Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami leo niweze kuchangia kwenye hii Wizara ya Nishati. Kwanza, kwa sababu muda siyo rafiki, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa alizozifanya hasa katika ukamilishaji wa Bwawa hili la Mwalimu Nyerere ambalo limegharimu jumla ya shilingi trilioni 6,500 ambazo zimekaribia kulipwa zote na bwawa limeanza kuzalisha. Tumeanza kupata Megawatts 235 ambazo zinaingia kwenye gridi ya Taifa. Hongera sana Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi hii ilikuwa imeachwa kwa 37% na sasa umeikamilisha kwa karibu 95%. Kwa hiyo, tunakupongeza. Umeongeza umeme katika gridi ya Taifa kutoka megawatts 1,872 mpaka megawatts 2,138 sawa na ongezeko la 14%. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Wizara kwa kusimamia vizuri mradi huu. Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko hatuna shida na wewe, unachapa kazi vizuri na tunakuamini kwamba, wewe ni mmoja wa Waheshimiwa Mawaziri wachapakazi na hodari.

Mheshimiwa Spika, pamoja na bwawa kukamilika, tunaamini pia, mmekamilisha njia ya kusafirishia umeme kutoka Hydropower Mwalimu Nyerere mpaka Chalinze, ni hatua kubwa sana, hongereni sana. Pia kukamilika kwa njia ya usafirishaji wa umeme kutoka Morogoro mpaka Dodoma kwa ajili ya treni ya umeme na yenyewe pia tunawapongeza. Naona kwenye kitabu chao wameweka bajeti ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme katika njia ya treni ya umeme ya SGR kutoka Dodoma mpaka Tabora. Nawapa pongezi nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaipongeza Wizara kwa kazi nzuri ya kukamilisha kupeleka umeme katika vijiji vyote nchi nzima, hasa jimboni kwangu, hongereni sana. Jimbo zima la Manonga, vijiji vyote vimefikiwa na umeme na sasa kazi inaelekea kwenye vitongoji.
Mheshimiwa Spika, tuna jumla ya vitongoji 31,000 Tanzania nzima ambavyo havina umeme. Hapa sasa namwaomba Waziri aweke uzito mkubwa kuhakikisha kwamba vijiji hivi 31,000 vilivyobaki nchini anavivalia njuga. Hapo awali bajeti ilikuwa ni karibu shilingi trilioni sita na yalikuwa ni matarajio. Kwa hiyo, naomba uangalie namna ya kuweza kuvikamilisha kwa wakati ili vitongoji vyote nchini viweze kunufaika na umeme.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mkurugenzi wa REA kwa kazi nzuri. Eng. Hassan nakupongeza sana kwa kusimamia vizuri miradi hii ya REA vijijini, endelea kuchapa kazi. Sisi Waheshimiwa Wabunge tunakuamini pamoja na Wizara yako tunaiamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri Dkt. Doto Biteko, kwenye suala zima la TPDC. TPDC ni uchumi wa nchi. Naomba Mheshimiwa Waziri apate muda akatembee Saudi Arabia, akatembee Oman, akayaone mashirika makubwa ya petroli yanavyoleta uchumi wa nchi hizo za Oman pamoja na Saudi Arabia. Oman kuna PDO na Saudi Arabia kuna RAMCO, Tanzania tuna TPDC.

Mheshimiwa Spika, naomba hili Shirika la TPDC tulipe fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya kazi ya kuhakikisha kwamba, tunazalisha mafuta kwa sababu, tumeanza kuona dalili za kupata mafuta. Katika njia ile ya pale Wilayani kwetu Igunga, kwenye lile Bwawa la Mto Eyasi Wembele, tunazo taarifa za kupatikana kwa mafuta. Tumeona mmeanza kuchakata kwa kutumia 2D. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri ongeza fedha twende kwenye 3D tuweze kupata haya mafuta ili tuweze kuyatumia kwa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TPDC inaidai TANESCO zaidi ya shilingi bilioni 700. Tunaomba TANESCO fedha hizo zirudishwe TPDC ili TPDC iweze kujisimamia na kuweza kufanya kazi nzuri. Pia napenda kukupongeza Mheshimiwa Waziri, bajeti yako mwaka huu unaoisha ilikuwa ni shilingi trilioni tatu, bajeti unayoiomba ni shilingi bilioni 1,800. Maana yake kuna punguzo la karibu shilingi bilioni 1,200. Hii inamaanisha nini?
Mheshimiwa Spika, miradi mikubwa ambayo mlikuwa mkiisimamia imepungua kwa maana sasa mnaenda kukamilisha, lakini fedha hizi Mheshimiwa Waziri mngezipeleka kwingine, mkazijaziliza kwenye umeme vijijini na vitongojini.

Mheshimiwa Spika, kingine, tunatambua mahitaji ya miundombinu, TANESCO Wilayani kwetu Igunga tuna uhaba wa magari. Mheshimiwa Waziri tunakuomba, Wilaya yetu ya Igunga ni kubwa sana, tunahitaji magari ya TANESCO.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Igunga inahudumia majimbo mawili, lakini sisi kwetu Jimbo la Manonga pamoja na miundombinu, unatambua jiografia yetu. Umeme wa Igunga unatoka Wilaya ya Nzega, unatembea zaidi ya kilometa 150 kuja Igunga na wakati mwingine huku mwanzoni ambako ni Chomachankola, Ziba, Nkinga, umeme huu unasafirishwa kutoka Nzega unakuja Igunga, unapelekwa Wilaya ya Uyui kwa ndugu yangu huyu Mzee wa Igalula, Loya. Umeme ukikatika huko, Wilaya ya Igunga yote umeme unakatika na miundombinu ya magari hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atupatie gari, pale Wilaya ya Igunga aongeze gari lingine, hasa maeneo ya Choma au Ziba, kwa ajili ya kurahisisha movement zile za watu, wapo ambao wanaweza kutembea. Kwa ujumla, Mheshimiwa Waziri, ninawapongeza sana Wizara kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupongeza kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Yangu yalikuwa ni hayo na ninaiunga mkono Bajeti ya Wizara hii ya Nishati. Ahsante sana. (Makofi)