Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia leo kwenye Wizara (Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji). Kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Mheshimiwa Waziri hapa amesema, nasi kule Manyoni tunasema, miradi mingi sana tumepata Jimbo la Manyoni Mashariki ya mabilioni ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nachukua nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Manyoni Mashariki kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa heshima ambayo ametupatia na ameiweka katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Profesa Kitila kwa kazi kubwa sana ambayo anaifanya.
Mheshimiwa Spika, natambua amepewa Wizara hii ikiwa changa lakini tunaona ameweka mifumo na inaenda vizuri. Namshukuru sana Msajili wa Hazina, ndugu yangu Mchechu, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, Mkurugenzi EPZA na Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi tumekuwa tuna-interact na hawa Wakurugenzi, Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Ofisi ya Waziri. Tunaona kuna mambo mazuri ambayo yatatokea hapo mbeleni hususani katika uandaaji wa dira hii ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, nina mambo mawili napenda kuchangia leo. Eneo la kwanza nitachangia kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma, pia kama muda utaniruhusu, nitachangia kuhusu fursa za uwekezaji pale Manyoni.
Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba Serikali imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 76 katika mitaji katika mashirika mbalimbali ambazo zimewekezwa na Serikali. Maana yake ni kwamba, kama tutasimamia vizuri, huu uwekezaji wa shilingi trilioni 76 ambao umewekezwa na mashirika yetu mbalimbali return on investment (tija/faida) ya huu uwekezaji unaweza ukaonekana. Kwa hiyo, hatutaweza kulalamika kwamba tumeshindwa kujenga labda zahanati, kukamilisha maboma pamoja na kutengeneza barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maana ya kuanzisha hii Wizara ya Mipango na Uwekezaji ni kutaka sasa ije isaidie katika huu uwekezaji ambao Serikali inafanya, lakini vilevile kusimamia uwekezaji katika sekta binafsi. Hivi karibuni, wote ni mashahidi, tulitakiwa kuleta muswada ambao unahusu sheria ya usimamizi wa mashirika ya umma.
Mheshimiwa Spika, mimi ni muumini wa hii reform na bahati nzuri Mheshimiwa Rais amekuja na zile 4Rs. Katika zile 4Rs, mojawapo ya R ni Reform, na mojawapo ya eneo ambalo tunahitaji kulifanyia kazi ni Reform, mabadiliko katika Mashirika ya Umma.
Mheshimiwa Spika, nimetangulia kusema kwamba Serikali imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 76 na ofisi ambayo inasimamia uwekezaji ni Ofisi ya Msajili wa Hazina. Ofisi ya Msajili wa Hazina ukiiangalia ni ofisi ya siku nyingi sana. Kimsingi, naweza nikasema imepitwa na wakati. Kuna mambo mengi sana ambayo tunahitaji kuyaboresha katika Ofisi ya Msajili wa Hazina ili awe na meno yatakayomwezesha kusimamia vizuri huu uwekezaji mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inawezekana tunapotosha. Huko zamani uwekezaji ulikuwa haujafika shilingi trilioni 76, lakini sasa hivi tunaongelea huge amount of investment, shilingi trilioni 76 ambayo Serikali imewekeza. Kwa hiyo, tunahitaji jicho la karibu kwa hii mifumo mizuri ambayo itahakikisha kwamba huu uwezekaji sasa unakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nini kifanyike? Bado naendelea kuishauri Serikali ikamilishe ule utaratibu wa kuleta Sheria ya Mabadiliko ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Bado naweka msisitizo kwamba tunahitaji mabadiliko ya sheria ya uwekezaji katika mitaji ya umma. Nakumbuka Mheshimiwa Profesa Kitila alianza huu mchakato wa kuleta ile sheria.
Mheshimiwa Spika, ile sheria itatupa mambo mawili; eneo la kwanza tunahitaji kubadilisha Ofisi ya Msajili wa Hazina; Ofisi ya Msajili wa Hazina imepitwa na wakati, tunahitaji kuja na taasisi kubwa, mamlaka, Public Investment Authority ambayo kwa kweli itaweza kusimamia haya mashirika mengine ili huo uwekezaji wa shilingi trilioni 76 uwe na tija.
Mheshimiwa Spika, hizo ni fedha za wananchi, tuna uhakika gani hizo fedha zinasimamiwa vizuri? Tunahitaji kuwa na mamlaka ambayo itakuwa na meno, ambayo itakuwa na nguvu ya kuhakikisha kwamba sasa uwekezaji ule ambao tumeufanya kule ambao Mheshimiwa Rais ameufanya, unaleta tija na hatimaye hizo fedha zirudi Serikalini ili zikasaidie kwenye suala la Bajeti ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nami naendelea kusisitiza na kumkumbusha Mheshimiwa Profesa Kitila, najua hili hawezi kushindwa. Atuletee Muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, tupitishe ili tuhakikishe kwamba tunaenda kusimamia fedha za wananchi ili tija iweze kuonekana.
Mheshimiwa Spika, tumewekeza kwenye maeneo mengi sana, ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, lakini Watanzania ni mashahidi. Tunahitaji kumsaidia Mheshimiwa Rais ili kuhakikisha kwamba zile fedha na yale mashirika yaliyowekeza yanakuwa yana tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, tuna taasisi nyingi zinatamani kuwekeza lakini hazina mitaji. Kuna fursa nyingi za uwekezaji na kuna taasisi nyingi zina maeneo potential ya uwekezaji, lakini hayana mitaji. Sasa kwenye ile sheria, eneo mojawapo ambalo nashauri liwekwe ni kuanzisha mfuko wa uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, tunapokuwa na ule mfuko wa uwekezaji itakuwa ni sehemu ya kutafuta fedha na kuziweka kwenye ule mfuko, then zile taasisi ambazo hazina uwezo wa ku-raise fedha zitaenda kwenye ule mfuko, zitapewa kwa mfumo wa revolving fund. Hata kama kutakuwa na interest ndogo, lakini at least wawe na uhakika wa kuwekeza.
Mheshimiwa Spika, naomba kusisitiza hili, hili ni eneo muhimu kwa sababu lazima tuzijengee uwezo taasisi zetu ziweke kuwekeza. Bado narudia kusisitiza, tunahitaji uwekezaji wenye tija (return on investment) ambayo itakuwa na tija ili iweze kusaidia nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni fursa za uwekezaji Manyoni. Manyoni tuna fursa nyingi za uwekezaji. Nimetangulia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kule kwetu Manyoni. Sisi Manyoni tuna maeneo mengi ya uwekezaji. Hawa ndugu zangu wa EPZA wana eneo la zaidi ya ekari 2,600 ambalo walilikamata tangu mwaka 2013. Hili eneo ni potential kwa uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, nawakumbusha watu wa EPZA kwamba hili eneo mnalo ingawa fidia mlikuwa hamjatoa. Haya ni maeneo potential, naomba mtafute wawekezaji waje wawekeze. Pia halmashauri imetenga eneo la zaidi ya ekari 250 kwa ajili ya viwanda mbalimbali kama vile viwanda vya korosho. Vilevile kule sisi tunafuga sana mifugo na hivyo kujengwe viwanda vya maziwa na kadhalika. Haya ni maeneo ambayo Mheshimiwa Profesa Kitila anahitaji kuvutia wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Majiri tuna ekari zaidi ya 100 kwa ajili ya kuwekeza viwanda vya chumvi. Nimeuliza sana swali hili Bungeni, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara anafahamu na bahati nzuri walishawahi kufika. Kuna potential kubwa sana ya uwekezaji kwenye suala la viwanda vya chumvi kule Manyoni hasa katika Vijiji vya Kinangali, Mpandagani na Majiri. Mheshimiwa Waziri, najua hili hawezi kushindwa. Namwomba sasa atafute wawekezaji, awalete Manyoni, maeneo yapo, sisi tutatoa maeneo ili wawekeze. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)