Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye hotuba hii muhimu sana ya Wizara ya Ofisi Rais, Mipango na Uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, nitaanza na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Pamoja na kwamba bado kuna mambo ambayo inabidi yaboreshwe, lakini natumia fursa hii kuwapongeza sana Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa kazi kubwa ambayo wamefanya mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kituo hiki cha uwekezaji unaweza kukipima kwa mambo matatu makubwa. Jambo la kwanza ni idadi ya miradi ya uwekezaji ambayo kituo kinasajili. Jambo la pili ni kiwango cha ajira ambacho kinazalishwa na hiyo miradi ya uwekezaji na kipimo cha tatu ni kiwango cha mtaji ambacho uwekezaji huo unaingiza nchini.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuangalia vigezo vyote hivyo vitatu ni kwamba hiki kituo cha uwekezaji tangu kianze, sasa hivi kina takribani miaka 27 kimeanza tangu mwaka 1996. Ukiangalia kwa wastani kwa miaka hii mitatu ambayo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeingia madarakani, kimekuwa na ongezeko kubwa sana la uwekezaji ambalo limefanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, idadi ya miradi ya uwekezaji kwa kipindi hiki, kituo hiki kimeweza kusajili miradi 1,004 kuzalisha ajira za moja kwa moja 248,000. Kutokana na uwekezaji huo, kituo hiki wameweza kuingiza nchini mtaji wa moja kwa moja (direct foreign investment) wa takribani Dola za Kimarekani bilioni 15. Wamefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kuna mambo ambayo inabidi yaboreshwe. Sisi kama Kamati tulifanya ziara ya kutembelea baadhi ya wawekezaji ambao wamesajiliwa na kituo hiki cha uwekezaji na wameingiza mitaji yao hapa nchini. Kwa ujumla, kazi ni nzuri na mambo yanakwenda vizuri. Ila kuna mambo madogo madogo ambayo hawa wawekezaji wali-raise concern. Kwa mfano, maeneo ya kikodi kama vile VAT Return na punguzo la Import Duty ambayo walikuwa wameahidiwa, yamekuwa yakichelewa sana.

Mheshimiwa Spika, pia kuna tatizo kubwa ambalo naungana na Mheshimiwa Neema Mgaya ambaye naye amelizungumzia, la kutokuweka vipaumbele katika kupeleka miundombinu muhimu kwenye maeneo ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, tumefika pale Kibaha, unakuta mwekezaji ameweka billions of dollars kwa ajili ya kutengeneza zile kongani za uwekezaji, industrial shade na kadhalika, lakini unakuta ana muda wa miezi kadhaa anahangaika umeme ufike pale kwake lakini inashindikana; anahangaika maji yafike kwake, lakini inashindikana; anahangaika barabara nzuri ifike, lakini jambo linakuwa gumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali hapa ni kwamba, miundombinu muhimu ya kuwawezesha wawekezaji waanze kufanya shughuli zao kama umeme, maji, barabaraba, yapewe kipaumbele kupelekwa maeneo ambayo wawekezaji wamewekeza dola zao ili uzalishaji uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kwamba, inabidi tuangalie faida za uwekezaji, tusiziangalie kwenye angle ya kodi peke yake, kwani faida za uwekezaji tunaweza tukazipata kwenye maeneo mengine kama ajira au local contents. Kwa hiyo, siyo lazima sana kumbana mwekezaji na wakati mwingine wawekezaji wanashindwa kwa sababu ya masharti ya kikodi, lakini kumbe ukiruhusu huo uwekezaji uje ndani, hata kama utakosa kwenye kodi, lakini utapata kwenye ajira na utapata kwenye local contents. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la muhimu sana ni ile skills transfer/knowledge transfer, kwamba wawekezaji wanapokuja wanakuja na teknolojia mbalimbali za kuzalisha bidhaa mbalimbali. Kwa hiyo, wananchi wetu wanapata fursa ya ku-acquire hizo knowledge na skills (ujuzi) ambao ni faida kubwa pengine kuliko tungetazama tu kodi na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, narudi kwenye eneo la uwekezaji kwenye maeneo ya Jimbo langu la Bukene na Halmashauri ya Wilaya ya Nzega. Pale sisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega tulitenga eneo la uwekezaji, tuna takribani ekari 46,000. Kuna eneo linaitwa Kisasiga pale kwenye Kata ya Igusule, mpaka sasa hivi tulishalipima, lina rutuba nzuri, linaweza kuzalisha mazao kadhaa, lakini mpaka leo ekari 46,000 zimekaa idle, hazitumiki.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwaalika Wizara ya Kilimo, njooni Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, njooni Kisasiga, kuna ekari 46,000 hazitumiki kuzalisha chochote. Kwa hiyo, hii mipango ya block farms ya ukulima mkubwa na wapi, tuna Serikali inahangaika kupata maeneo, lakini kuna maeneo ambayo tayari yapo makubwa yanahitaji tu uwekezaji pale ili yaanze kuzalisha. Kwa hiyo, Wizara ya Kilimo njooni Kisasiga Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, kuna ekari 46,000 zinafaa kwa block farm na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tuna mabonde makubwa ya umwagiliaji ambayo Wizara ya Kilimo pia tunawaalika waje kwa ajili ya kufanya uthamini na kuanza Miradi ya Kilimo. Kuna mabonde makubwa maeneo ya Budushi, kuna mabonde ya Manonga huko Kata za Sigili – Mwangoye, kuna mabonde makubwa Mambali – Kahamanhalanga – Kasela ambayo yapo idle yanafaa kwa miradi mikubwa ya Umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji iangalie kwamba tunayo ardhi na mabonde makubwa ambayo yangeweza kutumika kikamilifu tungeweza kupata uzalishaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono kwamba Serikali iendelee kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambayo pia inapita jimboni kwangu. Tunajua faida ya Miundombinu ya Reli kwa uwekezaji. Wawekezaji wanataka facility za usafiri kwa ajili ya kusafirisha bidhaa, kwa ajili ya kusafirisha raw material. Kwa hiyo, ujenzi wa reli hii hauna shaka yoyote kwamba unakwenda kuongeza na kuimarisha uwekezaji katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kwenye kipande cha Tabora – Isaka ambacho ukamilishaji wake umefikia asilimia tano, kuna shida kubwa ya wale wananchi waliopisha maeneo ili reli ya SGR ijengwe, hadi sasa hawajalipwa fidia. Wananchi wanadai fidia yao, na kimekuwa ni kilio, kwa sababu ni muda mrefu zaidi ya mwaka wananchi wamepisha mashamba yao, hawajalipwa fidia. Masika imefika, hawana hela ya kununua mashamba mengine, kwa hiyo, wamepata kwa tabu sana kipindi hiki cha masika mpaka leo ninavyoongea.

Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara ya Uwekezaji, kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Miundombinu ili kuharakisha bajeti kutoa fedha ili wananchi waliopisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa, walipwe fedha zao, walipwe fidia yao kwa sababu imekuwa ni muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono suala la kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuendelea kuchangia kwenye hisa zetu za bomba la mafuta na ukamilishaji wa process nzima ya bomba la mafuta. Niseme tu kwamba, hapa changamoto kubwa ni local contents kwamba mambo mengine kwa mfano suala la fidia, kama kuna mradi ambao umeendesha zoezi la fidia kwa wananchi vizuri sana mo huu Mradi wa Bomba la Mafuta.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli wananchi waliopisha maeneo yao wamelipwa fidia ipasavyo na hakuna malalamiko yoyote isipokuwa inabidi tuendelee kuboresha eneo la local contents kwa maana ya ajira kwa wazawa hasa wanaozunguka eneo lile. Wale ambao hawana skill sana, wananchi wa kawaida, wapate ajira za vibarua.

Mheshimiwa Spika, local contents nyingine, ni kwa wale wazabuni ambao wanatoa huduma katika eneo lile, basi wawe ni Watanzania wenye uwezo wa kutoa huduma ile na hasa wale ambao wanakaa maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hiyo, naunga mkono hoja kwa 100%. Ahsante sana. (Makofi)