Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii ambayo ni kichocheo kikubwa sana cha maendeleo katika nchi yetu na katika dunia kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, nami nianze na shukurani kubwa sana kwa Rais wetu jinsi ambavyo katika sekta hii amefanya mambo makubwa sana kwa muda mfupi sana. Tunapomsifu Mheshimiwa Rais, mara nyingi tuna-relate na muda.
Mheshimiwa Spika, unakuta jambo linafanyika kubwa kwa muda mfupi sana. Kwa hiyo, hata tunapopongeza kila wakati naomba sana Watanzania wawe wanaelewa kwa nini tunampongeza Mheshimiwa Rais kiasi hiki na kila anayesimama, ni kwa sababu usipompongeza Rais, kwa haya aliyoyafanya kweli wewe utakuwa ni mtu usiye na shukurani.
Mheshimiwa Spika, Rais alikuta Bwawa la Mwalimu Nyerere lina 37%, leo tunaongelea 99%, kwa miaka mitatu. Mradi wa takribani trilioni saba, wananchi waelewe tunapompongeza. Sisi wananchi wa Mkalama shukurani yetu tutaionesha mwaka 2025 kwa kufanya maajabu kwa kupiga kura kwa wale wote watakaojiandikisha kwa asilimia, tutaomba Mungu zifike 100%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninampongeza pia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Wizara hii kwa kazi anayoifanya. Waziri ni mnyenyekevu, mtu mwenye hofu ya Mungu, msikivu lakini zaidi ni mchapakazi. Nadhani hii ndiyo sababu, nadhani hata Mama aliona, akaona amwongezee jukumu la kumsaidia Waziri Mkuu kwa mambo haya ambayo anayafanya. Mungu aendelee kukupa maisha marefu kijana wetu Mheshimiwa Dkt. Doto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawaomba tu Wizara, suala la kufikisha umeme kwenye vitongoji, wananchi wetu wameshauona umeme umefika kwenye vijiji. Jambo kubwa sana katika Afrika limefanyika, lakini wananchi wanaishi vitongojini, wanahitaji kuona umeme umewaka kwenye nyumba zao. Kwa hiyo, naomba sana hili zoezi ambalo sasa Serikali inajikita la kwenda kupeleka umeme kwenye vitongoji, lifanyike haraka na kwa umakini zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba REA wawezeshwe fedha sasa za kununua transformer kubwa. Mawazo tuliyokuwanayo zamani ya KVA 50, tulikuwa tunaviona vijiji kama vijiji, lakini vijiji vyetu vya Tanzania leo hii ni vijiji vyenye maendeleo, ndiyo maana tuna Shule za Kata kwenye Kata zetu zaidi ya tatu au nne. Watu wamesoma, watu wana kazi za kuchomelea na vitu vingine. Vijiji ni utawala tu, lakini shughuli zinazoendelea kule ni kubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sasa REA wapewe fedha ambazo watanunua transformer zenye KVA kuanzia 200 mpaka 315 ili ku-cover eneo kubwa la kijiji au kitongoji. Hata wale wananchi walioko pembezoni mwa kijiji au kitongoji waweze kufikiwa, hizi transformer kubwa zinakwenda mpaka kilomita sita. Kilomita sita ukienda unakuwa umemaliza takribani kitongoji au kijiji kizima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaposema vitongoji, vitongoji vyetu wengine sisi ni sawa na vijiji vya maeneo mengine, tuna vitongoji vikubwa sana havina umeme. Kwa hiyo, tunaomba sana sasa REA waachane na habari ya kwenda na KVA 50. Hizi 50 wapeleke kwa mtu mmoja ana shamba lake au ana nini, ndiyo apelekewe hizo KVA 50, lakini kwenye vijiji na vitongoji vyetu ni KVA kuanzia 200 kwenda juu ndiyo zinaweza ku-cover eneo kubwa na ndiyo tutakuwa tunamaliza moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, maana yake mpaka sasa wale wenye umeme wanalalamika, kwa sababu wanauona kwa majirani, lakini na wale ambao hawajafikiwa wanalalamika. Sasa badala ya kupeleka hii kitu kuwa neema inakuwa sasa kero. Kwa hiyo, naomba sana REA twende na mtazamo wa kuwa na kitu kikubwa kwa sababu wananchi wetu wa Tanzania wanapenda mambo makubwa kama Rais wao anavyowafanyia mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vitongoji vyetu vikubwa, kwa mfano Kitongoji kama cha Tatazi ni kitongoji kikubwa sana, kipo Kata ya Mbambala. Kitongoji cha Nzinziru, Mwadada hivi ni vitongoji sawa na vijiji havijapata umeme. Kitongoji cha Senene, Midibwi, Matere, Mtaa wa Singida pale Mwanga, hivi tunasema ni vitongoji kwa sababau ya utawala, lakini ukienda pale unashangaa ni kijiji kikubwa ambacho kina kaya nyingi na shughuli ni nyingi. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ya uchapakazi wako, hakikisha tunapata umeme kwenye vitongoji hivyo ili wananchi wa Tanzania waendelee kula mema ambayo Mama yao anawapatia katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)