase III, vijiji hivi viwekewe umeme, nimeongea na wewe Mheshimiwa Waziri, nimeongea na Naibu Waziri, nimeongea na Meneja wa Kanda, naomba sasa vijiji hivi kwa kweli viweze kupatiwa umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni declare interest nilikua mchimbaji mdogo mwaka 1993 katika machimbo ya Ulyankulu na huko ndiko nimeanzia maisha. Wachimbaji hawa wanateseka sana kila siku, wanahama kila leo, lakini wachimbaji hawa ni ajira yao. Tunapozungumzia Tanzanite, wachimbaji wale sio wa Arusha tu, wa Magu wapo, wa Bariadi wapo, wa Sengerema wapo. Tunapozungumzia almasi, wachimbaji wa nchi nzima wako kule na wa Magu wapo, tunapozungumzia dhahabu, wachimbaji wa Magu wapo. Kama walivyolalamika Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ninaomba hawa wachimbaji wadogo wadogo kama azma ya Serikali ni kuwatafutia maeneo iwatafutie maeneo ili waweze kupatiwa maeneo ya uchimbaji, hiyo ndio ajira yao ya kudumu.
Mhehimiwa Mwenyekiti, yako malalamiko kwamba mikataba ya madini tunapata fedha kidogo sana kama nchi. Ninaomba sasa haya nayo ni maeneo ambayo yanalalamikiwa na kila mmoja wetu ili yaweze kupitiwa na kuangaliwa ili Serikalil iweze kupata mapata ambayo kwa kweli yatanufaisha Taifa letu la Tanzania. Maana tunaweza kuwa na madini baadaye tukaachiwa mashimo na nchi isinufaike. Naishauri Serikali iangalie kwa uhakika ili kuhakikisha kwamba mikataba hii inawanufaisha watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ambayo yamewekewa umeme wa REA wananchi wanashukuru sana, sasa niguse tu kwamba tutakapokamilisha maeneo ya vijiji, viko vitongoji ambavyo navyo ni kama vijiji, kwa hiyo, tusiishie REA Phase III, lazima tuende na REA Phase IV. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo na niunge mkono hoja, ahsante sana.