Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja kuhusu Halmashauri za Miji na Wilaya Kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kutatua Tatizo la Upungufu wa Magari ya Zimamoto pamoja na Vifaa Vinavyotumika Kuzima Moto na Uokoaji

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja kuhusu Halmashauri za Miji na Wilaya Kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kutatua Tatizo la Upungufu wa Magari ya Zimamoto pamoja na Vifaa Vinavyotumika Kuzima Moto na Uokoaji

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu na mimi ninampongeza sana Mheshimiwa Tarimo kwa jambo hili muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia jambo lenyewe linazungumzia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Kwa hiyo, ni jeshi, lakini inahusika zimamoto na uokoaji. Siyo uokoaji tu kwa sababu moto umetokea, ina maana ni uokoaji kwenye majanga yote.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninajiuliza, wajibu wetu kama Wabunge ni kutenga bajeti na kupitisha na wajibu wa Serikali ni kutekeleza sasa, kupeleka fedha na kutekeleza yale ambayo Bunge limepitisha. Pamoja na jambo jema ambalo amekuja nalo Mheshimiwa Mbunge na ushauri ambao ameutoa, bado ninakubaliana na hoja yake isipokuwa kama ambavyo Wabunge wengine wamezungumza, halmashauri zetu zinatofautiana isipokuwa kama kwa sasa sheria tuliyonayo tu haijazuia halmashauri yenye uwezo kuweza kununua magari na kusaidia zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninajiuliza, hivi kama hili ni jeshi na changamoto zote ambazo tunakutana nazo kama Taifa, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa jambo hili kupeleka fedha? Leo tunapozungumzia halmashauri, halmashauri inahusika na upangaji wa miji, ni wajibu wao. Kwa sababu hata kama zimamoto watapewa fedha kiasi gani, kama mipango yetu ya kupanga miji itakuwa hovyo hawatafanya chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna haki bila wajibu, ili zimamoto walaumiwe ni lazima askari hao wawepo, wawepo na vitendea kazi, lakini Serikali iwape fedha. Wakati ninaendelea kujiuliza maswali nikasema...

NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani, kuna Taarifa. Inatokea wapi?

NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, inatokea hapa.

SPIKA: Ahaa, Mheshimiwa Hamad Chande.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninapenda nimpe Taarifa dada yangu, anachangia vizuri sana, lakini tayari Serikali imeshatoa fedha USD milioni 100 mwezi uliopita na wapo katika mchakato wa manunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tena Serikali imeenda mbali sana, siyo vifaa vya magari tu. Helikopta zitanunuliwa na boti za zimamoto zitanunuliwa, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani, unapokea Taarifa hiyo?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, Mheshimiwa Naibu Waziri ninakuheshimu sana, kwa sababu unasema bado hamjapeleka, kwa hiyo ninakubaliana mpeleke sasa kwa sababu ni wajibu wenu kupeleka hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninataka nizungumze jambo moja.

SPIKA: Amesema wameshapeleka.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, wako kwenye manunuzi, hazijakwenda bado.

SPIKA: Yeye amesema wameshapeleka, ndiyo neno alilotumia. (Makofi)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, haya sawa, wamepeleka ya magari mangapi na mahitaji ya nchi hii ni kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo ninaweza nikashauri ni kama jambo hili ni kipaumbele chetu tupunguze baadhi ya matumizi ambayo hayana ulazima.

Mheshimiwa Spika, tulipitisha hapa kununua magari ya ma-DC zaidi ya shilingi milioni 400. Kama kipaumbele chetu ni magari ya zimamoto, kulikuwa na sababu gani ya kupeleka hizi fedha zote kwenye magari ya ma-DC? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, magari ya ma-DC wanaweza wakatumia hata magari yaliyopo kwenye halmashauri; zimamoto inahitajika kila siku. Kwa hiyo, lazima tuwe na kipaumbele kama Serikali na hata kama tunasema tumepeleka, mimi ninaamini hata nusu... (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo wafanyabiashara wanalipa hizi fedha kila mwaka kwa ajili ya zimamoto. Sasa wanapolipa zinakwenda wapi? Kwa nini zisiende kufanya hizo kazi. Kwa hiyo na wao wenyewe wafanyabiashara na nikwambie; mimi nimekaa nao Ijumaa wafanyabiashara wa kwenye jimbo langu. Wanasema hatutalipa kuanzia leo, hatujawahi kuliona gari la zimamoto hata siku moja lakini wakija hapa wanatukaba tunalipa fedha. Tunalipa fedha za nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali, tusipeleke huu mzigo kwa halmashauri, ni wajibu wa Serikali Kuu, tutimize wajibu wetu. Hili jeshi tunalihitaji, lina kazi muhimu, liwasaidie Watanzania. Halmashauri ambazo zina uwezo zifanye kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kusisitiza na kumpongeza Mbunge kwa jambo hili muhimu sana, lakini tuwe na kipaumbele tupunguze matumizi ambayo hayana ulazima kwa Taifa letu, ahsante sana. (Makofi)