Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia.

Mheshimiwa Spika, kwanza, naipongeza Serikali na nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweza kufanya mabadiliko na kumweka Waziri mpya, Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko. Tunakupongeza sana na kwa kweli umefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuwepo humu huu ni mwaka wa nane. Wizara hii ni moja ya Wizara ambayo leo humu tusingekuwa tunaongea, lakini tangu jana kwa kweli kila Mbunge ameona jitihada zako, hongera sana kwa unyenyekevu wako, pia hongera kwa timu yako.

Mheshimiwa Spika, nadhani na timu yako sasa umeipa nafasi ya kuwa na afya ya akili ya kufikiria vizuri jinsi gani tunaweza tukalipeleka shirika vizuri kuliko vitisho na mambo mengine yaliyotokea huko nyuma. Nakupongeza sana, na ninaamini mtaendelea kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TANESCO tunawafahamu vizuri, mmepata Mwenyekiti mzuri, Bwana Nyansaho amefanya vizuri sana kwenye benki, nami ni mkopaji kwake. Ulifanya vizuri benki, sasa ukija kutuzamisha huku, nadhani hatutaelewana. Ukifanya vibaya, Bunge lijalo tutakushughulikia vizuri.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie mambo machache. Kwanza Mheshimiwa Waziri tunakupongeza kwa hali ya umeme na jinsi mlivyokuwa watulivu, hamko mitandaoni na hamko kwenye TV na watu wanaona jinsi mnavyofanya kazi. Hongereni sana. Umeme kwa sasa umeimarika ukilinganisha na hali ya nyuma pale ulivyokuwa unaingia, tulikuwa kwenye hali mbaya sana. Mungu awabariki sana, mwendelee kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati, nina baadhi ya mambo nataka kushauri. Kuna baadhi ya sehemu humo TANESCO siyo nzuri. Mheshimiwa Dkt. Doto fanya reshuffle, na ulishapewa hilo rungu na Mheshimiwa Rais. Tunaona kuna sehemu ambazo siyo nzuri, nami nitatoa mfano wa sehemu moja.

Mheshimiwa Spika, nenda kaangalie mkataba wa uwekaji umeme wa Mji wa Serikali. Umeme wa chini ule kwa kizungu mnaita underground, au siyo, ule umeme kwenye mikataba ya kuomba kwenye tender, yaani mtu wa mwisho alikuwepo wa shilingi bilioni 37, shilingi bilioni 39 na shilingi 41, lakini kwenye kusaini mkataba umesainiwa kwa shilingi bilioni 55, yaani shilingi bilioni 14 zimeongezeka kutoka wanakojua wataalam.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi ninakushauri tu Mheshimiwa Waziri, mimi ni wa muda mrefu; naomba uende kwenye manunuzi, mle angalia kuna watu urekebishe ili pakae vizuri. Model nzuri anzia huo Mji wa Serikali kwenye umeme wa underground, utagundua kitu kilichofanyika.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, sisi tunatoka vijijini, na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wengi humu wanatoka vijijini. Tulianzisha vituo vya kuwasaidia wananchi wetu kule vijijini, lakini ghafla vikafungwa, watu waanze kushughulika na simu aliyoisema Mheshimiwa Mpina. Natoa mfano, jana tu, sisi na Nyehunge tuko Jirani. Kumetokea short ya umeme, nyumba imekata umeme na kurudi zaidi ya mara kumi. Watu wanapiga simu Dar es Salaam, simu haishikwi, nyumba imeungua mpaka imeteketea.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na Kituo cha Nzera ambacho kilikuwa kinaweza kufanya kila kitu, kimenyang’anywa mamlaka mpaka upige simu Dar es Salaam. Hii siyo sawa. Sisi tunakoishi, kwingine kuna umeme, lakini hakuna network ya simu. Sasa ni vizuri kwa sababu vituo hivi mmesambaza umeme vijijini kwa watu maskini, ni lazima kuwe na sehemu ambazo mtu anaweza akakimbia kwa miguu, siyo lazima apande gari.

Mheshimiwa Spika, suala la tatu nataka kuchangia kuhusiana na suala la gesi. Mimi ni Mjumbe wa Kamati, tumeenda India na Dar es Salaam tumeona. Wenzangu wamesema, ukitaka kuweka gesi leo kwenye vile vituo viwili vya Dar es Salaam unaenda saa tisa usiku. Tumefika pale saa tano, watu wanaongea kutuelimisha, wale watu waliopanga foleni wanasema hivi, hawa ni Wabunge au ni akina nani? Wamekuja kufanya nini? Hatuna shida ya Wabunge, tunataka gesi. Kwa saa tisa mtu anakaa kwenye foleni kwenda kujaza gesi.

Mheshimiwa Spika, mimi ninashauri, kitu kizuri huwa kinaanzia kwenye Serikali na ukiangalia masharti, yaani wale wale wenye sheli ndiyo watengeneza mfumo. Hii mifumo inaweza kutengezwa na mtu yeyote kwa sababu hakuna kitu kigeni. Kwa mimi genius niliangalia mara moja tu, hata ukinipa gari lako leo nakuundia. Sasa masharti yamewekwa kwenye kituo, bei anapanga yeye na bei ya gesi yeye na kutengeneza mfumo yeye.

Mheshimiwa Spika, kitu kizuri ambacho nilijifunza, gari kama V8 kutoka Dar es Salaam kuja hapa Dodoma ukitumia mafuta utatumia kama shilingi 500,000 lakini ukitumia gesi, utatumia shilingi 94,000 kwenda na kurudi.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu tunahangaika na Mr. Kichere sana kwenye matumizi mabovu ya Serikalini, ninashauri V8 zote za Mawaziri tuzifunge mfumo wa gesi. Kwa sababu kwanza sasa hivi muda mwingi na mko Dar es Salaam, mko Dodoma, sasa kwa kubana matumizi tukiwapiga ile mitungi kule nyuma msafiri hata kila wiki kwenda mara tatu Serikali itakuwa ime-save kutoka shilingi 480,000 mpaka shilingi 97,000 kwenda na kurudi.

Mheshimiwa Spika, nadhani na watu wengine tungeanzia hapo ili hata tukisema humu suala la kuongeza vituo vya gesi mtakuwa na uhitaji kwa sababu ya zile routes zenu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, ni kengele ya pili!

SPIKA: Ya pili, ahsante sana.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)