Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kuendelea kutupa afya na uzima, ili kuendelea kuwatumikia wananchi waliotuchagua. Tunajadili Bajeti ya Wizara ya Nishati kukiwa na utulivu mkubwa sana. Hii inatokana na sababu mbili; ya kwanza, ni hali ya umeme nchini ni nzuri sana na ya pili ni hali ya upatikanaji wa nishati ya mafuta kwenye vituo ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kuchukua nafasi hii, kwanza kabisa kumshukuru Kinara na Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais wetu, kwa kusimamia vizuri Serikali kiasi mbacho mambo haya yanakwenda vizuri kiasi hiki.

Mheshimiwa Spika, pia nachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ambaye pia ni Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara, Manaibu na watendaji wote wa taasisi za TANESCO, REA, TPDC, PBPA, EWRUA, PURA na TGDC. Hawa wote kwa sababu mimi niko kwenye Kamati hii, kwa kweli wanatoa ushirikiano mzuri sana kwa Kamati yetu kiasi ambacho na sisi tunaona kazi wanayoifanya ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa hali nzuri ya umeme nataka kutoa ushauri ufuatao; la kwanza ni TANESCO waendelee na kasi ya kuunganisha mikoa ambayo haiko kwenye Gridi ya Taifa, hasa inayotumia umeme wa mafuta, ili kuendelea kuwasaidia katika kupunguza gharama za uendeshaji na uzalishaji wa umeme. Mkoa kama Kigoma umeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa katika wilaya tatu tu, waendelee kukamilisha kwa sababu, hizi wilaya zilizobaki ambazo zinatumia umeme wa mafuta, zinawalia gharama kubwa sana ya uzalishaji wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kwa sababu sasa wanakwenda kuzalisha umeme wa gharama nafuu, yaani wa maji, na kupunguza umeme wa gesi na mafuta, basi TANESCO nayo ioneshe uungwana kwa kuwalipa TPDC deni lao awamu kwa awamu kuliko sasa hivi ambapo TANESCO inadaiwa shilingi bilioni 720 bila kutikisika kwa muda mrefu. Kwa hiyo, tunaomba sana TANESCO wachukue hizo hatua mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa REA, ndugu zangu kazi kubwa sana imefanyika. Ni basi tu, sisi wengine inawezekana hatupati nafasi ya kwenda kuona kwenye nchi za wenzetu, lakini zipo nchi za wenzetu tena jirani hapa, Makao Makuu ya Kata hakuna umeme, Makao Makuu ya Vijiji hakuna umeme, sisi sasa hivi tunazungumza habari ya kupeleka umeme kwenye vitongoji. Napenda kuwapongeza sana REA pamoja na kwamba changamoto bado ipo, lakini kuwatia moyo ni kuwaongezea ari ya kuifanya kazi hii vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzangu wengi wamezungumzia mafanikio tunayoyapata katika suala zima la kutumia CNG, yaani gesi kwa ajili ya uendeshaji wa magari. Kwa sababu ninahudumu kwenye Kamati hii nimepata nafasi ya kuona, lakini jambo ambalo nataka kuishauri Serikali ni kwamba, suala la kuweka vituo vya kujaza gesi kwenye magari, msihangaike nalo ninyi kama Serikali, itisheni sekta binafsi. Mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe umeona, kituo kile cha Taqwa ni cha sekta binafsi, ukifika unaona kweli hiki ni kituo cha kuweka CNG. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda katika kituo chetu kina pump mbili tu, hawa wana pump sita halafu zipo vizuri, wanahudumia watu 1,000 kwa siku. Sisi katika sera yetu, katika miaka ya 1990 tulibadili sera. Serikali haimiliki njia kuu za uchumi. Serikali sasa imebaki ni mhimili wa uchumi. Njia kuu za uchumi sasa zinasimamiwa na sekta binafsi. Kote ambako tumeshirikisha sekta binafsi, tumefanikiwa na hata pale tulipoingia ubia na sekta binafsi tumefanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii unaangalia TANOIL inayosimamiwa na Serikali imeanza kufa, lakini kule kote ambako tumewekeza pesa za Serikali kwenye sekta binafsi kama vile Puma Energy, kwenye Benki za CRDB, NMB, TBL, TCC, ALAF, kote huko tunapata gawio na mashirika haya yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, msijibebeshe mzigo wa kuhangaika na vituo vya CNG, itisheni sekta binafsi wafanye hii kazi. Mheshimiwa Waziri kama unavyofahamu kuna maombi 11 ya kuweka vituo pale Dar es Salaam, harakisheni kuwapa vibali hawa waweke vituo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni jambo la aibu, tumewahamasisha watu kutoka magari 1,000 mwaka 2023 mpaka magari 3,000 mwaka huu, halafu watu wanapanga foleni masaa matano, sita, wanasubiri kujaza gesi. Waruhusuni hawa walioomba wapewe vibali waweke vituo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala zima la gesi kwa matumizi ya kupikia nyumbani. Kwa sasa tunatumia natural gas kwa sehemu ndogo sana ambayo imepelekewa hizi pipe kule Dar es Salaam. Natural gas ambayo inatumika Dar es Salaam, ambayo imeanza kuunganishwa katika taasisi, gharama yake ni nafuu sana. Kilo moja ni kama shilingi 1,000, lakini LPG hii ya mitungi ambayo tunasambazia watu, gharama yake kilo moja ni shilingi 4,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima tufike mahali Serikali ije na mkakati. Serikali ilikuwa imeanza kufanya utafiti wa kuona namna ya kuweza kufika mahali kutumia natural gas iweze kuwa LPG ili kuweza kuisambaza kwa urahisi zaidi. Endeleeni na utafiti huo ili utafiti ukikamilika basi tuweze kuanzisha plant ya LPG, ili iweze kusaidia kusindika hiyo gesi na kuiweka kwenye matenki na kuipeleka maeneo mbalimbali kwa matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli, jambo moja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Ooh!

Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia kwa kusema kwamba, kwa sababu hii LPG kwa sasa ina gharama kubwa na wananchi wetu wanavutiwa kuitumia, Serikali sasa iangalie uwezekano wa kufika mahali ianzishe utaratibu wa ununuzi wa pamoja wa gesi hii ya LPG kama ilivyofanya kwa mafuta, ili wananchi waweze kuipata kwa gharama nafuu. Ahsante sana. (Makofi)