Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa ya kuweza kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya leo. Pia, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya, bila kusahau kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wa Jimbo la Msalala, tuna imani kubwa sana na Waziri. Naendelea kumwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, apatapo wasaa, basi wananchi wa Jimbo la Msalala wanamwalika aweze kufika kuzungumza nao. Wanatamani sana waweze kusikia sauti yake. Karibu sana Jimbo la Msalala Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Nakiri kwamba Sekta hii ya Nishati ilifikia wakati watu wakatunga nyimbo mbalimbali, wakatunga misemo mbalimbali, kwa ajili ya kukosekana kwa umeme.
Mheshimiw aSpika, ilifikia kipindi TANESCO ikawa inatumika kwenye kibonzo kimoja nilikiangalia, mtu mmoja anamwambia mpenzi wake kwamba, mimi siwezi kuwa kama TANESCO kwa hiyo, naomba uniamini. Maana yake TANESCO ilifikia hatua mpaka ikaonekana kwamba, hawana uaminifu na hawaaminiki katika nchi hii, lakini wewe Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko umeweza kurudisha hali na ikawa sawa na sasa watasema kauli zilizonyooka kama TANESCO, kwa sababu TANESCO kwa sasa imetulia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naanza kwa kuipongeza Taasisi ya TANESCO, pia nawapongeza sana watu wa REA. Katika Jimbo la Msalala, vijiji takribani 64 vilikuwa havina umeme, lakini tunavyozungumza hivi, tayari jitihada zinaendelea kuhakikisha ya kwamba vyote 64 wanapatiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, naomba sana kuleta ombi langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwamba, katika Wilaya ya Kahama kuna halmashauri tatu na halmashauri zote hizi tatu tuna kata zaidi ya 58 ambazo tayari zote tunaenda kupatiwa umeme vijiji vyote.
Mheshimiwa Spika, tunaomba sana, kwa ukubwa wa Wilaya ya Kahama, utenge fedha katika bajeti hii, Mheshimiwa Waziri, twende pale tukaanzishe Wilaya ya ki-TANESCO kwenye Wilaya ya Kahama, kwa sababu vijiji vyote ukiangalia, kwa mfano kama mimi nina vijiji 92, na vijiji vyote hivi viko mbalimbali. Kwa hiyo, tunapata taabu sana pale tatizo la umeme linapotokea, ukizingatia tuna uhaba wa magari kwenye eneo lile, basi inatusababishia ugumu sana kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, kingine ninachoomba ni Wizara iweze kuwatengea watu wa TANESCO fedha za kutosha. Tunatumia fedha nyingi kupeleka umeme vijijini, lakini umeme hausambai, matokeo yake sasa tunajikuta tunatumia gharama kubwa kupeleka umeme na umeme hausambai kwa sababu, wananchi hawapati huduma ya kuvutiwa umeme. Hii ni kwa sababu ya bajeti ya kusambaza umeme. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye Kata ya Segese, miji mingi inakua sana kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwenye Kata ya Segese, Kata ya Bulyanhulu, Kata ya Isaka na kata nyingine wanahitaji huduma ya umeme, lakini bado bajeti ya usambazaji wa umeme kwenye maeneo hayo imekuwa ni ngumu sana. Kwa hiyo, naendelea kukuomba sana kutenga fedha kwa ajili ya kwenda kusambaza umeme kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri kwenye suala zima la gesi. Ni kweli Wizara imefanya jitihada kubwa kuhakikisha kwamba inasambaza gesi za nyumbani. Nakushukuru sana kwa kutupatia kibali kwenda kufanya ziara nchini India, tumeenda pale tumejifunza. Nami nataka kuiomba Wizara, kupitia yale ambayo tumejifunza na ushauri wetu, ni wakati sasa umefika wa kuanza kubuni njia mbadala za kwenda kuzalisha gesi ambayo itasaidia kupunguza gharama kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, leo hii ukiangalia kwa mfano Wilaya ya Kahama, pale tunalo dampo la uchafu wa taka ngumu na taka za vyakula ambazo tulipoenda India kujifunza, tumeona ni namna gani wenzetu wanatumia taka za chakula na takataka nyingine kutengeneza gesi. Hiyo inawezekana kabisa.
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu tutengeneze mfano kwenye Wilaya na Halmashauri ya Msalala. Dampo tunalo, tupeni fedha sasa tuweze kujenga kiwanda kile ambacho hakina gharama yoyote. Inaweza ikawa ni dola 100,000 au 200,000 kujenga kiwanda kile cha kutengeneza gesi asilia na wananchi wetu wakapata gesi ambayo kimsingi ina gharama nafuu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naendelea kuzungumza kwenye suala zima la wakandarasi na uzambazaji wa umeme. Nataka kushauri kwenye suala hili, tunapoenda kuwapatia wakandarasi kazi za kufanya, utaona wakandarasi wageni wanakuja na kuchukua zile kazi, lakini nani anafanya kazi zile za kusambaza umeme kwenye maeneo hayo? Kwa sehemu kubwa bado unakuta ni Watanzania ndio ambao wanafanya kazi hizo za kusambaza umeme.
Mheshimiwa Spika, naomba watu wa TANESCO, watu wa REA, Mheshimiwa Waziri, nenda kaliangalie hili. Punguzeni masharti ili kuwawezesha wakandarasi wa ndani kuweza kufanya shughuli hizi kwa sababu, hata kama mtawapa wakandarasi hawa wakubwa, hawafanyi kazi hizo, wanaofanya ni wananchi wa Tanzania na uwezo huo wanao. Kwa hiyo, naomba sana TANESCO nendeni mkaone namna ya kuanza kuwakuza wawekezaji na wakandarasi wa humu ndani waweze kufanya shughuli hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapata changamoto nyingi sana, watu wetu wanateseka kule, lakini mkiweza kuwawezesha hawa wakandarasi maana yake ni nini? Fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya miradi hii itabaki hapa hapa ndani na pia, mtasaidia zaidi kutengeneza ajira kwa vijana wetu kwenye maeneo haya. Kwa hiyo, naomba sana suala hili, Wizara na Mheshimiwa Waziri mwende kulifanyia kazi ili wakandarasi wetu hawa waweze kupunguziwa masharti na waweze kutumia fursa hii kwenda kupata ajira na kazi hizi za umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri, lakini naomba uzingatie hili kwamba, tunahitaji Wilaya ya ki-TANESCO katika Wilaya ya Kahama ili kuweza kufanya facilitation katika maeneo yetu ya vijijini na wananchi wa vijijini waweze kupata haki ya kupata umeme.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, nakupongeza sana kuhakikisha kwamba umepeleka umeme kwenye maeneo ya wachimbaji. Wachimbaji wanahitaji nishati hii ya umeme. Naendelea kuomba mwendelee kuongeza kasi kubwa ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kupunguza gharama za kufanya shughuli kule kwenye maeneo yao na kuweza kujitengenezea uchumi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo, nashukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)