Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ili nitoe machache kwenye hii Wizara ambayo kimsingi ndio catalyst ya uchumi (ndio inachochea ukuaji wa uchumi), ni kwamba bila umeme uchumi hauwezi kukua. Tunaweza tukaona mfano mdogo tu wa nchi ambazo tulikuwa tunadhani zimeenda mbele, lakini leo zina-suffer sana kwa sababu ya umeme. Mfano kama South Africa, leo tunavyoongea South Africa ina mgao wa umeme mpaka masaa nane. Kwa hiyo sasa unaweza uka-imagine kama nchi ina mgao wa umeme kwa masaa nane; je, uzalishaji wake ukoje? Kama unatumia generator ni gharama kiasi gani inatumika kuzalisha umeme?
Mheshimiwa Spika, niongelee tu kitu kidogo sana, mfano kama wafanyabiashara wa Kariakoo, niongee kwa niaba yao. Kumekuwa na tendency ya kukatika kwa umeme tukijua nature na mazingira ya Soko la Kariakoo kweli biashara zina-suffer sana. Unakuta wamefungua generators, ni makelele lakini pia wanatumia gharama kubwa sana na hiyo gharama si kwamba wanaibeba wao, at the end of the day gharama hiyo inaenda kwa yule anayeenda kununua biashara zao, kwa hiyo tuliangalie sana.
Mheshimiwa Spika, nitaanza kwa ku-scrutinize budget kwa sababu mwisho wa yote yaliyofanyika katika Wizara husika yanapimwa kwa fedha kiasi gani imeenda kule chini. Utekelezaji wa bajeti ya hii Wizara bado ni mdogo kwa maana fedha iliyoenda mpaka mwezi Februari ni 52.27% roughly, ukiona mfano mishahara ni 69%, OC ni 17%, fedha ya maendeleo kutoka kwenye fungu la ndani ni 50% kutoka nje 69% ambayo bottom line inaleta 52.27%.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo bajeti kwa kutotimia walau hata ingefika 70% au 80% tungejua kwamba miradi mingi tuliyokaa kuijadili Bungeni imetekelezwa, lakini kwa bajeti kuwa 52% ni lazima miradi mingi haijatekelezwa na imeelezwa kwenye Taarifa ya Kamati. Nisisitize kwamba at least hii Sekta ya Umeme tukijua umuhimu na ukubwa wake katika uchumi, bajeti yake basi iende hata kwa 100%. Ndiyo namna pekee ya kuzuia kukatika kwa umeme, ndiyo namna pekee ya kuzuia kero za umeme ambazo tumekuwa tukizisikia hapa na hapa. Pia, itaondoa hata Mawaziri wenyewe, watu wanakuwa wanasema Waziri huyu ameshindwa hii wizara imeshindikana, ni kwa sababu ya fedha. Fedha isipoenda hata mshahara wa Waziri hautoshi kusema kwamba atachukua hela yake au maduhuli yaweze kusaidia upatikanaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, niende kuongelea changamoto ya umeme katika Wilaya ya Kyerwa. Kyerwa tuna vijiji 99, tunashukuru mpaka sasa naongea vijiji 92 vimewaka umeme bado vijiji saba. Naomba sana hivi vijiji viwashwe umeme. Vijiji hivyo nitavitaja; kuna Kijiji cha Rwamashaju, kinapatikana Kaisho, kuna Kijiji cha Kakerere. Hiki Kijiji cha Kakerere kinapatikana katika Kata ya Nkwenda ya Mjini kabisa. Sasa unajiuliza hii inakuwaje? Kijiji cha Ruhita, Kamuli; Kijiji cha Nsunga kiko katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa yenyewe, Kijiji cha Kijumbula, Kijiji cha Kitega. Hii Kitega nimewahi kusema kwamba Kitega ipo mpakani mwa Rwanda, ilikuwa na changamoto ya mawasiliano na vitu kadha wa kadha. Kwa kipekee sana eneo la Kibare nilikuwa nikiongelea hapa Kijiji kinaitwa Kigorogoro kina changamoto ya maji na umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naomba hivi vijiji vyetu saba Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri vipelekewe umeme na vyenyewe vijione ni vijiji sawa na vijiji vingine. Ni kwa nini naombea umeme specific katika haya maeneo? Ni kwa sababu umeme ndio catalyst, umeme ndio tunauhitaji kwa ajili ya kuendesha maisha na Uchumi, lakini wamewawekea nguzo, wamebaki kuziona zile nguzo kama mapambo, si sawa.
Mheshimiwa Spika, nikiongelea Jimbo la Karagwe ambalo ni jimbo jirani. Karagwe ina vijiji 77 na vijiji 76 vimewashwa umeme kuondoa Kijiji kimoja tu cha Nyabiyonza, si sawa. Nawaombea watu wa Nyabiyonza pia waunganishiwe umeme ili wawe pamoja na wenzao. Kwa hiyo katika masuala ya umeme naomba niishie hapo. Tumekuwa tukiongelea…
Mheshimiwa Spika, nina dakika 10, naona kama kengele imewahi, mimi sina dakika saba. Tumekuwa tukiongelea matumizi ya nishati safi ya kupikia. Hakuna anayebisha kwamba matumizi ya kuni yanaharibu mazingira, hakuna anayebisha matumizi ya kuni ni ghali; hakuna anayebisha katika hilo, lakini nataka niulize ni kwa kiwango gani sasa tumeweza kusaidia upatikanaji wa miundombinu ya mabomba au ya kuwezesha kupatikana kwa nishati hiyo tunayoisema ni nishati safi ya kupikia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, Taarifa ya Kamati imeonesha ukitumia hiyo nishati mbadala ya kupikia utaweza ku-save kiasi gani. Hiyo gesi asilia imeonyesha unatumia shilingi 27,000, lakini kwa kitu kilekile utakachokipika kwenye mkaa utatumia shilingi 40,000 ambayo una-save 32%. Kitu kile kile ukitumia gesi ya mtungi ya LPG utatumia shilingi 76,000 ambayo ni sawa na 64%, lakini kitu hichohicho chenye quantity hiyo utakachokipikia kwa umeme utatumia shilingi 105,000 ambayo ni sawa na 74%.
Mheshimiwa Spika, leo tunavyoongea naishukuru Wizara, wametusaidia, tumepata mitungi ya gesi, lakini watu wakija kujaza gesi watahitaji gesi ya LPG ambayo it is too expensive. Kwa hiyo, namna pekee ya kuwezesha upatikanaji wa nishati ambayo ni nafuu ni kwa kutumia LNG. Sasa ni lazima mitambo iwekwe ili hii gesi iweze kuwafikia watumiaji.
Mheshimiwa Spika, kwa Dar es Salaam pekee, habari ya kusambaza gesi hiyo ili itumike viwandani na nyumbani imekuwa ni story ya muda mrefu, lakini kimekuwa ni kitu ambacho hakitekelezeki. Kwa nini? Hiyo gesi inapatikana hapa nchini, kwa hiyo, itatumia gharama kidogo. Hizo tunazoita LPG zinatoka nje, na kwa hiyo, tunatumia dola kununua hizo LPG ambazo ni expensive, kumbe hiyo LNG tutapata hapa nchini na tutaokoa fedha.
Mheshimiwa Spika, Wabunge wengine wengi sana wameongelea matumizi ya gesi kwenye gari, nasi tuseme basi na Dodoma hicho kituo kijengwe haraka sana ili kusaidia kupunguza matumizi ya petrol na diesel. Diesel na petrol zinaagizwa nje kwa dola ilhali gesi inapatikana hapa nchini. Hivyo, tungeweza kuokoa fedha ya kutosha na kwa sababu hiyo tungeweza kupunguza gharama kwenye uendeshaji.
Mheshimiwa Spika, hii Wizara isipowekewa bajeti ya kutosha na isipoweza kukusanya fedha, haitaweza kutekeleza malengo yake. TANESCO unayoiona hapa imekuwa ikidai fedha nyingi sana. TANESCO inadai Wizara kadhaa ambazo hazilipi ankara lakini Wizara hizo hizo zimekuwa zikija hapa Bungeni, tunapitisha bajeti zao ikiwa ni pamoja na kununua umeme.
Mheshimiwa Spika, nataka nijue, ni kwa nini wanakuwa hawalipi ankara zao na hivyo kuifanya TANESCO ishindwe kujiendesha? Mwaka hadi mwaka unaambiwa TANESCO mizania yake iko chini, haijatengeneza faida, lakini Wizara hizo hizo zimekuja, tumezipitishia na zina hela ya kununua umeme, lakini hazilipii umeme.
Mheshimiwa Spika, hiyo hiyo TANESCO imekuwa ikidaiwa. Yaani ni mchezo wa kuku na yai. TANESCO inadaiwa. Mfano mdogo tu, TPDC inaidai TANESCO zaidi ya shilingi bilioni 720. Yaani ni wale wale watoto wa baba mmoja, kati ya kuku na yai ametangulia nani? Sasa hicho ni kitu gani? Ninadhani ifikie wakati hizi Wizara ziwe harmonised. Kama ni Wizara ya Maji ama Wizara nyingine zozote unazoweza kuzitaja, zinunue umeme kwa kulipa kwa kuwekewa mita. Kama ni pre au post, zilipe, lakini vilevile na TANESCO ilipe. Hiyo ndiyo namna pekee ambayo tunaweza kuondoa hiki tunachokiona.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, nakushukuru, lakini nisisitize juu ya vijiji vyangu vya Kyerwa na hivyo vijiji ambavyo sasa vimewashwa umeme. Kule ni pakubwa, yaani unakuta kijiji kimoja, ndiyo zimewashwa sasa nyumba 20, lakini hicho kijiji ni kikubwa sana kiasi kwamba ukishaondoka, inakuwa kwamba wale wajiunganishie umeme kwa mfumo wa TANESCO ambao ni shilingi 300,000. Hii haitakaa iwezekane, hawataweza.
Mheshimiwa Spika, Kyerwa ni moja kati ya Wilaya ambazo zinatajwa kuwa maskini. Sasa maskini kama sisi tunawezaje kuunganisha umeme kwa shilingi 300,000? Kwa hiyo, narudia, nasimama pamoja na Wabunge wengine ambao wamesisitiza umuhimu wa shilingi 27,000 kuendelea kutumika. Hata kama hiyo REA ikiwa imekamilika, ikirudi kwenye TANESCO, basi baadhi ya maeneo yawe considered na hivyo wawafungie umeme kwa gharama hiyo. Nakushukuru sana kwa nafasi.