Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii vilevile kukushukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia leo kwenye hii Wizara ya Katiba na Sheria. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Balozi Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri kaka yangu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nachukua nafasi hii vilevile kumshukuru sana Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, mtani wangu Mary Makondo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Profesa Ole Gabriel, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais, leo naomba nimshukuru na nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika maeneo mawili yanayoendana na masuala ya Katiba na Sheria. Mwaka jana Mheshimiwa Rais aliunda Tume ya Rais ya Haki Jinai, ambayo hiyo Tume imekuja na mapendekezo 18. Hayo mapendekezo yote yamejikita katika kuhakikisha kwamba, wananchi wetu hususani wananchi wa kawaida wanapata fursa ya kupata haki ya kusikilizwa kwenye masuala ya kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni eneo la muhimu sana ambalo kimsingi ni utekelezaji wa zile 4Rs za Mheshimiwa Rais, kwa upande wa (reform) maboresho. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa sababu mapendekezo haya 18, yanaenda kuleta mabadiliko makubwa sana kwa wananchi wetu hususani katika utoaji wa haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ambalo ningependa kumpongeza Mheshimiwa Rais, ni ile Kampeni yake ya Mama Samia Legal Aid Campaign, Kampeni ya Kisheria ya Mama Samia. Wachangiaji wengi wameeleza huu ni ubunifu mkubwa ambao sasa tunaenda kuwafikia wananchi wa kawaida kule chini, ndugu zetu wa kawaida kule chini wanapata shida sana za wapi wanaweza kupata misaada ya kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia kampeni hii tumeona, hata Singida alikuja Waziri akazindua, sasa wananchi wetu wa kutoka vijijini, Vijiji vya Sanza, Makuru, Kintinku na kwingineko sasa watakuwa na usaidizi wa masuala ya kisheria. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, hii ni mojawapo ya utekelezaji wa zile 4Rs, (Reform). Namwomba Waziri sasa hii kampeni ya Rais iende ikafanye kazi. Tunataka kuona matokeo, tunataka kuona wananchi wetu wanatetewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hizo shukrani, nina maeneo makubwa mawili ningependa kuchangia leo. Eneo la kwanza, ni kuhusu ufaulu wa Law School, wote ni mashahidi kwenye mitandao ya kijamii tulishuhudia kelele nyingi sana za wanachuo na wanafunzi kuhusu matokeo ya Law School. Naomba nirejee taarifa za mwaka 2021/2022 kwa batch ya 33 ya wanafunzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi waliofanya mitihani walikuwa 633, kati ya wale wanafunzi 633, wanafunzi 26 tu waliofanya mtihani kwa mara moja (first sitting) ndiyo waliofaulu mtihani, hii ni sawa na asilimia nne. Kati ya wale wanafunzi 633, wanafunzi 342 walitakiwa kurudia masomo yao (supplementary) ambao ni sawa na 54%, lakini kati ya wale wanafunzi 633, wanafunzi 265 walifeli kabisa, walikuwa (discontinued) na hawa walitakiwa kurudia masomo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni uwekezaji wa nchi kama tuna wanafunzi 633 waliolipa ada then asilimia nne tu ndiyo wanafaulu kuna tatizo sehemu. Sasa tatizo ni nini? Analysis yangu inanionesha kuna maeneo matatu ambayo inawezekana ikawa ni challenge. Kwanza ni vyuo vyetu havifanani, ukiacha kwamba TCU ina-regulate, ina-standardize vyuo vyetu, bado vyuo vyetu havifanani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtoto anayetoka UDSM, anayetoka Mzumbe, anayetoka SAUT na kwingine amesoma sheria, kwingine wanasoma miaka mitatu, kwingine miaka minne hawafanani. Hawafanani capacities vilevile ufundishaji haufanani. Kwa hiyo, nimwombe Waziri wa Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Mheshimiwa Waziri Profesa Mkenda, wakafanye utafiti wajue kwa nini wanafunzi wanafeli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine utafiti wangu umenionesha kwamba, wanafunzi wanafanya masomo 11 ndani ya mwaka mmoja na wana miezi sita ya kuingia darasani na miezi sita ya kwenda kwa ajili ya mafunzo. Kitu nilichojifunza kuna wanafunzi wengine wanakutana na yale masomo 11 kwa sababu ya utofauti wa vyuo anakutana nalo hilo somo mara ya kwanza Law School, hilo ni tatizo. Kwa hiyo, ndiyo maana tunajikuta ni asilimia nne tu ya wale ambao wamejiunga kwa ajili ya Law School ndiyo wanaofaulu, kwa hiyo, kuna tatizo sehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la tatu, taarifa nilizopata kutoka kwa hawa ambao waliwahi kufanya hii mitihani, ule utoaji wa zile regular assessment, continuous assessment matokeo yake unachelewa. Mtu anafanya test one, anaenda test two na anaenda test three hajawahi kupewa matokeo, sasa mtu ataji-assess vipi kama amefaulu ili aweze ku-make progress, hilo nalo ni tatizo. Kwa hiyo, ni eneo ambalo ningeshauri waweze kuliangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri nini? Jambo la kwanza, utafiti unaonesha kwamba ile asilimia nne inawezekana ikawa ni asilimia sahihi, kwa sababu wanafunzi wetu wanatoka kwenye vyuo tofauti tofauti, ambao wamefundishwa tofauti tofauti, vyuo vyenye uwekezaji tofauti tofauti na walimu wenye capacity tofauti tofauti. Tunahitaji kuwa na entry exam, tuwachuje kabla hawajaingia kwenye Law School ili tupate wale ambao wataenda kwenye Law School, kwa sababu haya malalamiko tunayoyapata kwamba tunafeli, tunaonewa nadhani tatizo ni competency ya wanafunzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tutawezaje kuwachuja tuwapate wale watu wanaoenda kwenye Law School, lazima tuwe na kitu kinaitwa screening test, tuwa-screen ili tuwapate. Hivi ni lazima kila mwanafunzi aende Law School? Kuna professional nyingine, kuna kazi nyingine hazihitaji mtu awe na Law School. Kwa hiyo, tuwapate wale wenye sifa ili wakajiunge na Law School. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Waziri, hebu tupitie mtaala wa Law School, tujiridhishe kile tunachoenda kuwapa wanafunzi wetu, je, wanastahili? Niliwahi kujiuliza kitu kimoja Law School should be a non-academic program. Walishasoma miaka minne huko walishawa-pump na theory na principles, tunahitaji waende kuwenye practice. Kwa hiyo, it is a non-academic program. Ndiyo maana inafundishwa na watu waliobobea walioko kwenye field kama Majaji na watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuangalie huu mtaala wetu tusije tukarudia yale yale tuliyomfundisha year one akiwa UDSM, year two akiwa Mzumbe, tunataka kuyarudisha tena kwenye Law School. Tutakuwa hatuwatendei haki, tuwafundishe vitu vitakavyowajenga professional yao. Kwa hiyo, hilo ni eneo la pili ambalo nashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo nimelieleza, tutumie walimu ambao kwa kweli ni wabobezi, wamekaa field, kwa sababu lengo letu hatutaki kurudia theories tulizowafundisha. Tunataka kuwafundisha kazi na ili kumfundisha kazi, watumie mtu ambaye yupo kazini na hilo najua wanalifanya lakini nasisitiza waendelee kulifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni ombi, kule kwangu Manyoni, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri ametujengea Mahakama ya kisasa ya Wilaya pale Manyoni, haijawahi kutokea, pia ametujengea Mahakama ya Mwanzo ambayo imeungana na Jengo la Mahakama ya Wilaya ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama zetu za Mwanzo nyingi zina hali mbaya. Bahati mbaya zaidi wananchi wetu wanapata shida wanatoka umbali mrefu kutembea kwenda kutafuta huduma za kisheria. Kwa mfano, Sanza hawana Mahakama kule, kuna jengo ni chumba kimoja, Heka, Chikola, Nkonko, Kintinku, hawana Mahakama za Mwanzo. Namwomba Mheshimiwa Waziri kwenye maeneo haya niliyoyataja eneo la Sanza, eneo la Nkonko, eneo la Chikola na eneo la Kitinku, tunaomba aje atuboreshee majengo ya Mahakama. Mheshimiwa Rais, anasisitiza 4Rs katika ile R ya (Reform) mojawapo lazima tuweke maboresho kwenye Mahakama zetu. Tuwe na Mahakimu wa kutosha, vilevile majengo yetu yavutie. Mtu hata anapoenda kudai haki awe kwenye mazingira salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni suala la Watumishi wa Mahakama, tuna upungufu mkubwa sana wa Watumishi wa Mahakama hususani pale Manyoni. Lingine unamkuta Hakimu wa Wilaya amepanga mtaani, Hakimu wa Wilaya amepanga mtaani na kwenye ile nyumba aliyopanga landlord ana kijana ambaye ni kibaka, kila siku anapelekwa Polisi, Mahakamani, huyo Hakimu atatenda haki? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri tuwajengee nyumba Mahakimu wa Wilaya hasa wale Viongozi wa Wilaya wawe kwenye mazingira salama, kuwaweka mitaani siyo salama kwao, it is very risk. Kwa hiyo, ningeshauri Mahakimu wale Viongozi wa Wilaya tuwaangalie, tuwajengee nyumba kama tunavyojenga Nyumba za Wakurugenzi, tunavyojenga Nyumba za Viongozi wengine Wakuu wa Wilaya, Mahakimu wa Wilaya nao tuwajengee nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru na naendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Nakushukuru sana. (Makofi)