Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu, Wizara ya Katiba na Sheria. Hii ni mara yangu ya nne nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu nikichangia Fungu – 55 ambalo ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu nimeingia katika Bunge hili, kama jinsi ambavyo nimesema, nimekuwa nachangia sana katika Tume hii ya Haki za Binadamu na michango yangu mikubwa imejikita kuhusu kuishauri Serikali iweke mkazo au ioneshe umuhimu wa hali ya juu kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya Tume hii ya Haki za Binadamu. Niombe, wakati naendelea kuchangia, kila nitakaposema Tume basi ichukuliwe kwamba, namaanisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kwa ajili ya kukomboa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takribani zaidi ya miaka mitano tume hii haijawahi kutengewa fedha za miradi ya maendeleo kwa mapato ya ndani. Fedha ambazo zimekuwa zikiisaidia tume hii ni fedha za wahisani. Hatukatai kupewa hisani kutoka kwa wenzetu kwa sababu, hata kuaminiwa kama nchi kusaidiwa ni jambo la kushukuru, lakini nilitegemea kwamba, sisi kama nchi tuoneshe mfano kwanza kwa kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya Tume hii kwa sababu, mwisho wa siku Tume hii ipo kikatiba kwa ajili ya kulinda na kutetea haki za Watanzania, kwa maana ya Tume ya Haki za Binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haileti ladha nzuri kwamba, wahisani wawe na uchungu juu ya haki za Watanzania wenzetu. Ndiyo maana hata hii leo nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuikumbusha Serikali na hususan Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria kuwa, utakapokuwa unakuja ku-windup leo, sina mpango na sijawahi kuwa na mpango wa kushika shilingi unless otherwise usinipe maelezo ya kutosha. Mheshimiwa Waziri, atwambie ni kwa nini Serikali haiwezi au inashindwa kutenga fedha hata kama ni kidogo, kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayohusiana na tume hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa dira ya wazi kabisa anaonesha ni namna gani ambavyo nia yake njema ni kuona kila Mtanzania haki yake inalindwa na siyo tu kulindwa, lakini inatetewa popote pale alipo. Kuonesha dira ya Mheshimiwa Rais, ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki zao za msingi. Juzi tarehe 22 Aprili, 2024, ilikuwepo hafla pale Chamwino Ikulu ya kuvisha Nishani ya Miaka 60 ya Muungano. Mheshimiwa Rais wakati anahutubia Taifa amekiri kupokea malalamiko yaliyotolewa na Wabunge ndani ya Bunge hili, lakini pia na wananchi na watumishi wakidai juu ya kikokotoo kwamba, hawaoni kama kinawatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hafla hiyo Mheshimiwa Rais amesema waziwazi kwamba, amepokea malalamiko yale na anakwenda kuyafanyia kazi tokea wakati ule ambapo alikuwa anavisha nishani pale. Jambo hili linaonesha wazi kabisa kwamba, Mheshimiwa Rais ana nia njema. Mheshimiwa Rais hataki kusikia haki ya mwananchi yeyote Mtanzania inavunjwa na asiwepo wa kwenda kumsemea wakati Tume hii ipo Kikatiba kwa ajili ya kuwasemea Watanzania kuhakikisha haki zao za msingi zinaweza kulindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niendelee kuchangia nikijikita katika changamoto zinazoikabili taasisi hii muhimu, ambayo ni nyeti na ambapo nimesema dira ya Mheshimiwa Rais juu ya tume hii kwa Watanzania iko wazi kabisa kwa matendo. Changamoto ya kwanza ni kukosekana kwa Jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya Tume, ni mambo ya ajabu kabisa. Tunaomba Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge hili shida ni nini? Ni nini changamoto inayozuia Tume hii nyeti isiweze kuwa na makao makuu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili wanasema ni upungufu wa watumishi 154 ambapo kwa sasa tume hii ina watumishi 150 tu. Haiwezekani tume nyeti namna hii ikawa ina watumishi 154 tu, lakini uhitaji wao ni watumishi 150 wa nyongeza. Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa naomba anieleze kinagaubaga shida ni nini? Ni nini tatizo? Waziri aajiri watumishi 150 waende kuungana na watumishi hawa 154 ili mwisho wa siku waende kusaidia nia njema ya Mheshimiwa Rais huko chini vijijini ambako, kama alivyosema Mheshimiwa aliyetangulia kuongea kwamba, haki imepotea. Watu hawapati haki zao za msingi kwa wakati, lakini hata zinapovunjwa waziwazi hakuna wa kuwasemea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya tatu wanasema ni kushindwa kufika maeneo ya matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kutokana na ufinyu wa bajeti. Nimesema kwamba shida ni bajeti, pamoja na kupata hela kutoka kwa wahisani, bado nayo ni ndogo haikidhi matakwa ya Tume hii. Sasa tujiulize, ni uvunjwaji wa kiasi gani ambao upo huko chini ambao Tume hii inapaswa kufika maeneo hayo kusaidia na kutoa huduma za kisheria, lakini watumishi hawa hawana hata magari?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze ni nini mpango mkakati kuhusiana na changamoto hii? Kwa sababu, mwisho wa siku kama watumishi hawa hawawezi kupata hivi vitendea kazi kwenda huko chini kuhakikisha kwamba, wanatimiza wajibu wao, basi Tume hii inakuwa haina haja hata ya kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ni kutokuwa na ofisi za matawi katika mikoa 23 ya Tanzania Bara na mikoa minne ya Zanzibar. Hebu tujiulize mbona huko chini tuna Ofisi za Serikali za Mitaa? Tuna ofisi katika ngazi ya kata, tuna ofisi katika ngazi za wilaya, kuna ofisi katika halmashauri na hadi ngazi za mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aeleze shida iko wapi? Tume yake hii kuwa na ofisi, kama wameshindwa ngazi ya vijiji, wameshindwa ngazi ya wilaya, what about ngazi ya mkoa? Kingine hii nchi ni moja, Serikali ni moja, wanashindwa nini hata kwenye halmashauri zetu wakatenga ofisi maalum wakawepo hawa watumishi ambao usiku na mchana wataweza kuwafikia wananchi hawa ambao wanahitaji msaada wa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyoongea na wewe Tume hii imeomba au niseme inaomba kuidhinishiwa shilingi milioni 522,058,000. Hii Tume siyo kwamba inaomba kwa mapato ya ndani, inategemea pesa hizi zitoke kwa wahisani. Tujaribu kujiuliza, ikitokea wahisani hawa wakasema kwamba kwa sasa hatuna uwezo wa kusaidia, hii tume itafanya kazi namna gani? Itaweza namna gani kutimiza majukumu yake ambayo kimsingi majukumu hayo ni ya kumsaidia Mheshimiwa Rais ambaye usiku na mchana anapopata nafasi ya kuongea na Watanzania anachokisema kwanza, anasema; “Watanzania haki zao zilindwe, haki zao zipatikane kwa haraka.” Mwisho wa siku haki wanayoichelewesha ni kama haijapatikana kabisa, hata ikija kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, atakapokuja hapa mbele ku-wind up atueleze kinagaubaga kama Wabunge tuelewe ni nini shida inayopelekea mambo yote haya yasiweze kutekelezeka. Wakati nachangia katika bajeti kama hii mwaka jana nilimwomba Mheshimiwa Waziri, nikasema ikiwa CAG analeta ripoti yake hapa Bungeni, ikiwa TAKUKURU wanawasilisha ripoti zao za kiutendaji kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, shida ipo wapi kwa Tume hii ya Haki za Binadamu kuwasilisha ripoti za mwenendo wa uchunguzi wa mambo ambayo wanakwenda kuyachunguza? Ni kwa nini wasituletee hapa Bungeni tukadadavua, tukaangalia nini shida ili mwisho wa siku kama Bunge tuweze kushauri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, atakapokuja hapa atueleze ni kwa nini, kwa sababu Tume hii imesema wazi ndani ya Kamati kwamba, wao ripoti zao wanazipeleka kwa Waziri wa Katiba na Sheria. Ni kwa nini hajazileta humu Bungeni tukazichambua, kama tunavyochambua taarifa za CAG? Wakati mwingine Bunge linatoa msimamo wa moja kwa moja, linatoa mapendekezo, linaweka msimamo wa pamoja kwamba jambo hili lazima litekelezwe ndani ya muda fulani, shida ipo wapi, kigugumizi kipo wapi taarifa hizi za Tume hii nyeti kuletwa hapa Bungeni? Mheshimiwa Waziri asiponiambia kiukweli nitashika shilingi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kwenye taarifa ya Tume wameeleza kinagaubaga mafanikio ambayo wao wanayaona ni kama mafanikio. Ukisikiliza huu utekelezaji wa bajeti ambayo wanasema ni mafanikio kwao utaona ni kwa namna gani Tume hii haijaweza kutimiza wajibu wake wa Kikatiba...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante...

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana hata vitu ambavyo ni vidogo vya kawaida...

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa...

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, wao wanaviona... (Makofi)

(Hapa Mhe. Agnesta L. Kaiza aliendelea kuongea bila kutumia kipaza sauti)