Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku njema ya leo. Kipekee na kwa dhati ya moyo, naomba kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaofanyika katika Sekta ya Nishati. Hii imejionesha kupitia miradi ya kielelezo na miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa kupitia sekta zetu ndogo za mafuta, gesi pamoja na umeme.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ni kielelezo cha uchapakazi na uzalendo wa kweli. Tunaendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu amwezeshe kutekeleza majukumu yake siku zote kwa heri na baraka tele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba kumshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango pamoja na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa kuendelea kutusimamia na kutuongoza vyema katika sekta yetu ya nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu mkubwa naomba kumshukuru sana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wangu wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Mshaka Biteko kwa kuendelea kutuongoza vyema. Amekuwa kiongozi mwema sana kwangu na watumishi wengine wote katika Wizara ya Nishati na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati. Amekuwa kiongozi anayetusimamia katika kutekeleza majukumu ya Wizara yetu kwa azma na neema. Tunamwombea Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia aweze kutumikia majukumu yake kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kukushukuru wewe, Naibu Spika pamoja na Katibu wa Bunge kwa kuendelea kutuongoza vizuri hapa Bungeni. Kipekee naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako hili Tukufu kwa kuendelea kutuunga mkono. Tunathamini sana maoni yenu ambayo mnatupatia na ushirikiano mkubwa mnaotupatia katika kutekeleza majukumu yaliyo katika Wizara yetu ya Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kipekee nilishukuru Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa ambao wao ndiyo walinipa dhamana ya Ubunge wa Vijana kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi. Baraza hili linaongozwa na kaka yangu Comrade Kawaida Mohammed Kawaida. Namshukuru sana yeye, Mwenyekiti wetu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Wajumbe wote wa Baraza kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika utekelezaji wa majukumu yangu ya Ubunge wa Vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nawashukuru Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvama. Ninapoelekea mwisho wa shukrani zangu, kwa kuwa mimi ni Diwani wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini, naomba niwashukuru wananchi wa Wilaya ya Mbinga kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika utekelezaji wa majukumu yangu. Naomba niwaahidi kwamba nitaendelea kuwapa ushirikiano katika kutekeleza majukumu hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninavyomaliza shukurani zangu, naomba nimshukuru sana mume wangu na familia yangu kwa kuendelea kunivumilia na upendo mkubwa wanaonipatia. Nathamini sana, nami ninawapenda na kuwathamini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya shukurani hizo, naomba nijielekeze sasa kwenye kuchangia hoja za Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na nishati safi ya kupikia, nitasema kidogo kwa sababu Profesa ameeleza vizuri sana. Uhai na afya ya dunia yetu ya sasa ipo kwenye kutunza mazingiara yetu. Linapokuja suala la nishati safi ya kupikia, hii ndiyo nyenzo muhimu ya kutusaidia kutunza mazingira yetu kwa ajili ya afya na dunia ambayo tunaishi.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, ule Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ambao tulikuwa tunaungoja, umeshapitishwa na Baraza la Mawaziri na upo tayari kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipomshukuru Mheshimiwa Rais ambaye ndiye amekuwa kinara wa nishati safi ya kupikia na ametusaidia sana kwa kuwa champion namba moja Tanzania, Afrika na ulimwenguni kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, azma yetu ni kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, lakini kubwa, pamoja na kuongeza kasi, tunataka tuwawezeshe wananchi waweze kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi ili tuweze kabisa kuondoa matumizi ya mkaa pamoja na kuni. Dhumuni la mkakati wetu ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati safi, salama, endelevu na yenye uhakika.
Mheshimiwa Spika, ninafahamu bado tuna hatua kubwa sana katika kuhakikisha tunaondoa kabisa matumizi ya mkaa, lakini ni suala ambalo hatuwezi sisi Serikali kulifanya peke yetu. Ndiyo maana tunaendelea kuomba Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kushirikiana katika kupiga vita matumizi ya mkaa na kuni ili kuhamasisha wananchi waendelee kwenda na matumizi ya nishati safi ya kupikia kama ambavyo tumeanza kupitia mitungi ambayo tunaigawa.
Mheshimiwa Spika, mikakati ambayo tunayo inatekelezeka sana. Jambo ambalo linatutesa sisi ni mazoea tu ya mkaa kwa sababu wapo wengi ambao wana uwezo wa kutumia nishati ya gesi. Ni kwamba tu watu hawaamini kuwa wali nazi wa gesi pia ni mtamu au maharage ya kutumia pressure cooker ambayo inatumia umeme mdogo pia ni mtamu. Ni kuongeza tu mapishi. Kwa hiyo, tuendelee kushirikiana kwa pamoja kutoa elimu tuweze kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumewasikia Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na gharama. Tayari tumeshaanza kufanyia kazi kupitia REA na wadau wetu wengine tunatoa ruzuku. Jambo kubwa lilikuwa ni kwenye kuanza matumizi ya gesi kwenye kupata jiko na vifaa, lakini kupitia REA tunatoa ruzuku ya mitungi na mpaka sasa hivi tumetoa mitungi 83,500 na tunao mkakati wa kutoa mitungi 450,000 ili kuweza kurahisisha matumizi ya awali ya gesi ili kuongeza kasi ya matumizi makubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, kwa kushirikiana na kampuni za gesi, tuna mpango wa kuongeza miundombinu ya kupokelea gesi pale bandarini kutoka tani 5,000 ambazo tunazo sasa hivi mpaka tani 45,000. Mikakati hiyo tunayo kwa sababu tunaamini tukifanya hivyo, basi tutakuwa tumepunguza bei. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine, tumewasikia Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na kuwa na mitungi ya kilo chache. Tayari kampuni zimeshaanza kufanyia kazi. Zipo kampuni ambazo zimeshaingiza sokoni mitungi ya kilo tatu. Tunaendelea kuzisihi kampuni nyingine waende na njia hiyo hiyo ili kuwarahisishia wananchi waweze kupata mitungi hii kwa gharama ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ameshafanya kikao na wadau wa LPG ili kuhakikisha tunakuwa na mawakala wengi zaidi hata kwenye maeneo ambayo yako mbali. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge hoja zenu zote tumezichukua na majibu yake tunayo na tunazifanyia kazi kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye suala la CNG. Waheshimiwa Wabunge tumewasikia kuhusiana na umuhimu wa kuongeza vituo vya kujazia gesi, lakini vilevile vituo vya kubadilisha mifumo ya magari ili yaweze kutumia gesi. Waheshimiwa Wabunge, maoni yenu tumesikia na vilevile ni kweli kabisa kwenye Kituo cha Ubungo foleni ni kubwa, lakini mikakati ya muda mfupi tunayo.
Mheshimiwa Spika, kupitia TPDC tayari tumeanza ujenzi wa kituo mama pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Vilevile tuna ujenzi wa vituo vingine viwili ambavyo vinaendelea na ujenzi katika eneo la Kairuki pamoja na Muhimbili. Kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, tunaenda kufanya ujenzi wa vituo vingine 20. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, kwa kipindi cha muda huu mfupi tunayo mikakati ya kuhakikisha tunamaliza foleni na kurahisishia wananchi upatikanaji wa gesi kwenye magari yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la vitongoji, ili leo tuweze kufikia hapa kwenye kudai vitongoji ilikuwa ni lazima tuanzie sehemu na tuliweza kuanza kwenye kupeleka miundombinu vijijini. Kwa kuwa tayari tumeshafika huko, vitongoji vyote ambavyo vimebaki tutaenda kuvifikishia umeme.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunao mkakati wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 20,000 na tunapeleka kwa awamu. Tutaanza na vile vya kila jimbo 3,060 ambapo tupo kwenye hatua za mwisho za manunuzi.
Mheshimiwa Spika, pia kwa mwaka huu wa fedha tunao mkakati wa kupeleka tena kwenye vitongoji 4,000. Kwa hiyo, mkakati wetu wa kupeleka kwenye vitongoji 20,000 ndiyo tunauanza Waheshimiwa Wabunge. Nawahakikishia kama ambavyo tunamaliza vijiji awamu kwa awamu, pia tutaenda kumaliza vitongoji.
Mheshimiwa Spika, ninapoenda kumalizia kuhusiana na wakandarasi ambao hawatekelezi majukumu yao vizuri. Waheshimiwa Wabunge tumewasikia na hususani mkandarasi wa Rukwa. Tuendelee kuwahimiza wakandarasi ambao tumewaamini katika utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi wafanye miradi hii kwa weledi mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu tulishatoa maelekezo kwamba wakandarasi wote ambao hawafanyi kazi zao kwa weledi hatutaenda kuwapatia kazi chini ya taasisi ambazo zipo katika Wizara yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, kuhusiana na suala la huduma kwa wateja, kulikuwa na malalamiko kwamba simu hazipokelewi. Ni kweli, kipindi tuna mgao wa umeme tulikuwa tunapokea mpaka simu 40,000 kwa siku, lakini kutokana na kufanyia kazi changamoto hizi za umeme na umeme kupatikana, simu zimepungua kutoka kati ya 20,000 mpaka 17,000 kwa siku na uwezo wa kituo chetu ni simu kwa 87%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu alitolea maelekezo ya namna ambavyo tutaweza kuwafikia wateja zaidi na tumefanyia kazi. Moja, tumerudisha huduma za simu kwenye kila mkoa. Kwa hiyo, kila mkoa wananchi wanaweza wakapiga simu kule. Pili, tumeboresha mawasiliano ya teknolojia kwa kuja na mbinu za kisasa. Tuna chatbot ambapo mtu kupitia WhatsApp anaweza akasema shida yake na akachati na akapata suluhisho la tatizo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, kuhusiana na toll-free, kwa kushirikiana na TCRA, tayari tumeshapata namba ambayo ni ya bure ambayo ni 180 na tupo kwenye mchakato wa mwisho wa kuhakikisha tunaanza kutumia namba ili wananchi waweze kupiga simu bure. Kwa hiyo, kwenye suala la huduma kwa wateja Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu alilitolea maelekezo na vilevile tumelifanyia kazi kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, kipekee naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa ushauri wenu na michango yenu. Yawezekana tusiwe tunaweza kuyajibu yote kwa mmoja mmoja, lakini nataka niwahakikishie, michango yenu tunaithamini sana sana na yale ambayo yanatekelezeka tutahakikisha yanafanyiwa kazi kwa mustakabali wa Taifa letu na sekta yetu ya nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)