Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii iliyoko mezani kwetu.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naunga hoja ya Mheshimiwa Mbunge aliyoileta hapa mbele yetu, naunga mkono kwa sababu haya mambo yalishanitokea mara tatu, siku moja nikiwa kwenye Mkoa wa Singida basi lilipata ajali mbele yetu, pale kuna Mji wa Ikungi ilivyoonekana fire mpaka itoke mkoani, lakini pia kwenye Jimbo langu yalishanitokea mara mbili kwenye Mji wa Lulembela.
Mheshimiwa Spika, hakuna umuhimu kama kuwa na gari la zimamoto kwenye mji. Sasa hivi dunia imebadilika, Serikali imepeleka umeme kila mahala, kila vijiji kwenye jimbo langu vimeishapata umeme, lakini huu umeme wakati mwingine huwa unapiga shoti. Utayajua siku shoti ikikutokea ukiwa jimboni na ukapigiwa mwalo na wananchi ukaenda kwenye sehemu ya tukio.
Mheshimiwa Spika, lakini Serikali kwanza inatakiwa ilichukue hili suala kama jinsi inavyochukua kwenye habari zingine za maendeleo. Pamoja na kwamba zipo halmashauri kiukweli zingine hazina uwezo wa kuweza kununua magari, lakini Serikali Kuu ikitoa maelekezo na maagizo kwamba kuhakikisha kila halmashauri iwe na gari la zimamoto ikiweza hata magari mawili, mimi ndiyo maana nasema namuunga mkono Mheshimiwa na ahsante sana Mheshimiwa Tarimo kwa kuleta hii habari kwa sababu mimi yalishanitokea pale mjini Masumbwe na Serikali iweke msisitizo tu, iwaelekeze halmashauri pamoja na Madiwani kushirikiana na Jeshi la Zimamoto ili kuweza kuhakikisha kwamba tunapata magari pamoja na vifaa vya kuzimia moto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, miji yetu inakuwa kwa kasi, mimi ninazo kata 17 ambazo kila siku wananchi wanapata pesa wanajenga, lakini umeme kila mahala kama nilivyosema umewekwa. Tunavyo viwanda kiasi kwamba ikitokea shoti ya moto, gari itokea Geita kuja Masumbwe umbali wa zaidi ya kilometa 120 utakuta hiyo nyumba imeteketea.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, mimi naomba Serikali kupitia mfumo wake iwasisitize halmashauri kuweza kununua haya magari ya zimamoto, mimi Mbogwe nipo tayari kwa niaba ya wananchi wa Mbogwe kwa sababu tumeishapoteza baadhi ya maeneo watu wanaouza hata mafuta haya ya madumu, inatokea mtu anavuta sigara, nyumba inalipuka unaenda kwa askari hawana vifaa.
Mheshimiwa Spika, lakini pia upande wa Wizara ya Mambo ya Ndani, hawa askari ni wachache sana. Kwa mfano kwangu nina askari wawili tu, ukiangalia askari wawili wananchi mko zaidi ya 400,000, nyumba ziko zaidi ya milioni mbili, sasa hawa askari na wenyewe hawatoshi waongezwe.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi Mheshimiwa Mbunge nakuunga mkono na una akili sana na Mungu akubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia kwa kuwa na wewe ni Mbunge mwenzetu nina imani hata Mbeya huwa zinatokea hizi ajali, tunaomba utuunge mkono kutoa msukumo kuhakikisha kwamba halmashauri jambo la kwanza kwenye bajeti, watenge bajeti ya kuweza kununua magari na maisha mengine yaweze kuendelea. Tukipeleka haya mambo kimasihara masihara tutakuwa tunapoteza binadamu wenzetu kwa uzembe kabisa ambapo kila halmashuri ina uwezo wa kufanya na pesa nyingi kwa kweli zinaibiwa tu, zinaliwa hovyo hovyo tu hata kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, lakini kungekuwa na umuhimu wa kusisitiza kwamba lazima muwe na gari kwenye wilaya hii, ingekuwa ni nafuu sana na tutaonekana viongozi wenye akili nzuri sana baada ya kuweka misingi imara ya kuweza kuhakikisha kwamba tunaboresha kwenye hii nafasi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi naunga mkono hoja. (Makofi)