Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nikupongeze kwa namna unavyoendesha kikao chetu, nikupongeze kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa kuendelea kusimamia na kuimarisha mhimili huu ambao unasimamia utoaji wa haki kwa wananchi wa Tanzania na ambao kama mwenzangu alivyosema ndiyo chanzo cha amani na utulivu tulionao katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii, nitoe pongezi kwa Naibu wake pamoja na Katibu Mkuu, bila kumsahau Jaji Mkuu, pamoja na AG. Nimkumbuke rafiki yangu na mtendaji mzuri sana, Ndugu Elisante OIe Gabriel, Mtendaji wa Mahakama hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa pongezi kidogo za kijumla halafu nitazungumza mambo ambayo nafikiri wengine wanastahili kuiga kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara hii, ambayo tumezungumza sisi tukiwa kwenye Kamati ya Bajeti. Pia nitazungumza kidogo kuhusu Jimbo langu, Mahakama za Mwanzo zilivyokaa, zilivyo duni na zinastahili ukarabati. Mwishoni nitajielekeza kwenye kushauri kwamba ni vizuri supporting institutions, mamlaka zingine zinazo-support Mahakama kama vile DPP, TAKUKURU, Magereza, Polisi, wakachukua hatua za haraka na mikakati ya haraka ili kwenda sambamba na mabadiliko ambayo yamefanyika kwenye Mhimili wa Mahakama, otherwise itakuwa haisaidii sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi za mwanzo na jumla ni kwamba na Watanzania wafahamu kwamba, Mahakama yetu ina jengo la state of art lililojengwa hapa Dodoma. Limejengwa kwa fedha siyo nyingi lakini ni jengo wanasema kwamba kimataifa pengine ni jengo la sita duniani la mahakama ambalo ni zuri zaidi. Jengo la sita is the state of art building watu wanaweza wakaja wakaliona, sisi tuliliona kwa kweli ni jengo lenye hadhi ya mahakama na ni jengo ambalo linatisha pia kwenda, utasema nisiende kule, nita-avoid kwenda kule kwa sababu unaweza ukapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pia pongezi kwa Mahakama hii especially kwa ubunifu wa Mtendaji wetu kuhusiana na mobile courts (mahakama zinazotembea). Naamini zimeshaanza, zimeanza mijini ila naamini zitasaidia sana kama wataweza kuziteremsha kwenye ngazi ya majimbo yale ambayo yako vijijini, kwa sababu kule juu kunahitajika sana na ndio kwenye ukandamizaji mkubwa na watu hawana fedha za kutafuta haki. Kwa hiyo, naamini kwamba hizi mobile courts zitafanya kazi yake na zitashushwa kwenye ngazi za chini kwa sababu zinatoa haki kwa namna ambayo ni gharama nafuu zaidi kwa wale watu ambao wanastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hawa ambao wamezungumza kuhusu TTS, huu mfumo ambao sasa ni wa kwanza naamini kwa macho yangu mimi nimekuwa wa kwanza kuona kumbe artificial intelligence inaweza ikatumika very effectively na naamini kwamba ni ubunifu mzuri, waliweza kufanya jambo hili ambalo limerahisisha sana utoaji na uandikaji wa hukumu na tafsiri za hukumu ambazo zinatolewa baada ya kesi kusikilizwa. Pia inaweka kumbukumbu nzuri zaidi kuliko ambapo kama imefanyika na binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la pili ambalo nataka kuchangia ni kwamba, kitu ambacho kimetufurahisha sana kwenye Kamati yetu ya Bajeti, ni namna ambavyo watendaji kwenye hiki kitengo utendaji wa Mahakama unafanya katika kutekeleza miradi. Wanaingia kwenye miradi na wakandarasi ambao wanapatikana kwa njia ya kawaida ambayo tunatumia NeST. Wakishafanya wanaandika mikataba ambayo inawaruhusu endapo baada ya mradi kutekelezwa wanaenda kufanya tathmini kuona kwamba, kweli ule mradi umetekelezwa kwa gharama zile walizokubaliana nazo au siyo na mara nyingi unakuta kwamba mradi umetekelezwa kwa gharama ambayo ni much less, kwa sababu wametumia vifaa pengine siyo vile. Nashukuru kwamba wanaweza kupata bakaa, wamekuwa wanapata bakaa kubwa kwenye utekelezaji wa miradi yao, bakaa ambayo wanaipeleka kwenye maeneo mengine, kwenye miradi mingine ambayo ilikuwa hata kwenye bajeti pengine haijapata nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashangaa na niliwauliza nikasema pengine ninyi kwa sababu ni Mahakama bado hawa jamaa wakandarasi wanaogopa kuwatapeli, kwa sababu sehemu nyingine wakandarasi hawa wanatapeli. Wewe unamwambia ajenge kitu cha gharama hii, value for money inashuka, wanatumia tu vitu wanavyotaka kutoka anywhere. Nashukuru na nasema kwamba, pengine tujifunze kwao mikataba ya utekelezaji miradi ya maendeleo nayo ifuate mkondo huo ili tuone kweli tunapata thamani ya fedha kwenye miradi yetu. Hilo ni jambo linalofurahisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanisi uliotekelezwa au miradi hii ya maboresho iliyotekelezwa kwenye Mahakama imewezesha kumkabidhisha miradi mingi na kesi nyingi zilizokuwa za muda mrefu, alisema 196,895 kesi za zamani. Wakaweza kuondoa 68% wakatekeleza, wakaondoa zile kesi ndani ya kipindi cha Julai kuja Februari, 2024. Ni jambo la kufurahisha sana na nawapongeza watendaji, ni jambo ambalo tunaona kwamba, kweli mwishoni tutaondokana na kesi za muda mrefu. Katika kesi hizi za muda mrefu, miezi sita tu wanasema ni ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya kutoa haki kwenye majimbo yetu imeharibika, wamesema wenzangu, inahitajika zaidi ya Mahakama za Mwanzo 3,000, lakini ziko kama 900, tofauti ni kubwa sana. Naangalia kule jimboni kwetu kwamba, kweli nashukuru kwamba nilipata ukarabati wa mahakama moja ya pale Kilema, lakini mahakama nilizonazo kwanza ni kama nne tu kwenye kata zaidi ya 16, lakini ukweli ni kwamba zimechakaa, ni za miaka, tena huwezi hata kukaa, ni mahali pachafu kabisa, hapafai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Mtendaji wa Mahakama, akatupatie Mahakama za Mwanzo kwenye Kata ile ya Kirua Vunjo Magharibi hatuna, Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Kata ya Marangu Mashariki na Magharibi hatuna, Kilema Kusini na Kati hatuna, pamoja na kule Kahe hakuna hata Mahakama moja. Nitaomba Mungu akituwezesha bajeti ile naona amepata 100,005 bilioni ya maendeleo atuangalie huko, atusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona changamoto kubwa ambayo imebaki kwa Watanzania sasa kupata full enjoyment ya maboresho yanayofanyika kwenye Mahakama zetu na utoaji wa haki. Suala hili la kwamba sasa Mifumo ya Jeshi la Polisi, Mifumo ya DPP iko vizuri lakini anatakiwa na yeye achukue hatua. Mifumo ya kule TAKUKURU na Magereza ambayo ndiyo inapeleka kesi kwa Mahakama, basi iboreshwe ipate bajeti za kutosha ili iweze kuendana na speed ya Mahakama inavyokwenda. Mandhari ya kutolea haki kwenye maeneo haya ya mahakama kwenye ngazi zote kuanzia Mahakama ya Mwanzo basi iweze kuboreka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kuona kwamba hivi vituo jumuishi vinakuwa mpaka na sehemu za watoto kucheza. Kuna vitu ambavyo unaanza kuona kweli nchi yetu ni nchi ya kipato cha kati, japokuwa kwenye kiwango cha chini kidogo, lakini kweli tumepiga hatua sana kwenye mambo ya haki. Namshukuru Mungu na atuwezeshe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nawatakieni Wenyeviti wa Kamati zote na Wajumbe wa Kamati zote zinazohusika na masuala haya, Kamati ya Bajeti na Kamati ya Utawala na wewe mwenyewe nawatakieni kila la kheri. (Makofi)