Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja kuhusu Halmashauri za Miji na Wilaya Kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kutatua Tatizo la Upungufu wa Magari ya Zimamoto pamoja na Vifaa Vinavyotumika Kuzima Moto na Uokoaji

Hon. Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja kuhusu Halmashauri za Miji na Wilaya Kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kutatua Tatizo la Upungufu wa Magari ya Zimamoto pamoja na Vifaa Vinavyotumika Kuzima Moto na Uokoaji

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niunge mkono hoja hii, lakini niombe kuwe na marekebisho kidogo kwenye ile hoja ya kwanza kipengele cha kwanza au Azimio la kwanza anasema; “Serikali ilete Muswada wa Sheria Bungeni ili kuweka utaratibu wa kuwezesha halmashauri kutenga fedha katika bajeti zake kwa ajili ya kununua magari ya zimamoto, vifaa na mambo mengine ya uokoaji.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe kuwe na option kwa sababu halmashauri hazifanani, kuna halmashauri huku chini ziko hoi kabisa, kwa hiyo, niombe kuwe na option halmashauri zenye uwezo kwa sababu chini huku tunajua kuna halmashauri haziwezi kabisa kufanya haya mambo, kwa sababu gari moja ni zaidi ya shilingi milioni 900 kwa hiyo, inawezekana kabisa kuna halmashauri hazitaweza, lakini naunga mkono hoja yake na mambo mengine yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu nishukuru mpaka sasa Jeshi la Zimamoto walipokea magari 12 ya kisasa ya kuzima moto na sisi tulienda kuyazindua. Hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais ambaye ameenda kutafuta fedha na kuleta magari haya. Zimamoto hawapati bajeti ya kutosha, tunaweza tukawapiga mawe, lakini mpaka mwezi wa pili hawakuwa wamepata hata mia. Sasa unawapigaje mawe hawa watu? Serikali ichukue jukumu lake, ipeleke fedha kwa wakati, halafu tuwabane wakiwa wana fedha, hawana kitu halafu tunawabana, tutakuwa tunawaonea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia Mheshimiwa Rais ameweka mkakati wa dola milioni 100 ambazo zitakuja na magari ya kisasa yatanunuliwa. Kama magari 12 tumeyaona hayo mengine yatakuja, lakini tusibweteke kwa sababu hili jukumu siyo la Mheshimiwa Rais. Hili jukumu ni la kwetu kama Wabunge na Bunge likitenga pesa ziende, tunatenga fedha haziendi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake halmashauri nyingi huku chini zinapata hizi shida, lakini Wizara ya Maji pia ina wajibu wa fire hydrants kule chini hakuna maji. Kuna sehemu nyingine zinapata majanga ya moto, watu wa Zimamoto wakienda hakuna maji. Kwa hiyo, Wizara ya Maji inawajibika, lakini kuna miundombinu, kuna sehemu kabisa kunatokea janga la moto gari haiwezi kufika, ni mpangilio holela. TAMISEMI na Wizara ya Ardhi washirikiane ili kuweka utaratibu mzuri ili hata likitokea janga la moto gari iweze kufika mahali, huwezi kuwalaumu Zimamoto wakati gari haiwezi kufika ikifika inakwama, wanaangalia nyumba zinateketea, miradi inateketea hawawezi kuruka juu wakafika pale wakaenda kuzima moto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sometimes tunaweza kuwalaumu na wananchi wanaweza kuwaona kama hawawezi kufanya kazi, lakini hawana namna ya kufanya kwa sababu wanakutana na vikwazo na vikwazo hivi ni vingi, ni lazima Wizara hizi zote zikae kuona namna gani ufanisi unaweza kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante na ninakushukuru sana. (Makofi)