Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, yeye aliyetupa uwezo kwa siku ya leo kuwepo katika Bunge hili kutekeleza majukumu yetu ya Kibunge. La pili, nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa jinsi ambavyo anafanya kazi yake vizuri ya kuliongoza Taifa letu ili kuhakikisha hatma na matumaini ya wananchi wa Tanzania yanafikiwa katika nyanja na sekta mbalimbali. Nisiache kupongeza Wizara nzima ikiongozwa na Waziri wetu na wataalamu wake wote wanaoshughulika na masuala ya Wizara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu moja kwa moja na changamoto zinazokabili Wizara hii ikiwemo Mahakama. Kwanza suala la ufinyu wa bajeti katika Mahakama na Wizara kwa ujumla, hasa Mahakama. Pale ambapo chombo kama Mahakama kinakosa uwezo wa kufanya shughuli zake za kutoa huduma na utoaji wa haki katika nchi ina maana kwamba suala la utawala bora halipo sawa. Kwa hiyo kitendo chochote cha kujaribu kuinyong’onyeza Mahakama kwa kutoipa bajeti yake kihalisia na jinsi ilivyopitishwa na Bunge na jinsi walivyokusudia, hiyo inamaanisha kwamba ni kudhoofisha utoaji wa haki na kukiuka misingi ya haki za kibinadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka kuiasa Serikali katika kutoa fedha kwa ajili ya kuipa Mahakama itoe OC kikamilifu ili iwezeshe Mahakama kutekeleza majukumu yake. Itoe pia suala la kuiwezesha Mahakama katika kuhakikisha kwamba imefika katika maeneo ya huduma. Hata hiyo Tume ya Haki za Binadamu kama kweli ukiweza kuunda chombo ambacho hukiwezi kukihudumia au kukipa fedha, basi ina maana gani? Haina maana ya kuwepo, sasa kama Serikali inataka kutuambia hiko chombo hakina maana, basi Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie kwamba kwa nini hiyo Tume ya Haki za Binadamu haipewi fedha zake na kama ina uhalali wa kuwepo kwa mujibu wa Katiba kwa sababu ipo kwenye Katiba kwa nini hamuipi fedha? Ni suala ambalo Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kama Serikali atujibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la OC lazima Mahakama ipewe, lakini siyo hilo tu pia suala la ukarabati wa Mahakama na ujenzi wa Mahakama. Tunashukuru kwa sababu Serikali imejitahidi kwa kiwango kikubwa sana katika suala la ukarabati wa Mahakama, lakini pia suala la ujenzi wa Mahakama mpya, tunaipongeza Serikali sana katika sehemu hiyo na tunampongeza Mheshimiwa Rais na Wizara kwa ujumla ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba ili mtu aweze kuona kwamba haki inaweza ikapatikana na ikatendeka ni pale tu ambapo anafika katika eneo la utoaji wa haki akaona eneo hilo linafaa, anaburudika kwa sababu ni eneo safi, ni eneo ambalo linaonesha kabisa kwamba kuna tafsiri na taswira ya yeye kupata haki zake za msingi. Sasa anapofika katika eneo ambalo ni la utoaji haki na yakawa ni maeneo ambayo ni mabovu, ni machakavu, anaona hivi hapa kweli nitapata haki yangu au ndiyo nimekuja kuangamia. Kwa hiyo, hili nalo ni suala ambalo lazima Serikali ilione kwa mapana yake, kwamba lazima Mahakama zote zile za zamani zikarabatiwe na maeneo mengine ambayo yanahitaji Mahakama yaweze kupata hizo Mahakama, ikiwemo katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi katika Kata ya Bwawani ambayo nilikwishaitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la upungufu wa watumishi. Suala la upungufu wa watumishi kwa maana ya Majaji, naona Mheshimiwa Rais, anajitahidi sana kuteua Majaji mara kwa mara, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini katika kada hii ya Mahakimu naona kama bado kuna changamoto. Pia, Mahakama ipewe uhuru wa kuajiri yenyewe kwa sababu yenyewe ndiyo inajua inahitaji watu kiasi gani na watu ambao wana-professional kiasi gani katika uzoefu wa kutoa haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo pia cha kutoipa Mahakama uhuru ni kuikiuka ile Ibara ya 4(i) ya Katiba ambayo imezungumzia kuhusu suala la separation of power ambayo ndiyo tunapata masuala ya executive, legislative na Judiciary. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama Serikali yenyewe inashindwa kutoa uhuru kwa Mahakama kwamba iajiri ina maana bado inaingilia (interference) ya Mhimili mwingine, inaonesha kwamba hatuheshimu misingi ya haki za kibinadamu. Pale unapogusa sheria yoyote ambayo inataka kuzuia haki yoyote una maana unakiuka haki za binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye marekebisho ya sheria mbalimbali, maana ya kuwepo kwa sheria ni kuweka sheria ili iweze kusaidia Taifa katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kadhalika, sasa kama kuna sheria ambazo zimepitwa na wakati lakini bado tunaendelea kuziangalia hatuzirekebishi ina maana kwamba, hapa ndipo ambapo pia tunaendelea kukiuka haki za binadamu na kurudisha uchumi wetu nyuma na kuwafanya wananchi wasiweze kuona Serikali kweli ina nia njema ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria kama Sheria ya Rushwa, The Prevention and Combating Corruption Act, Cap 329 na marekebisho yake ya mwaka 2022. Sheria hii bado haiipi TAKUKURU uwezo wa kupambana na rushwa kikamilifu. Nikisema hivi waliosoma hiyo sheria na hata AG anaweza kukubaliana na mimi kwamba, tunahitajika kufanya marekebisho makubwa sana kwenye hiyo sheria ili kuiwezesha TAKUKURU kuwa na uwezo mkubwa na kuiimarisha ili kuwa na adhabu ambazo zinaendana na suala lenyewe la rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo chochote cha kuhujumu mali ya umma si suala la kufumbia macho, ni suala la sisi wote kukazia macho ili tuweze kujenga uchumi ambao Serikali ikikusanya kodi yake pasiwepo na panya yeyote ambaye anaingiza mikono yake kwa sababu ya udhaifu wa sheria, pia kutokuwepo kwa maadili. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ije kuirekebisha sheria hii kwa sababu haipo sawa, imepungua nguvu zake kwa mujibu wa jinsi ambavyo tutaitazama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la marekebisho ya sheria mbalimbali kama nilivyosema, sheria za kurekebisha ni nyingi, lakini najaribu kutaja haya ambayo nimeona yapo hapa. Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1979, kwanza nasikitika sana, Mahakama imetoa hukumu kwamba sheria hii irekebishwe na ikatoa na muda specific, lakini mpaka leo Serikali imekuwa na kigugumizi, ina maana Serikali haitaki kusikia Mahakama imesema kama Mhimili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya wananchi kule nje wanaona kwamba, kumbe Serikali yenyewe kwa sababu ni Serikali inaweza kukataa kutekeleza sheria au kutekeleza hukumu ya Mahakama, ni kwa nini? Nadhani Mheshimiwa Waziri akija hapa katika ku-windup atueleze ni kwa nini Serikali haitaki kuhitimisha jambo la kutekeleza hukumu ya Mahakama ya kurekebisha Sheria ya Ndoa kuhusiana na umri wa kuolewa watoto wa kike? Kwa nini na matatizo hayo bado yanaendelea mpaka leo? (Makofi)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa mzungumzaji kwamba, kuna sheria zinazohusu wanadamu, pia zina maadili ya kidini na maadili mengine ya kibinadamu na utamaduni wao katika nchi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mollel.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo siipokei, mtoa taarifa labda angesoma sheria na kuunganisha pia Sheria za Dini ya Kikristo, Sheria ya Kiislamu, hakuna sheria inayosema kwamba mtoto wa umri wa miaka 16 au 13 aolewe. Kwa hiyo, naomba mzungumzaji asipotoshe Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hiyo ni kengele ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sheria hiyo naomba irekebishwe na Mheshimiwa Waziri atuambie kwa nini Serikali haitaki kurekebisha sheria hii au inakataa uamuzi wa Mahakama ambapo Mahakama ambayo ndiyo chombo pekee kichopewa uwezo wa kutafsiri sheria na kutoa haki katika Taifa hili, otherwise tuambiwe kuna namna nyingine ambayo tunaweza tukapata haki kwa kupitia chombo kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kusema Sheria ya Wanyamapori. Sheria ya Wanyamapori imekuwa na yenyewe ni sheria kandamizi, wanyamapori wana thamani zaidi kuliko binadamu. Binadamu anapouawa fidia anayopewa sijui ni shilingi 500,000, sijui 1,000,000 lakini mnyama akiuawa au akikutwa mtu na ngozi ina maana atapigwa faini ya uhaini ya kuua mnyama ambayo atatozwa faini labda mamilioni ya shilingi au akafungwa hata maisha, hapa binadamu haangaliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii sheria nayo ni ya kuitazama ili fidia ya raia nayo iongezeke kwa kiwango ambacho hakiwezi kumlipa binadamu, lakini kitoe matumaini kwamba, angalau binadamu nao wameonekana ni watu. Kwa hiyo, sheria hii nayo inatakiwa kurekebishwa kwa sababu haitendi haki kwa wananchi wa Tanzania, tunaona wanyama wana thamani zaidi ya binadamu au Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Mabaraza ya Ardhi kwa maana ya Land Disputes Act. Cap. 216 na marekebisho ya 2019 na yenyewe inatakiwa irekebishwe. Mabaraza haya hayatoi haki kwa wananchi wa Tanzania. Mabaraza haya yenyewe katika mikoa, unaweza kukuta kwa mfano, Mkoa wa Arusha, Mabaraza ya Ardhi yapo mawili katika wilaya saba, sasa haki inapatikana wapi hapo na migogoro ya ardhi ni mingi? Naomba sheria hii irekebishe Mabaraza yote ya Ardhi yapitishwe kwenye mkondo wa Kimahakama, kwa sababu itatusaidia sana kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata haki na kuepukana na mambo ya rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta kwenye Baraza la Ardhi la Wilaya, kesi inapigwa kwa mara moja miezi sita. Mtu anakaa miezi sita ndiyo aende kwenye kesi au mwaka mzima ndiyo aende kwenye kesi. Sasa hiyo ni kesi au ni kitu gani? Hiyo ni kudhulumu na ni kwamba, sisi kwa upande wa Sheria tunasema the right delayed is the right denied kwamba, haki iliyochelewa kutolewa ni sawa na haki iliyonyimwa. Sasa sidhani kama Serikali inakusudia kufanya hivyo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kengele ya pili hiyo…

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia dakika moja kidogo tu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili, utachukua muda wa mwingine.

Tunaendelea na Mheshimiwa Dkt. Chaya, ajiandae Mheshimiwa Kilumbe. (Makofi)

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)