Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Innocent Edward Kalogeris

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ambayo iko mbele yetu. Nitumie nafasi hii ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kung’ara.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Morogoro Kusini kwenye upande wa umeme, mwaka huu tumeweza kupewa zaidi ya bilioni 20 kwa ajili ya kufanikisha jambo hilo. Nitumie nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati pamoja na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya. Kiuhalisia na kwa kweli nina imani kubwa na wao na naamini kwamba imani yangu kwao wataweza kumsaidia sana Mheshimiwa Rais, Mama huyu ili aweze kuifikisha nchi pale ambapo anataka ifike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Meneja wangu wa TANESCO wa Wilaya na Watendaji wote ambao wako chini ya Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Vilevile, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa umeme ambao tumeupata.

Mheshimiwa Spika, tunavyo vijiji 89 tunapozungumza leo hapa tayari vijiji 83 vyote vinawaka umeme na dada yangu Kapinga tulikuwa wote katika Kata ya Lundi kwa ajili ya kuwasha umeme na hivi sasa vimebaki vijiji sita ambavyo tayari kila kitu kimekamilika isipokuwa ku-charge na kuviwasha. Wananchi wa Morogoro Kusini tuna kila sababu ya kumpongeza Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya.

Mheshimiwa Spika, katika vitongoji ambavyo tunavyo ni 437 lakini mpaka leo hii tunavyozungumza, vitongoji 162 vina umeme na vitongoji 60 vipo katika utaratibu wa kuwekwa umeme (nguzo zimekwishasimamishwa na waya zimekwishawekwa bado kuwashwa tu). Vilevile, tuna vitongoji 15 ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza kwamba vitakuja. Hivyo, tutakuwa tumebakiwa na vitongoji 200 ambavyo havina umeme. Ombi langu kwa Serikali, tuhakikishe na kuangalia tunafanya vipi ili kuhakikisha hivi vitongoji navyo vinawaka umeme ili tutakapokuwa tunakwenda kwenye uchaguzi 2025, Wanamorogoro Kusini tuseme hakika Mama Samia Suluhu Hassan, ameitendea haki nafasi ambayo amepewa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo nitumie nafasi hii kuwasilisha ombi maalum kwa TANESCO. Sisi Halmashauri ya Morogoro Vijijini tunapata umeme kutokea Pwani lakini pia tunapata umeme kutokea Morogoro Mjini. Hatuna kituo cha kupoza umeme. Mara tu itakapotokea hitilafu, halmashauri yote inakosa umeme.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo tayari sasa hivi limekwishapeleka umeme kwenye gridi ya Taifa, tunawaomba watupatie line ndogo ikaunganishwe na mvua ili lolote litakalotokea, halmashauri yetu iendelee kuwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii pia kuwaomba Makao Makuu ya TANESCO, Ofisi ya TANESCO katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini wako ndani ya container. Ni vizuri basi Meneja wa TANESCO wa Morogoro DC akapata ofisi na gari litakalomfanya akafike katika maeneo ya mbali. Pia katika hilo suala la magari kwenye Mkoa wa Morogoro ambao ni Mkoa wa Kimkakati kwa TANESCO, bado tuna upungufu wa magari. Mwaka 2023 nilisema na nikapata ahadi kwamba watafanya lakini hawajafanya. Niiombe Wizara ikamilishe jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, sasa nije kwenye suala la Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tunayo kila sababu ya kumpongeza Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ya ukamilishaji wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tunapoingia sasa hivi, tayari 98% limekamilika, nina shida moja ambayo mwaka jana nilisema na mwaka juzi pia nilisema. Hadi tunakamilisha kufikia asilimia hiyo, bado CSR ya Bwawa la Mwalimu Nyerere haijafika kwa walengwa wenyewe ambao ni Mkoa wa Morogoro, Pwani na Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Pwani na Lindi tuna shida, jana ndugu yangu Kuchauka alikuwa amezungumza na akafika mahali hapa akasema anataka kukamata shilingi ya Mheshimiwa Waziri. Kwangu mimi nasema sitokamata shilingi ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu Waziri na msaidizi wake ni watu wema na wenye hofu ya Mungu. Tulipofikia hapa ni kwa sababu ya watangulizi wake kwenye TANESCO na watangulizi kwenye Wizara. Waliweka mbele maslahi binafsi na wakaamua kudhulumu haki ya Wanamorogoro na wananchi wa Pwani.

Mheshimiwa Spika, ninachojua ni kwamba, Lindi wamepewa bilioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha TEHAMA. Nimwombe Ndugu yangu Mheshimiwa Kuchauka, Lindi imeguswa, amwachie shilingi yake ndugu yangu Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ili akatekeleze majukumu. Pia imepelekwa shilingi bilioni 80 Kigoma, shilingi bilioni 40 Dodoma, shilingi bilioni 40 Tanga. Tunaomba shilingi bilioni 80 iende Morogoro ambayo ni ya Kigoma, shilingi bilioni 40 Dodoma na ile ya Tanga iende Pwani. Wananchi wa Morogoro na Pwani tuna haki hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mafuriko ambayo yanatokea leo hii Mlimba, Malinyi, Ifakara, Rufiji na Morogoro ni kutokana na uhifadhi wa mazingira ambayo yanapeleka maji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, tuna haki ya msingi kupata hela hiyo. Kwa hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ni mtu mwema na muungwana sana, kupitia timu yake ya TANESCO ambako Mtendaji mpya amepatikana watupe haki yetu Wanamorogoro. CAG amekwishasema kwamba wakae, walishakaa zaidi ya mara mbili, Wizara na Mkandarasi, Mkandarasi anawakatalia kwa sababu miradi waliyoipeleka haihusiani na mkataba unavyosema.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba, sisi wananchi wa Morogoro na wananchi wa Pwani tuko tayari kukaa pamoja na Wizara watupatie haki yetu, naomba sana Ndugu yangu Mheshimiwa Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ni mtu makini na naamini kama nilivyosema ana hofu ya Mungu, sitaki kukamata shilingi yake, lakini naomba atusaidie Wana-Morogoro.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)