Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja kuhusu Halmashauri za Miji na Wilaya Kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kutatua Tatizo la Upungufu wa Magari ya Zimamoto pamoja na Vifaa Vinavyotumika Kuzima Moto na Uokoaji

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja kuhusu Halmashauri za Miji na Wilaya Kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kutatua Tatizo la Upungufu wa Magari ya Zimamoto pamoja na Vifaa Vinavyotumika Kuzima Moto na Uokoaji

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu juu ya hoja iliyowasilishwa na Mheshimiwa Tarimo.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Tarimo kwa hoja hii ambayo binafsi imenisumbua kwa muda mrefu sana, hata nilivyoingia asubuhi nikamuwahi kumwambia hongera sana na nitapata bahati ya mimi kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili nikushukuru wewe kwa kuniona nje ya utaratibu na mwongozo wa kikanuni, lakini ukatupa nafasi kama alivyosema Mheshimiwa Michael Mwakamo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda niseme tu tafsiri ya kwanza ya Jeshi letu la Zimamoto, kwenye taarifa amejaribu kuisema kwamba kabla ya mwaka 2007 tulikuwa tuna taratibu hizi ndani ya halmashauri zetu, lakini Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaundwa kufanya kazi chini ya Sheria Namba 14 ya mwaka 2007 (Fire and Rescue Force Act). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi sana lazima tuyafahamu, moja, ni kuzima moto na kuokoa maisha na mali katika majanga yatokanayo na moto, mafuriko, tetemeko la ardhi, ajali za barabarani pamoja na majanga mengineyo.

Mheshimiwa Spika, sasa katika upana huu wote hatuoni jeshi hili likiwa na majukumu yote manne haya kama niliyoyasema. Tukiangalia haraka na maono ya wananchi dhidi ya jeshi lenyewe unaweza ukamuona yupo tu kwenye eneo la kuzima moto, lakini humwoni kwenye mafuriko, majanga ya barabarani na majanga mengine ambayo nimejaribu kuyasema hapa kama vile matetemeko ya ardhi na kadhalika. Kule Kagera yalitokea, lakini na maeneo ya hapa Dodoma hatukuwahi kuwaona.

Mheshimiwa Spika, niseme naunga hoja mkono katika mapana ya kwamba pawepo na MoU kati ya halmashauri na Jeshi la Zimamoto. Pia na mimi hapa niwe very specific ishuke chini, lakini katika zile halmashauri za miji na majiji zenye uwezo zikaisaidie bajeti ya zimamoto kwa sababu kwa Serikali Kuu peke yake kwa majukumu haya niliyoyasema yote kwa majukumu haya kwa mujibu wa sheri inayounda zimamoto, haiwezi kuutekeleza. Kwa hiyo, wakisaidiwa inawezekana wakaweza kufanikisha lakini wale wasio…

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, muda wenyewe jamani.

SPIKA: Mtajuana na ninyi huko ni majirani. Kwa hiyo, mtajuana baadaye. Mheshimiwa Mtemvu kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Neema Mwandabila. (Makofi)
TAARIFA

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ninataka nimwambie kwamba yeye anatoka halmashauri ya mjini Dar es Salaam, haya mambo ya ununuzi wa haya magari ya fire inawezekana. Kama halmashauri ya Mji wa Tunduma imeweza kununua, wenyewe Dar es Salaam wanashindwa kitu gani? Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mtemvu, Taarifa hiyo unaipokea?

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, hajanielewa tu hoja yangu, ninaona kaunga mkono tu ambacho nilikuwa nakisema, sikukataa kwamba halmashauri za miji na majiji makubwa ziweze kusaidia bajeti kuu ya Serikali kununua ili hawa wadogo wasinunue na ndicho alichokuwa ananiambia nyie mnaweza. Ni kweli tunaweza katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, niweze kukwambia kwa haraka tu, katika majanga haya kama majukumu ya jeshi hili limeshindwa kutokana na vifaa, mimi ninatoa mfano tu mafuriko. Katika kipindi hiki cha mafuriko ndani ya jimbo langu nimepoteza watoto wawili, lakini jinsi gani ambavyo nilikuwa ninajaribu kushirikiana na jeshi hili, lilikuja tu na maji na magari yake, lakini jambo lenyewe ni mafuriko, hawakuja na vifaa vingine.

Mheshimiwa Spika, siku tatu wananchi wa pale wa jimbo lile tulikaa kwenye maji tunatafuta katika njia zetu za local, lakini na wenyewe wakaja wakatuunga mkono kwenye kutembea na fimbo. Tukawauliza je, mngekuwa na mbwa si angenusa kwenye vichaka vilivyojifunika?

Mheshimiwa Spika, huwezi amini, ndani ya muda mdogo baada ya siku kumi akapatikana yule mtoto ndani ya kichaka ambacho hakipo hata zaidi ya meta 200. Kwa hiyo, wangekuwa na mbwa ingetusaidia.

SPIKA: Haya, ngoja twende vizuri. Mheshimiwa muda wako umeisha lakini unayo hii hoja ya Mheshimiwa Mbunge?
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ninayo hoja hii.

SPIKA: Uko nayo?

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kifungu (b) yake umeisoma inasomeka namna gani? Muda wako ulikuwa umeisha. Kwa hiyo, huu unaotumia ni wa kwangu. Fungua tu, halafu soma (b) yake anasema nini. Au ni kusomee? Au umepapata?

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nisaidie, ninaona hitimisho. Juu ya hitimisho (b) ... (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Spika, haya, (b) yake inasomeka hivi na anasema; “Serikali ilete Bungeni Muswada wa Sheria utakaoweka utaratibu wa kuwezesha halmashauri za miji na wilaya kuingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ya kununua magari ya zimamoto na vifaa vya uokoaji. (Makofi)

Haya, ahsante sana, ni hapo nilitaka nikusomee.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na kwa hiyo, ninaiunga hoja mkono ya Mheshimiwa Tarimo. (Makofi)