Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii. Naomba nichangie mambo matatu tu. Kwanza naungana na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza sana mtoa hoja, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na timu yake akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba sisi ambao tunamsaidia anayetusimamia, ana sifa nyingi, lakini utulivu ni jambo la msingi sana. Hapa katikati tulikuwa na wakati mgumu sana wa hali ya umeme kutokana na upungufu uliokuwepo, lakini Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko alikuwa ametulia, anafanya kazi kwa utulivu wa hali ya juu. Nadhani hiyo ni shule kubwa sana ambayo ametufundisha. Nawashukuru wataalamu wake kwa ushirikiano ambao wanampa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni muktadha kidogo tu. Katika miaka 20 iliyopita, mwaka 2001 – 2021 nchi yetu ilipoteza hekta milioni 2.86 za misitu na nchi yetu wataalam wa misitu wanasema angalau 40% ni forest cover, na tunapoteza takribani asilimia moja ya misitu kila mwaka ukilinganisha na wastani wa dunia ambayo inapoteza, ni 0.5%. Sababu kubwa ni kukosekana kwa nishati mbadala ya kupikia.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia unaona kwamba, pamoja na jitihada kubwa ambazo tumezifanya kati ya mwaka 2002 – 2022 tulipunguza kiwango cha kutumia kuni kwa takribani 20% kutoka 77% mpaka 55.5%. Kwa hiyo, tumepiga hatua katika miaka 20 lakini bado watu wetu 55.5% wanatumia kuni kwa takwimu za NBS mwaka 2022, na 26% wanatumia mkaa, na kama 14% wanatumia gesi ama umeme. Sasa tunafanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, tunafanya nini? Ndiyo maana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, moja ya eneo kubwa ambalo amelikazania ni suala la kutoa nishati safi kwa ajili ya kupikia. Jambo hili kwa bahati nzuri, mwaka 2023 kwenye Dubai Expo aliweza kuzindua programu maalum ya kuwapa akina mama siyo tu Watanzania, lakini Waafrika, programu maalum ya kupeleka nishati safi ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kazi yetu sisi kama wasaidizi wake ni kuweka sera na mipango mizuri kukamilisha hiyo vision. Tunayo mambo matatu ambayo tunayafanya. Moja ni miradi hii ya REA. Focus kubwa tukishapeleka miradi ya REA vijijini inamaanisha kwamba, wanawake wengi watatumia umeme kwa ajili ya kupikia na kwa hiyo, kuokoa afya zao, pia kuokoa misitu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa ni suala la bei. Wengi wamesema hapa, bei ni kubwa. Kuanzia mwaka huu wa fedha na mipango ijayo, mambo mawili ya kuzingatia ambayo tutaenda kuyafanya, na tutaomba Waheshimiwa Wabunge waangalie kwa muda mfupi, ni Finance Bill ya mwaka huu. Tulikuwa tunaongea na Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa kwamba lazima tuweke hatua za kikodi ambazo zitaelekeza kupunguza gharama za matumizi ya gesi na umeme kwa wanawake hususan vijijni.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la kodi ni suala la Bunge na Serikali tutaleta mapendekezo hapa tuliangalie ili bei zipungue na wanawake wengi zaidi waweze kutumia njia hii.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, hii miradi mikubwa ya umeme ambayo tunaizungumzia, matumizi yake ni mawili tu. Matumizi ya kijamii kama hayo ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza hapa, nyumbani kuwasha taa na kupikia, pia matumizi makubwa sana ni kwenye suala la uzalishaji, viwanda, kilimo na kadhalika. Kwa sasa takribani zaidi ya 50% ya umeme wote ambao tunautumia hapa Tanzania, unatumika Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani kwa sababu ndiko ambako kuna viwanda vingi. Kwa hiyo, hili suala la kuendelea kuzalisha umeme mwingi ni muhimu, na Serikali katika mipango yake itaendelea kuweka mkazo, kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri Mtoa Hoja.
Mheshimiwa Spika, suala la energy mix ni muhimu kwa sababu tunatumia zaidi gesi pamoja na maji, lakini huko mbele lazima umeme wa jua na upepo pamoja na ule wa geothermal ambao Mheshimiwa Waziri aliongea jana, tuendelee kuukazania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lengo la Mheshimiwa Rais ambalo ametupatia, tupunguze matumizi ya kuni na mkaa kwa 88% ifikapo mwaka 2034, na ametuwekea lengo kwamba by 2034 angalau 10% peke yake ya watu wetu wanaotumia kuni na mkaa wabaki huko, lakini 90% watumie nishati safi.
Mheshimiwa Spika, hili ni lengo kubwa ametupatia kwa kushirikiana nanyi Waheshimiwa Wabunge na sekta binafsi. Tunaamini ni lengo ambalo linaweza likakamilishwa. Tutafanya kila liwezekanalo na katika mipango ijayo mtaona, tutaendeleza vizuri sana mikakati ambayo tunayo kufikisha 10% ifikapo mwaka 2034 wanaotumia mkaa pamoja na kuni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, nchi yetu katika kipindi hiki cha mvua imejaliwa mvua nyingi ambayo inageuka kuwa adha. Mpango wa Serikali ni kuendelea kujenga mabwawa ili haya maji mengi tuweze kuyaokota, tuweze kuyadaka ili yatumike siyo tu kwenye umeme, lakini pia kwa lengo la kutumika katika maeneo ya kilimo kama ambavyo tumesema kwenye mpango wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu, katika mpango ambao tutawasilisha tarehe 13 Juni, mwaka huu, 2024 mambo haya tutayaainisha kwa kina, lakini lengo ni kuona kwamba tunaokoa afya za wananchi wetu kwa kuwapa nishati safi ya kupikia lakini pia tunaokoa misitu yetu na kulinda mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)