Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi ya kuchangia, katika Wizara yetu mpya hii ya Mipango na Uwekezaji. Mahususi naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kweli ameanzisha Wizara hii na kwa umakini kabisa akaweka Wizara hii chini ya Ofisi yake ili aweze kuisimamia vizuri.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Profesa Kitila Mkumbo kwa kuwa Waziri wa kwanza kuongoza wizara hii. Naamini ndugu yangu kwa weledi wake amepewa ukapteni kuhakikisha kwamba sasa jahazi linakwenda vizuri akisaidiana na wenzake Katibu Mkuu, Dada yetu Dkt. Tausi Kida na watendaji wake wakuu wote; Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Ndugu Lawrence Mafuru, Msajili wa Hazina, Ndugu Nehemia Mchechu, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Charles Itembe na Mkurugenzi wa TIC, Gilead Teri pamoja na watumishi wote ndani ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, mahususi kabisa naomba kutumia mchango wangu katika Wizara hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jambo la kihistoria katika uwekezaji ndani ya Taifa letu. Jambo lenyewe ni jana tumeona treni yetu ya SGR kwa mara ya kwanza inatembea kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma na ikibeba viongozi na imetumia takribani masaa manne. Ni jambo la kujipongeza sana katika ukombozi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaona kazi njema ya Wizara hii na mimi nikisema ni Mjumbe wa Kamati na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ambayo inasimamia Kamati hii, wanafanya kazi nzuri sana. Tumeona katika mpango wa kurekebisha mazingira ya biashara (blue print) kuna mambo mengi ambayo mpaka leo yamefanyika. Tunaona mapitio ya sheria ambazo zilikuwa zinabainika kuchelewesha au kukwamisha uwekezaji ndani ya nchi yetu. Mpaka leo tunaona zaidi ya sheria 55 zimeshafanyiwa mapitio.
Mheshimiwa Spika, tunaona tozo mbalimbali ambazo zilionekana kwamba hizi tozo zinaweza kuleta kero na zimeweza kupunguzwa au nyingine kufutwa. Zaidi ya tozo 374 zimefanyiwa marekebisho. Ni jambo la kujipongeza sana kwa kuleta mazingira ya uwekezaji ndani ya nchi yetu yakawe huru zaidi na kuvutia sana wawekezaji wetu.
Mheshimiwa Spika, Wizara hii haijaishia hapo, imeendelea kuunganisha majukumu ya taasisi, yale yanayofanana na kuondoa yale yanayoingiliana. Tumeona Taarifa ya Mheshimiwa Waziri asubuhi hapa, ameunganisha taasisi nyingi, lakini tukiangalia mahususi tunaona kweli wakati mwingine unasema wakati wote tulikuwa wapi. Ukiona Bodi ya Maziwa na Bodi ya Nyama, sasa hivi zinaenda kutengeneza Bodi ya Mifugo.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli ukiangalia yale majukumu yaliyopo ndani ya bodi hizo ni kama yanafanana. Ukiangalia sasa katika Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku, ilikuwa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa na sasa hivi tunaona Taasisi ya Utafiti wa Kilimo. Ni mambo ambayo kwa kweli ukiyaangalia na matokeo yake unajivunia kwamba kwa kweli nchi yetu imedhamiria kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji lakini pia na kurahisisha uwekezaji ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, katika maeneo haya tunaona kweli pia kuna Tume ya Mipango ambayo ipo katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Tunaona dira ndiyo kiongozi na mwongozo unaosaidia katika kuendesha nchi. Kwa hiyo tunaamini Dira hii ya 2050 ikishakamilika, basi nchi yetu itakuwa katika mwelekeo ambao kila kiongozi anayekuja anafuata mwongozo huo.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hilo tunaona dira yetu lazima ifungamanishe nchi yetu na malengo ya kikanda na kimataifa. Tunayo malengo ya Africa Agenda 2063 ambayo lazima tujifungamanishe nayo. Pia, tunayo malengo ya East Africa Vision 2050, lakini pia tunayo malengo ya SADC Vision 2050. Haya yote na nchi yetu ikiwa na dira ambayo imekuwa reflected katika eneo hilo basi tunaamini kwamba tutakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili, niombe tu ufafanuzi wa Wizara wakija kuhitimisha. Tunaona mchakato wa kutengeneza hii Dira ya Taifa ya 2050 inapitia kama hatua tatu. Tunaona katika maandalizi ya awali, tunaona katika usanifu na uidhinishaji. Tukiangalia huu muda na tukiangalia katikati hapo inapitia katika maeneo mbalimbali kukusanya maoni ya wadau. Kwa kweli ni process ambayo ni ndefu.
Mheshimiwa Spika, sasa hii Dira yetu ya 2025 inakaribia mwisho. Kwa hiyo watupe comfort na msimamo wa Serikali kwamba ni kwa jinsi gani wataweza ku-catch up katika muda huo kabla ya Dira 2025 haijaisha, basi na hii angalau imeshakuwa in place kwa ajili ya ku-take over na nchi yetu sasa iendelee kusonga mbele.
Mheshimiwa Spika, kimsingi nitaongelea katika suala la kujumuisha mienendo ya kikanda na kimataifa na hivyo kutuleta sisi tukawa sehemu ya malengo uliyotaja Africa Agenda 2063, East Africa Vision na SADC na za kimataifa. Nitaongelea suala la health safety na nitaangalia vis a vis Bureau of Standards.
Mheshimiwa Spika, na-declare kwamba once upon a time nilikuwa mtumishi ndani ya taasisi ambayo inasimamia suala la afya. Katika eneo hili kwa weledi ambao nimeuona ndani ya Wizara hii ya Mipango na Uwekezaji, kwa weledi ninaouona kwa wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri hili suala sitaki kulisema na Mheshimiwa Waziri, naomba anisikilize vizuri. Hapa nina-deal na health safety vis a vis Bureau of Standards.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2003, Bodi ya Madawa na Tume ya Kudhibiti Chakula Salama Tanzania ziliunganishwa. Hiyo Tume ya Chakula ilikuwa inaitwa TUKTA na lengo la kuunganisha Bodi ya Dawa na Tume ya Kudhibiti Chakula ilikuwa kuunganisha nguvu moja ya udhibiti na kuunda chombo ambacho ni kimoja, yaani kuleta harmonization. Pia, ililenga kupanua wigo katika udhibiti, kuongeza bidhaa nyingine za vifaa tiba na vipodozi, viungane na dawa na chakula iwe moja.
Mheshimiwa Spika, msingi wa udhibiti huu unazingatia malengo ya kikanda na malengo ya kitaifa (Regional and International Best Practice) duniani kote. Ukiangalia katika maeneo hayo upande wa Bureau of Standard si wadhibiti wa bidhaa ambazo zinahusiana na afya ya binadamu, si wadhibiti wa bidhaa ambazo zinahusiana na afya ya wanyama, si wadhibiti wa bidhaa ambazo zinahusiana na afya ya mimea. Maana yake viongozi wangu wakienda kuangalia kwenye Sanitary and Phytosanitary Agreement ya World Trade Organization watakuta haya mambo yote yameainishwa pale yanaenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali; ukiangalia duniani kote zimeunda chombo cha udhibiti na kuweka bidhaa zote ndani ya mamlaka moja. Wameweka dawa ndani ya mamlaka moja, wameweka chakula ndani ya mamlaka moja, wameweka vipodozi na vifaa tiba. Naelewa inawezekana nchi yetu kuna vitu ambavyo iliona na hasa najua changamoto ilikuwa ni tozo mbalimbali, lakini si huo uhalisia wa health safety katika bidhaa hizo.
Mheshimiwa Spika, tukitoka hapa twende Kenya hapa jirani wanayo Kenya Food and Drugs Authority ambayo inasimamia bidhaa zote. Ukienda Marekani utakuta kuna USFDA, Canada, heath Canada inasimamia vyote, China utakuta CFDA, India kuna India FDA, Thailand utakuta Thailand FDA, Singapore na Ghana FDA.
Mheshimiwa Spika, kitu cha kushangaza na kizuri zaidi mtoto wetu ambaye amezaliwa hapa Zanzibar Visiwani, Zanzibar Food and Drugs Authority ambaye tumemlea sisi na sasa hivi anafanya kazi nzuri iliyotukuka, yeye bado ni taasisi moja ambayo inasimamia bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.
Mheshimiwa Spika, naongea haya kama sehemu ya utaalamu wangu kwamba pamoja na changamoto za kibiashara ambazo naungana na Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya, zitatuliwe. Tunapokuja kwenye suala la afya kidunia niombe Mheshimiwa Profesa Kitila, yeye ni mweledi pamoja na wasaidizi wake, hili suala tusilichukulie kwa mtazamo wa kawaida, wa juu juu. Leo tunazo bidhaa nyingi mtaani ambazo ni za chakula, leo tunazo bidhaa nyingi za vipodozi na kila nikisimama nasema kuhusu suala hilo. Hii nchi tunaendelea kubana matumizi, hatuwezi kuwa tunatafuta dawa lakini vyakula vilivyopo huku mtaani na vipodozi vinaenda kutumia zile dawa na nyingine kuathiri hata afya za wananchi. Kwa hiyo niombe, tukiweka udhibiti mzuri katika bidhaa hizi na sioni Serikali inakosa nini kwenda na mfumo kama ambavyo malengo yetu katika blue print yanatutaka kujumuisha mienendo ya kikanda na mataifa, tukaenda kama nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika, niombe sana katika eneo hili, suala la vyakula na vipodozi. Sina interest na Wizara yoyote lakini naiangalia Serikali yangu ifanye kazi vizuri, imsaidie mwananchi kulinda afya yake, isaidie kabisa katika udhibiti bidhaa hizo ambazo zote zina market sana sokoni. Tukisikiliza wafanyabiashara wetu wakataka mteremko bila sisi kuweka udhibiti ambao unatakiwa kidunia na kikanda nasita kusema huko mbele tunapokwenda bajeti ya dawa itaongezeka, vifaa tiba ambavyo tunanunua havitatosha na hospitali anazojenga Mheshimiwa Rais hazitatosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niombe sana na nihitimishe kwa kusema, Mheshimiwa Waziri aangalie kwenye blue print yake. Page nyingi zimeelezea kinagaubaga kwamba, hizi bidhaa zinatakiwa kusimamia nini na naamini kwa weledi wake ataweza kufanya vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa kengele ya pili, naomba nikushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)