Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia machache katika Wizara hii muhimu. Awali ya yote, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo ameonesha kufungua milango ya kiuwekezaji na anaendelea kufungua milango mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona jinsi ambavyo wawekezaji wengi wanaendelea kuingia nchini kwa ajili ya kuwekeza. Hii ni ishara tosha kwamba, Mheshimiwa Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweka demokrasia, na pia kuna utulivu na amani ya kweli inayosababisha wawekezaji hawa waone kwamba kuna tija kuwekeza hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijachangia naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Kitila pamoja na timu yako nzima, kwa maana ya watendaji wote kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya. Nasema mnafanya kazi nzuri kwa sababu hii ni Wizara mpya na leo ndiyo kwa mara ya kwanza tunakwenda kupitisha bajeti yenu. Pamoja na huo upya, Wizara hii imefanya mambo mengi; imeweza kuipeleka Kamati ambayo mimi ni Mjumbe, kwenda kujionea kwa macho hizi kongani za viwanda ambazo wawekezaji wetu wanawekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ziara yetu, kama jinsi ambavyo mjumbe mwenzangu Mheshimiwa Zedi amesema, tumekutana na mambo mengi sana sambamba na changamoto nyingi ambazo tumezikuta kule kwa wawekezaji wetu ikiwa ni pamoja na miundombinu. Huko katika kongani ambazo tulikwenda Mkoa wa Dar es Salaam kwa maana ya Kigamboni, Ubungo, Pwani kwa maana ya Jimbo la Kibaha Vijijini kule Kwala, tumekuta jinsi ambavyo miundombinu kwa kweli haijakaa sawa, hususan barabara, maji na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema umeme kwa sababu, kule kongani ni kubwa, nitaelezea baadaye jinsi ambavyo uwekezaji ni mkubwa. Umeme uliopo ni mdogo na hivyo, unahitajika umeme mkubwa ambao utekwenda kuwasaidia hawa wawekezaji waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi. Pamoja na changamoto hizo za miundombinu, lakini tumeona jinsi ambavyo Sheria yetu ya Uwekezaji iko vizuri, lakini ni kama haisomani na sheria nyingine zilizopo nchini.

Mheshimiwa Spika, Sheria hii ya Uwekezaji…

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, Taarifa. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Michael Mwakamo.

TAARIFA

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na mchango mzuri ambao anaendelea nao Mheshimiwa Mbunge, napenda kumpa taarifa kwamba, pamoja na hiyo Kongani ya Kwala anayoizungumza, hilo Jimbo la Kibaha analolitaja kuna eneo lingine la uwekezaji lipo pale Soga. Eneo hili nalo lina tatizo la barabara kwenda kwa wawekezaji wa Tanchoice. (Makofi)

SPIKA: Nikawa nawaza, mbona makofi yamekuwa ya ziada? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, naomba niipokee hiyo taarifa kwa sababu, kwanza kabisa inatoka kwa Mbunge wa Jimbo na analifahamu jimbo lake kuliko sisi ambao tumekwenda siku moja. Naomba niendelee.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naendelea kuelezea Sheria za Uwekezaji. Nimesema Sheria za Uwekezaji hazisomani na sheria nyingine. Kwa mfano, mwekezaji akiwa China, Uturuki au Marekani, anapokuwa anasoma Sheria hii ya Uwekezaji, anasoma yale yanayohusiana na uwekezaji, lakini anapoingia nchini hapa sasa, tayari anaanza uwekezaji, ndipo anapokutana na sheria nyingine ambazo kimsingi, kama angekutana nazo day one anavyokuwa anasoma kwenye Sheria ya Uwekezaji ni aidha angeamua kuongeza mtaji aliokusudia au angeamua asubiri kwanza na vitu kama hivyo. Mwekezaji huyu anapoingia nchini anakutana na Sheria ya Ardhi, anakutana na Sheria ya Mazingira, mambo ya Uhamiaji, mara OSHA, NEMC pamoja na mambo ya CEA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najaribu kuwaza na siku hiyo tuko kwenye ziara tuliuliza, hivi ni kwa nini hizi sheria zisisomane? Kwa mfano, mwekezaji anapokuwa anasoma ile Sheria ya Uwekezaji afahamu moja kwa moja, kwenye ardhi kuna nini? Kwenye suala la mazingira kuna nini? OSHA wanataka nini? Ili anapokuwa anaamua kuwekeza awe kweli amejifunga mkanda akijua ugumu au wepesi anaokwenda kukutananao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna hili suala la CEA. Natambua eneo lile kongani, mfano ya kule Kwala ambako tulienda ukiondoa ile ya Ubungo pamoja na Kigamboni, huu ni mpango mkakati wa Serikali kwamba, kule ni sehemu ya Kongani za Viwanda.

Mheshimiwa Spika, sasa kama ni jukumu la Serikali kutenga lile eneo, wakati mnalitenga ni kwa nini hamkufanya hii CEA? Kwa sababu, mwisho wa siku ninyi ndio mnaomwambia mwekezaji tunataka ukae hapa. Huenda usingemwambia akae hapo, angeenda kuwekeza kwetu Kagera ambako labda hakuna hayo mambo ya kufanya CEA na vitu kama hivyo, lakini kama Serikali mkasema hili eneo tunaliweka maalumu kwa ajili ya Kongani za Viwanda, ni kwa nini sasa gharama hizi zimwendee mwekezaji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu tumekutana na wawekezaji wa namna hiyo. Hii inanipeleka sasa moja kwa moja kwa mwekezaji mmoja ambaye ana kiwanda kinachoitwa Modern Industrial Park. Mwekezaji huyu ni Mtanzania mwenzetu ambaye ameamua kuwekeza a lot of money kwenye hii kongani. Kiwanda chake ndani yake kuna viwanda 202, pia ajira rasmi kwenye hii kongani ni 30,000. Hizi ni ajira direct, lakini ajira ambazo ni indirect ni 200,000. Kwa hiyo, kwa jumla mwekezaji huyu anakwenda kutoa ajira kwa Watanzania 230,000.

Mheshimiwa Spika, pia mwekezaji huyu gharama za uwekezaji wake wote mpaka unakamilika ni shilingi trilioni 3.5. Hii ni pesa nyingi, ni uwekezaji ambao kama Serikali, kiukweli tunapaswa kuuangalia kwa jicho la pili, kuwaondolea kadhia ambazo walizieleza siku ile tukiwa kwenye ziara. Kwenye hii kongani huyu mwenyeji ambaye nimesema kwamba ni mzawa, ni Mtanzania, ameweza kufanya mambo mengi sana.

Mheshimiwa Spika, wakati anaendelea kusubiri mfumo wa maji rasmi, ameweza kuchimba visima vingi sana pale. Ametengeneza barabara mwenyewe zenye kilometa 29, kwa maana ya ndani kwa ndani, ule mzunguko wa ndani na wa nje, kwa fedha zake yeye mwenyewe. Hii inaonesha ni namna gani mwekezaji huyu amedhamiria kabisa kuwekeza nchini, lakini anakumbana na hizi changamoto ambazo nimesema ziweze kufanyiwa kazi ili mwisho wa siku uwekezaji uweze kuwa na tija.

Mheshimiwa Spika, katika kiwanda hicho wameenda mbali, wameweka kituo cha zimamoto, wameweka zahanati, wamefanya kila kitu na wakati wanasubiri umeme wa TANESCO ambao uko kwenye process nzuri sana, hapa ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kwani mwekezaji huyu ameamua kuvuta mwenyewe umeme wa Megawati 52. Kwa sasa, anahitaji ile kazi ya kupeleka umeme mkubwa zaidi iweze kufanyika, ili mwisho wa siku uwekezaji wake uweze kuwa na tija.

Mheshimiwa Spika, tumeenda kwenye Kiwanda cha SINO TANS. Kiwanda hiki ndani yake kuna viwanda vidogo 200, ajira rasmi ni 100,000 na ajira ambazo ni indirect ni 500,000. Mradi huu mpaka unakamilika unakwenda kutumia dola za Kimarekani 300,000,000. This is a lot of money. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema ni pesa nyingi kwa sababu, ukiangalia mazingira, siyo rafiki sana pamoja na jitihada zote ambazo tunaziona. Sasa naishauri Serikali, hizi changamoto ambazo nimezielezea, Mheshimiwa Waziri Profesa Kitila sina wasiwasi na wewe, sina shida na wewe, najua nia yako njema ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, naijua vizuri sana. Hata kule katika ziara yetu tumeambiwa jinsi ambavyo una PR nzuri sana na wale wawekezaji. Hiyo haitatosha kama wawekezaji hawa hamtawapa vile vitu ambavyo mliwaahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mliahidi vivutio vya kikodi. Mheshimiwa Profesa Kitila wakati tupo kwenye ziara wawekezaji wote tuliokutananao wameongelea suala hili. Mnawaahidi vivutio, lakini wakija mambo yanakuwa siyo shwari.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Profesa Kitila, wakati anakuja hapa ku-wind up anisaidie huu mkwamo wa kufanikisha jambo hili la vivutio vya kikodi, umekwama wapi? Atueleze amekwama wapi, ili kama Bunge sasa tuweze kusaidia kwa nia njema ya kuweza kutimiza ile nia njema ya Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niseme jambo moja lingine, katika nchi yetu tunatambua pamoja na jitihada za Serikali za kuleta ajira, bado suala la ajira ni changamoto kubwa sana, lakini wawekezaji hawa, nimesema na nimetaja kwa baadhi, unaweza ukaona jinsi ambavyo wanaajiri vijana wengi, akinamama wengi na baba zetu walio wengi.

Mheshimiwa Spika, tulienda kwenye kiwanda kimoja cha kutengeneza nguo pale Ubungo, tulipoingia kwenye kile kiwanda tulitiwa moyo sana. Kwanza, tulikuta wanawake ni wengi kuliko wanaume ambao wanashona zile nguo; jeans, ambayo kushona huitaji elimu ya kuwa na degree. Hata kama ni darasa la saba anafundishwa mpaka anakwenda kuwa fundi mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ungefika pale ungeona jinsi ambavyo wanawake wale, mabinti wale, kama siyo kwa ajira ile ungewakuta wanavuta bangi mtaani, ungewakuta wanajiuza barabarani kwa sababu hawana kipato. Kupitia ajira hizi, tuna akina dada wameajiriwa wanasaidia familia zao, mama zetu na mashangazi zetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, wawekezaji hawa (investors) tukiwatengenezea mazingira rafiki ya kuwekeza zaidi, tutakuwa tunakwenda kutatua changamoto kubwa sana ya ajira kwa vijana waliosoma, ambao hawajasoma, mama zetu na kila namna ya watu wa aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia…

SPIKA: Kengele ya pili ilikuwa imeshagonga. Dakika moja, malizia.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa, kwa nia yake njema ile ile ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, atuelezee kabisa haya mambo niliyoyasema akianza na lile la vivutio, kwa sababu, wameeleza kinagaubaga wakasema mpaka wanafika sehemu wanatamani kwenda kuwekeza kwa wenzetu. Ni kwa nini tuondoe ajira? Ni kwa nini tuondoe mzunguko wa pesa ndani ya nchi wakati vitu vidogo vinaweza kupatiwa ufumbuzi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa machache hayo, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi, pia ahsante kwa kunivumilia. (Makofi)