Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mungu kwa siku hii njema ambayo leo tumepokea bajeti ya mhimili mwingine katika mihimili mitatu iliyo katika nchi yetu ikiwepo Executive, Parliament na hii ni Judiciary. Kwa hiyo, leo tuna bajeti nzito sana na ina mafungu takribani saba na hili ninalokwenda kulizungumzia mimi, ni lile la nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mhimili una baraka sana kwa sababu una tafsiri zile sheria tunazozitunga hapa ndani, lakini haitafsiri tu, pia inazifanyia kazi sheria hizo na inasimamia kwamba kila mtu anapata haki. Mhimili huu umefanikiwa kutumia bajeti yake ya mwaka wa awali kabla ya huu ambao unaenda kumalizika vizuri na ilipata Hati safi. Kwa hiyo, matumizi yake ni mazuri. Ile minong’ono ya rushwa, rushwa imepungua. Nakiri wazi kwamba huu mhimili unafanya kazi zake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama kuchangia kama Mjumbe wa Bajeti na nawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tuwape walichoomba ili wakatekeleze kazi zao vizuri kwa sababu nyongeza ya bajeti ya mwaka uliopita na hapa ni 10% tu, wala hawaombi vitu vingi sana vya ajabu. Mwaka huu wanaomba takribani shilingi bilioni 241.6, ni bajeti ambayo inatamkika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama kuzungumzia yale machache ambayo tuliona kama ni changamoto. Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Oran Njeza ameyasema, lakini nina msisitizo kwenye mambo kadhaa ikiwemo kumaliza mlundikano wa kesi katika Mahakama zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitaenda moja kwa moja kwenye kesi za mauaji. Kesi hizi zimekuweko muda mrefu na zinawaweka wale washtakiwa kuwa kwenye hali ya suspense, hali isiyojulikana, hali ya sintofahamu. Mshtakiwa anaumia, familia inaumia na wale waliomshtaki pia wanaumia sana kwa sababu kama ni mtu wao ameuawa, sasa kama ameuawa hukumu ni auawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua atakapokuja mtoa hoja, ni hukumu ngapi za kifo zimetekelezeka kwa kipindi cha muda wa siku za usoni? Tanzania hakuna au sisi tuna huruma sana! Huko Mahakamani hakujaenda shahidi za kutosha! Tayari mtu amehukumiwa, hajahukumiwa, mtu ameshtakiwa kwa kuua, inachukua miaka zaidi ya 10 au 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa kawaida ambao ni layman, mimi ni mmojawapo, nashangaa na ninajiuliza, kama hii hukumu ya kifo haitekelezeki, kwa nini ipo? Muswada uletwe hapa na Serkali tubadili, tuseme Tanzania haitekelezi au haipo tayari kutoa hukumu ya kifo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nalisema kwa uchungu, lakini kwa vile jambo liko Mahakamani, siruhusiwi kutamka ila nina mtu wa karibu na nitasema mtu wa karibu kwa sababu ni mtoto wa kaka yangu. Aliuawa na akalimwa mgongoni kwa rato na ikaonekana na yule mtu akakamatwa akapelekwa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukifika hapo huu mhimili au tunaambiwa usiseme zaidi, ni miaka imepita sasa takribani miaka 10, familia inaumia na familia ya mshtakiwa inaumia, lakini haitekelezeki. Nimeona niliseme wazi, huenda pia tuna huruma sana Tanzania, hata mimi sitaki kuua, lakini tujue ni nini kinachoenda tunapomweka mtu anakaa mahabusu kwa muda mrefu miaka nenda rudi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mnatuambia hapa justice delayed is justice denied. Iko wapi hiyo justice hapa? Nataka mnapokuja kutueleza tuelezwe kinagaubaga, ni nini kifanyike, kwa sababu hiyo pia ni kati ya kesi ambazo ni za mlundikano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi nyingine ni hizi kesi za kubakwa. Watoto wadogo wanafanyiwa vitu vibaya, kesi inakwenda inaulizwa, haitekelezeki, au hukumu haitoki. Inafika mwisho, mtu anawekewa dhamana. Sikatai, dhamana ni haki ya mtu, lakini kwa nini usiletwe Muswada hapa kwamba watu wanaobaka (mwanzoni tulipendekeza hapa mmoja mmoja katika kuchangia), labda wapunguziwe hizo kasi kwa kufanyiwa kile kitendo kitaalamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vipi, lakini wachomwe labda sindano ya kuwafanya wasiweze tena lile tendo. Imekuwa ngumu kutekelezeka, lakini watoto wanatendewa vitu vibaya (watoto wa gender ya Ke na watoto wa gender ya Me). Lile jambo tuliloliomba hapa liletwe sasa. Hao wenye tabia mbaya mbaya sana, hata nashindwa kutamka hayo maneno, washughulikiwe. Hayo maneno hayatamkiki, ulimi unakuwa mzito. Washughulikiwe na tujue kabisa kwamba wamekomeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utekelezaji wa maombi ya bejeti, kwenye randama, kwenye ile kasma ya 21,112 ambayo ni Basic Salary Non-Pensionable, mwaka 2023 waliomba shilingi 66,000,000 tu, mwaka huu wameomba shilingi 382,320,000, nasema ni kama zaidi ya mara tano, karibu mara sita ya walichoomba. Sababu ni nini? Wanasema ongezeko la bajeti kwa kasma hii limetokana na ongezeko la watumishi wa mikataba wakiwemo madereva na mafundi sanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kila siku tunasema tumepata wahitimu wa vyuo vya VETA, tumepata wahitimu labda wa vyuo vingine, lakini ajira hazitoki. Mimi naiomba sana Serikali kutoka kwenye hiyo Wizara ya Utumishi, mwafungulie Mahakama waajiri wenyewe, kwa sababu unapotaka kupeleka bajeti mara 500 kwa ajili ya mkataba, kisa tu mmewazuia wasiajiri; kwa nini, wakati wana mlundikano hivyo wa graduates wa level mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawape uhuru, waupe huu mhimili uhuru wa kuajiri, la sivyo zitatumika hela nyingi sana na tayari tumeona. Leo nimekwishawaomba kwamba tuwaruhusu wapewe hili fungu waliloomba, lakini sasa kwenye ajira wanapopeleka watumishi wa mkataba ilhali ma-graduate tunao wengi na wahitimu wa level nyingine wapo wengi barabarani, siyo sahihi kabisa. Hili nalisema kwa uchungu, naomba Utumishi waangalie jinsi gani watu hawa watasaidika. Kwa bahati nzuri sana hawa ni watu ambao wanaweza kutafuta, kama ni Mahakimu wakafungua ofisi zao wakaanza kutoa huduma, lakini siyo wote. Naomba jambo hili liangaliwe kwa jicho la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Jaji Mkuu Mheshimiwa Profesa Ibrahim Hamis Juma kwa jinsi ambavyo anaulea huu mhimili na niwapongeze pia wote wanaohusika kwenye mhimili huu. Kwa kweli ni watu ambao wanapendeza na tunawa-admire sana. Huku ndani tuko na Mheshimiwa Jaji, Dkt. Eliezer Feleshi na tunamwona anavyotekeleza kazi, lakini wajue pia na Spika wetu ni mmoja wa upande huo huo na wanauona huu mhimili ulivyokaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Ole Gabriel. Niseme kwa kweli amekuwa ni mtu ambaye anapenda kuelimisha watu tukiwemo sisi. Kila akiona kwamba kuna jambo tunalotaka kufahamu anatuelimisha, ndiyo maana tunaweza tukasimama tukausemea mhimili huu. Nimpongeze zaidi pia huyu huyu Profesa Ole Gabriel kwa kusimamia ujenzi wa majengo ya Mahakama katika Jiji hili la Dodoma. Tumeona majengo yote yanayojengwa na Mahakama ni majengo ambayo yana mvuto; ukiambiwa hapa ni kiasi gani unaweza ukakubali, ndiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili moja ambalo usiku na mchana linapeperusha bendera kidijitali, lakini linaandika pia Mahakama zilizomo, linaandika vitu vyote. Ni jengo zuri na niseme kwamba huu mhimili umeipendezesha Dodoma. Sasa pamoja na kuipendezesha Dodoma tusiishie kwenye majengo. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti vitu vyote twende navyo kwa kasi ikiwemo kuajiri na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kama umewasha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana, muda wako umekwisha.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)