Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nami niungane na Wajumbe waliozungumza kwa dhamira ya kuimarisha huduma za zimamoto na uokoaji katika nchi yetu, lakini nichelee tu kukubaliana na hoja hizi kama zilivyotolewa zote na kama lengo lake ni kwenda kufanya marekebisho kuanzia mwaka ujao wa fedha wa kile kinachoendelea wa kile kinachoendelea au kilichokwisharidhiwa na Bunge lako kwenye halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tayari tumeshapitisha bajeti za TAMISEMI zikiwemo mikoa na halmashauri na sidhani kama tulikuja na mtazamo huu ambao tunataka resources zilizopo kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya msingi ya Serikali za Mitaa yaliyoko sasa zihamishwe ziende kugharamia majukumu ya zimamoto na uokoaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba kwa miaka mingi eneo hili la zimamoto na uokoaji lilikuwa halijawekezwa vya kutosha, lilikuwa halijaimarishwa, lakini Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miaka mitatu iliyopita ameonesha dhamira na utendaji. Kwanza kwa kuwaongezea nguvu kazi, zaidi ya watumishi 800 wameajiriwa kama askari wa zimamoto na uokoaji, lakini nikiri pia nilikuwa kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi miezi michache iliyopita, mafunzo yenyewe ya uokoaji yalijikita zaidi kwenye kuzima moto. Uokoaji wa baharini, ziwani ilikuwa ni changamoto. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, lakini...
SPIKA: Mheshimiwa Jumanne Sagini, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere.
TAARIFA
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ninataka kumpa taarifa mzungumzaji, hili jambo ni pana sana.
Mheshimiwa Spika, mimi ninadhani aliyeleta hoja hii ametukumbusha kwamba suala la majanga ni kubwa sana katika nchi yetu kwenye halmashauri zetu. Kwa hiyo, amekuja kutupatia mawazo kwamba tuteremke mpaka chini huko ndani. Halmashauri zetu ziungane na Idara ya Zimamoto zisaidie namna ya kuokoa wananchi kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukilizungumza kama kupata chanzo cha mapato hatutaweza kuliokoa hili jambo. Tuongee kama kwamba halmashauri ziungane na upande huu wa zimamoto, kwa maana hata kabla ya mikataba hiyo kuwepo na mawazo ya kuzuia majanga badala ya kufikiria zaidi kwenye hela. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Jumanne Sagini, unapokea Taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninatafuta ipi niipokee, lakini ninashukuru. Ni kweli lengo ni kuimarisha kama Mheshimiwa Mbunge mmoja alivyozungumza.
Mheshimiwa Spika, kwa infrastructure iliyopo sasa hivi ya kisheria na kisera, hakuna kikwazo chochote cha zimamoto kushirikiana na halmashauri na wamekuwa wakifanya mambo mengi kushirikiana na Serikali Kuu.
Kwa hiyo, ambacho ninataka kushauri wakati ninazungumza nini kimefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, ni pamoja na kuwaingiza vijana wetu hawa wa fire na uokoaji kuingia ushirikiano na timu kama hii Zanzibar kwa KMKM kwa ajili ya uzamiaji na mambo yanayotokea kwenye majanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kubwa lingine amelisema Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, mwaka huu tayari wamepewa fedha za kuwezesha kununua magari yatakayopelekwa kwenye taasisi 150 zikiwemo halmashauri zetu zote na mikoa yote na lengo ni kuimarisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu; sipingani kabisa na dhana ya kuimarisha uhusiano kati ya zimamoto na uokoaji.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Taarifa inatoka wapi?
Mheshimiwa Jumanne Sagini kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Reuben Kwagilwa.
TAARIFA
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, Taarifa niliyokuwa ninataka kumpa mzungumzaji ni kwamba wakati akiongelea habari ya fedha zilizotengwa mwaka huu ninamkumbusha kwamba mwaka 2023/2024 tulitenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kununua magari matano na magari hayo hayajanunuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye magari hayo ulikuwepo mgao wa gari kwenda Handeni ambako ndiyo kuna Msomera, Mradi wa Kitaifa ambapo tumewapokea wenzetu kutoka kule Ngorongoro, lakini si tu hivyo mahali ambapo tuna highway kubwa ambayo kila siku magari yanayobeba gesi yanaungua na kuteketeza watu pale. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele imeshakugongea.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ukiachia mbali matukio matukio ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mji wa Handeni kama kuunguliwa nyumba kwa Mzee Ally Mhandeni, Mzee wangu Asenga na Mzee Mwingwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana ninashukuru.
SPIKA: Haya muda wa kuchangia Mheshimiwa Mbunge umeisha. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Sagini, muda wako amemalizia Mheshimiwa Mbunge. Haya ninakupa dakika mbili malizia. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninataka kushauri kwamba jambo lenyewe kama lilivyozungumzwa tunaona ni multisectoral, ni suala mtambuka. Limegusa Wizara ya Maji, limegusa Wizara ya Ardhi kwenye mipango miji, limegusa TAMISEMI, limegusa Mambo ya Ndani ya Nchi yenyewe, Ofisi ya Rais kwenye miundo na taasisi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, ungetoa nafasi Serikali ilichukue jambo hili ili lichambuliwe na wadau wote hawa ili tunapolizungumza kama Wabunge wengi walivyosema, tulizungumze comprehensively kwa upana wake kuliko kuangalia maeneo ya uwezeshaji wa vitendea kazi tu, kwa sababu hata elimu inatakiwa ili watu wetu wawe na utayari na vitu kama hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)