Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye hotuba hii ambayo inahusu Wizara nyeti kabisa ya Katiba na Sheria. Awali ya yote nitumie fursa hii kwa dhati kabisa ya moyo wangu kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa kwa kuhakikisha kwamba mifumo ya utoaji haki katika nchi hii inaendelea kuboreka siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria na Kamati yetu tunapokea taarifa za taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria na haina shaka yoyote kwa vigezo vyovyote vile ambavyo utatumia, ni kwamba mifumo ya utoaji haki inaendelea kuboreka siku hadi siku. Nakiri kwamba changamoto zote hazijaisha lakini kwa kiwango kikubwa sana mifumo ya utoaji haki imeboreka sana katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Wazari wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Balozi, Dkt. Pindi Chana kwa namna ambavyo anajitoa kuhakikisha kwamba Wizara yake inakwenda vizuri. Pia, nimpongeze sana Naibu Waziri Mheshimiwa Jumanne Sagini, kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais, kukabidhiwa hii Wizara kama Naibu Waziri na sisi kama Kamati na Wabunge wote tuna matumaini makubwa kwamba atafanya kazi kama kawaida yake kwa weledi wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina kama mambo mawili, matatu ya kuzungumzia. Jambo la kwanza ni kuhusu Mpango wa Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign), mpango huu haujajulikana sana, lakini ni mpango muhimu sana hasa kwetu sisi Wabunge ambao tunaongoza majimbo ambayo maeneo makubwa ni vijijini. Mpango huu kwetu sisi ni mkombozi mkubwa sana kwa sababu lengo lake kubwa ni kuhakikisha wananchi wetu katika maeneo yetu wanapopata kesi au mashauri ya kisheria basi waweze kupata msaada wa kisheria bure bila gharama yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu wengi katika maeneo yetu hasa yale ya vijijini hawawezi kumudu gharama za mawakili. Gharama za mawakili ni kubwa wanapokuwa na kesi hawawezi kuwalipa mawakili na mwisho wa siku wananchi wetu wengine wanaishia kupata vifungo na hukumu mbalimbali, lakini si kwa sababu ni wakosefu, ni kwa sababu hawana utaalam wa kisheria. Vilevile, hawana uwezo wa kifedha wa kumudu gharama za mawakili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huu Mpango wa Mama Samia Legal Aid Campaign lengo lake ni kuhakikisha kwamba maeneo yetu ya vijijini kunakuwa na watu ambao wanaishi maeneo yale yale, lakini wanapewa elimu ya sheria kwa kiwango fulani. Kazi yao kubwa ni kuwasaidia wananchi bure wale ambao wana uhitaji wa kupata msaada huu wa kisheria pale ambapo wanapata kesi au mashauri mbalimbali ya kimahakama. Kwa hiyo kwangu, jambo hili ni muhimu sana na kama Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, mwaka jana nilipata fursa ya kuhudhuria uzinduzi wa mojawapo wa hizi programu za Mama Samia Legal Aid pale Bariadi, tulikuwa na Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Balozi, Dkt. Pindi Chana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nilikuwa impressed sana, namna ambavyo set up ilivyokuwa, wananchi wenye shida mbalimbali za kisheria ambao ni wananchi wa kawaida kabisa ambao hawana kabisa uwezo wa kumudu gharama za mawakili, namna ambavyo wanasaidiwa na wanaweza kutoka kwenye shida hiyo ya kuwa na mashauri na kesi mbalimbali. Nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Balozi, Dkt. Pindi Chana, kwamba tulivyokuwa pale na nilimwomba na yeye aliahidi kwamba katika bajeti ya mwaka huu ya fedha ambazo tunazipitisha kwa ajili ya Mama Samia Legal Aid Campaign ambayo kuna baadhi ya mikoa nadhani kama 20 ambayo haijafikiwa. Kwa bajeti hii tunayoipitisha ita-cover baadhi ya mikoa na nikaomba kwamba Mkoa wa Tabora uwe ni mmojawapo kati ya mikoa ambayo safari hii Mama Samia Legal Aid Campaign itafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alikubali na tulikubaliana kwamba Mkoa wa Tabora utakuwa ni mmojawapo ambao utapata fedha hizi na campaign hiyo ifanyike na Tabora pale shughuli hii itafanyika Wilaya ya Nzega. Pia, tulikubaliana kwamba itafanyika kwenye Jimbo langu la Bukene. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri, tunapitisha hela za Legal Aid Campaign naomba ahadi yako kwamba Mkoa wa Tabora utakuwa ni mmojawapo, Wilaya ya Nzega na Jimbo la Bukene ili shughuli hii iende ikafanyike pale na wananchi wangu wa Bukene waweze kupata huduma hii nzuri kabisa ya ushauri wa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutoa wito kwamba Wizara iendelee kusajili hawa watu wa maeneo yetu wanaitwa Paralegal, wale watoa msaada wa kisheria ambao wanakaa kwenye kata zetu, waweze kuwa recruited, wapewe elimu inayostahili na misaada kama ambavyo tulikuwa tumezungumza na kupewa maeneo ambayo watakuwa wanakaa, watakuwa wanapatikana ili wananchi waweze kufaidika na hii nia njema kabisa ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi hasa wa vijijini wasiokuwa na uwezo wanapata huduma ya kisheria bure, kwa sababu tunajua hawana uwezo wa kuwalipa mawakili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni hoja ambayo Mheshimiwa Kakunda ameigusia na Mheshimiwa Agnesta pia ameigusia, kuhusu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Kwa mtazamo wangu inahitajika elimu kubwa sana kwa wananchi ili wajue hasa hii tunayoisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni nini? Inafanya kazi gani? Ipo wapi na inapatikana vipi? Inaonekana kabisa kwamba wananchi wengi hawajui hii ni Tume muhimu sana, sana, sana, kwa sababu ndiyo Tume ambayo inapokea malalamiko yote ya wananchi kuhusu pale ambapo haki za binadamu zimekiukwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, haki za binadamu zinaweza zikakiukwa kwa namna nyingi tu tofauti tofauti. Kwa mfano Mheshimiwa Kakunda, ametoa mfano hapa wa maeneo ambayo yanapakana na hifadhi, wakati fulani kwa mfano tu unaweza ukakuta labda Askari wale wa TFS wanaingia pale wanafanya mambo ambayo ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Labda kuchukua mazao ya watu, labda kuchukua mali za watu na chakula. Vitu kama hivyo mahali sahihi kwa kupeleka malalamiko hayo ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wengi maeneo yetu ya vijijini hata hawajui hiyo Tume unaipataje, ukipata hilo tatizo unakwenda wapi ili ndiyo ufike Tume ya Haki za Binadamu. Mheshimiwa Agnesta, amezungumza hii Tume inakabiliwa na changamoto nyingi sana. Katika mikoa 31 tuliyonayo hii Tume inapatikana kwenye mikoa mitano tu, maeneo mengine yote haipo na hii Tume kwa takwimu zao wakati fulani wanapokea malalamiko mengi sana, lakini wakipokea malalamiko wanapaswa waende wakayafanyie uchunguzi lakini hawana uwezo kabisa wa kwenda kufanya uchunguzi. Hawana magari, hawana fedha, hawana chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wanapokea malalamiko halafu wanakaa nayo tu, wanayakusanya tu kwa sababu uwezo wa kuyafanyia uchunguzi hawana. Ni ushauri wangu moja kati ya maeneo ambayo yanatakiwa yatengewe fedha na fedha ziende, basi ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Kama ambavyo waheshimiwa wengine wamesema, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ana dhamira ya dhati ambayo kila mmoja anaiona waziwazi ya kuhakikisha kwamba uonevu wa namna yoyote ule unakomeshwa kabisa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kumekuwa na maeneo kama ambavyo hasa Mheshimiwa Kakunda, amezungumza maeneo ya vijijini kule wakati fulani kunakuwa na uonevu wa waziwazi wa wananchi kuchukuliwa vitu vyao, kupewa hukumu zingine hazistahiki. Unakuta ofisi za vijiji wakati mwingine zimegeuka kuwa kama Mahakama na mambo kama hayo. Sasa yote hayo yanaweza yakashughulikiwa kama tutakuwa na Tume ya Haki za Binadamu ambayo inafanya kazi ipasavyo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Zedi.

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)