Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo kwa hotuba yake iliyojaa taarifa muhimu zinazotuwezesha kushauri mambo mbalimbali kuhusu Ofisi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mashirika ya umma 16 kuunganishwa na manne kufutwa; taarifa kwa vyombo vya habari ya tarehe 15 Disemba, 2023 aliyoitoa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo akieleza kuwa Serikali imeridhia na kuelekeza kuunganishwa kwa mashirika na taasisi 16 na kufuta mashirika na taasisi za umma nne. Maamuzi haya yamerejewa na Waziri katika Hotuba yake ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, ibara ya 29 na 30. 2.1. Changamoto kufuatia uamuzi huu wa Serikali wa kuunganisha na kufuta mashirika na taasisi za umma ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, Mashirika na Taasisi za Umma yalianzishwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge na hivyo hayawezi kufutwa na tamko la Waziri bila ridhaa ya Bunge. Suala la kuunganisha na kufuta mashirika na taasisi za umma ni la kisera na kisheria na linahitaji mjadala mpana kwa kushirikisha wadau na Bunge. Nimefuatilia taarifa ya Kamati za Bajeti na PIC za mwezi Februari, 2024, suala hili halikujadiliwa na Kamati husika na wala hoja hii haijaletwa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali kuingilia kazi za mhimili wa Bunge na kuharibu mahusiano mema yaliyopo. Bunge linaweza kukataa kufuta au kufanyia marekebisho sheria zilizoanzisha mashirika hayo huku Serikali imeshatangaza hadharani uamuzi wa kuunganisha au kufuta mashirika hayo. Tangazo la Waziri la kufuta na kuunganisha mashirika na taasisi za umma halijaainisha sheria iliyompa mamlaka kutoa tamko hilo na hakuna GN. Tangazo la Waziri la kufuta na kuunganisha mashirika hayo liko kwenye mchakato wa awali kwa kuwa Serikali bado ina mchakato unaoendelea katika Wizara husika hivyo hatua hizi hazikuwa zimefikiwa kutangazwa kwenye umma kama ilivyooneshwa katika kipengele cha 5(ii) na (iii) ya tangazo la Waziri. Tangazo hilo la Serikali kwa sehemu kubwa limerudisha nyuma kasi ya utekelezaji wa mikakati na programu ya mashirika husika, lakini pia imeshusha morali kwa watumishi wa mashirika hayo yaliyotangazwa kufutwa au kuunganishwa kutojua hatma yao.

Mheshimiwa Spika, tatu, tangazo la kufuta au kuunganisha mashirika na taasisi za umma halina maelezo na taarifa muhimu zinazothibitisha uhalali wa maamuzi hayo. Hivyo Waziri, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo alijielekeza vibaya kufikia maamuzi haya katika kipengele cha 4 cha tamko lake kwani badala ya kutangaza kufuta mashirika manne na kuunganisha mashirika ya umma 16 alipaswa kuwasilisha mapendekezo Bungeni kama sheria, kanuni na taratibu zinavyotaka.

Mheshimiwa Spika, Bunge halifanyii kazi maamuzi ya Serikali bali linajadili na kupitisha mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali. Kwa urahisi wa rejea nanukuu kipengele cha 4 cha tamko la Waziri kama ifuatavyo; “Kufuatia taarifa na mapendekezo ya timu ya wataalam, katika awamu ya kwanza, Serikali imeridhia na kuelekeza kuunganishwa kwa mashirika na taasisi 16 na kufuta mashirika ya umma manne. Natangaza mashirika na taasisi za umma zinazounganishwa na kufutwa ni kama ifuatavyo...” mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mashirika yanayounganishwa au kufutwa, kwa muda mrefu tumekuwa tukiishauri Serikali kuunganisha au kufuta baadhi ya mashirika na taasisi za umma ambazo zina majukumu yanayofanana na kuingiliana kiutendaji, yanayojiendesha kwa hasara na kutegemea ruzuku ya Serikali. Kiujumla sina tatizo na uelekeo huo isipokuwa naukosoa utaratibu uliotumika kufikia maamuzi. Taarifa ya uchambuzi wa timu ya wataalam kuhusu utendaji wa mashirika ya umma inapaswa iwasilishwe kwa Bunge ili kukaribisha majadiliano zaidi kuhusu uamuzi huu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu tangazo la Waziri kuna baadhi ya mashirika na taasisi za umma ambazo binafsi naridhia kufutwa au kuunganishwa, lakini zipo baadhi ya taasisi na mashirika ya umma ambazo haziwezi kuunganishwa wala kufutwa kulingana na unyeti wake katika Taifa. Kwa mfano, sioni mbadala wa Taasisi ya Chakula na Lishe (Tanzania Food and Nutrition Centre-TFNC) katika kipengele cha 4B(ii) ambapo inapendekezwa kufutwa taasisi hiyo. Vilevile sio mantiki ya kuunganisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Uzalishaji wa Mauzo Nje (EPZA) kama ilivyooneshwa kwenye kipengele cha 4A(vi) ya Tangazo la Waziri.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuunganishwa EPZA na TIC; EPZA na TIC ni taasisi nyeti na zilianzishwa kwa malengo na majukumu tofauti na hivyo itakuwa vigumu kuunganisha mashirika hayo. Malengo mahususi ya TIC kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania Na. 26 ya mwaka 1997 iliyorejewa mwaka 2022, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimepewa jukumu la kukuza, kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji nchini Tanzania. Kwa kifupi lengo kuu la TIC ni kuvutia uwekezaji Tanzania. Malengo mahususi ya EPZA, kwa mujibu wa Sheria ya Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje, Sura ya 373 malengo ya kisera yaliyotajwa, kazi za EPZA kwa mujibu wa Sheria ya EPZ na SEZ ni kuendeleza, kusimamia na kukuza kanda maalum za kiuchumi pamoja na kanda za uzalishaji kwa mauzo ya nje ya nchi kwa dhana pana ya kuchochea uzalishaji kupitia viwanda hususani vinavyoongeza thamani. Katika kutekeleza azma hiyo EZPA hutwaa ardhi na kuweka miundombinu na mahitaji mengine muhimu katika maeneo ya kiuchumi ili kuvutia wawekezaji na kutoa leseni ya uendelezaji na uendeshaji wa maeneo maalum ya uwekezaji na kanda maalum za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, changamoto za kuunganisha EPZA na TIC ni pamoja na:-

(i) Kupoteza malengo na mikakati iliyopo ya kila taasisi; itakuwa vigumu kupatanisha na kulinganisha vipaumbele na mikakati ya kufikia malengo ya kisera;

(ii) Kupoteza au kufifisha dira na dhamira ya uwekezaji, maendeleo na ukuzaji wa viwanda nchini;

(iii) Kupoteza imani kwa wawekezaji, uzoefu duniani ni kuwa taasisi hizi ni tofauti na hivyo kuunganishwa kutapelekea kuoanisha na kuunganisha sera, sheria, kanuni na vivutio vya uwekezaji jambo ambalo litaonekana kwa wawekezaji kuwa nchi yetu ina sera zisizotabirika;

(iv) Mgongano wa kimaslahi, kuunganisha EPZA na TIC kuwa taasisi moja tutapelekea taasisi mpya kutekeleza majukumu yanayokinzana. Mgongano wa kimaslahi utatokea kwa sababu taasisi mpya itatekeleza kazi inayofanywa na TIC ya kukuza na kuwezesha na kutumika kama kituo cha kutatua malalamiko ya uwekezaji wakati huo huo ikitekeleza majukumu ya udhibiti (authority) wa utoaji wa leseni za SEZ na EPZ pamoja na kuhakikisha kuwa wawekezaji wanafuata sheria na kanuni za nchi na mamlaka yake; na

(v) Mchakato wa kuziunganisha taasisi hizi utapelekea kuchelewa kutekeleza mambo muhimu yanayozikabili taasisi hizi kwa sasa, hivyo badala ya kukimbilia kuziunganisha taasisi hizi, Serikali iziongezee uwezo hususan mtaji stahiki wa ujenzi wa maeneo maalum ya kiuchumi na mahitaji maalum ya kitaasisi yatakayoboresha taswira ya nchi kiuwekezaji. Nimeshindwa kupata ushahidi wa moja kwa moja kwamba kuunganishwa kwa taasisi hizi mbili kutapunguza gharama za uendeshaji ama kuongeza ufanisi wa utendaji wa mashirika haya na zaidi naona kwamba tunakwenda kubomoa badala ya kujenga.

Mheshimiwa Spika, nilitegemea Serikali ingeweka nguvu kubwa kutafuta suluhisho la matatizo ya msingi yanayozikabili programu ya EPZ na SEZ ambalo ni hitaji la rasilimali za kifedha kuwezesha kutwaa ardhi na kuendeleza miundombinu ya SEZ kwa madhumuni ya kustawisha ukuaji wa viwanda. Hivi sasa EPZA imeshindwa kulipa fidia na kusababisha kuongezeka kwa deni kutokana na riba ya ucheleweshaji wa malipo ya fidia katika kanda maalum za kiuchumi zilizoainishwa na Serikali. Tatizo la mtaji haliwezi kutatuliwa kwa kuunganisha mashirika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa muda mrefu pia imeshindwa kutatua changamoto za kisheria zinazokikabili Kituo cha Uwekezaji na Mamlaka ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje na hata baada ya kutolewa mapendekezo ya mpango wa kuboresha mazingira ya biashara nchini (blueprint), hivyo changamoto za kisheria zilizopo baina ya taasisi hizi haziwezi kutatuliwa kwa kuunganisha mashirika. Serikali irejee malengo na madhumuni ya kuanzisha taasisi hizi, pia huko nyuma Serikali baada ya kuona ufanisi mdogo kwa taasisi moja kusimamia sheria na programu zaidi ya moja iliamua kuhamisha majukumu ya programu za EPZ kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na SEZ kutoka Tume ya Taifa ya Mipango (NPC).

Mheshimiwa Spika, uzoefu wa baadhi ya Nchi nyingine duniani kama China, Malaysia, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Ghana, Mauritius, Afrika Kusini na Misri taasisi hizi hazijaunganishwa. Huu ni mfano tu wa mambo ambayo hayako sawa katika tamko la Waziri na ndiyo maana nashauri Serikali ifute tamko lake hili na badala yake ifuate utaratibu wa kuwasilisha Bungeni pendekezo la kuunganisha na kufuta baadhi ya mashirika ya umma ili kupata uwanda mpana wa kupata maoni ya wadau na maamuzi ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.